Somo la 11: Yusufu, Mjuzi wa Ndoto

Mwanzo 37–41
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
2
Lesson Number: 
11

Somo la 11: Yusufu, Mjuzi wa Ndoto

(Mwanzo 37–41)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, umewahi kupitia nyakati ngumu maishani mwako na hukuelewa kwa nini Mungu aliruhusu mambo hayo yatokee? Au, je, umewahi kupitia nyakati ngumu na ukaelewa jinsi kushindwa kwako kutawala hisia kulivyochukua nafasi kubwa kwenye matatizo yako? Katika somo letu la leo, matatizo ya Yusufu kwa kiasi kikubwa yanaonekana kuwa matokea ya uamuzi wake mbaya na wa baba yake. Licha ya hayo, Mungu anatenda mambo makubwa kupitia kwa Yusufu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi juu ya kumtumaini Mungu!

  1.    Mchongezi
    1.    Soma Mwanzo 37:2-4. Kuna hisia nyingi ndani ya hivi vifungu vitatu. Je, ni sahihi kutoa taarifa juu ya kasoro za wafanyakazi wenzako?
      1.    Soma Mithali 17:9 na Mithali 9:8. Je, hii inatupatia mwongozo juu ya kutoa taarifa za wafanyakazi wenzetu?
    1.    Angalia tena Mwanzo 37:3. Kama una mawasiliano ya moja kwa moja na kiongozi wa juu kabisa, je, hiyo inakufanya uwe na uwezekano mkubwa wa kumpelekea taariza za wafanyakazi wenzako?
    1.    Angalia tena Mwanzo 37:4. Je, mtazamo wa vijana wengine unatokana na dosari ya Yakobo (Israeli) kwa asilimia zote? (Baba hasaidii chochote, lakini Yusufu anaitumia vizuri fursa ya uhusiano wake.)
      1.    Je, ungependa kuwa kwenye mazingira ya Yusufu?  Je, ungepeleka taarifa za tabia mbaya kama “malipo” ya chuki?
  1.   Ndoto za Awali
    1.    Soma Mwanzo 37:5-7. Unadhani Yusufu aliielezeaje ndoto yake? Kwa staha? Au, kwa majivuno na kiburi?
      1.    Kwa nini anahabarisha juu ya ndoto hii?
      1.    Kwa nini Mungu anampa hii ndoto?
    1.    Soma Mwanzo 37:8. Je, unashangazwa na mjibizo (reaction) wa nduguze? Unadhani Yusufu alishangazwa?
      1.    Kama Yusufu hakushangazwa, alikuwa anafikiria nini?
    1.    Soma Mwanzo 37:9-10. Jambo gani linamhamasisha Yusufu kuwaambia nduguze ndoto hii? (Yusufu hatumii mantiki. Hawezi kutawala hisia. Anatambua kwamba jambo hili halitakuwa jema kwenye uhusiano wake na ndugu zake.)
    1.    Soma Mwanzo 37:11. Taarifa ya kwamba ndugu zake “walimhusudu” ni tofauti sana na ndugu zake kumchukia tu Yusufu na kutozungumza naye. Kitu gani kiliwafanya nduguze wawe na husuda? (Wangekuwa na husuda endapo tu kama walidhani jambo hili linaweza kuwa la kweli. Walikuwa na wasiwasi kuwa Yusufu atawatawala.)
      1.    Je, Yakobo aliiamini ndoto?
  1.      Msimamizi
    1.    Soma Mwanzo 37:12-14. Kumbuka kwamba Yusufu ni mdogo kuliko ndugu yake yeyote anayechunga mifugo. Kwa nini Yakobo anamchagua kumpelekea habari za kazi inayofanywa na kaka zake wakubwa?
      1.    Je, Yusufu anaanza kutawala?
      1.    Zingatia mahali pale. Je, hii inapiga kengele akilini mwako? (Soma Mwanzo 34:24-26. Hapa ndipo mahali ambapo ndugu wawili wa Yusufu waliwaua wanaume wote katika mji. Yakobo anafahamu kuwa anamtuma Yusufu kwa wauaji wanaomchukia. Yumkini hataki kukubaliana na ukweli huu.)
    1.    Yusufu anakutana na kaka zake. Soma Mwanzo 37:18-20. Je, bado kaka zake ni wauaji?
      1.    Je, wanaamini kuwa ndoto za Yusufu zinaweza kuwa za kweli? (Kwa kufikiria kuwa zinaweza kuwa za kweli ndio huamsha nia ya kutaka kuua.)
    1.    Soma Mwanzo 37:21-22 na Mwanzo 37:25-29. Sio ndugu zake Yusufu wote ni wauaji. Jambo gani linamtofautisha Reubeni na ndugu zake wote? (Yeye pekee ndiye aliyetaka kumwokoa Yusufu na kumrudisha nyumbani.)
    1.    Soma Mwanzo 37:32-35. Je, Yakobo yuko sahihi kwamba “mnyama mkali” ndiye aliyefanya kitendo kama hicho?
      1.    Fikiria kwamba wewe ndiye mmojawapo wa ndugu hawa na unajaribu kumliwaza baba yako?
  1.   Mtumwa
    1.    Soma Mwanzo 37:36, Mwanzo 39:1, na Mwanzo 39:5-7. Kama ungekuwa kwenye nafasi ya Yusufu, hili ni jaribu kubwa kiasi gani? Au, hili si jaribu hata kidogo, bali hatari ya kuiepuka bila kudhuriwa?
    1.    Soma Mwanzo 39:8-9. Yusufu anakataa ombi la mke wa bosi wake kwa msingi gani? (Ananukuu uaminifu kwa bwana wake na uaminifu kwa Mungu.)
    1.    Soma Mwanzo 39:11-15. Kitu gani kinamhamasisha mke kusema uongo huu? Kwa nini anataka kumdhuru Yusufu?
      1.    Je, hamasa hii ni ya kishetani? Yaani, nguvu zisizo za kawaida zimekuja ili kumdhuru Yusufu?
      1.    Kuna vuguvugu linaloendelea nchini Marekani linalojenga hoja kwenye mazingira kama haya, kwamba wanawake wote wanatakiwa kuaminiwa. Au, je, hali hii ni tofauti?
  1.    Mfungwa
    1.    Soma Mwanzo 39:19-20. Je, kuna sababu yoyote kudhani kuwa Potifa anatilia shaka kisa cha mkewe? (Anamweka Yusufu kwenye gereza maalumu, ambapo ninadhani wahalifu wabaya kabisa wanafungwa hapo.)
    1.    Soma Mwanzo 39:21-22. Biblia inatuambia kuwa Mungu “akamfadhili” Yusufu. Je, hivyo ndivyo ungeiangalia hali yako kama ungekuwa Yusufu? (Yusufu ametoka kuwa mwana mpendwa wa mtu tajiri mwenye nguvu na uwezo mkubwa, hadi kuwa mtumwa ambaye yuko gerezani.)
      1.    Kuna mfanano kati ya maisha ya Yusufu na Yesu. Wote wawili wanapata mateso kama sehemu ya safari ya kuwaokoa wengine. Je, unadhani kuwa Yusufu anaelewa jambo hili? Je, ana hasira juu ya kiburi cha ujanani mwake kwa kuwashirikisha nduguze ndoto zake – ndoto zilizomuweka kwenye njia ya utumwani?
    1.    Mnyweshaji mkuu wa Farao na mkuu wa waokaji wa mfalme wanatupwa gerezani kwa muda fulani. Soma Mwanzo 40:9-13 na Mwanzo 40:16-19. Kwa muda wa siku tatu ndoto hizi, kama zilivyotafsiriwa na Yusufu, zinatimia. Soma Mwanzo 40:14-15. Yusufu anatafuta fursa gani kwenye mazingira haya?
      1.    Je, huu ni uhalisia? Je, Farao atajali juu ya haki kwa mtumwa wa Kiebrania? (Soma Mwanzo 40:23. Mambo ni mabaya zaidi, mkuu wa wanyweshaji anamsahau Yusufu.)
    1.    Miaka miwili baadaye, Farao anaota ndoto juu ya ng’ombe. Soma Mwanzo 41:8-10 na Mwanzo 41:12-13. Vipi kama hapo awali mkuu wa wanyweshaji asingesahau habari za Yusufu? Vipi kama Farao angeingilia kati na kumwachia Yusufu kutoka gerezani? Hilo lingeathirije mambo hapa?
    1.    Soma Mwanzo 41:14-16. Je, ungeshawishika kumtoa Mungu kwenye jibu lako? Je, kitendo cha Yusufu kumpa Mungu utukufu kinamzungumziaje baada ya matukio yote ya kukatisha tamaa maishani mwake?
    1.    Soma Mwanzo 41:25-30. Kama ungekuwa Yusufu, na kuambiwa kuwa unaweza kuepuka mambo yote mabaya yaliyokutokea kuanzia kwenye safari yako ya kuwasimamia kaka zako, lakini matokeo yatakuwa ni kwamba makumi kwa maelfu ya watu watapigwa na njaa kali, je, ungeridhika na safari ya maisha yako?
    1.    Soma Mwanzo 41:33-36. Ni punde tu umetoka kutolewa gerezani na kuwekwa mbele ya Farao. Je, ungeenda mbali zaidi ya ndoto na kumpendekezea Farao mkakati wa kukabiliana na baa la njaa inayotarajiwa? (Lazima Roho Mtakatifu atakuwa amemtia msukumo wa kuendelea. Vinginevyo, inaonekana kama ni majisifu.)
      1.    Je, unadhani Yusufu alikuwa anajiwazia nafsini mwake kwamba yeye ni “mtu mwenye akili na hekima?”
    1.    Rafiki, kisa hiki kinatufundisha jinsi Mungu atakavyotuokoa kutokana na kutokuwa/kupungukiwa busara. Kinatufundisha jinsi tunavyotakiwa kumtumaini Mungu kwa taswira pana maishani. Tukimtumaini katika masumbufu yetu, atakuwa mwaminifu kwa wakati wake! Je, utadhamiria, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kumtumaini Mungu?
  1.   Juma lijalo: Yusufu, Mtawala wa Misri.