Somo la 12: Mhuri wa Mungu na Alama ya Mnyama : Sehemu ya 2

2 Wathesalonike 2, Ufunuo 17
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
2
Lesson Number: 
12

Somo la 12: Mhuri wa Mungu na Alama ya Mnyama : Sehemu ya 2

(2 Wathesalonike 2, Ufunuo 17)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Juma lililopita tulijifunza kuwa uchaguzi wa wanadamu ni ama kumtegemea Mungu au kuzitegemea nadharia na matendo ya wanadamu. Hili sio suala la juujuu. Wakristo wengi kwa namna fulani wanayategemea matendo na nadharia za wanadamu kuenenda katika mwenendo wao wa Kikristo. Kwa upande mmoja kuna Wakristo wanaoamini kuwa matendo yao ya kiMungu yanawapa sifa ya kwenda mbinguni. Kwa upande mwingine kuna Wakristo wanaoamini kuwa utamaduni wa kisasa unaweza kuwa na kura ya turufu dhidi ya mafundisho ya wazi kabisa ya Biblia. Kisha kuna wasioamini ambao wanamkataa kabisa Mungu wa Kikristo. Njia zote hizi zinaelezea utegemezi katika nadharia ya kibinadamu na sio kumtegemea Mungu. Juma hili tunaangalia kwa kina falsafa ya mpinga Kristo, falsafa inayojikita katika kumzingatia mwanadamu.

I.  Uasi

A.  Soma 2 Wathesalonike 2:3. Majuma mawili yaliyopita tuliona kuwa huu ni ujio wa bandia wa Yesu Mara ya Pili. Udanganyifu huu unaakisi mtazamo gani? (Uasi dhidi ya Mungu.)

1.  Uasi huo ukoje? (Usiotii sheria. Shetani anaipinga sheria ya Mungu.)

2.  Ni nini hatima ya uasi? (Uangamivu.)

B.  Soma 2 Wathesalonike 2:4. Ni yepi yaliyo madai ya uasi? (Kujiweka juu kwenye kila chenye kuabudiwa, na kila mungu, ikiwemo Mungu wa kweli.)

1.  Utaona kuwa madai sio ya ukuu tu, lakini mtu asiyeshika sheria yoyote anapinga ibada za aina zote. Unadhani hilo litatokeaje? Kitu gani kitakuwa sehemu ya juhudi hiyo? (Huku sio kuishi tu na kuishi. Huu ni upinzani hai wa ibada za aina zote, ikiwemo kumwabudu Mungu wa kweli.)

2.  Je, hii leo kuna vuguvugu linaloonekana kupinga dini zote za jadi?

C.  Soma 2 Wathesalonike 2:5. Ombi hili kwa wale ambao hapo awali walionywa linaashiria nini kwetu leo? (Tunatakiwa kulitafakari au kuliangalia upya onyo hili.)

1.  Hebu tufanye hivyo. Unadhani uasi ni upi? Ni kuzikataa kanuni za zamani za Kikristo. Shetani anafanya ujio bandia wa Yesu Mara ya Pili na anataka kukataa utiifu wa zamani kwa Mungu wa kweli.)

a.  Je, mabadiliko ni jambo baya? (Mambo mengi mapya ni maboresho ya mambo ya zamani. Suala ni kama sheria ya Mungu ndio inayobadilishwa. Tunalifahamu hili kwa kuwa ufafanuzi unaofuata ni “kutokuwa na sheria.”)

b.  Ni njia gani moja tunayoweza kuitumia kujua kama mabadiliko yanayopendekezwa sio sahihi? (Je, matokeo ni uangamivu?)

(1)  Tafakari idadi ya mawazo mapya yanayotetea machafuko ili kuleta mabadiliko. Je, hiyo inatupatia jambo la uhakika kama dhana iliyopo ni sehemu ya uasi wa jumla?

II.  Mnyama Mwenye Pembe Kumi wa Kale

A.  Soma Ufunuo 12:3-5 na Ufunuo 12:9. Biblia inambainisha huyu “joka kubwa jekundu” kama Shetani. Kwa nini anaelezewa kama “jekundu?” (Nyekundu inaweza pia kuwakilisha damu. Hii inaendana na uangamivu tulioujadili hivi punde.)

1.  Kwa nini Shetani anaelezewa kuwa na vichwa saba na pembe kumi? (Waprotestanti, kama tutakavyoona hapa chini, kihistoria wamemhusisha mnyama mwenye Pembe Kumi na Ufalme wa Rumi. Kwa kuwa Ufalme wa Rumi haukuwa sehemu ya pambano mbinguni, tunatakiwa kuhitimisha kuwa pembe kumi ina maana kubwa, ya kina, na pana. Saba ni namba ya ukamilifu katika Biblia. Hiyo inaweza kumaanisha kuwa Shetani ni mwovu kabisa.)

2.  Kwa nini vichwa vinavishwa mataji ikiwa vinaashiria uovu kamili? (Lazima hii imaanishe kuwa watawala kumi wanahusika kwenye huu uovu kamili. Shetani ana mawakala.)

3.  Unadhani pembe zinawakilisha nini? (Pembe kwa mnyama huwakilisha silaha. Kwa mara nyingine, hii inaendana na dhana ya uangamivu.)

B.  Soma Ufunuo 17:7. Tunaahidiwa nini? (Maajabu ya Pembe Kumi ya Kale yatahitimishwa! Hatutakuwa na haja ya kukisia.)

C.  Soma Ufunuo 17:8-9. Je, hiyo imekutatulia fumbo? (Sio kwa uhakika. Utaona kuwa Pembe Kumi zinainuka kutoka kuzimu.)

D.  Soma Ufunuo 9:11. Mfalme wa kuzimu ni nani? (Jina la Kiebrania Abadoni linamaanisha uangamivu. Huu ni uthibitisho zaidi kuwa tunamzungumzia Shetani. Inaonekana kuwa “Abyss” ni kuzimu. Katika Ufunuo 20 tutaona kuwa Shetani anafungwa Kuzimu.)

E.  Hebu turejee kwenye Ufunuo 17:8. Unadhani inamaanisha nini kwamba Yule Mnyama “alikuwako, naye hayuko, naye atakuwako?” Je, inamaanisha kuwa Shetani ameshindwa na kisha anarejea kwa kishindo?

F.  Soma Ufunuo 13:1-2. Je, huyu mnyama mwenye Pembe Kumi ni Shetani? (Hawezi kuwa kwa sababu kifungu kinasema kwamba joka (Shetani) anampa nguvu na mamlaka huyu mnyama mwenye Pembe Kumi.

1.  Tunawezaje kuwa na mnyama zaidi ya mmoja mwenye Pembe Kumi? (Hitimisho lenye mantiki ni kwamba Shetani ana mawakala wanaoyabeba mamlaka yake.)

G.  Hebu turejee kwenye Ufunuo 17. Soma Ufunuo 17:9-13. Kwa kuwa tumeona kuna mnyama mwenye Pembe Kumi zaidi ya mmoja, je, huyu ni mnyama wa tatu? (Katika somo la 9 tulijadili uelewa wa kihistoria wa kiprotestanti wa “vilima saba” au “milima saba.” Rumi imejengwa juu ya vilima saba, jambo linalounga mkono dhana ya kwamba Pembe Kumi inainuka kutoka Ufalme wa Rumi na ni Rumi ya Kipapa. Ingawa tafsiri ya Biblia ya NIV (pamoja na tafsiri nyinginezo) inatafsiri Ufunuo 17:9 kama “vilima,” inaonekana kufaa (appropriate) zaidi kuitafsiri kama “mlima.” Je, “mlima” unaweza kuwa unarejelea eneo lenye ushawishi hapa duniani? Kwa mfano, milima inaweza kuwa sheria, maburudisho, biashara, na serikali, kutaja tu baadhi. Hivyo, hii inaweza kumaanisha kuwa ushawishi wa Kishetani unajumuisha maeneo mengi muhimu na yenye ushawishi maishani.)

H.  Hebu tujikite kidogo kwenye Ufunuo 17:12. Hii inaashiria kuwa asili ya pembe kumi ni ipi? (Sehemu ya ufunuo wa fumbo ni kwamba hadi kufikia hapa pembe zinawakilisha wafalme wanaoungana dhidi ya watu wa Mungu. Kuna ufafanuzi mwingi wa wafalme hawa na falme hizi. Hata hivyo, tumekuwa tukijadili kuwa mnyama mwenye Pembe Kumi hamwakilishi Shetani pekee, bali pia ni ishara ya mamlaka ya kidini na kidunia, mamlaka zinazopambana na Mungu na wafuasi wake.)

I.  Kwenye utangulizi niliandika kuwa tutaangalia kwa kina falsafa ya mpinga Kristo na falsafa inayojikita katika kumzingatia mwanadamu. Je, kujikita huku kwa kina kumetufunulia nini? (Shetani wa kale mwenye Pembe Kumi ana mawakala wake duniani. Wana nguvu kubwa na wako vitani dhidi ya Wakristo wanaomtegemea Mungu na sio uwezo wa kibinadamu. Hii leo ninadhani ishara ya wazi kwa wale wanaomtegemea Mungu ni wale wanaopokea na kukubali maelezo ya kitabu cha Mwanzo juu ya mianzo na masuala yote yanayotokana na hilo – Sabato, familia, na mahala pa mwanadamu katika uumbaji.)

III.  Ushindi

A.  Soma Ufunuo 17:14. Nani anayeshinda katika pambano dhidi ya mnyama mwenye Pembe Kumi? (Mungu wetu! Upande wetu!)

B.  Soma Ufunuo 17:16-18. Tunaona ushindi gani mwingine? (Kuna mgongano miongoni mwa wapinzani wa Mungu. Mnyama mwenye Pembe Kumi na mawakala na washirika wake wanaanguka.)

C.  Rafiki, muda wa kuwa tayari ni sasa! Kuwa mwanafunzi makini wa Biblia ili usidanganywe na Pembe Kumi ya Kale na washirika wake!

IV.  Juma lijalo: Kuteketezwa kwa Utukufu wa Mungu.