Somo la 5: Ufufuo Kabla ya Msalaba
Somo la 5: Ufufuo Kabla ya Msalaba
(Yuda 9, Zakaria 3, 1 Wafalme 17, 2 Wafalme 4, Marko 5, Yohana 11)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Biblia imeandika juu ya manabii wa Agano la Kale waliowafufua wafu. Agano Jipya linatuambia kuwa Yesu aliwafufua wafu, na kwamba Petro na Paulo pia walifanya hivyo. Ufufuo huu una lengo gani? Inaonekana kuwa wale waliofufuliwa baadaye walikufa. Kwa nini? Kwa upande mwingine, tunaye Musa ambaye alifufuliwa baada ya kufa, na alionekana kutokufa kwa sababu anaonekana tena miaka elfu moja baadaye. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza juu ya miujiza hii isiyo ya kawaida!
I. Agano la Kale: Musa
A. Soma Yuda 9. Ufufuo wa Musa unazungukwa na ushindani na mabishano na Shetani. Je, huu ndio ufufuo wa kwanza unaoandikwa katika Biblia? (Ndiyo. Tukichukulia kwamba kipindi hiki ni karibu kabisa na wakati wa kifo cha Musa, ufufuo mwingine wa Agano la Kale unatokea baadaye sana.)
1. Unadhani asili ya ugomvi huu ni nini? (Kwa kuwa huu ni ufufuo wa kwanza, uwezekano mkubwa ni kwamba mabishano haya yanahusu mamlaka ya Mungu kumfufua Musa.)
B. Soma Waebrania 2:14. Biblia inasema kuwa nani alikuwa na “nguvu za mauti” katika kipindi hicho? (Shetani! Tunaweza kukisia kwa usahihi kabisa kile ambacho Shetani alikuwa anakisema: “Musa alikuwa mdhambi. Alikufa. Nina mamlaka juu ya kifo na wewe (Mungu) huna mamlaka ya kutotii uwezo wangu na kumfufua Musa.”)
C. Angalia tena Yuda 9. Inamaanisha nini kusema kuwa Mikaeli “hakuthubutu kumshitaki kwa kumlaumu?” (Kufuru inaeleweka kuwa ni kumtukana Mungu. Inawezekana Shetani anadai kuwa yeye ni “mungu” wa dunia. Mikaeli haingii kwenye mjadala huu, bali anamkemea tu Shetani.)
D. Hebu tuangalie mazingira yanayofanana. Soma Zekaria 3:1-2. Hiki ni kisa kingine katika Agano la Kale ambapo Shetani anamshutumu kiongozi wa dini. Mungu anajibuje shutuma za Shetani? (Kama ilivyokuwa kwa Musa, anamkemea lakini hajadiliani naye.)
E. Soma Zekaria 3:3-5. Kuna suala gani hapa? (Hali ya dhambi ya Kuhani Mkuu.)
1. Mungu anatibuje tatizo la dhambi ya Yoshua? (Soma Isaya 61:10. Yoshua anapewa vazi la haki. Hii ni haki kwa imani pekee.)
2. Uwezo wa Yoshua kuvishwa vazi la haki unategemea jambo gani? (Ushindi wa Yesu msalabani.)
3. Kuna uhusiano gani kati ya mjadala juu ya Musa na Yoshua? (Uwezo wa Mungu kutenda mambo haya unageukia kwa Yesu katika siku zijazo. Sidhani kama Mungu alitaka kujiingiza kwenye mjadala kwa kina katika kipindi hicho, hivyo anamkemea tu Shetani.)
F. Unadhani kwa nini Mungu alimfufua Musa?
II. Agano la Kale: Mwana wa Mjane wa Sarepta
A. Soma 1 Wafalme 17:17-18. Sehemu ya kwanza ya sura hii inaelezea jinsi Mungu alivyoyaokoa maisha ya Eliya, mjane huyu, na mwanaye kwa kutenda kazi kupitia kwa Eliya kuwapatia wote mafuta na unga katika kipindi cha baa la njaa. Kwa kuyazingatia hayo, kwa nini mjane huyu azungumze na Eliya kwa ukali kiasi hiki? Kwa nini amshutumu mtu aliyemwokoa mwanaye kisha amuue baadaye? (Anaamini kuwa Mungu alitenda kazi kupitia kwa Eliya, na kama mwanaye amefariki basi lazima Eliya ana mkono wake katika hilo.)
1. Soma 1 Wafalme 17:19-22. Eliya aliamini kuwa sababu ya kifo cha kijana huyu ni ipi? (Yeye pia anaamini kuwa Mungu alisababisha kifo hiki.)
B. Unadhani kwa nini Mungu alimfufua kijana huyu? (1 Wafalme 17:22 inasema kuwa Mungu alimsikiliza Eliya. Inaonekana kuwa Mungu anaithibitisha sifa yake njema.)
C. Soma Kumbukumbu la Torati 32:50-51. Kwa nini Musa alikufa? (Alikufa ikiwa ni matokeo ya adhabu ya Mungu.)
D. Je, unaona uhusiano kati ya kifo cha Musa na kile cha mwana wa Mjane wa Sarepta? (Wote wanaonekana kufa mkononi mwa Mungu.)
III. Agano la Kale: Mwana wa Mshunami
A. Soma 2 Wafalme 4:28 na 2 Wafalme 4:32-35. Ukisoma sura hii, utaona kwamba wazazi wa kijana huyu walijenga mahali kwa ajili ya Elisha kuishi alipokuwa katika eneo hili. Kama sehemu ya shukurani, Elisha anawauliza wangependa awatendee nini. Walichokitaka ni kupata mtoto wa kiume, na Elisha aliahidi kuwa watampata (2 Wafalme 4:16). Kwa nini Mungu alitenda muujiza huu?
B. Linganisha 2 Wafalme 4:16 na 2 Wafalme 4:28. Shutuma gani ilitolewa dhidi ya Elisha na Mungu? (Wamemdanganya mama huyu. Walimwambia kuwa atapata mwana, na sasa Mungu amevunja ahadi hii kwa kuruhusu kijana huyu kufariki.)
C. Unadhani kwa nini Mungu alimfufua mwana huyu? (Kwa mara nyingine, Mungu analithibitisha jina lake.)
IV. Agano Jipya: Binti wa Yairo
A. Soma Marko 5:22-24. Kama ungekuwa Yairo, ungekuwa na matarajio gani juu ya Yesu kumponya binti yako?
B. Katika mkusanyiko huu kuna huyu mwanamke ambaye amekuwa mgonjwa kwa miaka kumi na miwili. Amejaribu aina mbalimbali za matibabu, lakini ugonjwa wake sugu unazidi kuwa mbaya. Soma Marko 5:27-29. Lengo la mwanamke huyu ni lipi? (Kumgusa mwanamke huyu na kuponywa.)
C. Soma Marko 5:30-32. Je, lengo la mwanamke huyu linakinzana na lengo la Yairo? (Ndiyo. Wanafunzi wanadhani kuwa Yesu anakuwa mpuuzi, na Yairo anatafakari juu ya kupiga kelele kwa kukatishwa tamaa huku kutokana na kuingiliwa kwa ombi lake.)
D. Soma Marko 5:34-35. Yairo anafikiria nini? (Yesu hatumii akili ya kawaida (mantiki). Hazingatii masuala ya dharura. Yesu hatendi kile ambacho Yairo anaamini kuwa Yesu alikubali kukitenda.)
E. Soma Marko 5:41-42. Kwa nini Yesu alitenda ufufuo huu? (Sababu mojawapo ni kuthibitisha sifa yake kwa Yairo.)
V. Agano Jipya: Lazaro
A. Soma Yohana 11:1-3. Ni nini matarajio ya Mariamu na Martha? (Yesu atamponya Lazaro kwa sababu anampenda.)
B. Soma Luka 10:38-39. Kwa nini Yesu anampenda Lazaro? (Walitoa mahali kwa ajili ya Yesu na wanafunzi wake kukaa. Hii inatukumbusha juu ya visa vyetu vya hifadhi kwa Eliya na Elisha.)
C. Soma Yohana 11:20-21 na Yohana 11:32. Dada wote wawili wanatoa shutuma gani dhidi ya Yesu? (Matokeo ya kuchelewa kwake ni kufariki kwa Lazaro.)
1. Hii inakukumbusha juu ya jambo gani? (Inatukumbusha juu ya mashtaka dhidi ya Mungu yaliyotolewa na Eliya na Elisha.)
D. Unadhani kwa nini Yesu alimfufua Lazaro? (Kwa mara nyingine Mungu anathibitisha sifa yake.)
1. Hebu tuangalie kwa kina zaidi. Soma Yohana 11:40-42. Kwa nini Yesu anasema kuwa anataka kumfufua Lazaro? (Ili watu “wapate kusadiki kwamba [Mungu Baba] ndiye aliyenituma.”)
2. Soma Yohana 11:4. Yesu anatoa sababu gani kwa wanafunzi wake? (Humpa Mungu na Yesu utukufu.)
VI. Kwa Nini
A. Katika kila ufufuo tulioujadili, isipokuwa ule wa Musa na Yairo, kwa mahsusi sifa ya Mungu ilikuwa chini ya shambulio. Yatafakari maisha na kifo cha Musa na Yairo. Je, sifa ya Mungu ilikuwa hatarini pale? (Musa alikuwa mtu wa Mungu wa kuwatoa watu wake Misri kuwapeleka katika Nchi ya Ahadi. Mungu alipomuadhibu Musa kwa kumnyima Nchi ya Ahadi na kumpeleka katika kifo chake, hii pia inaweza kuharibu sifa ya Mungu. Shetani anaweza kujenga hoja kwamba Mungu hakutenda haki kwa jinsi alivyomtendea kiongozi huyu.)
B. Soma 1 Wakorintho 15:22 na 1 Wakorintho 15:24-26. Je, ufufuo wako utakuwa ni uthibitisho wa kile kilichotokea Edeni? Je, ufufuo wako, pamoja na mambo mengine, utakuwa uthibitisho wa sifa ya Mungu?
C. Kwa nini ni baadhi tu ndio wanafufuliwa kwenye uzima wa milele? (Ukichukuliwa mbinguni, basi unakuwa na uwezo wa kuufikia Mti wa Uzima na hivyo uzima wa milele. Ufunuo 22:2.)
D. Rafiki, Mungu ndiye mwanzilishi wa maisha. Kwa asili Mungu alitupatia uhai, na endapo tutamchagua, atatupatia uhai tena. Je, utamchagua? Je, utasaidia katika kumpa Mungu utukufu?
VII. Juma lijalo: Alikufa kwa Ajili Yetu.