Somo la 1: Paulo na Waefeso

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Waefeso 1, Matendo 19
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
3
Lesson Number: 
1

Somo la 1: Paulo na Waefeso

(Waefeso 1, Matendo 19)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Tunaanza mfululizo mpya wa masomo, safari hii ni kuhusu kitabu cha Waefeso. Ingawa masomo ya siku hizi ni ya muhimu, ninapendelea kuandika masomo juu ya vitabu mahsusi vya Biblia. Kwa nini? Kwa miaka mingi ya kujifunza Biblia, nimeamini kuwa sio tu kwamba kauli za kwenye Biblia zinaongozwa na Roho Mtakatifu, bali mpangilio wa mawazo pia umevuviwa na Roho. Kwa nini nibadilishe mpangilio wa ujifunzaji wa mwanadamu na ule wa Roho? Somo la juma hili ni la utangulizi. Baada ya hapo tutafuata mpangilio wa kitabu cha Waefeso.

I.  Salaam!

A.  Soma Waefeso 1:1. Kitabu cha Waefeso kinasema kuwa mwandishi wake ni nani? (Paulo.)

1.  Imekuwa kawaida kubisha kuwa Paulo hakuandika kitabu cha Waefeso. Kama hakukiandika, hiyo inazungumzia nini kuhusu kile tunachoelekea kujifunza? (Ikiwa mwandishi anadanganya kuwa yeye ni Paulo, tunaweza tusiamini kitu kingine chochote kwenye kitabu hicho.)

2.  Inamaanisha nini kusema kuwa Paulo ni “mtume?” (Mtume ni mjumbe au mshiriki. Baadaye anajiita “mjumbe [balozi].” Waefeso 6:20.)

3.  Inamaanisha nini kuwa yeye ni mjumbe “kwa mapenzi ya Mungu?” (Soma Wagalatia 1:1. Paulo anasema alikasimishwa na Mungu moja kwa moja.)

B.  Utaona kuwa Waefeso 1:1 inasema kuwa ujumbe huu unaelekezwa kwa “watakatifu walioko Efeso wanaomwamini Kristo Yesu.” Unadhani Paulo anawaandikia waaminifu pekee katika kanisa hilo mahsusi? (Ninadhani Paulo anawaandikia wale waliopo Efeso na waaminifu wengine kwa Yesu waliopo mahali pote. Maoni ya Vernon McGee’s katika baadhi ya miswada bora “katika Efeso” hayajitokezi. Kuna Ushahidi wa hilo. Ikiwa ni kweli, hiyo inasaidia kutangaza dhana ya kwamba kitabu hiki ni kwa ajili yetu sote tulio wafuasi wa Yesu.)

C.  Soma Waefeso 6:20. Paulo alikuwa katika mazingira gani alipoandika kitabu cha Waefeso? (Alikuwa amefugwa gerezani.)

1.  Wapi na katika hali gani ambapo Paulo alikuwa amefungwa mnyororo? (Soma Matendo 28:16. Kipindi ambacho Paulo aliandika kitabu hiki hakina uhakika, lakini uwezekano mkubwa ni kwamba alikuwa Rumi akiwa na askari wa Kirumi. Hayuko ndani ya gereza.)

D.  Soma Waefeso 3:13. Kama ungekuwa umefungwa gerezani, je, ungejali zaidi juu ya mustakabali wako au ungejali mustakabali wa wale walio huru? (Hii inaonesha moyo wa Paulo wa waumini katika Efeso.)

1.  Kwa nini wakate tamaa kwa hali aliyokuwa anaipitia Paulo? (Mazingira ya hali ya kisiasa sio mazuri. Wanatangaza ujumbe kuhusu mtu aliyesulubiwa kupitia kwa mtu ambaye amefungwa minyororo.)

2.  Kwa nini hali ya Paulo ni “utukufu” kwao? (Soma Warumi 8:18. Kwa sababu Paulo alikuwa anashiriki nao injili, wana fursa ya kuuendea utukufu. Kitabu cha Warumi kinatuambia kuwa hatima ya mateso ni utukufu.)

E.  Soma Waefeso 1:2. Paulo anatutamania nini sisi tunaojifunza kitabu hiki? (Neema na amani. Fikiria Paulo anatamani neema na amani wakati akiwa amefungwa gerezani.)

II.  Historia ya Paulo na Waefeso

A.  Katika Matendo 18:19-21 tunasoma habari za Paulo kuitembelea Efeso kwa kipindi kifupi. Paulo anasema kuwa angependa kurudi na anarejea katika sura inayofuata. Soma matendo 19:1-3. Kuna jambo gani la kipekee kuhusu ubatizo wa waumini katika Efeso? (Hawabatizwi kwa Roho Mtakatifu. Hata hawamjui Roho Mtakatifu.)

1.  Unadhani “ubatizo wa Yohana” ni kitu gani? (Lazima watakuwa wanamrejelea Yohana Mbatizaji aliyekuwa akibatiza katika maandalizi ya ujio wa Yesu.)

B.  Soma Matendo 19:5. Kasoro gani nyingine katika ubatizo wao inapendekezwa hapa? (Hawakubatizwa katika jina la Yesu.)

C.  Soma Matendo 19:6. Tuna uthibitisho gani kwamba sasa wamempokea Roho Mtakatifu? (Wananena kwa lugha na kutabiri.)

1.  Je, kuna ulazima wa kunena kwa lugha ili kuthibitisha kuwa umebatizwa kwa Roho Mtakatifu? (Soma 1 Wakorintho 12:30-31 na uilinganishe na 1 Wakorintho 12:10. Kunena kwa lugha ni uthibitisho wa karama ya Roho Mtakatifu. Lakini 1 Wakorintho inatuambia mambo mawili kuhusu karama hii. Kwanza, sio wote wananena kwa lugha. Pili, ni karama ya hali ya chini. Tunapaswa kutamani karama za juu zaidi.)

2.  Je, umewahi kumwona mtu ambaye amebatizwa kwa jina la Yesu ambaye hakunena kwa lugha mara moja? (Ninapoyaandika masomo haya sina shaka kuwa Roho Mtakatifu anayaongoza mawazo yangu.  Miaka michache iliyopita nilikuwa kwenye mkutano ambapo mzungumzaji (mhubiri) aliwaita watu wajongee mbele ili wapokee karama ya kunena kwa lugha. Nilienda mbele haraka na mtu mmoja akaweka mikono yake kichwani mwangu na kuniombea. Ombi langu kwa Mungu lilikuwa “Hebu hili litendeke ikiwa unaniwazia hivyo.” Hakuna kilichotokea. Biblia iko wazi kuhusu karama ya kunena kwa lugha, lakini kwa dhahiri karama hiyo haipo kwa ajili yangu.)

D.  Soma Matendo 19:7-8. Paulo anaanza na waumini wa kiume kumi na wawili katika Efeso na kuanzia hapo anaanza kupeleka injili katika sinagogi lililopo eneo hilo. Kwa nini anaanzia kwenye sinagogi? (Angewapata Wayahudi waliokuwa wakimtafuta Masihi. Bila shaka ndio maana ujumbe wa Paulo ulikuwa ni kwamba Masihi alishakuja.)

E.  Soma Matendo 18:19-20. Tunaona sababu gani nyingine ya Paulo kuzungumza kwenye hili sinagogi? (Katika safari yake fupi ya kwanza viongozi wa sinagogi walimtaka akae na kuongea nao kwa kipindi kirefu zaidi. Ana mwaliko.)

F.  Soma Matendo 19:9. Hatimaye Paulo anakabiliana na tatizo gani? (Wengine waliizungumzia uovu “ile Njia.” Watu hawa wanaweza kuzungumza mbele ya umati katika sinagogi.)

1.  Paulo anafanya nini pale alipopeleka injili, lakini akakutana na upinzani? (Anarudi nyuma. Utaona kuwa kupeleka injili katika sinagogi kunachukua kipindi cha miezi mitatu.)

2.  Je, kuna fundisho lolote kwa ajili yetu katika hili? (Hatupaswi kuwasumbua/kuwaudhi maadui kwa injili. Shiriki nao injili, na wakiipinga, jiondoshe kwa kurudi nyuma.)

G.  Angalia tena Matendo 19:9 na uongezee Matendo 19:10. “Darasa la Tirano” ni kitu gani? Na, hadhira yake mpya ni ipi? (Mojawapo ya maoni yanasema kuwa mtazamo wa jumla ni kwamba Tirano alikuwa Myunani, na alifundisha madarasa ya falsafa au balagha (elimu ya usemaji). Paulo alikaa hapo kwa muda wa miaka miwili.)

1.  Ni nini matokeo ya miaka miwili ya Paulo kufundisha katika Darasa la Tirano? (Wayahudi na Wayunani katika Asia waliisikia injili.)

H.  Tafakari jinsi Paulo alivyotumia mbinu za kupeleka injili katika Efeso na Asia. Tunaweza kujifunza nini kutokana na hili? (Anza na waumini wa msingi. Zungumza kwanza na wale mnaofanana kimtazamo kwenye masuala ya Kibiblia. Kisha itisha mikutano kwa ajili ya watu wote.)

1.  Baadhi ya mbinu za uinjilisti mbovu kabisa na zisizo na ufanisi kwa miaka mingi zilinihusisha kwenda nyumba kwa nyumba kupeleka injili. Njia ya Paulo inapendekeza nini kuhusu kwenda nyumba kwa nyumba? (Katika maeneo ya Marekani ambapo nimeishi na ninaendelea kuishi, watu wanapinga kitendo cha wengine kwenda katika nyumba zao ili kubadili mtazamo wao. Paulo alipokutana na upinzani, alirudi nyuma. Njia bora ni kuwa na mkutano ambapo Roho Mtakatifu atawavuvia watu kuhudhuria na kusikiliza kile utakachokisema kuhusu injili.)

III.  Misaada na Changamoto za Uinjilishaji

A.  Soma Matendo 19:11-12. Kama miujiza ya kiwango hiki ingekuwa inatokea kanisani kwako, watu wangapi wangehudhuria mikutano yako ya injili?

1.  Kwa nini hilo halijitokezi kanisani kwako? (Kwa sababu ile ile ambayo hadi kufikia sasa sijapewa karama ya kunena kwa lugha. Roho Mtakatifu ndiye mtendaji. Utaona kuwa, hiki ni kipindi kilichofuatia baada ya udhihirishwaji usio wa kawaida wa nguvu na uwezo wa Roho Mtakatifu wakati wa Pentekoste (Matendo 2).)

B.  Soma Matendo 19:13-16. Ni nini onyo kwa wale wanaotumia jina la Yesu kwa ajili ya miujiza bila uwezo wa Roho Mtakatifu kuwa nyuma ya matumizi ya jina hilo? (Pepo hawajibu vizuri.)

1.  Kwa nini pepo hakuwapuuzia tu wana wa Kuhani Mkuu? Kwa nini aliwajeruhi? (Hii inadhihirisha mawazo ya malaika walioanguka wanaoipinga injili.)

C.  Soma Matendo 19:26-29. Tunaona mwitiko gani mwingine kwenye ujumbe wa injili? (Machafuko.)

D.  Soma Matendo 19:34-36. Tunaona njia gani nyingine ambapo ukweli unapingwa? (Wanamzuia msemaji asinene. Wanajaribu kumzuia asisikike.)

1.  Angalia mbinu za nguvu za giza: usulubishaji, kufungwa gezezani, kujeruhi, na kuzuia uhuru wa kutoa maoni. Kwa nini mbinu hizo kali? (Uinjilishaji wenye nguvu nyingi unakutana na upinzani mkali.)

E.  Rafiki, je, ungependa kusikia zaidi matukio ya Paulo na Waefeso? Kaa nasi tunapoendelea kujifunza kupitia kitabu hiki.

IV.  Juma lijalo: Mpango Mkuu wa Mungu Uliojengwa Juu ya Kristo.