Somo la 5: Visingizio vya Kukwepa Utume
Somo la 5: Visingizio vya Kukwepa Utume
(Yona 1-4)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Mojawapo ya hoja madhubuti za kuiamini Biblia ni namna inavyowaelezea mashujaa wake. Uzoefu wangu kama mwanasheria ni kwamba watu (ikiwemo mimi) hupenda kuelezea kisa kwa namna inayomfanya msimuliaji aonekane kuwa ni mtu mwema. Baada ya muda tunaweza hata kusahau taarifa zisizo za kufurahisha. Kisa cha Yona kimejaa taarifa zinazomfanya aonekane mtu mbaya. Na sio kuwa mtu mbaya tu, anaonekana kama mwanadamu wa kutisha! Lengo la somo letu ni kuachana na visingizio vya kukwepa kushiriki kwenye utume wetu. Tatizo la kumtumia Yona kama kielelezo cha kujifunza kwetu ni kwamba hatutaki kuamini kwamba sisi ni wabaya kiasi hicho. Tunapoingia kwenye somo letu la Biblia, tafakari kwa nini Mungu alimtumia mtu mwenye dosari/upungufu kuwafikia watu wabaya sana!
I. Shujaa wa Taifa
A. Soma Yona 1:1. Tunaona ujumbe gani chanya kumhusu Yona? (Mungu anazungumza naye moja kwa moja.)
B. Soma 2 Wafalme 14:25. Je, huyu ni Yona yule yule kama ilivyo katika Yona 1:1? (Ndiyo. Huyu ni Yona mwana wa Amitai kutoka Gath-heferi.)
1. Ni nini kazi ya Yona kama ilivyobainishwa katika 2 Wafalme 14:25? (Kwa mara nyingine, Mungu anazungumza kupitia kwa Yona. Yona ni nabii anayetabiri kuwa Israeli itashinda mapambano yatakayorejesha utukufu wake wa zamani.)
a. Unadhani wananchi wa Israeli walimchukuliaje Yona? (Alikuwa shujaa mkuu wa taifa! Aliwafunulia kuwa Mungu alikuwa upande wao. Alitabiri kuwa Israeli itawashinda maadui wake. Ilikuwa jambo zuri sana kuwa Yona.)
II. Jukumu Jipya
A. Soma Yona 1:2. Mungu anampa Yona jukumu gani jipya? (Kuusonda uovu unaofanywa katika mji wa Ninawi.)
1. Je, kazi hiyo ni tofauti sana na kazi ya awali ya Yona? Bado ananena dhidi ya watu wabaya. (Yona hazungumzi tena kutoka katika hali ya usalama ya Israeli, ambapo yeye ni shujaa wa nyumbani. Badala yake, anaingia katika kiini cha taifa la adui kuwaambia ana kwa ana kwamba Mungu anauona uovu wao.)
2. Je, kuiita dhambi kwa jina lake ni maadili ya kawaida katika zama za leo?
B. Soma Yona 1:3. Je, Yona anapenda kazi yake mpya? (Hapana. Maneno “akaondoka akimbilie” yanaashiria kuwa Yona anaogopa. Ninawi ulikuwa mji mkuu wa Waashuru. Hapo awali nilijifunza habari zao na walikuwa watu katili na dhalimu. Ilikuwa jambo la kawaida kuhofia kuwasonda.)
C, Soma Yona 4:2. Yona anatoa sababu ya ziada kwa nini alikimbia. Ni sababu gani hiyo? (Tunasoma katika Yona 3:10 kwamba baada ya Yona kuwahukumu watu wa Ninawi walitubu dhambi zao na Mungu aliamua kutowaangamiza. Hili lilimhuzunisha Yona kwa sababu alidhani atachukuliwa kama nabii wa uongo. Sio tu kwamba Yona alikuwa na hofu, lakini hata kama angechukua ujasiri na kwenda, alijua kuwa Mungu hatawaangamiza waovu – na hilo lingemfanya Yona aonekane mbaya.)
1. Kama ungetakiwa kubainisha dhambi kuu ya Yona, ungeibainisha dhambi gani? (Alijijali sana – usalama wake, hadhi yake. Na kwa kuongezea, hakumwamini Mungu.)
a. Je, hapo kabla Mungu alimjaribu Yona kwenye masuala hayo? (Kwa hakika hatuna habari za kutosha kumhusu Yona, lakini hii kazi ya awali ilikuwa maarufu na salama ya kutabiri maangamizi kwa maadui wa Israeli akiwa kwenye eneo salama la nyumbani kwao.)
III. Merikebu, Samaki, na Uhuru wa Uchaguzi
A. Kinachofuata ni kwamba dhoruba ya kutisha inatokea inayowafanya mabaharia wa merikebu aliyopanda Yona waamini kuwa watakufa. Dhoruba ni mbaya sana kiasi kwamba wanahitimisha kuwa miungu pekee ndio inayoweza kuwaokoa. Soma Yona 1:6-9. Yona anasema nini kumhusu Mungu wake na bahari? (Mungu aliumba bahari.)
1. Hebu tusome tena Yona 1:3. Hii inaashiria kuwa Yona ana mtazamo gani juu ya mipaka ya ushawishi wa Mungu? (Hapa zamani ilikuwa kawaida kuamini kuwa mungu alikuwa mtawala wa mamlaka fulani au vitu vya asili. Yona anasema kuwa atatorokea mahali ambapo Mungu hana mamlaka. Sasa tunaona Yona akikiri kuwa Mungu ni mdhibiti wa mbingu, bahari na nchi kavu.)
B. Soma Yona 1:11-12 na Yona 1:14-16. Mabaharia waliongolewa. Unaweza kuelezeaje mtazamo wa Yona na mabaharia kwa Mungu? (Huyu ni Mungu wa hukumu. Upendo wa Mungu hauonekani kuwa suala linalozungumziwa hapa.)
C. Soma Yona 1:17 na Yona 2:1-10. Hebu tujikite katika Yona 2:9-10. Yona anadhani kuwa atakufa, lakini hakani uwezo wa Mungu, bali anaukumbatia. Mtazamo gani wa Yona unaakisiwa katika Yona 2:9-10? (Yona anajitoa kwa mamlaka ya Mungu. Yona anasema kuwa atafanya “kile nilichoapa.”)
1. Hii inazungumzia nini kuhusu Mungu na uhuru wa uchaguzi wa mwanadamu?
2. Je, umewahi kufanya uamuzi mbaya katika siku za nyuma na Mungu akakuokoa kutokana na uamuzi huo? (Njia moja ya kuliangalia hili ni kwamba Mungu anashinikiza uchaguzi wa Yona ingawa bado Yona ana uhuru wa uchaguzi wenye matokeo (consequences). Njia nzuri ya kuliangalia hili kwa sehemu fulani imejengwa juu ya uzoefu wangu binafsi. Kuna nyakati ambazo nimeukataa uovu, na nyakati zingine ambapo Mungu aliniokoa kutoka katika uovu nilipokuwa mnyonge. Mungu ni nguvu ya wema katika maisha ya Yona.)
3. Tunapaswa kujifunza nini kutokana na hili linapokuja suala la utume wa Mungu kwa ajili yetu? (Mungu anataka watu wanaojitolea bila kulazimishwa! Yona alipaswa kumwogopa Mungu zaidi kuliko Waashuru. Lakini Mungu hakumkatia Yona tamaa.)
IV. Muujiza
A. Soma Yona 3:1-3. Je, Yona angeweza kuukataa wito huu?
B. Soma Yona 3:4-6. Muujiza gani unatokea? (Yona, kwa uwezo wa Mungu, anauongoa mji. Watu wote wanatubu.)
C. Soma Yona 3:7-9. Je, huu ni mmojawapo ya uongoaji wa watu wengi katika historia?
1. Hebu tusimame kidogo na tutafakari maswali machache. Je, matokeo haya yanastahili hali ya kutokuwa na furaha iliyomtokea Yona hivi karibuni? (Naam. Hawa walikuwa watu wabaya sana.)
2. Ujumbe gani uliwafanya watu wa Ninawi wamgeukie Mungu? (Angalia tena Yona 3:9. Uongofu huu unatokea kutokana na hofu ya hasira ya Mungu. Yesu alikuja duniani kuonesha upendo wa Mungu kwetu usio na kipimo. Lazima kanisa liwe kwenye mizania katika kumwakilisha kwetu Mungu. Sasa hivi baadhi ya watu wanadhani kuwa dhambi ya hadharani inapaswa kuheshimiwa kwa sababu ya nguvu ya upendo. Hilo halina mizania. Yesu alilipa adhabu ya dhambi. Hilo haliifanyi dhambi ikubalike. Inaifanya iwe ya kutisha zaidi kwa sababu ilimgharimu sana Yesu.)
D. Soma Yona 3:10. Mungu anawaonesha nini watu wa Ninawi? Na kwa nini Mungu anawaonesha? (Waligeuka na kuuacha uovu na Mungu akawaonesha rehema.)
V. Nabii Aliyekasirika
A. Soma Yona 4:1. Yona ni wakala wa Mungu wa namna gani? (Sio wakala mzuri sana. Amekasirika kwamba zaidi ya watu 120,000 (Yona 4:11) hawakuuawa.)
B. Soma Yona 4:5-6. Kwa nini Yona anakaa chini ili kuuangalia mji wa Ninawi? (Anatumaini kuuona ukiangamizwa na Mungu.)
C. Soma Yona 4:7-9. Yona ana ukomavu wa kiwango gani? (Anaenenda kama mtoto mdogo.)
1. Je, unatiwa moyo na hilo? (Mimi ninatiwa moyo! Tafakari taswira hii ya upendo wa Mungu kwa Yona. Yona anakuwa zuzu/mpumbavu na Mungu anakaa naye.)
D. Soma Yona 4:10-11. Katika somo la juma lililopita tuliona Mungu akiwaangamiza watu waovu sana. Suala lililojaliwa Sodoma, kwa mujibu wa maelezo ya Biblia, ilikuwa watu wenye haki. Mungu anamjali nani Ninawi? (Waovu waliotubu.)
1. Tofauti na kauli ya kushangaza kuhusu kutojua mkono wa kulia na mkono wa kushoto, unaona kauli gani nyingine ya ajabu kwenye vifungu hivi? (Kauli ya mkono wa kulia na mkono wa kushoto yumkini inawarejelea watoto. Inaweza kurejelea ukweli kwamba watu wa Ninawi hawakuwa na uelewa wa Mungu kwa upande wangu, kauli ya ajabu kabisa ni kwamba upendo na kujali kwa Mungu kunaenda mbali zaidi hadi kwa ng’ombe.)
E. Rafiki, kisa cha Yona kinahusu upendo na hukumu kwa watu wenye upungufu. Kwanza, Yona mwenye upungufu, na pili wananchi wa Ninawi wenye upungufu. Mungu yuko radhi kutekeleza hukumu, lakini anachukua hatua zisizo za kawaida kuwaokoa wadhambi. Mungu anataka kukuokoa? Je, utachukua uamuzi, sasa hivi, wa kumfanya Mungu kuwa Bwana na Mwokozi wako?
VI. Juma lijalo: Motisha na Maandalizi kwa Ajili ya Utume.