Somo la 4: Tumaini la Agano la Kale

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Zaburi 49 & 71, Isaya 26, Danieli 12
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
4
Lesson Number: 
4

Somo la 4: Tumaini la Agano la Kale

(Zaburi 49 & 71, Isaya 26, Danieli 12)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kwa nini umesalia kuwa Mkristo? Nilipotafakari kuachana na Ukristo kilichonizuia ilikuwa ni fikra za kuishi maisha bila Mungu. Jambo la msingi maishani mwangu ni kutambua kwamba Mungu yu pamoja nami katika kila changamoto. Paulo anasema katika 1 Wakorintho 15:19 “Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote.” Sikubaliani na hili. Hata bila maisha baada ya haya ya hapa duniani, nimebarikiwa kupita kiasi katika maisha haya kwa ushirika [urafiki] wangu na Mungu. Tambua kwamba nimeyachukulia maneno ya Paulo nje ya muktadha. Muktadha wake ni kwamba tumetekwa na uongo ikiwa mbingu sio halisi. Kimuktadha, kauli ya Paulo inaendana na shukrani kwa uwepo wa Mungu. Yesu ni halisi. Ufufuo wake ni halisia. Ushirika/urafiki wake nasi ni halisia na utaendelea milele endapo tutachagua iwe hivyo. Yesu ndiye kiini cha hoja ya Paulo kuhusu maisha baada ya haya. Watu wa Mungu waliamini nini kabla Yesu hajaja? Je, waliamini katika ushirika/urafiki wa kudumu na Mungu? Hebu tuligeukie hilo juma hili katika mwendelezo wa somo letu la Biblia!

I.  Mjadala wa Ayubu

A.  Unakifahamu kisa cha Ayubu. Mungu anajivuna kwamba Ayubu ni mfuasi mkamilifu, na Shetani anajibu kuwa Ayubu anamfuata Mungu kutokana na kile anachoweza kukipata. Jambo hilo linajaribiwa kwa kumchukulia Ayubu kila kitu isipokuwa mkewe. Soma AYubu 2:9. Chukulia kwamba mke wa Ayubu anampenda mumewe na anamuwazia mambo mema. Kwa nini apendekeze jambo hili? (Linahitimisha mateso ya Ayubu. Hayatafakari maisha baada ya haya ya hapa duniani.)

B.  Soma Ayubu 2:10. Ayubu anatoa hoja gani kwa mkewe? Je, inahusisha maisha baada ya haya ya hapa duniani? (Ni kauli inayohusu haki hapa duniani. Ayubu haibui suala la maisha baada ya haya ya hapa duniani.)

C.  Soma Ayubu 19:25-27. Ayubu anamaanisha nini kwa kusema, “na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi?” (Lazima atakuwa anarejelea kipindi cha baada ya kifo chake.)

1.  Ayubu atamwonaje Mungu baada ya kufa kwake? (Kauli ya Ayubu inaonesha kuwa anaamini katika maisha baada ya haya ya hapa duniani. Hii inampa mantiki ya kuendelea kuvumilia licha ya kupoteza kwake mali kiasi cha kutisha na mateso binafsi.)

II.  Ujasiri wa Kipumbavu

A.  Soma Zaburi 49:5-6. Mtunga Zaburi anaandika juu ya hofu. Kwa nini haogopi? Kuna tofauti gani juu ya chanzo chake cha ujasiri? (Hitimisho ni kwamba mtunga Zaburi anamwamini Mungu wakati wengine wanaweka imani zao kwenye mali zao.)

B.  Soma Zaburi 49:7-9. Ni nini tatizo la kuitegemea mali ili kuepuka “shimo?” (Shimo ni kifo, na wenye mali sio matajiri kiasi cha “kukomboana.”)

C.  Soma Zaburi 49:10-12. Ukiandika jina lako kwenye jengo, je, utakumbukwa daima? (Kifungu kinasema kuwa hata katika hilo utafanana na wanyama wanaokufa – hata “fahari yako haitasalia.” Shule ya bweni katika eneo letu ilikuwa na bweni lililopewa jina la mtu ambaye ninaamini alitoa fedha ili kujenga bweni hilo. (Mjane wake alikuwa mshiriki wa kanisa langu nilipokuwa mdogo.) Nilipokuwa mtu mzima, kuna mtu ambaye alitoa fedha ili kulifanyia ukarabati bweni hilo na shule ikalipa jina jipya bweni hilo na kulipa jina la mtu aliyechangia ukarabati!)

D.  Soma Zaburi 49:14-15. Unadhani hii “asubuhi” ni kitu gani? (Hii ni rejea ya Ujio wa Yesu Mara ya Pili. Kifungu kinasema kuwa wenye haki na wasio haki watafufuliwa “asubuhu,” lakini baadaye wasio haki “watachukuliwa kuzimu.” Kwa nini? Kwa sababu hakuna nafasi kwa ajili yao, lakini mtunga Zaburi atapokelewa na Mungu kutegemeana na kikombozi!)

E.  Utaona kwamba mjadala huu kuhusu maisha baada ya haya unaanza kwa mjadala wa uaminifu kwa urafiki na Mungu katika kipindi cha uhai.

III.  Ujasiri wa Busara

A.  Soma Zaburi 71:1-4. Mtunga Zaburi (Mfalme Daudi) anamtumaini nani katika nyakati za dhiki? (Mungu. Daudi anasema kuwa Mungu ndiye “mwamba wa makazi yangu.”)

1.  Unadhani Daudi angesema nini juu ya maisha yasiyo ya kumtegemea Mungu?

B.  Soma Zaburi 71:9-11. Ni wakati gani Daudi anasema kuwa msaada wa Mungu ni wa muhimu sana kwake? (Atakapokuwa mzee, wakati “nguvu zake zitakapopungua.”)

C.  Soma Zaburi 71:20-21. “Pande za chini ya nchi” ni kitu gani? (Kifo. Kaburi.)

1.  Kadiri Daudi anapozidi kukua kutoka ujanani akimtegemea Mungu, hadi kuwa mtu mzima akihitaji msaada wa Mungu kwa udi na uvumba, hadi kwa yule aliyezikwa, Mungu anafanya wajibu gani? (Mungu anamhuisha (anamwamsha), anamwokoa, na anamliwaza Daudi.)

2.  Je, Mfalme Daudi aliamini katika mbingu? (Ndiyo.)

a.  Imani hiyo ilijengwa juu ya nini? (Mwendelezo wa urafiki wake na Mungu. Uhusiano huu unakiepuka kifo.)

IV.  Amani Kamilifu

A.  Soma Isaya 26:1-3. Tukimtumaini Mungu wakati wa maisha yetu ya hapa duniani, matokeo yake ni nini? (Amani kamilifu.)

1.  Je, kifungu hiki kinaashiria kuwa kwa mtu anayemtumaini Mungu mambo yote yatakuwa shwari? (Kinyume chake ndio ukweli wenyewe. Zingatia nukuu ya “kuta na maboma,” “malango,” na “mji ulio na nguvu.” Haya yote yasingekuwepo kama isingekuwepo hatari ya kweli maeneo ya nje.)

B.  Soma Isaya 26:10-11. Ni kwa njia gani tofauti wenye haki na wasio haki wanaziangalia baraka na fadhila za Mungu? (Wasio haki hawajifunzi lolote kutokana na hilo. Hawamwoni Mungu katika baraka zao, wanadhani udanganyifu wao ndio unaowanufaisha.)

C.  Soma Isaya 26:18. Je, wenye haki watawashinda wasio haki tunapoishi pamoja hapa duniani? (Hatuwezi kuwashinda au kusababisha uovu wa dunia kupotea kwa kuzitegemea juhudi zetu pekee.)

D.  Soma Isaya 26:19 na Isaya 26:21. Jambo gani ni la muhimu ili uovu uweze kukomeshwa? (Mungu atakuja na kuwashinda waovu, lakini wenye haki “wakaao duniani” wataishi!)

1.  Hii inazungumzia nini juu ya maisha baada ya haya ya hapa duniani?

E.  Soma Isaya 26:20. Kwa wakati huu tunapaswa kufanya nini? (Tunapokabiliana na ghadhabu halisi tunapaswa kujificha hadi ghadhabu inapopita.)

1.  Kweli? Je, tunapaswa kujificha? Vipi kuhusu Isaya 26:1-3 inayozungumzia amani kamilifu kwa wale wanaozitumaini “kuta na maboma?” (Yumkini muda unakuja ambapo tutahitajika kujificha “kwa muda,” lakini ninadhani maelekezo ya jumla ni kujificha ndani ya nguvu za Mungu.)

V.  Maelezo ya Danieli

A.  Soma Danieli 12:1. Je, wenye haki watakabiliana na taabu katika nyakati za mwisho? (Matatizo yatakuwepo kuliko ilivyowahi kushuhudiwa. Lakini wenye haki “wataokolewa.”)

B.  Soma Danieli 12:2. Hii inazungumzia nini juu ya maisha baada ya haya ya hapa duniani? (Inatabiri ufufuo wa jumla kwa wema na wabaya. Wenye haki watafufuliwa na kuingia kwenye “uzima wa milele.” Hatutaingia kwa kina kwenye yale yaliyobainishwa kwenye vifungu kama vile vya 1 Wathesalonike 4:16 au Ufunuo 20:4-15. Kwa wakati huu tunajadili mtazamo wa Agano la Kale juu ya maisha baada ya haya ya hapa duniani.)

C.  Soma Danieli 12:3. Tunaona mustakabali gani kwa “walio na hekima” na “hao waongozao wengi kutenda haki?” (Watang’aa kama nyota milele na milele.)

1.  Angalia asili ya analojia. Milima sio inayolinganishwa, bali nyota. Kwa nini? (Hii inaongezea kwenye dhana ya kwamba maisha yetu baada ya hapa duniani yako mbinguni.)

D.  Soma Danieli 12:4. Hii inawaambia nini wasomaji wa Agano la Kale? (Kwamba “kitabu” cha Danieli hakiwezi kueleweka kikamilifu hadi mwisho wa wakati.)

1.  Jambo gani lilikuwa ndilo uelewa wa kipindi hicho? (Danieli anaelezea kwa uwazi kabisa kwamba hukumu itatolewa kwa watu na kuna maisha baada ya haya. Wale wanaofaulu watasajiliwa kwenye maisha baada ya haya “yanayofanana na nyota.”)

VI.  Nadharia Iliyojaribiwa

A.  Soma Yohana 11:23-26. Martha aliyaelewaje mafundisho ya Agano la Kale na mjadala wake na Yesu? (Palikuwepo na ufufuo wa nyakati za mwisho.)

1.  Kama hili lisingekuwa kweli, je, Yesu alipaswa kumsahihisha? (Badala ya kumrekebisha Martha, Yesu anasema kuwa yeye ndiye “huo ufufuo na uzima.” Hapo awali Yesu alikuwa amemwambia Martha (Yohana 11:23) kwamba ndugu yake “atafufuka.”)

2.  Utaona kwamba Yesu pia anasema kuwa anayemwamini “kamwe hatakufa.” Tunapaswa kulielewaje hili kutokana na ukweli kwamba Lazaro alikuwa amekufa? (Lazima Yesu atakuwa anatuahidi kuwa kamwe hatutakufa milele kama tukimchagua.)

B.  Rafiki, katika maandiko ya Agano la Kale Mungu ametoa ahadi za wazi kabisa kwa wale wanaomchagua. Ataendeleza ushirika/urafiki wake kwao katika uzima wa milele. Je, utamchagua Mungu sasa hivi, kama bado hujafanya hivyo?

VII.  Juma lijalo: Ufufuo Kabla ya Msalaba.