Somo la 6: Motisha na Maandalizi kwa Ajili ya Utume

Luka 24, Matendo 1 & 2
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
4
Lesson Number: 
6

Somo la 6: Motisha na Maandalizi kwa Ajili ya Utume

(Luka 24, Matendo 1 & 2)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Jambo gani linakupa motisha ya kupeleka injili kwa wengine? Nilikuwa na kawaida ya kujichunguza na kujifanyia tathmini kuhusu hamasa yangu ya kufundisha na kuhubiri. Je, nilipenda kuwa mtu wa kusimama mbele ya watu? Je, nilipenda pale watu waliponiambia kuwa nilifanya vizuri? Ndiyo, hilo lilinitia moyo. Wakati huo huo, nilipenda sana pale mtu aliponiambia kuwa alimkaribia Mungu zaidi kutokana na jambo nililolifundisha. Tukiuangalia ujumbe wa Biblia kwa uaminifu, tunaona kuwa Mungu anazingatia mambo tunayoyapendelea. Matokeo ya kutoa zaka ni mtu kupata fedha nyingi zaidi (Malaki 3:10-12). Mbingu imejaa dhahabu na yaspi (Ufunuo 21:18). Hadi pale Yesu alipowaacha wanafunzi ili kurejea mbinguni, walidhani watakuwa watawala wa kidunia (Matendo 1:6). Mungu anaelewa kujipenda kwetu, lakini anatutaka tukue na kufikia hamasa ya kuwapenda wengine (Marko 12:31). Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tutafakari motisha yetu na maandalizi kwa ajili ya kazi yetu ya injili!

I. Uzoefu Wetu

A. Soma Luka 24:1-3. Jambo gani liliwahamasisha wale waliotaka kuutia manukato mwili wa Yesu? (Upendo kwa Yesu. Hawakudhani kuwa hili lilikuwa jambo salama kulitenda. Hawakuhamasishwa na upendo wao binafsi.)

B. Soma Luka 24:4-5. Kwa nini malaika waliuliza swali hili badala ya kutangaza tu kwamba, “Yesu yu hai?” (Malaika walikuwa wanawafundisha wanawake. Tayari wanawake walikuwa wamebaini kuwa Yesu hakuwepo. Hii ilisababisha mkanganyiko (“waliingiwa na hofu”). Malaika walitaka wanawake walifanyie kazi tatizo hiki kimantiki.)

C. Soma Luka 24:6-8. Hapa msingi ni upi kwa fundisho la malaika? (Maneno ya Yesu akitabiri mustakabali wake.)

D. Soma Luka 24:9. Huu ni utume halisi – kupeleka habari njema za ufufuo wa Yesu. Ni nini uliokuwa msingi wa kauli hii? (Kwanza, wanawake walikuwa wamehamasika kutokana na upendo wa Yesu. Halafu, wanawake walikuwa na maswali ambayo hawakuweza kuyajibu. Tatu, malaika waliwafundisha wanawake majibu kwa njia ya mantiki na unabii. Walitaka wanawake wahitimishe kwamba ni kweli Yesu alikuwa hai. Mwisho, wanawake walikuwa na furaha kushiriki na wengine uzoefu wao kwa sababu lilikuwa jambo ambalo wengine wangependa kulijua.)

E. Soma Luka 24:10-11. Hii inatufundisha nini kuhusu ushiriki wetu kwenye utume? (Hata watu wema wanaweza kuukataa ujumbe wa utume.)

1. Je, wanafunzi wanakuwa na dhihaka? (Ndiyo, endapo walielezea hitimisho lao. Hii ni kinyume na “kisa kisichofaa.” Wanaume walipaswa kuwepo kaburini. Wao ndio hawakutumika ipasavyo/hawakuwa na kazi (idle).)

F. Soma Luka 24:12. Hii inamzungumziaje Petro? (Hakuwa mvivu! Alitaka kuthibitisha habari hizi njema.)

1. Jambo gani linamaanishwa kuhusu “vitambaa vya sanda?” (Vinaashiria mpangilio, badala ya uporaji. Mtu fulani alivikusanya vipande vya nguo pamoja.)

2. Kifungu kinasema kuwa Petro “akaenda zake akiyastaajabu yaliyotukia.” Badala yake Petro alipaswa kufanya nini? (Kuwaamini wanawake. Hii inaonesha kuwa tunapopeleka injili, baadhi ya watu watatukataa na baadhi watataka kuitafakari zaidi hiyo injili.)

G. Tafakari swali kuu. Ilikuwa na ugumu kiasi gani kwa wanawake kushiriki na wengine habari hizi? (Walipiga hatua ya kwanza kutokana na upendo. Kisha mbingu ikawaelekeza cha kufanya katika hatua zilizosalia kufanya ushuhudiaji. Hatua hizi zilijengwa juu ya uzoefu wao binafsi.)

H. Je, kujipenda kuna wajibu katika utume wa wanawake? (Kwa sehemu fulani. Walimpoteza Yesu. Walitaka kujisikia vizuri kuhusu upotevu huu. Huenda waliwaeleza wanaume kisa chao kwa sababu malaika waliwaendea kwanza.)

II. Mungu Anatoa Uthibitisho

A. Hebu turuke hadi chini na tusome Luka 24:36. Unawalinganishaje wanafunzi na wanawake? (Bado wanaume wengi wanaongea!)

B. Soma Luka 24:37. Kwa nini wadhani kuwa walikuwa wanaona “roho,” zimwi? Walikuwa wamedhamiria kutowaamini wanawake. Vifungu tulivyoviruka vinamwelezea Yesu akijidhihirisha kwa wanaume. Wale waliokuwa katika chumba pia hawakuamini maelezo ya wanaume.)

C. Soma Luka 24:38. Yesu anauliza swali zuri. Ungelijibuje?

D. Soma Luka 24:39-43. Yesu anakwenda mbali kiasi gani ili kuthibitisha kuwa yeye sio roho? (Yesu anawapatia uthibitisho kamili kuwa yu hai na kwamba yeye si roho.)

1. Hiyo inatufundisha nini kuhusu utume? (Yesu hataacha msingi wowote wa mashaka kama uko tayari kumpokea.)

E. Soma Luka 24:44-46. Yesu anatumia njia gani nyingine kuwashawishi wanafunzi? (Anawaonesha jinsi unabii wa Biblia unavyounga mkono kusulubiwa kwake na kufufuka kwake. Anawakumbusha kile alichowaambia kabla kuhusu mustakabali wa siku zijazo.)

1. Utazitumiaje zana hizi kupeleka injili?

F. Soma Luka 24:47-48. Baada ya uthibitisho huu, Yesu anawataka wanafunzi wafanye nini? (Yesu anawataka wawe mashahidi.)

1. Unadhani Yesu anawataka wafanye nini hasa anaposema kuwa wanapaswa kushuhudia? (Sehemu rahisi ni kuhusianisha kile walichokiona na kukisikia kutoka kwa Yesu. Nadhani pia Yesu anawataka walinganishe kile walichokiona na kukisikia kwenye unabii unaomhusu.)

2. Ni muhimu kiasi gani kushiriki msamaha wa dhambi katika jina la Yesu?

G. Mojawapo ya mada zetu ni motisha kwa ajili ya utume. Mwingiliano/mchangamano wa Yesu na wanafunzi unatufundisha nini kuhusu motisha? (Mungu anakwenda mbali zaidi kuwahamasisha wanafunzi kwa kuthibitisha kuwa yu hai. Yesu hatatuacha tukiwa na mashaka.)

H. Soma Luka 24:49. Je, kuwa na uelewa wa Yesu kutoka kwake moja kwa moja inatosha kuwa shahidi mahiri (effective)? (Hapana. Wanahitaji “uwezo utokao juu.”) 

III. Maandalizi

A. Soma Matendo 1:12-14. Kifungu kinasema kuwa walikuwa “wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali.” Jambo gani limebadilika? (Hawakudumu pamoja waliposikia kuwa Yesu alikuwa anajidhihirisha kwa baadhi yao. Sasa Yesu ametatua jambo hilo. Wanakubaliana kuwa Yesu amefufuka, yuko mbinguni, na wana kazi ya utume ya kuwaambia wengine.)

1. Unadhani mada ya maombi yao ni ipi?  (Rudi nyuma hadi Luka 24:49 na usome Matendo 1:8. Nadhani wanaomba kwa ajili ya “uwezo utokao juu.” Wanaomba kwa ajili ya Roho Mtakatifu.)

2. Litafakari kanisa lako. Ni mara ngapi mnakusanyika pamoja na kuomba kwa dhati kwa ajili ya uwezo wa Roho Mtakatifu?

3. Roho Mtakatifu alikuwa wa muhimu kiasi gani katika utume wao? (Yesu aliwaambia katika Luka 24:49 wasianze bila kuwa na Roho Mtakatifu.)

B. Soma Matendo 2:1-2 na Matendo 2:6. Je, unadhani wanafunzi walipiga kelele kama sehemu ya mpango wao?

C. Soma Matendo 2:3-5. Unadhani wanafunzi walidhani kuwa Pentekoste ilikuwa fursa ya pekee ya kupeleka injili kwa wengine?

1. Unadhani wanafunzi walidhani kuwa walipaswa kujaribu kujifunza lugha nyingine? (Nina mashaka kama jambo hili liliakisiwa kwenye mipango ya wanafunzi. Mungu alichukua mzigo wote.)

2. Mimi ni mtu ambaye ninapangilia mambo. Sijawahi kuona mpango wa kupeleka injili kwa watu katika kanisa langu mahalia ambao haukupangiliwa. Je, tunapaswa kuachana na mipango? Je, tunapaswa kuomba tu? (Nilipanga kuwa mwanasheria. Nilipanga kumfanyia Mungu kazi. Mungu amebariki mipango hiyo. Lakini ninahisi mafanikio yangu makubwa ni kuandika masomo haya ya Biblia na kuyaweka kwenye mtandao (intaneti) – jambo ambalo kamwe sikulipanga. Mungu alilipangilia.)

IV. Roho Mtakatifu

A. Soma Matendo 2:16-18. “Siku za mwisho” zilianza lini? (Wakati wa Pentekoste.)

1. Je, tunaishi katika siku za mwisho? (Ndiyo.)

2. Je, tutarajie Roho Mtakatifu atatutendea kama alivyowatendea wanafunzi? (Roho Mtakatifu, kama tulivyojadili, ndiye aliyepanga tukio hili na sio wanafunzi. Lakini Roho Mtakatifu anaahidiwa kuwa nasi leo kwa sababu tunaishi katika siku za mwisho.)

B. Rafiki, je, utamwomba Mungu akupatie motisha na moyo wa kujitoa kwa ajili ya kazi yako ya utume na kumtuma Roho Mtakatifu ili afanikishe kazi yako? Kwa nini usifanye hivyo sasa hivi?

V. Juma lijalo: Utume kwa Jirani Yangu.