Somo la 6: Chimbuko la Ibrahimu

Mwanzo 12 – 14
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
2
Lesson Number: 
6

Somo la 6: Chimbuko la Ibrahimu

(Mwanzo 12 – 14)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Mara nyingi katika siku za hivi karibuni nimesoma habari za vijana kushikwa na wasiwasi na hofu. Kwa kawaida huwa tuna hofu ya mambo tusiyoyajua. Somo letu juma hili linamhusu mtu ambaye ana kila sababu ya asili ya kujawa na hofu kutokana na kukabiliana na mambo yasiyojulikana. Ibrahimu anaondoka nchini kwake na kuwaacha marafiki zake na kwenda katika nchi ambayo kamwe hajawahi kuiona. Kinachobadili hali ya Ibrahimu si cha dunia hii (supernatural). Lakini, badiliko halitokei kwa ghafla. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza juu ya Ibrahim na kuishinda hofu!

I.        Nenda

A.        Soma Mwanzo 12:1. Abramu anaondoka na nani? (Familia yake yote).

1.        Anakwenda wapi? (Mungu anasema tu kwamba “atamwonyesha” Abramu nchi yake mpya. Inaonekana Abramu hajui!)

B.        Soma Mwanzo 11:31-32. Asili ya Abramu ilikuwa katika nchi gani? (Uru wa Wakaldayo. Utakumbuka katika somo letu juma lililopita watu walipingana na amri ya Mungu (Mwanzo 9:1) ya “kuijaza dunia.”)

1.        Baada ya gharika, Tera anaelekea wapi? (Kaanani. Hii inaashiria kwamba tayari baba yake Abramu alikuwa anaelekea Kaanani, lakini kamwe hakuvuka Harani.)

C.        Soma Mwanzo 12:2. Nina uhakika Abramu anashangaa kwa nini aondoke ili aweze kubarikiwa. Unaona kidokezo gani kwenye kifungu hiki juu ya sababu ya kuondoka? (Mungu anakwenda kufanya “taifa kubwa” kutoka kwa Abramu. Uru wa Wakaldayo inahusiana na kile kitakachokuwa Babeli. Mataifa mawili makubwa mahali pamoja itakuwa tatizo.)

D.        Soma Mwanzo 12:3. Unadhani ahadi ya kwamba jamaa zote za dunia zitabarikiwa kupitia kwa Abramu inamaanisha nini? (Soma Matendo 3:25-26. Huu ni unabii kwamba Yesu atakuja kutoka katika uzao wa Abramu.)

E.        Soma Mwanzo 12:4. Abramu anaondoka kutoka wapi katika kujibu wito wa Mungu? (Harani.)

1.        Angalia tena Mwanzo 11:31 na usome Matendo 7:2-4. Mwanzo 11:31 inaashiria kwamba baba yake Abramu alianza safari ya kwenda Kaanani, na tayari Abramu alijua anakokwenda. Kitabu cha Matendo kinafafanuaje jambo hili? (Kitabu cha Matendo kinafafanua kwamba Abramu anapokea wito wa asili kutoka kwa Mungu na anachelewa Harani hadi baba yake anafariki. Kisha Mungu anatoa upya wito wake kwa Abramu.)

II.        Misri na Gerari

A.        Soma Mwanzo 12:10. Je, hii inaonyesha uhaba wa imani kwa Mungu? Au, Abramu anazingatia tu uhalisia? (Inaonyesha kuwa Abramu anaogopa mustakabali wake.)

B.        Soma Mwanzo 12:11-13. Je, hii inadhihirisha kutomtumaini Mungu? Au, hili ni suala la kiuhalisia zaidi? (Safari ya kwenda Misri inazua mjadala, lakini hapa inavuka msitari. Abramu anautegemea uongo wake na akili zake kwa ajili ya usalama wake badala ya kumtegemea Mungu.)

1.        Itafakari mantiki ya Abramu. Kama Wamisri wangemuua Abramu ili wamchukue mkewe, kwa dhahiri wasingekuwa na kikwazo cha kumchukua dada yake kama mke! Kwa namna yoyote ile Abramu anampoteza mkewe. Je, una hoja yoyote inayounga mkono mantiki ya Abramu? (Augustine anajenga hoja kwamba huu haukuwa uongo kwa sababu Sara alikuwa “karibu kidamu.” Ni kwamba tu Abramu hakuweka wazi kuwa Sara pia alikuwa mkewe. Sidhani kama ningenunua gari (au ngamia kwa muktadha wake) kutoka kwa Augustine.)

C.        Soma Mwanzo 12:14-15. Je, sasa Sara amekuwa mke wa Farao? (Soma Esta 2:12. Watoa maoni wanatuambia kuwa kitendo hiki kilianzisha tu mchakato wa Sara kuwa mke wa Farao.)

D.        Soma Mwanzo 12:16-17. Abramu anafanya nini juu ya matukio haya ya kutisha kabisa? (Anakubali kupokea upendeleo kutoka kwa Farao!)

1.        Mungu anafanya nini juu ya haya matukio ya kutisha? (Anapeleka mapigo kwa Farao!)

2.        Hii inatupatia fundisho gani juu ya wema wa Mungu kwetu hata pale tusipowajibika?

E.        Soma Mwanzo 12:18-20. Unadhani Abramu alihitimisha nini kuhusu uongo wake? (Bado yu hai na amerejeshewa mkewe.)

1.        Hii inaakisiwaje kwa Mungu wa Abramu?

F.        Soma Mwanzo 20:1-3. Unadhani ni kwa nini Abramu anadanganya tena? Je, hajajifunza chochote?

G.        Soma Mwanzo 20:4-6. Nani mwingine anadanganya? (Sara! Mtu mwadilifu ni mfalme wa kipagani.)

H.        Soma Mwanzo 20:9-11. Je, Abramu alidanganya kutokana na hofu?

1.        Ni nani anayeonyesha uadilifi katika mazingira haya? Mungu anazungumza na nani? (Tunatakiwa kutambua kwamba nyakati zingine wapagani wataenenda kwa usahihi zaidi kuliko wafuasi wa Mungu.)

I.        Soma Mwanzo 20:12-13. Biblia inaandika kwamba Abramu alidanganya mara mbili kuhusu uhusiano wake na Sara, lakini hii inatuambia kuwa hii ilikuwa ni kawaida ya Abramu mara kwa mara kutokana na hofu yake. Kabla hatujajadili hili, soma Mwanzo 11:31. Hii haisemi kuwa Sara ni binti wa Tera, kifungu kinasema kuwa yeye ni mkwewe Tera. Ikiwa hilo ni sahihi, basi Abramu pia amedanganya juu ya msingi wa madai ya kwamba Sara ni dada yake. Hii inazungumzia nini kuhusu Abramu?

J.        Soma Mwanzo 20:17-18. Litafakari hili. Abimeleki hana hatia na Mungu anakubaliana na hili (angalia Mwanzo 20:4-6). Soma pia Mwanzo 12:3. Je, ahadi kwa Abramu inasambaa hadi kwa wale wote wanaomfuata Mungu? Je, uwanja umeinamia upande wetu na dhidi ya wapagani?

K.        Soma Zaburi 23:3. Jina la nani linapigwa kutokana na shari za kutisha za Abramu? (Mungu anatutaka katika njia zake kwa kiasi fulani ili kulinda jina lake. Abramu, mfuasi wa Mungu wa kweli, anaonekana kuwa na maadili ya chini kuliko wapagani. Abramu, kutokana na hofu isiyo na msingi, anachukulia kimakosa kwamba wapagani wako radhi kumwua kwa ajili ya kumpata mkewe.)

L.        Soma Isaya 41:8. Mungu anamuita Ibrahimu “Rafiki yangu.” Je, unaweza kutilia shaka upendo wa Mungu kwetu wadhambi?

M.        Soma Waebrania 11:8-10. Je, Mungu anatuchukulia kwa namna ya upendeleo mkuu kwa kadiri inavyowezekana? Je, tunampa Mungu faida ya mashaka?

III.        Lutu

A.        Soma Mwanzo 13:7-9. Nani ambaye kwa kawaida alikuwa na nafasi ya kwanza ya kuchagua nchi ya kwenda? (Abramu, kwa sababu alikuwa mkubwa na alikuwa na ahadi ya Mungu.)

1.        Hii inatuambia nini kumhusu Abramu na ubinafsi? (Yeye si mbinafsi.)

2.        Hivi punde tu tumetoka kujadili kwamba Abramu alikuwa mtu mwenye hofu na mwenye mazoea ya kudanganya. Tunapaswa kuhitimisha nini kuhusu tabia yake? (Abramu anafanana na wewe na mimi. Ana kasoro fulani za kitabia, lakini pia ana tabia fulani nzuri.)

B.        Soma Mwanzo 13:10-12. Je, Lutu ni mbinafsi? (Ndiyo. Alijichukulia ardhi bora.)

C.        Soma Mwanzo 13:14-15. Utaona kwamba Abramu alipokuwa mdogo kwa Abimeleki Mungu aliwasiliana na Abimeleki na sio Abramu. Kwa kuwa sasa Abrahamu anadhihirisha kwamba yeye si mbinafsi, Mungu anawasiliana na Abramu. Hii inaongezea nini kwenye taswira yetu ya Mungu mwenye upendo? (Mungu anaendelea kuwa mwaminifu kwa Abramu, lakini Mungu hamwonyeshi Abramu upendeleo wa kuzungumza naye moja kwa moja.)

IV.        Vita

A.        Abramu anaishi kwa amani Kaanani, lakini matukio ya dunia yanakwenda kwa kasi katika maeneo yanayomzunguka. Warithi wa Nimrodi wanaungana, muungano unaoishia kufanya vita dhidi ya muungano wa wafalme katika eneo alilopo Lutu. Hili ni tukio la maana sana. Soma Mwanzo 14:11-12. Uchaguzi wa Lutu wa ardhi bora unageuka na kuwaje? (Ni janga. Lutu anapoteza kila kitu, ikiwemo uhuru wake, ikiwa ni matokeo ya vita.)

B.        Soma Mwanzo 14:13-14. Abramu ana jeshi “lililofunzwa.” Hiyo inatuambia jambo gani, kama lipo, kuhusu Mkristo na matumizi ya nguvu?

C.        Soma Mwanzo 14:15-17. Inashawishi kusema kwamba Abramu alishambulia sehemu ndogo tu ya jeshi la muungano, lakini hii inatuambia kuwa Abramu alimshinda “Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa Pamoja naye.” Utakumbuka Abramu alidanganya kwa sababu alikuwa na wasiwasi juu ya maisha yake? Hii inatuambia nini juu ya kukua kwa imani ya Abramu? (Abramu hana woga. Mungu anampatia ushindi wa kustaajabisha.)

D.        Soma Mwanzo 14:18-20. Abramu anampa nani sifa kwa ushindi wake? (Anaamini kuwa Mungu alimpa ushindi kwani anatoa zaka kwa Melkizedeki ambaye ni mfalme na kuhani wa Mungu wa kweli.)

E.        Hebu tupitie swali ambalo nimekuwa nikiliuliza: Abramu anafanya nini kwa ajili ya hadhi ya Mungu? (Abramu asiye na woga sasa ni shahidi anayeng’aa wa uwezo wa Mungu.)

F.        Rafiki, je, unaona jinsi Abramu alivyopiga hatua kutoka kwenye hofu hadi kutokuwa na hofu na kumtumaini Mungu? Unaona jinsi Abramu alivyopiga hatua kutoka kwenye kudhuru hadhi ya Mungu hadi kuwa shahidi mkuu wa Mungu? Je, utadhamiria leo, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kumtumaini Mungu na hivyo kuwa shahidi mkuu?

V.        Juma lijalo: Agano na Ibrahimu.