Somo la 5: Kukabiliana na Deni

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Kumbukumbu la Torati 15 & 28, 1 Yohana 2, Mathayo 18
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
1
Lesson Number: 
5

Somo la 5: Kukabiliana na Deni

(Kumbukumbu la Torati 15 & 28, 1 Yohana 2, Mathayo 18)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Zaidi ya nusu ya Wamarekani wanasema kwamba madeni yanaathiri maisha yao katika hali hasi. Ninadhani jambo hilo ni kweli pia kwa jamii yoyote inayoruhusu mkopo wa haraka haraka unaopatikana kiurahisi. Kama kuna jambo lolote maishani linalosababisha matatizo kwa zaidi ya nusu ya watu wa jamii hiyo, basi jambo hilo linatakiwa kuchukuliwa kwa umakini. Na Biblia inalichukulia jambo hili kwa dhati. Biblia inatoa ushauri mwingi juu ya uhusiano wetu na fedha. Sehemu ya uhusiano huo ni kuepuka madeni. Kuna nyakati inaweza kuonekana kwamba deni haliepukiki. Dharura ya kiafya inaweza kusababisha deni. Biashara iliyoshindwa kufanya vizuri inaweza kusababisha deni. Mtu anawezaje kumiliki nyumba bila kuchukua mkopo wa kuijenga? Hata kumiliki gari la uhakika inaweza kuhitaji mtu kuchukua mkopo. Je, unafahamu kwamba Mungu alikuwa na kanuni rasmi kwa ajili ya watu wake na madeni? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi kuhusu deni!

I.  Baraka ya Kuepuka Deni

A.  Masomo kadhaa yaliyopita yanazungumzia jinsi ambavyo kuwa mkarimu kwa Mungu hutuletea baraka (zikiwemo baraka za fedha.) Soma Kumbukumbu la Torati 28:1-2 na Kumbukumbu la Torati 28:12-13. Unapovitafakari vifungu hivi vinne, vinaashiria nini kuhusu deni? (Deni ni kinyume cha baraka. Linakuweka chini na sio juu. Kuwakopesha wengine hukuweka juu.)

B.  Soma Mithali 22:7. Hakuna anayetaka kuwa maskini, au kibaya zaidi kuwa mtumwa. Unadhani kwa nini Biblia inasema kwamba mtu anayekopa anafanana na mtumwa?

1.  Mithali hii haitoi ufafanuzi wowote juu ya kauli yake kuhusu utumwa, isipokuwa kuonyesha mfanano kwenye uhusiano kati ya tajiri na maskini. Kwa nini zinafanana? (Fedha huwapatia matajiri uchaguzi. Mfanano ni kwamba mtu aliye kwenye deni ana upungufu wa fedha na upungufu wa chaguzi.)

II.  Majivuno na Deni

A.  Soma 1 Yohana 2:15-16. Kwa nini mtu anachukua mkopo kwa hiari? (Sehemu ya hii inahusiana na “kiburi cha uzima.” Marafiki wako wana magari mapya. Huenda pia wana boti, gari linalotumika kuwekea kambi (camping trailer), au kitu ambacho ungependa “kuwashirikisha.”)

1.  Unapolifikiria deni lako binafsi, kiwango gani cha deni hilo kimejengwa juu ya majivuno?

2.  Kuna msemo, “kuukaribia sana uzee, kuchelewa sana kuwa mwerevu.” Ninakumbuka kipindi fulani nikiwa nimesimama mbele ya nyumba yangu ya kwanza. Ilikuwa ndogo sana na haikuwa na gereji. Mbele ya nyumba yangu yalikuwa yameegeshwa magari mawili mapya – gari aina ya Thunderbird na Mustang. Nilipoitafakari mandhari ile nilidhani kuwa kuna jambo haliko sawa hata kidogo. Unaweza kuniambia ni jambo gani hilo? (Nilikuwa nimekopa fedha kununua magari hayo na yalikuwa ni mali inayoshuka thamani (depreciating) kadiri yanavyoendelea kuzeeka!)

B.  Nilipaswa kufanya nini ili kubadili taswira ile? (Kuna kipindi niliacha kununua magari mapya na kwa miongo kadhaa niliendesha magari yaliyouzwa kwa bei iliyopunguzwa yaliyokuwa yanatangwazwa kwa kuegeshwa pembezoni mwa barabara au niliyoambiwa na marafiki. Niliendesha gari aina ya Honda Accord lenye thamani ya $200, Chevy LUV truck lenye thamani ya $1,000, na Mercedes lenye thamani ya $3,000 Mercedes. Ilikuwa aibu nilipoendesha kwenda kwenye vikao ambapo watu walijua kwamba mimi ni mwanasheria.)

C.  Je, kuna namna ya kununua gari jipya na la kuaminika bila kuchukua mkopo? (Kwa sasa mimi ni mzee, tunaweka akiba ya kununua gari jipya kila mwezi. Tunapohitaji gari jipya, tunalinunua kwa kulipa fedha taslimu. Tunajaribu kununua magari yasiyopoteza thamani kwa kasi.)

III.  Upendo na Deni

A.  Soma Mithali 6:1-3 na Mithali 22:26-27. Tatizo gani linajadiliwa hapa? (Hiki ndicho kile ambacho tunaweza kukiita “kudhamini mkopo.” Unakubali kulipa mkopo ikiwa mtu anayechukua mkopo atashindwa kulipa.)

1.  Je, hili si jambo la upendo kulitenda? Je, hiki sicho ambacho wazazi wenye upendo wanachopaswa kukifanya kwa ajili ya watoto wao? (Angalia kwa uhakika kile kinachosemwa kwenye vifungu hivi. Mithali 22:26-27 inachukulia kwamba huna fedha za kulipa deni. Mithali 6:1 inaashiria kwamba unafanya hivi kwa jirani au hata kwa mtu usiyemjua.)

a.  Je, itakuwa sahihi kuliita “deni” ikiwa una fedha zinazoweza kulipa mkopo uliodhaminiwa kwa mwanafamilia? (Sidhani kama ni deni ikiwa unazo fedha hizo. Fikiria manufaa ya kumpa fedha mkopeshaji ili kumwepusha mkopaji kulipa riba.)

B.  Soma Kumbukumbu la Torati 15:1-3. Mungu ameweka mfumo gani rasmi kwa ajili ya watu wake? (Kila baada ya miaka saba mkopaji alikuwa anaachiliwa kutoka kwenye deni lake. Hii ilihusika kwa Wayahudi wenzako, haikuhusika kwa wageni.)

1.  Kuna mtazamo gani nyuma ya huu uachiliwaji wa Kisabato (Sabbatical)? (Mungu hakutaka deni liendelee kukua.)

2.  Hii ina athari gani kwa wakopeshaji? (Hii ingekatisha tamaa ukopeshaji.)

C.  Soma Kumbukumbu la Torati 15:7-9. Mungu Anasema nini kuhusu kukatisha tamaa suala la ukopeshaji? (Mungu anasema kuwa wakopeshaji wanapaswa kuwakopesha maskini hata kama walikuwa wanakaribia mwaka wa maachilio. Tusipowapatia maskini chochote tuna hatia ya dhambi.)

D.  Soma Kumbukumbu la Torati 15:10. Tunapaswa kulichukuliaje suala la kuwakopesha maskini? (Hii ni fursa ya baraka kutoka kwa Mungu.)

E.  Linganisha Kumbukumbu la Torati 15:11 na Kumbukumbu la Torati 15:4-5. Unalinganishaje vifungu hivi viwili? (Kuna uwezekano wa majibu mawili. Kwanza, maskini hawazitii amri na matokeo yake wanakuwa maskini na kuhitaji msaada. Wanapaswa kuzishika amri ili kuepuka umaskini. Pili, tukichukulia kwa umakini wajibu wetu kwa maskini waliopo kanisani, hatutakuwa na watu maskini ndani ya kanisa.

1.  Utaona kwamba katika “mfumo rasmi” wale wasio waamini hawajumuishwi. Kuna fundisho gani katika hilo? (Siamini kwamba Mungu anatutaka tutoe ruzuku kwenye tabia mbaya za makusudi. Sio upendo kuwezesha tabia zinazoangamiza.)

F.  Soma tena Kumbukumbu la Torati 15:1. Kwa wale wenye uelewa juu ya mfumo wa sheria wa Marekani, je, hii inakukumbusha jambo lolote? (Hii kwa kiasi fulani inafanana na sheria za ufilisi za Marekani. Ni jibu kwa deni kubwa lisilohimilika. Ni mfumo wa utoaji unafuu ambao kila mkopeshaji anaujua.)

IV.  Teolojia ya Msamaha

A.  Mathayo 18 inaelezea kisa cha mfalme aliyemalizana na watumwa aliokuwa anawadai fedha. Mtumwa mmoja alidaiwa talanta 10,000. Soma Mathayo 18:25-27. Ungekuwa na mwitikio gani kwa mfalme kama wewe ndiye ungekuwa huyu mdeni? (Mfalme anafanya zaidi ya kile kilichoombwa. Haongezi muda zaidi wa kulipa deni, bali anasamehe deni.)

1.  Unadhani mtumwa huyu aliwezaje kumshawishi mfalme kumkopesha kiasi hicho kikubwa cha fedha? (Lazima huyu alikuwa mtumwa wa pekee, mwenye kipaji.)

B.  Soma Mathayo 18:28-30. Je, huu ni mrejesho wa kutisha kwa mtu aliyesamehewa talanta 10,000? (Soma Mathayo 18:31. Jambo hili lilikuwa la kutisha sana kiasi kwamba wajoli wengine walipolishuhudia walimfikishia taarifa mfalme.)

C.  Soma Mathayo 18:32-34. Je, unakubaliana na matendo ya mfalme?

1.  Je, umegundua kuwa adhabu hii haifanani na ile ya kwanza? Haihusishi familia ya mdeni au kuwataka wauzwe kama watumwa. Hata hivyo, neno la Kiyunani linalotafsiriwa kama “mabwana jela” ni “watesaji.” Hiyo inaashiria nini? (Inaashiria kwamba mdaiwa huyu amevuka kutoka kuwa mtu asiyeweza kulipa madeni yake hadi kuwa mtu anayestahili adhabu kwa kile ambacho kimsingi ni kitendo cha jinai.)

D.  Soma Mathayo 18:35. Muktadha wa kisa hiki ni wa muhimu sana. Kilichomhamasisha Yesu kuelezea kisa hiki ni mjadala kuhusu kuwasamehe wale wanaotutenda dhambi. Angalia Mathayo 18:21. Je, nimekupotezea muda wako kwa kisa hiki, au unadhani kuna jambo la kujifunza kuhusu kukopesha na madeni? (Nadhani kisa hiki kina mafunzo mawili yanayotuhusu. Kwanza, kinaonesha hali isiyo salama (vulnerable) ya mdaiwa. Pili, ninadhani fedha ni mojawapo tu ya namna ya kuweka kivitendo wajibu wetu wa kuwasamehe wengine kwa kuzingatia kile ambacho Baba wetu wa Mbinguni ametusamehe. Kama Mungu ameturejeshea uhai wetu (jambo ambalo thamani yake haina ukomo), tunawezaje kushindwa kuwarehemu watu waliopo kanisani tunaowadai fedha?

1.  Hatujagusia hali adimu ambapo watu wako kwenye madeni pasipo wao kufanya kosa lolote. Kisa hiki kinaashiria nini juu ya kuwasaidia watu hao? (Muktadha wa kuwasamehe watu wanaotutenda dhambi unapaswa kutumika kwa wale ambao madeni yao yanatokana na makossa yao wenyewe. Tunapaswa kuwaje watu wa msaada zaidi kwa wale ambao deni lao halitokani na makosa yao?)

E.  Rafiki, je, utauchukulia ushauri wa Mungu juu ya deni kama baraka nyingine? Ukiepuka madeni, maisha yako yatabarikiwa. Kwa nini usiachane na majivuno yako na kuchukulia kwa umakini fundisho la Biblia juu ya madeni?

V.  Juma lijalo: Kujiwekea Hazina Mbinguni.