Somo la 1: Uasi Ndani ya Ulimwengu Mkamilifu

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Mathayo 13, Ezekieli 28, 1 Yohana 4
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
4
Lesson Number: 
1

Somo la 1: Uasi Ndani ya Ulimwengu Mkamilifu

(Mathayo 13, Ezekieli 28, 1 Yohana 4)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Uovu uliibukaje kwenye ulimwengu mkamilifu ulioumbwa na Mungu? Baadhi ya Wakristo wanasema kuwa wanadamu wasio wakamilifu kamwe hawawezi kumwelewa Mungu mkamilifu ajuaye mambo yote. Hilo ni kweli, lakini baadhi ya maswali yanarejelea kwenye asili ile ile ya uhusiano wetu na Mungu. Je, uovu uliibuka kwa kuwa sehemu ya Mungu ina uovu? Yumkini ulimwengu wetu mkamilifu haukuwa mkamilifu kivile? Wakati Mungu anatuambia katika kitabu cha Mwanzo jinsi uovu ulivyoingia duniani kwetu ikiwa ni matokeo ya uamuzi wa Adamu na Eva, uovu uliuingiaje moyo wa nyoka (Shetani) aliyewajaribu kuukumbatia uovu? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kukiona ambacho kimefunuliwa kwetu na Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo!

I.  Fumbo

A.  Soma Mathayo 13:27. Je, kimsingi hili ndilo swali tulilo nalo kuhusu jinsi uovu ulivyokuja wakati Mungu wetu alipandikiza “mbegu njema?” (Ndiyo.)

B.  Soma Mathayo 13:24-26 ili tuone jibu la Yesu. Yesu anasema kuwa kisa hiki kinatufundisha somo juu ya Ufalme wa Mbinguni. Je, inatufundisha nini juu ya chanzo cha uovu katika hili shamba? (Adui alipanda magugu. Hivyo ndivyo “uovu” ulivyojitokeza kwenye shamba hili lenye mbegu njema. “Mtu” alipanda mbegu njema.)

1.  Kwa kawaida hii inaibua maswali gani? (Adui huyu ni nani, ametokea wapi, na ana sababu gani za kujaribu kuharibu shamba la ngano?)

2.  Tunapokitumia kisa hiki kwa wanadamu lipo tatizo moja, “mbegu njema” ndio iliyotenda dhambi. Shetani hakuwapeleka watu wabaya katika bustani ya Edeni. Unalielezeaje hili?

II.  Chanzo cha Uovu

A.  Soma Ezekiel 28:12. Tunajifunza nini juu ya asili ya “Mfalme wa Tiro?” (Alikuwa “muhuri” wa kipimo na “ukamilifu wa uzuri.” Muhuri unatukumbusha “muhuri wa pete” unaotumika kusaini nyaraka. Hivyo, hii inamaanisha kwamba mtu huyu ana muhuri wa ukamilifu.)

B.  Soma Ezekieli 28:13. Hebu subiri kidogo! Watu wangapi walikuwa Edeni, kwa mujibu wa kitabu cha Mwanzo? (Tunaambiwa juu ya Adamu na Eva, na hakuna mtu mwingine anayeelezewa kuwepo isipokuwa Mungu na nyoka aliyemjaribu Eva.)

1.  Kwa kutumia kutaratibu wa uondoshaji, Mfalme wa Tiro ni nani? (Lazima atakuwa nyoka.)

C.  Soma Mwanzo 3:1 na Ufunuo 12:9. Hebu tulitafakari hili kidogo. Kimsingi Shetani sio nyoka. Bali alikuwa nguvu iliyokuwa nyuma ya nyoka (au alichukua umbo la nyoka). Je, unaweza kuona mfanano na Mfalme wa Tiro – kwamba Shetani ndio nguvu iliyo nyuma ya Mfalme au alichukua umbo la Mfalme? (Nadhani lazima iko hivyo kwa sababu nina uhakika Edeni haikuwa na mfalme, tofauti na Mungu, na hatokei Tiro!)

D.  Soma Ezekieli 28:14. Mfalme huyu yupo wapi kwingine? (“Juu ya mlima mtakatifu wa Mungu.”)

1.  Ni wapi huko? (Soma Isaya 14:12-14. Hii ni rejea ya mbinguni. Huyu mtu yupo!)

E.  Soma Ezekieli 28:15. Utaona hii inasema kuwa Shetani aliumbwa na kwamba katika kipindi fulani “uovu ulionekana ndani yake.”

1.  Je, hii inafafanua jinsi ambavyo mwanadamu aliyeumbwa kwa ukamilifu angeweza kuwa na uovu ghafla? (Hapana.)

F.  Soma Ezekieli 28:17-18. Kitu gani kinaonekana kuwa na kasoro ndani ya Shetani? (Majivuno kutokana na uzuri wake.)

1.  Unadhani kauli ya “uovu wa uchuuzi wako “uliopatia unajisi patakatifu pako” inamaanisha nini?

2.  Soma tena Isaya 14:12-14 na usome Ayubu 1:6-9. Rejea hizi mbili zinaashiria kuwa asili ya uhusiano kati ya Mungu na Shetani ikoje? (Ni washindani kwa maana ya kwamba Shetani anataka kuwa Mungu. Hii inaendana na majisifu ya Shetani.)

3.  Je, kuwa mkamilifu na mzuri inaweza kuwa kasoro??

4.  Yatafakari maisha yako. Ikiwa dhambi ya asili ni kiburi (kutokana na uzuri), kwa nini Shetani aamini kwamba anapaswa kuchukua nafasi ya Mungu?

a.  Je, majivuno yote hayana mantiki?

G.  Ninataka kuingia kwa kina kwenye suala la majisifu, uzuri, na thamani. Soma tena Ezekieli 28:13. Kito hiki kilitengenezwa lini kwa ajili ya Shetani? (“Katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari.”)

1.  Nani aliyeandaa kito hiki kwa ajili ya Shetani? (Lazima itakuwa ni Mungu. Kwa dhahiri, itakuwa kiliandaliwa kwa maelekezo yake.)

2.  Je, kito hiki ni sehemu ya suala la majisifu ya uzuri? (Hicho ndicho kinachoashiriwa kwenye kifungu hiki.)

3.  Unajifunza nini kutokana na hili? (Uzuri, mawe ya thamani, dhahabu (kama vile fedha) havina ubaya wowote. Kinyume chake ndio ukweli, ni vitu vizuri sana. Tatizo linakuja pale mwanadamu anapofanya kile alichokifanya Shetani – kuanza kuamini kuwa vinakufanya kuwa mtu wa muhimu kuliko wengine. Kwa upande wa Shetani, alidhani kuwa vilimfanya kuwa wa muhimu zaidi kuliko Mungu. Hii ni asili ya majivuno isiyo na mantiki.)

H.  Soma Ufunuo 12:4. Ni nini matokeo ya ushindani baina ya Shetani na Mungu? (Kwamba theluthi ya malaika walimuunga mkono Shetani katika changamoto aliyompa Mungu.)

1.  Hilo liliwezekanaje? (Tunafahamu kwamba pale Edeni Adamu na Eva walikuwa na uhuru wa kuchagua. Hii inaonesha kwamba mbinguni, malaika walikuwa na uhuru wa kuchagua.)

I.  Chukulia kwamba tumeziangalia kweli zote muhimu katika Biblia kuhusu asili ya dhambi. Unahitimisha kwamba “kasoro” ni ipi kwenye uumbaji mkamilifu ulioruhusu dhambi kuingia? (Kiburi/majivuno ni tatizo linaloendana na uhuru wa kuchagua. Shetani alichagua kutoa changamoto kwenye enzi ya Mungu. Malaika walichagua kumkataa Mungu. Tuliona jambo hilo hilo kwa Adamu na Eva katika bustani ya Edeni.)

1.  Je, uhuru wa kuchagua una kasoro? Je, ungependa kuishi miongoni mwa watu wasio na uhuru wa kuchagua juu ya endapo wanataka kuwa marafiki wako?

J.  Soma 1 Yohana 4:7. Jibu swali la msingi kabisa, je, upendo wa kweli unahitaji uhuru wa kuchagua? Je, kweli ungejisikia kupendwa kama mwenzi wako na watoto wako hawakuwa na uchaguzi katika suala hilo?

III.  Mtazamo wa Mungu

A.  Tumeangalia suala la “kasoro.” Upendo huhitaji uhuru wa kuchagua na uhuru wa kuchagua ulioambatana na majivuno yasiyo na mantiki hufungua mlango wa kuingia dhambini. Je, una hisia mseto juu ya hitaji la kuwa na uhuru wa uchaguzi kamili? 

1.  Kuna vuguvugu lenye nguvu miongoni mwa vijana wadogo leo kwamba watu hawapaswi kuwa na uhuru wa kuchagua – kwa mfano asiwepo mtu wa kuchagua kutekeleza chuki. Je, unakubaliana na hili?

2.  Tatizo moja ni kufasili (defining) “chuki.”  Miongoni mwa vijana wengi wadogo, “chuki” ni jambo lolote wasilolipenda. Biblia, kwa mfano, ni chanzo cha “chuki” kwa sababu inatangaza kwamba chaguzi fulani-fulani ni dhambi na hujielekeza kwenye mauti. Je, ukomo wowote katika dhana ya uhuru wa kuchagua huwasilisha matatizo ya mapenzi?

B.  Soma 1 Yohana 4:9. Jiweke kwenye nafasi ya Mungu. Unajua kwamba kuonesha upendo kamili, upendo unaohitaji uhuru wa uchaguzi mkamilifu, inamaanisha kwamba Mwanao atapitia fedheha, mateso makali, na kifo. Je, ungeachana na uhuru wa kuchagua kama hiyo ndio ingekuwa thamani yake? (Akili zetu haziwezi kufumbata akili ya Mungu, lakini tunaweza kuziangalia chaguzi alizozifanya na kufikia hitimisho kutokana na chaguzi hizo. Hitimisho la dhahiri ni kwamba kama Mungu angekuwa na njia nyingine na kuonesha upendo kamili, basi angeichagua njia hiyo.)

C.  Soma Mathayo 26:39. Je, Mungu Baba alikuwa analisikiliza ombi la Yesu?

1.  Jibu kwa ombi la Yesu ni lipi? (Hapakuwepo na njia nyingine. Sasa tuna uhakika kuwa uamuzi uliochukuliwa na Mungu ulikuwa kama vile tulivyoujadili. Hakuwa na njia nyingine ya kuonesha upendo kamili na uhuru wa kuchagua.)

2.  Litafakari hili kwa kuzingatia uamuzi muhimu unaoufanya katika maisha yako. Je, kuwapa wanadamu uhuru wa kuchagua ni jambo la muhimu kiasi gani linapokuja suala la uhusiano wao na Mungu?

3.  Je, ni muhimu kiasi gani maishani mwako kutenganisha uzuri na majivuno?

D.  Rafiki, uovu unapoingia maishani mwako na ukajaribiwa kumlaumu Mungu, fikiria kile tulichotoka kujifunza. Mungu ana upendo mkubwa kwetu kiasi kwamba alikuwa radhi kufa ili tufanye uchaguzi wa kumkataa. Je, utaitikia upendo wa Mungu kwa kumchagua yeye?

IV.  Juma lijalo: Mauti Katika Ulimwengu wa Dhambi.