Somo la 4: Jinsi Mungu Anavyotuokoa
Somo la 4: Jinsi Mungu Anavyotuokoa
(Waefeso 2)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Mara ya kwanza nilipokuwa ninaishi peke yangu kabisa ni pale nilipoanza kusoma shule ya sheria Atlanta, Georgia. Wakati wa masomo yangu ya shahada ya kwanza nilikuwa ninaishi nyumbani. Kanisa langu kule Atlanta lilikuwa katikati ya mjadala wa kufurahisha sana kuhusu kuhesabiwa haki kwa imani. Jambo moja ninalolikumbuka vizuri sana katika kipindi hicho ni pale mshiriki mmoja wa kanisa “alipopatia” na kuelezea furaha isiyo kifani kutokana na ukweli kwamba angeweza kuwa na uhakika wa wokovu wake. Hakuwa na haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu endapo alikuwa “mwema kiasi cha kutosha” ili kuokolewa. Sasa ni takriban miaka hamsini iliyopita na mada ya kuhesabiwa haki kwa imani imezeeka sana kwa upande wangu. Ingawa imezeeka, ni mada ambayo kamwe haiachi kuleta furaha juu ya kile ambacho Bwana wetu mwenye Upendo ametutendea. Hebu tuzame kwenye somo letu la Waefeso na tujihabarishe upya na hizi habari njema sana!
I. Hali Mbaya, Kimsingi Mauti
A. Soma Waefeso 2:1-2. Ungependa kusomaje wasifu wako baada ya kufa? (Wakati hilo litakuwa jambo la kupendeza, tatizo ni kwamba umefariki!)
1. Vifungu hivi vinatuambia nini kuhusu kufa kwetu? (Kiuhalisia tulikuwa wafu watembeao. Kama hakuna kilichobadilika tutakufa milele.)
2. Paulo anatuambia kuwa njia ya wafu imetiwa alama inayoonekana vizuri. Anasema kuwa tumeifuata “kawaida ya ulimwengu huu.” Unadhani kwa nini Paulo anatukumbusha kuwa ulimwengu wote kwa kipindi fulani ulikuwa kielelezo chetu na ilifanana nasi?
3. Ni nani mwingine ambaye tulikuwa tukimfuata? Na, je, bado hili ni tatizo duniani? (Tulikuwa tunamfuata Shetani. Na, ndiyo, bado hili ni tatizo kwa ulimwengu.)
a. Angalia mambo mawili chanya ambayo Shetani anaelezewa kwayo. Paulo anamuita “mfalme” na mwenye “uwezo.” Hiyo inamaanisha nini kivitendo? (Soma 1 Yohana 5:19. Hata baada ya Yesu kumshinda Shetani pale msalabani, Yohana anatuambia kuwa “dunia yote pia hukaa katika yule mwovu.”)
B. Angalia tena Waefeso 2:2. Tukisalia na suala la uwezo wa Shetani, Paulo analihusisha na “uwezo wa anga.” Anamaanisha nini kwa kusema hivyo? (Tulikuwa na mazoea ya kufanya utani kuwa mikrofoni zisizo na waya zilikuwa na matatizo kanisani kwa sababu Shetani alikuwa “mfalme wa uwezo wa anga.”)
C. Soma Waefeso 6:12. Hapa Paulo anazungumzia kuhusu “majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.” Tunapaswa kuhitimisha nini juu ya hizi rejea zinazomrejelea Shetani, anga, na ulimwengu wa roho? (Ninadhani hii inamaanisha kuwa malaika wapotovu (akiwemo Shetani) kamwe hawakupoteza uwezo wao wa kupaa. Kwa hakika hapa ndipo wanapokaa – angani juu yetu. Hii pia inazungumzia jambo kuhusu uwezo wao wa kwenda haraka.)
D. Soma Luka 4:5-6. Shetani anasema kuwa amepataje uwezo wake? (Anasema kuwa “alipewa.” Ukisoma muktadha, kamwe Yesu hakani madai ya Shetani ingawa Shetani anahafifisha suala la Yesu kuwa Mwana wa Mungu.)
E. Soma 1 Timotheo 6:14-15. Mfalme wa ulimwengu huu ni nani? (Yesu. Lazima hiyo ndio sababu ya Paulo kumuita Shetani “mfalme.”)
1. Kwa nini Shetani anakuwa na uwezo hapa duniani mbele ya msalaba? (Soma Luka 13:16 na 2 Wakorintho 12:7. Shetani na malaika wake waapotofu walishindwa, na sio kuangamizwa pale msalabani. Bila shaka yoyote Shetani anasalia kuwa na uwezo mkubwa na adui mwovu hata kama alishindwa.)
F. Angalia tena Waefeso 2:2. Je, Paulo anamuita Shetani kuwa ni “roho?” Nilidhani kuwa Mungu pekee ndiye anaweza kuwepo mahali pote kwa wakati mmoja. (Kwa dhahiri kabisa hakuna uthibitisho katika Biblia kwamba Shetani ni “roho” anayeweza kuwatesa watu wengi kwa wakati mmoja. Badala yake, “roho” inatumika kwa mantiki ya mtazamo. Asiye mtiifu ana mtazamo kama wa Shetani.)
1. Kwa nini tumetumia muda mrefu sana kujadili uwezo wa Shetani? (Tusisahau kwamba yeye ni adui mwenye nguvu kubwa. Adui ambaye hawezi kushindwa nje ya utiifu kwa Mungu.)
G. Soma Waefeso 2:3. Asili yako ikoje? (Kufuata “tamaa za miili yetu,” na “mapenzi ya mwili na ya nia.”)
1. Ninadhani watu wengi wanafanana na mimi kwa maana ya kwamba ninaweza kubainisha maeneo kadhaa maishani mwangu yanayosababisha matatizo ya dhambi. Nimesema, “ole wake mtu ajaribiwaye na kila jambo.” Mtazamo wangu umenifanya “nifanyie kazi” maeneo yangu ya dhambi nikidhani kuwa nikifanikiwa kuachana nayo Mungu atafurahishwa nami. Je, Paulo anasema kuwa fikra yangu si sahihi? (Inaonekana fikra yangu si sahihi. Paulo anazungumzia tatizo la kilimwengu la matamanio na tamaa zetu za dhambi. Hatupaswi kuwa na makadirio pungufu (underestimate) ya asili yetu ya hali ya dhambi.)
2. Utaona kuwa kifungu hiki kinatumia maneno “nasi tulienenda,” na Waefeso 2:2 inatumia maneno “ambazo mliziendea zamani.” Jambo gani linaakisiwa kwenye maneno haya?
II. Kuhuishwa
A. Soma Waefeso 2:4-5. Tulitokaje katika “wafu kwa sababu ya makosa yetu” hadi “kuhuishwa pamoja na Kristo?” (Kwa neema ya Mungu ambayo imejengwa juu ya “mapenzi yake makuu aliyotupenda.”)
B. Soma Waefeso 2:6 na uzingatie Waefeso 2:5. Angalia maneno yanayoainisha matendo ya pamoja: “alituhuisha pamoja na Kristo,” “akatufufua pamoja naye,” na “akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho.” Unadhani hii inamaanisha nini? (Soma Wakolosai 2:12-13. Huu ndio msingi wa imani kwamba katika ubatizo tunashiriki katika kifo cha Yesu, na ufufuo wa uzima wa milele pamoja na Yesu. Dhana iliyopo ni kwamba tunashiriki pamoja na Yesu katika kifo kwa ajili ya dhambi zetu na kisha ufufuo kutoka katika mauti hayo. Hatimaye, tutashiriki na Yesu kiuhalisia kwenda naye mbinguni.)
1. Je, kuna mantiki yoyote ambapo sasa hivi, “tumekaa pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Yesu Kristo?” Waefeso 2:6. (Sasa hivi sisi ni raia wa mbinguni.)
2. Ilimaanisha nini hasa kwa Yesu kukaa upande wa kuume wa Mungu katika ulimwengu wa roho? (Soma Waefeso 1:20-22. Huu ni ushindi wa Yesu dhidi ya dhambi. Kukwezwa kwake.)
a. Je, tunao ushindi kama huo sasa hivi?
C. Soma Wakolosai 3:1-3. Hii inatuambia nini kuhusu kile inachomaanisha kukaa na Kristo katika ulimwengu wa roho? (Hii inaashiria kuwa tuna wajibu unaoendana na uraia wetu mbinguni. Wanatakiwa kutafuta mambo ya juu na kuyaweka mawazo yetu kwenye mambo ya juu na sio kwenye mambo ya kilimwengu.)
1. Unadhani hii inamaanisha nini kivitendo katika maisha ya kila siku?
D. Soma Waefeso 2:7. Neema itatumika kwetu kwa muda gani? (Katika zama zinazokuja.)
E. Soma Waefeso 2:8-9. Je, unajisikia kuwa bora zaidi kuliko watu wengine ambao sio watiifu kwa Mungu kama wewe? Je, kuna washiriki wa kanisa wasioendana na viwango vyako vya hali ya juu? (Paulo anasema kuwa kujisifu, tukiamini kuwa sisi ni bora kuliko waumini wengine, hakupaswi kuwepo kwa sababu hatufanyi chochote ili kuupata wokovu wetu. Ni zawadi tunayoipokea. Sio kwa “matendo yako.”)
F. Soma Waefeso 2:10. Lengo la maisha yako linapaswa kuwa lipi? Kujikalia zako tu katika wokovu wako ukitambua kuwa matendo yako hayahusiani kivyovyote vile na wokovu wako? (Kwa dhahiri hapana. “Tuliumbwa katika Yesu tutende matendo mema.”)
1. Inamaanisha nini kusema kuwa tunapaswa “kuenenda nayo?” “Nayo” ni kitu gani? Tunapaswa kuenenda katika jambo gani? (“Nayo” ni matendo mema. Kuenenda huakisi mwelekeo, mwenendo wa maisha yako. Unapaswa kuenenda katika matendo mema. Matendo mema ndio yanayopaswa kuwa lengo la maisha yako.)
G. Rafiki, habari njema kiasi gani! Yesu ameshatenda yote hayo kwa ajili yako. Amekuokoa kutoka kwenye mauti ya milele, aliishi maisha makamilifu kwa ajili yako kiasi kwamba sasa wewe ni raia rasmi wa mbinguni. Na, amekupatia kazi – ishi maisha yenye matendo mema. Je, utakubali kile ambacho Yesu amekutendea na kuupokea utume wake kwa ajili ya maisha yako? Kwa nini usichukue uamuzi huo sasa hivi?
III. Juma lijalo: Upatanisho Mlalo: Msalaba na Kanisa.