Somo la 12: Kufa Kama Mbegu 

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Yohana 12, Luka 14, Wafilipi 2
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
3
Lesson Number: 
12

Somo la 12: Kufa Kama Mbegu 

(Yohana 12, Luka 14, Wafilipi 2) 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza. 

Utangulizi: Katika Yohana 12:23 Yesu alielezea kipindi cha mpito kutoka kwenye huduma yake hadi kipindi cha kujaribiwa kwake hadi kifo chake. Katika muktadha huu Yesu alijilinganisha (Yohana 12:24) na punje ya ngano inayokufa na matokeo yake “hutoa mazao mengi.” Yesu anazungumzia kifo chake kinachokaribia. Je, hii dhana ya kufa inahusika kwetu? Ikizingatiwa kwamba kiuhalisia Yesu alikuwa anazungumzia kifo chake kinachokaribia na imani yetu haijajengwa juu ya mauti yetu, bali juu ya jinsi tunavyoishi maisha yetu. Tunapaswa kuelewaje dhana ya kufa kama mbegu? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi! 

I.  Yesu, Ngano, na Chuki 

A.  Soma Yohana 12:17-19. Ni nini tathmini ya viongozi wa dini wa Kiyahudi kuhusu mgogoro wao na Yesu dhidi ya uongozi wa kiroho wa taifa? (Wanaamini kuwa wamepotea. “Ulimwengu umekwenda nyuma yake.”) 

B.  Soma Yohana 12:9-11. Ni nini jibu la viongozi wa Kiyahudi kwenye suala la umaarufu wa Yesu? (Hawatamuua Yesu tu, bali pia watamuua Lazaro kwa sababu yeye ndiye shuhuda aliye hai juu ya uwezo wa Yesu wa kufufua wafu.) 

C.  Soma Yohana 12:20-21. Kwa nini miadi hii inayoombwa ya kumwona Yesu ni muhimu katika muktadha wa umashuhuri wa Yesu? (Inaonyesha kwamba hadhi ya Yesu sasa imesambaa kuvuka mipaka ya taifa la Kiyahudi hadi kwenye ulimwengu wa Mataifa.) 

D.  Soma Yohana 12:23. Yesu anatoa jibu gani kwa Wayunani waliotaka kumwona na kujifunza zaidi habari zake? (Anaonekana kusema kwamba muda wa huduma yake binafsi umekwisha. Anaingia katika kipindi cha mwisho cha maisha yake duniani.) 

1.  Una maoni gani juu ya kipindi hiki? Jinsi umaarufu wa Yesu unavyozidi kupaa, anaelekea kufa? 

E.  Soma Yohana 12:24. Yesu anamzungumzia nani? (Haturejelei sisi, bali anajirejelea mwenyewe. Katika mzunguko wa maisha anaelekea katika kipindi cha kufa kwake.) 

1.  Ni vigumu kulinganisha rejea ya Yesu ya “hukaa hali iyo hiyo peke yake” na mazingira yake ya sasa. Yesu ni mashuhuri sana, maarufu mno kiasi kwamba viongozi wa Kiyahudi wanadhani kuwa ameshinda. Yesu anamaanisha nini anaposema hivi? (Anasema kuwa huduma yake itasambaa kwa umaarufu mkubwa atakapokuwa ametoweka.) 

a.  Je, hiyo ni kwa sababu ya kifo chake? (Sababu sio kifo chake tu, bali maisha yake makamilifu yakifuatiwa na kifo chake kwa ajili yetu. Hili ni swali kubwa na gumu zaidi kuliko kujitoa nafsi tu.) 

b.  Je, tunapaswa kuangalia kauli ya Yesu kwa mtazamo rahisi kabisa? (Yesu anazungumzia jambo ambalo kila msikilizaji wake analifahamu kuwa ni kweli. Lazima ngano ife ili iweze kuzaa. Yesu anafanya mlinganisho unaomhusisha yeye.) 

F.  Soma Yohana 12:25. Je, bado Yesu anajizungumzia nafsi yake? (Hapana. Anasema “yeyote.” Hii inamrejelea kila mtu.) 

1.  Je, tunapaswa kuelewa jambo hili kumaanisha kwamba lazima tuyachukie maisha? Kwa dhahiri siyachukii maisha yangu. Na, simfahamu mtu yeyote ambaye ni Mkristo wa dhati ambaye anayachukia maisha yake. Je, unayachukia maisha yako? 

a.  Kama umejibu kwamba unayachukia maisha yako, je, hiyo ni kwa sababu ya shughuli zako za kupeleka injili kwa wengine? (Binafsi hilo ninaona haliwezekani.) 

G.  Soma Luka 14:26 na Yohana 19:27. Yesu anatuambia kuwa tusiyachukie maisha yetu tu, bali pia tuichukie familia yetu. Kisha baadaye tunaona kwamba Yesu anamwambia Yohana amhudumie mama yake kabla tu Yesu hajafa. Je, Yesu alimchukia mama yake? (Kwa dhahiri hapana. Alikuwa anaangalia mambo mazuri kwa ajili ya mama yake. Anamwonyesha mama yake upendo.) 

1.  Hivyo, Yesu anatutaka tufanye nini anapoturejelea sisi kuyachukia maisha yetu na familia zetu? Yesu anatutaka tufanye nini ili kufa kama yeye? 

II.  Muktadha wa Chuki 

A.  Tunatakiwa kuchunguza kwa kina kisa alichokielezea Yesu kabla tu hajatupatia wito wa kuyachukia maisha yetu na familia zetu. Soma Luka 14:16-20. Je, shughuli zote hizi zinaheshimika? (Ndiyo. Watu hawa wanaonesha bidii ya kazi.) 

1.  Je, unaona tatizo lolote kwenye visingizio hivyo? (Waalikwa wanatoa kipaumbele kwenye kazi zao dhidi ya kumuunga mkono mtu aliyewaalika chakula.) 

2.  Ninataka tuchungulie Mathayo 22:2-3. Hapa Yesu anazungumzia nini hasa? (Wokovu! Hivyo, moja kwa moja hii inazungumzia suala la “chuki” na kumfuata Yesu.) 

B.  Soma Luka 14:21-22. Kwa nini raia hawa wako tayari kuja? (Wako radhi kuupa mwaliko kipaumbele dhidi ya chochote walichokuwa wanakifanya!) 

1.  Je, umeshangazwa? 

C.  Soma Luka 14:23. Kitu gani kiliwahamasisha watu hawa kuja kwenye karamu? (Walivutiwa!) 

1.  Hawa ni watu wa namna gani? (Ni watu walioko barabarani na maeneo ya pembezoni. Je, hawa ni raia wazalishaji katika jamii ile? Yumkini, Yesu anawazungumzia watu wa Mataifa.) 

D.  Soma Luka 14:24. Unaweza kuelezeaje kwa muhtasari kisa hiki kwa kuzingatia vigezo vya wale waliohudhuria karamu ya mkuu yule? 

E.  Sasa soma vifungu vinavyofuatia: Luka 14:25-26. Hii inaashiria kuwa kuichukia familia na maisha yetu wenyewe inamaanisha nini? (Utaona kwamba wale walioukataa mwaliko walifanya hivyo kwa sababu walitoa upendeleo kwa mwanafamilia au kile ambacho kwa wakati huo kilikuwa na kipaumbele maishani mwao. Yesu anapotumia neno “chuki” hazungumzii juu ya kutokupenda au karaha, anazungumzia juu ya kufanya uchaguzi.) 

F.  Soma Luka 14:27-28. Utaona kwamba bado Yesu alikuwa hajasulubiwa, na wanafunzi wa Yesu hawakuelewa kwamba hilo litatokea. Unadhani walielewaje dhana ya kuuchukua msalaba wako mwenyewe? (Ilikuwa sehemu ya adhabu na fedheha ya mtu ambaye Rumi ilidhani kuwa anapaswa kufa. Baadaye, wanafunzi walielewa hasa kile alichokimaanisha Yesu.) 

1.  Tunapaswa kuelewaje vifungu hivi viwili? (Kabla hatujaamua kuwa Wakristo, tunatakiwa kukubali kwamba itahitajika kujitoa kwa njia ya chaguzi tuzifanyazo maishani na chaguzi hizo zinaweza kumaanisha kwamba tunadhihakiwa kwa kuzichagua chaguzi hizo.) 

III.  Kutembea Katika Njia Sahihi 

A.  Soma Wafilipi 2:1-2. Kujitoa kwa namna gani kunaandikiwa hapa? (Kuendana na kundi la waamini.) 

B.  Soma Wafilipi 2:3. “Kushindana” ni kupi? (Mtoa maoni mmoja anasema ni, “majivuno.” Inamaanisha kusababisha ugomvi ili tu kukuza majivuno yako.) 

1.  Nimehudhuria vikao vingi vya kanisa. Sikumchukulia kila mtu kuwa wa muhimu zaidi yangu kwa sababu nilidhani kuwa baadhi ya watu walikuwa na mawazo ya kipumbavu au yenye ubinafsi. Je, sikuwa sahihi? (“Wanavyopendelea watu wengine,” kimantiki itajumuisha kanisa zima. Kuangalia yale wanayoyapendelea kutahitaji kuyakataa mawazo ya kipumbavu au yaliyojaa ubinafsi.) 

a.  Kwa nini mimi ni hakimu mwenye kustahili? 

C.  Soma Wafilipi 2:4. Je, ni jambo lenye kufaa kuyaangalia mambo yako mwenyewe? (Ndiyo. Lakini, wakati huo huo tunapaswa kuyaangalia mambo ya watu wengine.) 

D.  Soma Wafilipi 2:5-7. Hii inatuambia kwamba Yesu ni mfano wetu. Jiweke kwenye nafasi ya Yesu na uniambie sababu zote unazoweza kuzifikiria kwamba hapaswi kuja duniani ili kukabiliana na kifo kichungu na kinachodhalilisha? 

E.  Soma Wafilipi 2:9-11. Je, lengo la Mungu kwetu ni kwamba tunapaswa kuchagua njia ya kafara? (Kafara (kujitoa) inalinganishwa na kusifiwa. Sio lengo la Mungu kwa sisi kudhuriwa na kudhalilishwa. Lengo lake ni kwamba tuinuliwe.) 

1.  Hivyo basi tunatakiwa kuzingatia nini katika uchaguzi wetu wa kumfuata Mungu ambacho tunapaswa kutarajia kukitoa sadaka? Huu ni “uchunguzi wa uhalisia.” Kuna ugomvi unaoendelea kati ya Yesu na Shetani. Hii ni vita, na wakati wa vita askari hujitoa. Vita sio lengo, vita ni vya muhimu ili kufikia amani na usitawi.)   

F.  Hebu turukie chini na kusoma Wafilipi 2:13-15. Ni nini lililo lengo la karibu la kumtumikia Mungu? (Kwamba tutakuwa mfano wa kile inachomaanisha kumtumikia Mungu.) 

1.  Kama dhana iliyopo ni kwamba tutateseka, kwa nini “mianga” ni njia nzuri ya kutuelezea sisi? (Wengine watayaangalia maisha yetu kama jambo zuri. Watatamani, huenda kwa dhati kabisa, kile tunachokifanya.) 

G.  Rafiki, kuchagua kumfuata Yesu hutupatia matakwa ya kuyatekeleza. Takwa la kwanza na la msingi ni kwamba tumchague Yesu dhidi ya kujichagua wenyewe. Je, uko radhi kufanya hivyo? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu akusaidie ufanye uchaguzi huo na kuusimamia? 

IV.  Juma lijalo: Kristo Ndani ya Tanuru (Kalibu).