Somo la 8: Utume kwa Wahitaji
Somo la 8: Utume kwa Wahitaji
(Luka 5, Yohana 5, Zaburi 146)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, unaweza kutofautisha kati ya mhitaji na tapeli? Nani wa kumsaidia halijawahi kuwa jambo rahisi kwangu. Hii leo, nchi ya Marekani inaonekana kupinduliwa juu-chini kwenye masuala ya msingi yaliyoibuliwa kwenye Biblia. Yakobo 2:15 inarejelea suala la kumsaidia mtu anayehitaji mavazi na chakula. Nchini Marekani matajiri, tofauti na maskini, ni wembamba. Watu wenye fedha nyingi wanavaa kana kwamba ni maskini. Kimsingi haya ni mambo ya jumla, lakini yanaakisi mabadiliko ikilinganishwa na nilipokuwa kijana mdogo. Tunazitumiaje kanuni za Kibiblia zisizo na ukomo katika zama za leo? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!
I. Mtu Mwenye Kupooza
A. Soma Luka 5:17-19. Unaona jambo gani lisilofaa katika kisa hiki? (Bila shaka kundi hili la watu linajumuisha kwa sehemu fulani watu wanaotaka kuponywa. Watu hawa wanaamua kutafuta njia fupi ya kufika mbele. Yesu anafundisha, watu hawa wanavuruga mafundisho yake. Mtu mwingine kabisa tofauti na watu hawa ndiye mmiliki wa nyumba ile. Wanatoboa nyumba ya mtu isiyo yao.)
B. Soma Luka 5:20. Miongoni mwa mambo yasiyo halali na yasiyo ya haki yanayofanywa na watu hawa, Yesu anaona jambo moja tu, imani yao. Kwa nini?
1. Je, hili ni fundisho kwetu? (Yesu anaonekana kulinganisha ubunifu wao wa kutafuta njia fupi wakiwa na dhamira ya kumsaidia rafiki yao. Wengine wanaweza kuwa wadadisi, lakini watu hawa wana imani na Yesu.)
2. Unadhani baadaye watu hawa walikarabati paa?
C. Angalia tena Luka 5:20. Je, ungesikitika kama ungekuwa mmojawapo wa watu waliomsaidia rafiki yao? (Ndiyo. Walikuja ili rafiki yao apate kuponywa.)
1. Kwa nini Yesu anatoa jibu la imani yao kwa kusema “umesamehewa dhambi zako?” (Yesu anaangalia kwa kina zaidi mahitaji yetu. Kuna uwezekano mkubwa kwamba mtu huyu alihisi kuwa amepooza kwa sababu alikuwa ametenda dhambi. Angalia Yohana 9:2.)
D. Soma Luka 5:21-23. Jibu la swali la Yesu ni lipi? (Ni rahisi kusema jambo lisiloweza kupimwa.)
E. Soma Luka 5:24-26. Unapokitafakari kisa hiki, ujumbe wa msingi ni upi? (Yesu ni Mungu. Anaweza kusamehe dhambi.)
1. Je, kipengele cha “kumsaidia rafiki yako mhitaji” kwenye kisa ni kitendo tu cha kubadili usikivu wa watu kwenye jambo? Nguzo ya ujumbe wa msingi? (Kwa nini Yesu anataka tuamini kuwa Yeye ni Mungu? Ni ili kutuokoa dhidi ya mauti ya milele. Kwa muktadha huo kisa hiki kina ujumbe usiobadilika – Mungu anatupenda.)
2. Mada yetu inahusu kuwasaidia wahitaji. Tunajifunza nini kutokana na kisa hiki? (Kipengele cha muhimu kabisa cha kuwasaidia wahitaji ni kuwafundisha habari za Yesu!)
3. Chukulia kwamba progamu ya kanisa, ili kuweza kupata ufadhili wa Serikali kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji, inatakiwa kutimiza vigezo vinavyoendana na sheria za serikali ya Marekani. Sheria hizo zinazuia kujaribu kuwaongoa wale wanaosaidiwa. Je, hilo litakuwa jambo lenye kufaa? Je, tunapaswa kuwasaidia wahitaji bila kuwapelekea injili? (Hii ni kinyume na kisa tulichojifunza hivi punde.)
II. Mtu Birikani
A. Soma Yohana 5:1-3. Watu wangapi walihitaji msaada? (“Jamii kubwa.”)
B. Soma Yohana 5:5-7. Mtu huyu anakabiliana na kikwazo gani katika lengo lake la kutaka kuponywa? (Watu wengine walimshinda na kumtangulia kuingia kwenye maji.)
1. Nimenunua kitabu kiitwacho, “Fast After 50,” kwa sehemu fulani kutokana na mjadala na mke wangu. Ninapoendesha baiskeli yangu ya mashindano yenye miguu mitatu huwa ninataka kuendesha kwa kasi ingawa ninazidi kuzeeka. Ananiambia kuwa ninapaswa kukubaliana na ukweli wa mambo kwa kupunguza mwendo kwa kadiri ninavyozidi kuzeeka. Unadhani mtu yule aliyekuwa birikani alikuwa na mtazamo gani baada ya miaka 38 ya kutoshinda pambano lile? (Alifahamu asingeweza kushinda pambano la kuingia birikani bila msaada.)
C. Hebu tujikite kwenye Yohana 5:6-7. Je, mtu huyu alijibu swali la Yesu? (Hapana. Badala yake, alielezea kwa nini hakuweza kuponywa kwa maji ya birika.)
1. Je, mtu huyu alionesha imani yoyote kwa Yesu?
D. Soma Yohana 5:8-9. Tunapaswa kujifunza nini kutokana na hili? (Watu wanaohitaji msaada wetu wanaweza kuwa na mawazo yasiyo sahihi ya kutafuta suluhisho. Wanaweza kujikita kwenye sababu za kwa nini hawawezi kuponywa (au kusaidiwa), badala ya kwenda moja kwa moja kwenye chanzo cha uponyaji na msaada.)
1. Hebu tumuingize Yakobo katika jambo hili. Yakobo 2:18 inasema kuwa atatuonesha imani yake kwa njia ya matendo yake. Je, Yakobo angeweza kukaa pembeni mwa mtu huyu na kumuingiza kwenye birika maji yalipotibuliwa? (Yakobo anasema jambo la msingi, lakini hazungumzii jambo la msingi zaidi. Jambo la msingi kabisa kuliko yote ni kuwa na imani kwenye uwezo wa Mungu.)
E. Soma Yohana 5:10. Viongozi wa Kiyahudi wana maswali kuhusu kisa hiki kama ambavyo nami nina maswali. Yohana 5:3 inasema kuwa jamii kubwa ya wagonjwa ilihitaji uponyaji. Kwa nini Yesu hakuwaponya wote? Ilikuwa ndani ya uwezo wake.
1. Kwa nini Yesu aliponya siku ya Sabato? Kwa nini Yesu alimwambia mtu yule kubeba godoro lake siku ya Sabato?
F. Soma Yohana 5:11-13. Yesu anatoa ujumbe gani? Alijitenga mbele ya mtu yule pale birikani hata hakujua utambulisho wa mponyaji wake!
G. Soma Yohana 5:14-15. Hii inajibu mojawapo ya maswali yetu. Baadaye, wakati hakuna kundi la watu, Yesu anamwambia mtu yule aliyekuwepo pale birikani kwamba yeye ni nani. Kwa nini Yesu anamwambia mtu yule asitende dhambi ili asije akapatwa na jambo “baya zaidi?”
1. Jambo gani linaweza kuwa baya zaidi kushinda kitendo cha mtu kuwa mgonjwa asiyejiweza kwa muda wa miaka 38? (Mauti ya milele.)
2. Hitimisho la mazungumzo haya ya kushangaza kati ya mtu yule na Yesu linajibu maswali yetu kadhaa ambayo yalikuwa hayajajibiwa. Je, sasa tunaona kwa nini Yesu alimponya mtu mmoja pekee? (Lengo halikuwa tu kuponya mwili wake, lengo lilikuwa kuponya roho yake. Ndio maana uwepo wa jamii kubwa ya wagonjwa haikuwa na maana yoyote kwenye lengo kuu la Yesu.)
3. Kwa nini Yesu aliikiuka Sabato mbele ya macho ya watu (akiwemo mtu aliyekuwepo pale birikani)? (Soma Yohana 5:17. Anachokimaanisha Yesu tangu mwanzo mwa kisa hiki ni kwamba Yeye ni Mungu. Hahitaji maji ya birika yatibuliwe ili aweze kuponya. Anasema kilicho sahihi kwake kukitenda siku ya Sabato.)
H. Kwa kuwa sasa tumeshamjadili mtu aliyepooza na yule aliyekuwepo birikani, jambo gani linapaswa kuwa lengo letu la msingi kwa kuwazingatia wahitaji? (Kuwaelekeza kwa Yesu. Lengo la msingi sio kuboresha hali yao ya kimwili. Kuwafanya wamjue Yesu ndilo lengo letu la msingi.)
III. Mgeni
A. Soma Mambo ya Walawi 23:22 na Zaburi 146:9. Vifungu vyote hivi viwili vinawarejelea “wageni.” Je, wageni ni akina nani? (Watu wanaosafiri na hawaishi katika eneo lako.)
B. Soma Kumbukumbu la Torati 10:18-19. Kitabu cha Kumbukumbu la Torati kinaweka kiwango cha juu kiasi gani linapokuja suala la kuwakarimu wageni? (Kinasema “wapende,” lakini Wamisri waliwafanya kuwa watumwa! Huu sio ulinganisho unaotia hamasa.)
C. Tunaposoma Zaburi 146:9 inatuambia kuwa “wasio haki” wataangamizwa. Soma Warumi 13:1-2. Je, wageni wasiotii “mamlaka” ni watu wasio haki? (Warumi inatuambia kuwa wasio haki “watajipatia hukumu.”)
D. Marekani (na Ulaya) inakabiliana na tatizo la kipekee na “wageni.” Ninafahamu kidogo tu kuhusu sheria ya wakimbizi nchini Marekani. Wageni wengi wanaokuja Marekani kupitia mpaka wa kusini hawana vigezo vya kuwa wakimbizi, wanatafuta tu maisha mazuri (na hili ni jambo linaloeleweka). Je, tunapaswa kuwasaidia ikiwa wanakiuka (na tunajua wanafanya hivyo) sheria za Marekani?
1. Je, kisa cha marafiki wa mtu mwenye kupooza wanaotoboa paa isivyo halali wanawaunga mkono wale wanaoingia nchini Marekani kinyume cha sheria?
E. Tafakari “taswira pana” ya somo letu juma hili. Je, kupooza kwa mtu yule au mtu aliyekuwa birikani ndio msingi wa visa hivyo? (Hapana. Ujumbe muhimu ulikuwa ni kufundisha injili – kwamba Yesu ni Mungu. Hakuna chochote kwenye Biblia kinachofundisha kuwa kukiuka sheria ni jambo linalofaa kwa sababu kuna mtu ambaye ni tajiri kuliko wewe.)
1. Kama lengo la kuwasaidia wahitaji ni kuitangaza injili, je, kwenda nchini Marekani ni njia ya kuwa kama Yesu? (Mgeni mtarajiwa anauliza swali lile kuhusu hali yao ya sasa. Kwa ujumla, ushawishi wa namna mbalimbali nchini Marekani hauutangazi Ufalme wa Mungu. Kuwa tajiri hakukufanyi kuwa mwenye haki zaidi.)
F. Rafiki, je, utatoa msaada wako kwa mhitaji kwa kufanya maombi ya dhati? Je, utadhamiria, kwa uongozi wa Roho Mtakatifu, kufanya suala la kuutangaza Ufalme wa Mungu kuwa lengo lako la msingi?
IV. Juma lijalo: Utume kwa Wenye Mamlaka.