Somo la 3: Uweza wa Yesu Aliyetukuzwa
Somo la 3: Uweza wa Yesu Aliyetukuzwa
(Waefeso 1 & 3)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Kwa miaka mingi nimekuwa nikiendesha magari ambayo niliyanunua kwa bei ya punguzo niliyoyapata wakati wa mojawapo wa matembezi yangu kwa ajili ya mazoezi. Magari haya yalikuwa ya thamani, lakini hayakuwa ya kuvutia sana, na hayakuwa na nguvu kiutendaji. Magari yangu ya sasa ni tofauti. Siku za nyuma nilipokabiliana na hali ya dharura barabarani, nilikuwa na machaguo mawili: ama nigeuze au nisimame. Hivi leo nina uchaguzi mwingine, kutumia nguvu zote na kuondosha gari kwenye mazingira hayo ya hali ya tahadhari. Wewe, msomaji wangu, una uchaguzi wa “nguvu ya kutoka kwenye matatizo” unapomkaribisha Roho Mtakatifu maishani mwako. Hebu tujifunze kuhusu jambo hili tunapokigeukia kitabu chetu cha Waefeso!
I. Nguvu na Sala
A. Soma Waefeso 1:13-15. Kuwa na Roho Mtakatifu maishani mwetu hutupatia nini? (Kitabu cha Waefeso kinabainisha sio tu uhakika wa urithi wetu (ikimaanisha mbingu na nchi mpya), bali pia tutakuwa na imani kamili kwa Yesu na upendo kwa Wakristo wengine.)
B. Soma Waefeso 1:16-17. Paulo anawaambia Waefeso kwamba ameisikia imani na upendo wao, na anawaombea. Ni jambo gani la kwanza analolitaja kuwahusu kwenye ombi lake? (Ana shukurani kwa kile ambacho Mungu anakitenda maishani mwao.)
1. Paulo anaomba baraka gani nyingine kwa ajili ya Waefeso? (Kwamba Roho Mtakatifu awapatie hekima na maarifa.)
2. Je, unawafahamu Wakristo wanaomjua sana Mungu lakini hawaonekani kuwa na busara sana? (Tunapojifunza zaidi habari za Mungu, tunahitaji kutafuta hekima ili kuendana na ufahamu huu.)
a. Hili ni ombi la Paulo kwa ajili ya Waefeso. Je, unaomba ombi kama hili kwa ajili yako? kwa ajili ya familia yako?
C. Soma Waefeso 1:18. Moyo wangu hauna macho. Kichwa changu kimeyashikilia macho yangu. Paulo anaweza kuwa anazungumzia jambo gani? (Maoni ya Alexander MacLaren yanamwonya “msomaji wa lugha ya Kiingereza” kuwa kifungu hiki hakirejelei “upendo” wetu. Hatuombwi kutazama kwa kutumia hisia zetu. Bali “moyo” unarejelea “maisha yote ya ndani.” Nafsi yako ya ndani, inayoongozwa na Roho Mtakatifu, inakuambia nini kuhusu hali hii?
1. Utaona kuwa kifungu hiki kinasihi kwamba tujue tumaini ambalo Mungu ametuitia. Unawezaje kulijua tumaini? Nafsi yako ya ndani inawezaje kulijua tumaini? (Tunatakiwa kupitia uzoefu wa tumaini hilo kwa kulifanya tumaini hilo kuwa letu. Tunatakiwa kuwa na hili tumaini.)
2. Utaona pia kwamba tumaini hili linahusisha “utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu.” Ni utajiri gani huu ambao wewe na mimi tunao ili kukuza tumaini letu? (Je, umewahi kuusikia msemo wa kale kwamba “fedha zina nguvu?” Hii inatuambia kuwa tunao utajiri katika kile ambacho Mungu ametupatia. Mungu ametupatia wokovu wetu katika Yesu. Pia tunao uwezo uliopo kwa ajili yetu kutoka kwa Roho Mtakatifu.)
D. Soma Waefeso 1:19. Ikiwa unaamini, nguvu kiasi gani ipo kwa ajili yako? (Nguvu hiyo ni kubwa sana kiasi kwamba haipimiki.)
1. Je, unakumbuka kwenye sehemu ya Utangulizi kwamba gari langu la sasa linanipatia uchaguzi mwingine – nguvu? Unaweza kuwa na uchaguzi huu maishani. Je, unaitumia?
E. Soma Waefeso 1:20. Watu wanapojadili magari yenye nguvu huwa wanalinganisha kiwango cha nguvu kinachotolewa na injini. Kuna sababu gani ya kulinganisha nguvu ulizopewa kwa njia ya Roho Mtakatifu? (Nguvu iliyomfufua Yesu. Nguvu iliyomketisha upande wa kuume wa Mungu.)
1. Nguvu ina manufaa gani ikiwa huitumii?
2. Je, umetafakari jinsi unavyoweza kutumia nguvu hii iliyopo kwa ajili yako?
F. Soma Waefeso 1:21-23. Je, tumevuka kutoka kwenye nguvu iliyopo kwa ajili yetu hadi kwenye nguvu ya Yesu? (Tumevuka na kuingia kwenye mjadala wa Yesu kuwa juu ya nguvu zote katika ulimwengu. Lakini utaona kwamba “kanisa” ni “mwili” na “ukamilifu” wa Yesu. Hiyo inamaanisha kuwa nguvu hii ipo kwenye mwili wa waamini.)
1. Kwa hiyo hii inafanyaje kazi? Kwenye gari unakanyaga tu mguu wako kwenye kichapuzi (accelerator) na tayari nguvu inakuwepo. Tunaidaije nguvu hii? (Mwongozo wa dhahiri ni kwamba nguvu yote ipo kwa Yesu. Nguvu inaonekana kufanyiwa kazi kwa njia ya kanisa. Tunatakiwa kutafuta kuyajua mapenzi ya Mungu kwa ajili ya nguvu yake na kufanyia kazi uwezo huu na waamini wenzetu.)
a. Baadhi yenu mnaweza kutoa changamoto kwenye dhana ya kwamba tunatakiwa kufanya kazi na waamini wenzetu. Huenda wanapungukiwa kiasi cha imani. Jibu kwa hilo ni lipi? (Waumini wenzetu ndio kipimo cha mipango yetu. Mara ngapi nimewasikiwa watu wakisema kuwa Roho Mtakatifu amewaambia watende jambo fulani wakati nina uhakika Roho Mtakatifu hakusema jambo kama hilo.)
II. Ombi na Madai ya Uwezo/Nguvu
A. Soma Waefeso 3:14-16. Ni jambo gani la kwanza tunaloambiwa kulitenda ili kuupata uwezo wa Yesu? (Tunapiga magoti na kuomba kupatiwa uwezo kwa njia ya Roho Mtakatifu.)
1. Inamaanisha nini kufanywa imara “utu wetu wa ndani?” (Suala la kwanza kabisa kiutendaji ni kukufanya kuwa imara kiroho.)
B. Katika Marko 9 tunaona kisa cha mvulana aliyepagawa pepo. Soma Marko 9:18-19. Kisha Yesu anamponya mvulana huyu. Soma Marko 9:28-29. Kisa hiki kinajihusishaje na mjadala wetu kuhusu utu wetu wa ndani na uwezo wa kiroho? (Wanafunzi hawakuwa na uwezo wa kutenda muujiza. Walipungukiwa imani na hawakuwa na uelewa wa kutumia nguvu ya maombi.)
1. Kila nikitafakari uwezo wote uliopo kwa ajili yetu, ninayafikiria mawazo makubwa – kutenda miujiza, kuwaongoa maelfu, kujenga kanisa kuushangaza ulimwengu wa kipagani kwa kutengeneza kitu kutokana na pasipo chochote. Je, unakubali kwamba nina mkokoteni kabla ya kuwa na farasi? (Suala la kwanza kiutendaji ni kujiimarisha kiroho.)
2. Hitimisho la awali linaendanaje na dhana ya haki kwa imani? (Mara nyingi Wakristo wanaiangalia haki kwa imani kama kuhalalisha kiasi kidogo cha juhudi kwa upande wetu. Tena ukizingatia kwamba, hatuwezi kujiokoa au kuishi maisha makamilifu. Hii inapoteza maana ya ukamilifu wa maisha ya Kikristo. Hii inapoteza maana ya nguvu iliyopo kwa ajili yetu.)
C. Soma Waefeso 3:17-18. Je, hii ni kazi ya kikundi? (Kwa mara nyingine tunaona rejea ya sisi kufanya kazi na waumini wenzetu ili kuielewa hii nguvu.)
D. Soma Waefeso 3:19. Hapa lengo la “utu wa ndani” (angalia kifungu cha 16) ni lipi? (“Kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu.”)
1. Mara kwa mara tunaambiwa na ulimwengu kuwa na upendo na tusiwe na chuki. Je, dunia inajua inachokizungumzia? (Kwa dhahiri sio kwa sababu kifungu hiki kinasema kuwa upendo wa Kristo hauelezeki kwa kipimo cha uelewa wa mwanadamu. Huu ni upendo unaotokana na uwezo wa Mungu ulioimarishwa kwenye utu wetu wa ndani.)
E. Soma Waefeso 3:20-21. Hapo awali nilipendekeza kuwa tunapaswa kutafakari jinsi tunavyoweza kutumia nguvu hii ya ajabu ya Mungu. Hii inatufundisha nini kuhusu mipango yetu mikubwa ya kutumia nguvu ya Mungu? (Mungu anatuwazia mambo makubwa zaidi.)
1. Je, hili limekutokea? Je, umemwomba Mungu jambo moja na akakupatia jambo kubwa zaidi? (Takriban miaka ishirini iliyopita nilifanya uamuzi kuwa ninataka kubadilisha mwelekeo wa maisha yangu kutoka kusimamia masuala ya kesi (litigation) hadi kufundisha. Mpango wangu ulikuwa kufundisha chuo katika mojawapo ya shule za kanisa. Mungu aliufanyia kazi mpango huo kiasi kwamba sasa ninafundisha kwenye shule ya sheria katika eneo la taaluma yangu. Ninapata fursa ya kufundisha kizazi kijacho cha wanasheria kutetea uhuru wa dini!)
F. Angalia tena Waefeso 3:21. Katika mipango yako yote mikubwa kwa ajili ya uwezo wako mkubwa kiroho, nani anayepaswa kutukuzwa? (Mungu na kanisa.)
1. Tunafikiria juu ya kumtukuza Mungu. Mara ngapi unafikiria juu ya kulitukuza kanisa?
G. Rafiki, je, utaomba ili Mungu akupatie nguvu? Nguvu ambayo ni zaidi ya kile unachoweza kukifikiria. Nguvu itakayokufanya uwe mwenye nguvu zaidi kiroho. Kwa nini usilifanye hilo kuwa lengo lako sasa hivi?
III. Juma lijalo: Jinsi Mungu anavyotuokoa.