Somo la 8: Maisha Yaliyoumbwa kwa Namna ya Kristo na Usemi Unaoongozwa na Roho

Waefeso 4:17-32
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
3
Lesson Number: 
8

Somo la 8: Maisha Yaliyoumbwa kwa Namna ya Kristo na Usemi Unaoongozwa na Roho

(Waefeso 4:17-32)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, umekuwa Mkristo maisha yako yote? Ikiwa ndivyo, baadhi ya yaliyoandikwa kwa Waefeso yanaweza kuwa vigumu kuendana na maisha yako leo. Hebu fikiria kwamba katika makuzi yako umekuwa ukiabudu sanamu. Mwelekeo wako wa kiroho utakuwa tofauti kabisa na wa watu ambao katika makuzi yao wamekuwa wakiukubali ukweli wa Biblia. Katika somo letu juma hili Paulo anatupatia mwongozo wa maisha ya Kikristo. Anasisitiza umuhimu wa kubadilika kutoka kwenye utu wetu wa kale na kuwa wapya katika Kristo. Mabadilikjo haya hayashawishi tu maendeleo ya mtu binafsi; yanaingia hadi kwenye uhusiano wetu, kanisani na katika nyumba zetu. Hebu tuangalie kwa kina kiini cha mabadiliko haya na jinsi yanavyojenga umoja miongoni mwa waumini!

I.  Utu wa Kale

A.  Soma Waefeso 4:17. Paulo anamaanisha nini anaposema kuwa tunatakiwa kubadilisha “mienendo” yetu? (Tunatakiwa kubadili mwelekeo wa maisha yetu.)

1.  Nini kinawafanya watu wa Mataifa kuwa nje ya msitari? (Kuna kasoro katika fikra yao. Mawazo yao hayafanyi kazi sawa sawa. Fikra yao imepotoshwa na imepungua.)

B.  Soma Waefeso 4:18. Je, watu wa Mataifa ni waathirika wa ujinga wasio na hatia? (Haionekani kuwa hivyo kwa sababu kifungu kinasema kuwa ujinga wao unatokana na “ugumu wa mioyo.” Kwa kuongezea, maneno “kutiwa giza” na “kufarikishwa” ni maneno yanayoakisi mwendo wa kuelekea kwenye upande wa giza wa mambo.)

C.  Soma Waefeso 4:19. Ni nini lengo la hawa watu wa Mataifa? (Wanatamani “wapate kufanyiza kila namna ya uchafu.”)

1.  Kwa nini wana hili lengo? (“Wamejitoa” kuingia kwenye njia hii ya maisha. Hii inatoa taswira ya kujiingiza kwenye uchafu. Kwa mara nyingine maneno “wakiisha kufa ganzi” yanaonesha mwendo wa kuelekea upande wa giza.)

2.  Fikiria kanisa ambalo tabia hizi za “kale” zinawakilisha mitazamo ya sasa ya washiriki. Hii ingeletaje mgawanyiko au changamoto miongoni mwa jamii ya waumini?

a.  Vipi kama kundi moja la washiriki wenye tabia za “kale” likiwa linajivunia tabia zao?

3.  Ni muhimu kiasi gani kwenye mabadiliko yetu kuzikiri tabia hizi na kuelewa matokeo yake?

II.  Kuukumbatia Upya wa Mtu

A.  Soma Waefeso 4:20-21. Ni jambo gani lililo la muhimu kwenye upya wa mtu? (Elimu. Angalia maneno yote yanayoakisi ujifunzaji: mlivyojifunza, mlisikia, mkafundishwa, na kweli.)

1.  Masuala hayo ya muhimu yanaashiria wajibu gani kwa kanisa na washiriki wake? (Tunatakiwa kuwa kwenye kazi ya kufundisha habari za Yesu. Kama anavyoandika Paulo “sivyo mlivyojifunza Kristo.”)

B.  Soma Waefeso 4:22-24. Unadhani Paulo anamaanisha nini anapotutaka “tuvue” na “kuvaa?” (Mtoa maoni mmoja anaiita hii kama “dini halisi.” Tunafanya uamuzi kila siku kuhusu jinsi tunavyopaswa kutafakari na kuishi. Huu ni uamuzi endelevu na wa makusudi katika safari yetu ya Kikristo.)

1.  Ni kwa jinsi gani haki, utakatifu, na kweli vinahusika katika hili?

2.  Roho Mtakatifu ana nafasi gani katika hili? (Inaonekana kuwa vigumu sana kwangu kubadili matamanio yangu. Ndio maana Waefeso 4:23 inazungumzia juu ya “kufanywa wapya katika roho ya nia zenu.”)

3.  Lengo hili linaathirije umoja kanisani? (Unaweza kufikiria juu ya kusanyiko la kupunguza uzito ambapo nusu ya watu katika kundi hilo inataka kuongezeka uzito na nusu nyingine inataka kupunguza uzito?)

C.  Vifungu vyote viwili vya Waefeso 4:22 na Waefeso 4:24 vinaonekana kulinganisha kubadilisha utu wa kale kwenda kwenye utu mpya na kubadilisha nguo – suala la nje ya mwili kabisa. Je, suala la uvaaji wetu ni suala la nje ya mwili kabisa? (Nina mtazamo chanya, kutokana na uzoefu binafsi, kwamba jinsi unavyovaa hutoa ushawishi wa vile ambavyo watu wanakufikiria. Ninadhani pia hushawishi namna tunavyojichukulia na kujitafakari.)

1.  Lengo letu sio kujikita kwenye mavazi, bali dhana ya kwamba tunafanya mabadiliko tunayoyaweza ambayo yataanzisha mabadiliko ya mitazamo. Je, kile nilichokiandika hivi punde kinaendana na kuhesabiwa haki kwa imani? Je, kinaendana na kazi ya Roho Mtakatifu? (Nguvu imo ndani ya Roho Mtakatifu. Lakini uamuzi ni wetu. Uamuzi wetu ni endelevu.)

III.  Hatua Halisi za Kuingia Kwenye Maisha Mapya

A.  Soma Waefeso 4:25. Unadhani kwa nini katika lengo letu la kuvaa utu upya Paulo anabainisha kuisema kweli kwanza? (Kusema ukweli ni msingi wa kuwa na uhusiano thabiti na wengine. Maoni ya Adam Clarke kwenye kifungu hiki yanasema “ukweli ulikuwa na nafasi ndogo miongoni mwa wengi hata kwa wapagani wazuri.”)

1.  Huwa unakuwa na mwitiko gani kwa watu wenye mazoea/desturi ya kukudanganya?

2.  Zingatia maneno “kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.” Unadhani hiyo inamaanisha nini na kwa nini ni muhimu kwenye ukweli? (Unakumbuka mjadala wetu kuhusu umoja? Sisi ni sehemu ya mwili wa Yesu. Mwili wako unawezaje kufanya kazi ikiwa sehemu moja ya mwili inaidanganya sehemu nyingine ya mwili?)

B.  Soma Waefeso 4:26. Aina gani ya hasira sio dhambi?

1.  Soma Marko 3:5. Hapa Yesu anaonesha aina gani ya hasira? (Muktadha unaonesha kuwa viongozi wa Kiyahudi walikuwa wanaangalia ili kuona kama Yesu angeikiuka Sabato kwa kumponya mtu yule mwenye kupooza mkono. Yesu alikuwa na hasira juu ya mtazamo wao (“ugumu wa mioyo yao”) kwamba haikuwa sahihi kutenda jema siku ya Sabato.)

2.  Soma Marko 3:6. Hii inatufundisha nini kuhusu asili ya mioyo yao migumu? (Walidhani kuwa ni makossa kufanya uponyaji siku ya Sabato, lakini iliruhusiwa kula njama ya kumwua Yesu siku ya Sabato.)

a.  Mtazamo wa viongozi hawa wa dini ulimaanisha nini kuhusu tabia ya Mungu?

b.  Zingatia tena mtazamo uliomfanya Yesu akasirike. Je, ulihusu tu kutenda kwake jambo jema siku ya Sabato, au ulikuwa unapotosha tabia ya Mungu, au jambo jingine?

3.  Kwa nini kuna kipengele cha muda kwenye hasira? Kwa nini itatuliwe ndani ya siku moja? (Tukiihodhi hasira inabadilika na kuwa uovu na chuki. Kwa maneno mengine, hali inakuwa mbaya zaidi.)

C.  Soma Waefeso 4:26-27. Nilidhani kuwa ni vyema kusoma vifungu hivi viwili pamoja. Je, vinahusiana? Ikiwa ndivyo, ni kwa namna gani? (Kwa kukilea kinyongo, kwa kuendelea kuwa mkali, tunafungua mlango kuingia kwenye dhambi kubwa zaidi.)

D.  Soma Waefeso 4:28. Nchini Marekani ombaomba sio jambo la kawaida nje ya majiji makubwa. Kila ninapowaona watu wenye uwezo wa kufanya kazi (hususan wanaume) huwa ninaudhika. Sehemu ya sababu ya kuudhika kwangu ni kwamba ombaomba ni mvivu, na sehemu nyingine ni kujisikia hatia kwa kukataa kwangu kumpatia fedha ombaomba. Yumkini, licha ya mionekano, hawezi kufanya kazi. Huenda ana tatizo la afya ya akili. Kifungu hiki kinazungumzia nini kuhusu manufaa ya kufanya kazi? (Inakupatia hisia za kujisikia kuwa na hadhi na inakufanya uwe na uwezo wa kuwasaidia wahitaji.)

1.  Je, suala la kufanya kazi ili kuwasaidia wengine linapaswa kunifanya nijisikie hatia zaidi? (Ninaamini hoja ya msingi ya Paulo ni kwamba unabadilika kutoka kuwa mtu unayepokea kutoka kwa wengine na kuwa mtu unayetoa kwa wengine.)

E.  Soma Waefeso 4:29. Kifungu kinatumia maneno mawili yanayohitaji tafakuri kuyaunganisha. Maneno hayo ni “lililo ovu” na “lililo jema.” Unayahusianishaje maneno hayo katika muktadha huu? (Ukimpotosha mtu kwa maneno yako unamdhuru. Ukimtia moyo mtu au kumuelimisha kwa maneno yako unamsaidia. Paulo anatuambia tutumie maneno yanayowasaidia wengine.)

F.  Soma Waefeso 4:30. Je, “kumhuzunisha” Roho Mtakatifu ni sawa na vitendo vya kusema uongo, kukasirika, au kuiba? (Soma Yohana 16:13. Kazi ya Roho Mtakatifu ni kutuelekeza kwenye ukweli. Tukishindwa kuishi maisha halisi ambayo Paulo anayapendekeza, Roho Mtakatifu anakata tamaa katika kazi yake. Paulo anatuambia tumtie moyo Roho Mtakatifu kwa kuishi kwa usahihi.)

1.  Kwa nini Paulo anabainisha katika Waefeso 4:30 kuhusu “kutiwa mhuri” na Roho Mtakatifu? (Hapo awali tumejadili kuwa uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yetu leo ni hakikisho la Mungu la uzima wetu wa milele pamoja naye. Tukilizingatia hili tutakuwa makini zaidi kutenda mambo sahihi.)

G.  Soma Waefeso 4:31-32. Je, unaweza kuvielezea kwa ufupi vifungu hivi viwili? Vinazungumzia jambo gani kwa pamoja? (Tunatakiwa kutendeana kwa wema na sio kwa kijicho.)

1.  Kwa nini? (Yesu alitusamehe. Tunatakiwa kuwa na roho ya kusameheana sisi kwa sisi.)

H.  Rafiki, unaokolewa kwa neema pekee. Wokovu hauyategemei matendo yako. Kuokolewa maana yake ni kwamba uko tofauti na jinsi ulivyokuwa huko nyuma. Inamaanisha kuwa unayaacha maisha yako ya kale na kuenenda kwa kuyazingatia mapenzi ya Roho Mtakatifu. Je, utadhamiria leo kuishi maisha yanayoendana na kuokolewa kwako?

IV.  Juma lijalo: Kuishi kwa Hekima.