Somo la 14: Mambo Yote Mapya
Somo la 14: Mambo Yote Mapya
(Ufunuo 21 & 22, Isaya 25)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, unakumbuka kipindi ulipokuwa unakua na kuwakumbuka wazazi wa marafiki wako? Nilikuwa na uhusiano mzuri na wazazi wa marafiki wangu wa karibu. Siku chache zilizopita mzazi wa mwisho wa kundi hilo alifariki. Kwa kawaida, kwa kadiri unavyozidi kuwa mzee ndivyo msiba wako unavyozidi kuwa mdogo kwa sababu unakuwa umeishi zaidi ya marafiki wako. Lakini hii haikuwa hivyo kwa huyu “mzazi wa mwisho.” Ingawa alikuwa katika umri wa miaka ya 90, mamia ya watu walihudhuria kwenye msiba wake. Kwa nini? Aliendelea hadi mwisho kuhudumia mahitaji ya wengine. Kifo chake kingekuwa cha kusikitisha sana kwa familia yake na jamii yake endapo isingekuwa kwa jambo moja – wale waliokuwepo kwenye msiba wake waliamini kuwa muda mfupi ujao wataungana naye mbinguni. Tofauti na kuungana na marafiki wake na familia yake, mbingu itafananaje? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!
I. Eneo Zuri la Jirani (A Better Neighborhood)
A. Soma Ufunuo 21:1-2. Tunapozungumzia juu ya “kwenda mbinguni,” tutaishia kuishi wapi? (Kwenye somo letu la mwisho (angalia Ufunuo 20:4) tuliona kwamba watakatifu watakwenda mbinguni na kukaa kwa miaka elfu. Baada ya hapo tutarejea na Yerusalemu Mpya katika “nchi mpya.”)
1. Utahitimisha nini kimantiki kutokana na kauli ya kwamba tutakaa katika “nchi” mpya na “wala hapana bahari tena?” (Kikubwa kinachomaanishwa hapa ni kwamba jiografia ya nchi mpya inafanana na nchi ya zamani, isipokuwa tu hakuna bahari. Kama usawa wa kijiografia usingekuwa wa kweli, kwa nini Biblia inabainisha kutokuwepo kwa bahari?)
a. Je, hiyo inamaanisha kuwa unaweza kuishi eneo lile lile kama unaloishi sasa? Je, unadhani kuwa marafiki wako waliookolewa wanaweza pia kuchagua kuishi mahali hapo?
b. Vipi kama mababu wako waliishi mahali hapo hapo?
B. Soma Ufunuo 21:3. Nani atakayekaa nasi katika nchi itakayofanywa upya? (Mungu!)
1. Kwa nini? Kwa nini Mungu atoke mbinguni? Kwa nini, kati ya sayari zote, Mungu aamue kukaa pamoja nasi? (Nadhani hii inasherehekea kushindwa kwa dhambi. Ni kumbukumbu ya sayari yetu kuwa eneo la vita, na Mungu wetu kuwa mshindi.)
II. Mazingira Mazuri
A. Huenda baadhi yenu mnajiuliza “Je, ninataka kuishi eneo nililokuwa ninaishi zamani? Kamwe sikuwapenda watu wa mahala pale.” Soma Ufunuo 21:4. Ni nini utakaokuwa mtazamo wa wale wanaotuzunguka? (Hapatakuwepo maumivu. Hapatakuwepo maombolezo. Hapatakuwepo kilio. Mambo yote hasi maishani yatatoweka. Ukizitafakari nyakati njema ulizozipitia wakati ukikua, hivyo ndivyo mustakabali wako utakavyokuwa.)
B. Soma Isaya 25:6. Je, utakuwa na vyakula vizuri mbinguni?
1. Je, tutakuwa na haja ya kuchunga uzito wetu na kuzingatia kalori tunazokula? (Kifungu hiki kinatuambia kuwa tunakula vyakula “vinono!”)
C. Soma Isaya 25:7. Unadhani hii inamaanisha nini?
1. Tutavaa taji lini? (Tutakapokuwa tunaomboleza au pale tusipotaka watu watutambue. Mantiki iliyopo ni kwamba mambo hasi maishani yametoweka.)
D. Soma Isaya 25:8. Je, kuna watu wanakudhihaki kwa sababu wewe ni Mkristo? Je, ungependa kuishi kwenye jamii ambapo kila mtu anafikiria mambo mema juu yako? Kuna mtazamo gani mbinguni? (Kifungu hiki kinatuambia kuwa kila “shutumu” tuliloteseka kutokana na utiifu wetu kwa Mungu limetoweka.)
E. Soma Ufunuo 21:8. Kitu gani kingine hakitakuwepo katika eneo ulilokuwa ukiishi zamani? (Wale ambao wangeweza kutudhuru.)
1. Kwa muda mrefu nimevutiwa sana na ukweli kwamba jambo la kwanza kwenye orodha ya mambo ambayo hayatakuwepo ni “waoga.” Jambo linalofuatia ni “wasioamini.” Hawa wanaorodheshwa kabla ya “wachukizao” na “wauaji.” Kwa nini? Kwa nini uoga na kutokuamini ni tatizo kubwa?
F. Soma Isaya 25:9. Ni nini mtazamo wa wale waliookolewa? (Wanaamini na kusubiri. Tafsiri ya Biblia ya NIV inasema kuwa “walitumaini.” Hawa sio watu waoga au wasio na imani. Wanamwamini Yesu na kwamba anakuja kuwaokoa.)
1. Je, unafurahia kuwa na watu wanaojiamini?
III. Miji (Nyumba) Mizuri
A. Soma Ufunuo 21:10-11. Je, Yerusalemu Mpya unashuka kutoka mbinguni ukiwa bado haujapangiliwa na kutua katika nchi mpya? (Hicho ndicho Biblia inachokisema.)
1. Ni nini unachokiwazia kwanza juu ya hilo? (Inaonekana kama kito. Baadhi ya magari yamepakwa rangi nzuri kuliko mengine. Sehemu ya nje ya Yerusalemu Mpya “inang’aa” kama “kito” hadimu kabisa. Ninayataja magari kwa sababu nina ufahamu mdogo wa vito vya thamani.)
B. Soma Ufunuo 21:12 na Ufunuo 21:15-17. Umbo la Yerusalemu Mpya likoje? Je, unaonekana kama mji wa kawaida? (Una umbo la mchemraba lenye urefu wa maili 1,380 au kilomita 2220 kila upande. Ni milki kubwa!)
C. Soma Yohana 14:2-3. Tafsiri ya Biblia ya ESV inasema kuwa “nyumbani mwa Baba” yangu “mna vyumba” vingi. Tafsiri ya KJV inasema “nyumbani mwa Baba” yangu mna “makao” mengi. Je, una wasiwasi wa kushushwa hadhi kutoka kwenye makao hadi kwenye chumba? (Haileti mantiki yoyote kwa “nyumba” kuwa na “makao.” Watafsiri wa Biblia ya KJV walikuwa wanapamba mambo ili kuyafanya makao yako ya mbinguni yaonekane mazuri. Juhudi zao zilizopotoka zilitokana, kwa sehemu fulani, na kutokuwa kwao na dhana ya majumba ya kisasa.)
D. Soma Ufunuo 21:18-21. Hili litakuwa jumba la namna gani? (Zuri sana!)
E. Soma Luka 13:29. Hii inatuambia nini juu ya aina ya Yerusalemu Mpya? (Hii inatuambia kuwa watu wanakaa nje ya mji. Ni mahala pa kusanyiko. Mahala pa kusherehekea. Hiyo inamaanisha una jumba lako kumbwa la Yerusalemu yako Mpya na nyumba yako ya kijijini.)
1. Angalia maneno “wataketi chakulani.” Hii inazungumzia nini kwa watu wasio na uhakika wa chakula chao cha kesho?
F. Soma Mathayo 7:13-14. Asilimia ngapi ya wale waliowahi kuishi watakuwa na makao katika Yerusalemu Mpya? (Idadi ndogo. Ni “wachache” dhidi ya “wengi.”)
1. Yerusalemu Mpya ni kubwa. Hiyo inaashiria nini juu ya ukubwa wa nyumba yako katika Yerusalemu Mpya? (Ni kubwa!)
G. Soma Ufunuo 21:22. Kuna rejea nyingi zinazorejelea hekalu kuwa mbinguni. Kwa mfano, angalia Ufunuo 11:19. Kwa nini uwe na hekalu mbinguni na katika nchi ya kale, lakini sio katika nchi itakayofanywa upya? (Hekalu katika nchi ya kale palikuwa mahali pa kumwabudu Mungu. Ufunuo 4 & 5 inajadili ibada ya mbinguni mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Katika nchi mpya lazima ibada iwe tofauti.)
1. Soma Ufunuo 3:12. Hii inasema kuwa hekalu katika nchi mpya ni kitu gani? (Hii inafafanua kwamba sisi ni nguzo katika hekalu la Mungu. Je, unaona taswira inayoibuka? Mungu Baba na Yesu ni hekalu (Ufunuo 21:22) na sisi ni nguzo katika hekalu hilo (Ufunuo 3:12). Linganisha hili na fundisho la kwamba kwa sasa sisi ni mahekalu ya Roho Mtakatifu (1 Wakorintho 3:16).)
H. Soma Ufunuo 22:1-2. Hii inazungumzia mji gani? (Yerusalemu Mpya.)
1. Tunawezaje kuwa na “mtaa” katika mji ambao ni mahala pakubwa sana?
2. Unadhani “kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo” kipo mahala gani katika Yerusalemu Mpya? (Mungu ana nyumba juu ya paa (penthouse). Yupo juu ya nyumba kubwa sana (condominium).)
3. Ni kwa jinsi gani basi Mto wa Maji ya Uzima unatiririka kutoka katika kiti cha enzi cha Mungu kupitia mitaa ya mji? (Taswira iliyopo kichwani mwangu ni kwamba mtaa unashuka kutoka ghorofa moja hadi jingine, vivyo hivyo kwa mto. Jumba kubwa ndio kile kinachojulikana kama “open atrium,” ikimaanisha kwamba pana nafasi ya wazi kuanzia chini hadi juu. Katika eneo hilo la wazi pana mtaa na mto.)
4. Unadhani Mti wa Uzima umekaakaaje? Kifungu kinasema upo “upande huu na upande huu wa ule mto.” (Mti wa Uzima umeota na kukua kupitia kwenye eneo la wazi. Upo katika pande zote mbili za mtaa na mto.)
5. Sasa fikiria kwamba nyumba yako iliyopo katika eneo la jumba kubwa katika Yerusalemu Mpya ipo katika ghorofa ya 200,000. (Kama Mji una urefu wa maili 1,380, hiyo itakuwa sawa na urefu wa futi 7,286,400. Kama kila ghorofa lina urefu wa futi 25, basi kuna ghorofa 291,456 katika Yerusalemu Mpya.) Unashukuru kwamba unaweza kuruka! Utakuwa na mtazamo gani juu ya eneo la wazi (atrium) (na mtaa, mto, na mti), na utakuwa na mitazamo gani nje ya mji? (Soma 1 Wakorintho 2:9. Mambo yote haya yanastaajabisha kiubunifu! Mji mzuri kiasi gani tuutarajiao!)
I. Rafiki, je, unapenda kuishi katika nchi itakayofanywa upya? Kwa nini usimkaribishe Yesu sasa hivi kuwa Bwana wako sasa na hata milele?
III. Juma lijalo tunaanza mfululizo mpya kuhusu fedha uitwao “Usimamizi kwa Bwana – Hadi Ajapo.”