Somo la 7: Mwili wa Kristo Uliounganishwa

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Waefeso 4:1-16
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
3
Lesson Number: 
7

Somo la 7: Mwili wa Kristo Uliounganishwa

(Waefeso 4:1-16)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, umoja kanisani ni jambo jepesi? Unaweza kuangalia katika madhehebu yote na kuhitimisha kuwa kwa dhahiri umoja ni jambo gumu. Vipi kuhusu umoja katika ndoa? Mara kwa mara ninawasikia wanandoa wakisema “ndoa ni kazi.” Sio rahisi. Watu ambao hawajaoa wala kuolewa wanazinyooshea kidole changamoto za ndoa ili kujenga hoja kuwa ni bora zaidi kwa wao kuendelea kuwa katika hali waliyonayo. Je, ndoa za Kikristo ni rahisi? Je, madhehebu yote haya yanaendana na umoja wa kanisa? Mjadala wa Biblia juu ya umoja unatufundisha nini kuhusu kanisa letu Mahalia, kanisa la kilimwengu, na uhalisia wa maisha? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

I.  Gharama

A.  Soma Waefeso 4:1-2. Paulo alianza kitabu cha Waefesop 3 kwa kauli ya kwamba yeye ni mfungwa. Tulijifunza juu ya ufafanuzi wake na kubaini kwa nini wasomaji wanapaswa kumzingatia mfungwa. Paulo anarudia katika sura ya 4 kwamba yeye ni mfungwa. Unadhani kwa nini anarudia jambo ambalo hapo awali alidhani alihitajika kulitolea ufafanuzi? (Hapa Paulo anamaanisha jambo tofauti. Anaelezea kwa nini umoja huja kwa gharama.)

1.  Kwa ujumla, tunawachukulia wafungwa kama watu waliotenda kosa kubwa na kwamba wao si mfano wa kuigwa. Kwa nini Paulo anawaambia wasomaji wake “waenende kama inavyostahili?” (Ukipewa changamoto, kuna mtu anaweza kukuambia “uistahili changamoto.”)

B.  Angalia tena Waefeso 4:2. Je, unaona jambo lolote lenye changamoto hapa? (Nani anayedhani kuwa unyenyekevu, upole/uungwana, na uvumilivu ni mambo marahisi? Hizi zote ni changamoto.)

1.  Unaweza kuona kwa nini Paulo anabainisha mfanano kati ya kuwa mfungwa na maelekezo yake ya “kuenenda” katika unyenyekevu, uungwana, na uvumilivu?

C.  Soma Waefeso 4:3. Paulo anatupatia dokezo gani kuhusu jinsi tunavyoweza kusonga mbele na jukumu hili gumu? (Roho Mtakatifu anatuwezesha kuwa na umoja. Tayari Yesu aliweka amani kati ya Wayahudi na Mataifa. Roho Mtakatifu anatuelekeza kwenye mambo ya msingi ya umoja: unyenyekevu, uungwana, uvumilivu, na upendo.)

II.  Mifano

A.  Soma Waefeso 4:4. “Mwili mmoja” na “Roho mmoja” ni kitu gani? (Mwili ni kanisa na Roho ni Roho Mtakatifu.)

1.  “Tumaini moja” ni lipi? (Uzima wa milele.)

2.  Kwa nini Paulo anatupatia hizi tatu “moja?” (Tunatakiwa kuangalia mambo haya matatu kama msingi wa imani yetu. Msingi wetu ni umoja.)

B.  Soma Waefeso 4:5-6. Sasa tunazo “moja” nne zaidi. Je, kweli tuna “imani moja,” na “ubatizo mmoja?” (Paulo anachukulia kwa urahisi tu kwamba kuna “imani moja” pekee nayo imo ndani ya Yesu.)

1.  Soma Warumi 6:3-5. “Ubatizo mmoja” wa Paulo ni upi? (Paulo anaamini katika ubatizo wa kuzamishwa. Anaandika juu ya “kuzikwa” katika ubatizo. Kwa njia hii tunashiriki katika mauti na ufufuo wa Bwana wetu.)

2.  “Bwana wetu mmoja” ni nani? (Paulo anamrejelea Yesu. Angalia Yohana 14:6. Tunamwendea Baba wa Mbinguni kwa njia ya Yesu pekee. Bwana mmoja, njia moja.)

C.  Angalia tena Waefeso 4:6. Paulo anaandika “Mungu mmoja, Baba wa wote.” Hii inazungumzia nini kuhusu fundisho la Utatu Mtakatifu – Mungu watatu katika Mungu mmoja?

D.  Soma 1 Wakorintho 8:4-6 ambapo tunaona Paulo akielezea zaidi mtazamo wake wa Mungu Baba na Yesu. Unauelezeaje mtazamo wa Paulo? (Utaona kuwa 1 Wakorintho 8:4 inasema “hakuna Mungu ila mmoja tu.” Soma Kumbukumbu la Torati 6:4-5 na Marko 12:29. Hii inaitwa “Shema,” tamko la Agano la Kale kwamba kuna Mungu mmoja pekee. Yesu anathibitisha hili katika Marko 12. Lakini utaona kuwa Paulo sio tu kwamba anamuita Yesu “Bwana” katika 1 Wakorintho 8:6, bali anamhusianisha Yesu na uumbaji na uwepo endelevu wa “vitu vyote.” Mungu pekee ndiye anayeweza kufanya hivyo, jambo linaloimarisha imani ya Utatu Mtakatifu, imani katika umoja.)

E.  Baada ya kutafakari kuhusu mifano hii ya umoja, je, Wakristo wamepoteza kabisa upeo wa lengo hili kutokana na kuwepo kwa madhehebu yetu yote? (Njia bora ya kuliangalia jambo hili ni kusema kuwa madhehebu mbalimbali yana njia mbalimbali za msisitizo. Kwa mfano, tumejadili “ubatizo mmoja.” Wabaptisti wamejikita katika hili. Jeshi la Wokovu limejikita kwenye huduma. Waadventista wa Sabato wamejikita kwenye Sabato na unabii. Yote haya ni ya muhimu katika kosongesha mbele kazi ya Mungu.)

III.  Umoja Kiuhalisia

A.  Soma Waefeso 4:7. Kwa nini Paulo anatuandikia juu ya neema ya Mungu katikati ya mjadala kuhusu umoja? (Hili ndilo jibu la jinsi kazi hii ngumu inavyotekelezwa. Yesu anatuwezesha kuishi katika umoja kanisani kwetu na katika ndoa zetu. Hiki ni kipawa.)

1.  Je, neema hii ni tofauti na kipawa cha Roho Mtakatifu tulichokijadili hapo awali?

B.  Soma Waefeso 4:8 na Zaburi 68:18. Paulo ananukuu kwa juujuu kifungu hiki katika Zaburi. Mtoa maoni mmoja alisema kuwa alikuwa ananukuu tafsiri ya kale sana. Unapata taswira gani akilini mwako unaposoma kifungu hiki? (Yesu akipaa mbinguni baada ya kufufuka kwake. Alikuja kama mshindi.)

1.  Ni “vipawa” gani hivi ambavyo Mungu aliwapa wanadamu? (Soma Matendo 2:32-33. Hivi ni vipawa vya Roho Mtakatifu ambavyo tunapewa. Hii inaunganisha pamoja dhana ya neema ya Yesu kwetu na kwa Roho Mtakatifu. Sehemu ya neema inayobubujika kutoka katika ushindi wa Yesu ni vipawa vya Roho Mtakatifu.)

C.  Waefeso 4:9-10 kimsingi ni rejeo/tanbihi inayofafanua kuwa Yesu alikuja duniani na kisha akarejea “kupita mbingu zote.” Soma Waefeso 4:11-12. Unalielewaje hili – je, karama ni mpangilio wa kanisa? Au, je, Paulo anasema kuwa wanadamu wamepewa vipawa ili kujaza nafasi hizi kanisani? (Nadhani jibu ni vyote viwili. Yesu anatupatia kipawa cha kufanya mpangilio wa kanisa na Roho Mtakatifu anawawezesha wale wanaojaza nafasi hizo.)

1.  Ni nini mantiki ya matokeo ya jambo hili?  Je, mwalimu hapaswi kujaribu kuwa mwinjilisti au mchungaji? (Kwa namna fulani inaishinda nguvu dhana ya mpangilio wa kanisa. Jambo lililonikera zamani ni kwamba mtu anayeombwa kuimba au kutoa ombi kanisani anaamua kutumia fursa hiyo kutoa hubiri fupi.)

2.  Unadhani inamaanisha nini kusema “kuwakamilisha watakatifu kwa kazi ya huduma?” Kuwafanya washiriki kuwa katika kundi mojawapo la kanisa? (Sidhani kama hicho ndicho kinachomaanishwa. Badala yake, ninadhani majukumu haya maalumu yanawasaidia washiriki kukua kiimani na katika huduma.)

D.  Soma Waefeso 4:13. Utakumbuka kuwa tulianza somo hili tukizungumzia kuhusu umoja kanisani na katika ndoa. Ni kwa jinsi gani jambo hili linalowezeshwa na Roho Mtakatifu linaleta umoja kanisani?

1.  Je, hali itakuwa vivyo hivyo kwenye suala la ndoa?

2.  Tofauti na umoja, vipawa vinavyowezeshwa na Roho Mtakatifu huleta mambo gani mengine kanisani? (Ukomavu. Kufanana na Yesu.)

E.  Hebu tuingize kwenye mjadala huu kitabu kingine cha Agano Jipya kilichoandikwa na Paulo. Soma 1 Wakorintho 12:28-31. Je, hizi ni “karama zinazopaswa kukaa kwenye msitari wako?” (Ndiyo na hapana. Kwa dhahiri Paulo anasema kuwa sio kila mtu ana kipawa kinachofanana. Lakini pia anasema “takeni sana karama zilizo kuu.”)

F.  Soma Waefeso 4:14. Ukiwa na timu ya uongozi imara iliyojawa Roho, matokeo yake ni yepi linapokuja suala la mafundisho ya uongo? (Inasaidia kukataa/kuzuia mafundisho ya uongo. Ugomvi juu ya mafundisho ni chanzo kikubwa cha kutokuwa na umoja.)

G.  Soma Waefeso 4:15. Je, ukweli unapaswa kusemwa? Je, tunapaswa kuogopa kuusema ukweli? (Suala la kwanza ni kwamba ukweli unapaswa kusemwa.)

1.  Tunapaswa kuusemaje ukweli? (Kwa upendo.)

a.  Hiyo inamaanisha nini? (Tunamtakia mtu jambo bora.)

H.  Soma Mathayo 12:34. Je, huu ndio mfano tunaopaswa kuufuata? (Muktadha ni muhimu. Yesu na Roho Mtakatifu wameshambuliwa kwa kuambiwa kuwa ni mawakala wa Shetani. “Wazao wa nyoka” ni waovu kweli kweli, na sio wale wanaopambania imani yao. Utaona kuwa sura hii hii (Mathayo 12:36) inasema kuwa tutatoa hesabu ya maneno yetu ya kizembe.)

I.  Soma Waefeso 4:16. Ni nini matokeo ya kanisa lililopangiliwa vizuri na linaloongozwa na Roho? (Linafanya kazi vizuri! Linakua katika upendo. Taswira nzuri kiasi gani ya aina ya kanisa ambalo Mungu anatutaka tuwe!)

J.  Rafiki, umoja ndilo lengo la kanisa lako na ndoa yako. Je, utafuata ushauri wa Mungu ili kuwa na taasisi inayoongozwa na Roho Mtakatifu?

IV.  Juma lijalo: Maisha Yaliyoumbwa kwa Namna ya Kristo na Usemi Unaoongozwa na Roho.