Somo la 9: Amebarikiwa Yeye Ajaye kwa Jina la Bwana

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Zaburi 2, 22, 23, 80, 118, Yohana 10, na Waebrania 7
Swahili
Year: 
2024
Quarter: 
1
Lesson Number: 
9

Somo la 9: Amebarikiwa Yeye Ajaye kwa Jina la Bwana

(Zaburi 2, 22, 23, 80, 118, Yohana 10, na Waebrania 7)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kwa sasa ninasikiliza hoja adhimu ya C. S. Lewis kuhusu uwepo wa Mungu na Shetani. Paulo anatuambia katika Warumi 1 kwamba uwepo wa Mungu uko wazi sana kiasi kwamba “hatuna kisingizio” endapo hatumwamini. Uumbaji unamdhihirisha Mungu. Mantiki ya Yesu kama Mungu akija duniani na kufanyika mwanadamu kamili haiko wazi sana – isipokuwa kama tutaiangalia kwa umakini. Sehemu mojawapo ambayo tunatakiwa kuiangalia ni kile Biblia ilichokisema katika Zaburi zamani kabla Yesu hajaja duniani. Hilo ndilo somo letu juma hili. Tunaona ushahidi gani katika Zaburi kutuonesha kwamba ulikuwa mpango wa Mungu tangu awali kumtuma Yesu ili kutuokoa? Hebu tuzame kwenye somo letu na tujifunze zaidi!

I.  Asili ya Mungu Wetu

A.  Soma Zaburi 23:1-5. Je, hii inaendana na asili ya jumla ya wafalme na viongozi? (Hapana. Sio aina ya wafalme na viongozi wanaositawisha. Hawaandai meza au kujali kwa upekee faraja yetu. Kinyume chake ni kweli. Tunawaandalia meza viongozi wetu na faraja yao ndio jambo kubwa tunalolijali.)

B.  Soma Yohana 10:14-17. Je, wachungaji ni viongozi? (Wa kondoo.)

1.  Unadhani uongozi wa Yesu unaendana na ule wa mchungaji? (Maisha yake ni mfano wa jinsi ambavyo mchungaji achungaye kondoo wake atakavyoongoza.)

2.  Tulianza kwa Zaburi ya Mfalme Daudi ikimlinganisha Mungu na mchungaji. Kwa nini mtu ambaye alikuwa mfalme, na aliyeongoza kwa njia ya kawaida, amlinganishe Mungu wake na mchungaji? (Tunapaswa kuhitimisha mara moja kwamba kuna jambo la tofauti kabisa linapokuja suala la Mfalme wetu wa mbinguni na Mungu.)

C.  Soma Zaburi 80:1-3. Hapa tumesoma habari za “Mchungaji wa Israeli” “aketiye” juu ya makerubi. Kwa nini mfalme awe msimamizi wa makerubi?

1.  Kwa nini mchungaji wa mbinguni awarejeshe na kuwaokoa wanadamu? (Maneno yote ya vitendo yanaakisi kile ambacho Yesu alitutendea. “Uje utuokoe.” “Uturudishe.” “Nasi tutaokoka.” Hii inaleta mantiki leo kwa kuzingatia kile ambacho Yesu alitutendea.)

D.  Soma Mwanzo 46:32-34. Wamisri waliwachukuliaje wachungaji? (Maoni ya Keil & Delitzsh yanasema kwamba Wamisri waliwachukulia wachungaji kuwa ni mafidhuli na washenzi/wakatili. Kwa nini? Hii ni kwa sababu uchumi wa Misri kwa kiasi kikubwa unategemea kilimo. Mpangilio wa kupanda mazao tofauti na vurugu za wanyama wakizungukazunguka. Kwa upande mwingine, maoni ya Finis Dake yanabainisha kuwa baadhi ya “wachungaji wafalme” waliitawala Misri. Apepi, Farao wa Yusufu, alikuwa mmoja wao. Hawa wachungaji wafalme walikuwa wakandamizaji na Wamisri wa kawaida waliwachukia.)

II.  Mfalme Aliyetukanwa

A.  Soma Zaburi 22:6-8 na Zaburi 22:12-15. Je, hivi ndivyo utakavyomwelezea mtawala? (Soma Mathayo 27:39-44 na Yohana 19:34. Wakati inaonekana kwamba Mfalme Daudi anajizungumzia wakati akiwa kwenye matatizo, tunachokiona kwenye vitabu vya injili ni kwamba huu ni unabii wa kile kitakachomtokea Yesu. Angalia hasa kile inachokifafanua kuhusu kitakachomtokea Yesu.)

1.  Kama ungekuwa unamwelezea mfalme wako ajaye, je, ungezungumzia kuhusu udhaifu wake katika maisha yake? Au, je, utazungumzia mafanikio yake?

2.  Unadhani kwa nini viongozi wa Kiyahudi walishangazwa sana kwa namna ambayo Yesu Masihi alikuja?

B.  Soma Zaburi 118:19-23. Mada kuu ya vifungu hivi ni ipi? (Wokovu. Kuingia kwenye haki.)

1.  Rejea inayojirudiarudia ya “lango” inamaanisha nini? (Inamaanisha kuwa wenye haki wana lango maalumu la kuupata wokovu. Wale wasioingia kupitia langoni wanaenguliwa.)

2.  Jiwe kuu la pembeni ni kitu gani? (Jiwe kuu la pembeni ni msingi wa jengo kwa maana ya kwamba linaamua namna ambavyo jengo linakaa.)

a.  Kwa nini rejea ya jiwe kuu la pembeni lilete mantiki hapa? (Kama una lango, una aina fulani hivi ya jengo. Jiwe kuu la pembeni na lango vinahusiana.)

C.  Soma Matendo 4:11-12 na 1 Petro 2:6-7. Agano Jipya linaelezeaje juu ya uhusiano kati ya Yesu na jiwe kuu la pembeni lililokataliwa katika Zaburi 118:22? (Waandishi wa Agano Jipya wanalinganisha kukataliwa kwa Yesu na viongozi wa Kiyahudi na kukataliwa kwa msingi wa imani ya Kikristo.)

1.  Kama ungekuwepo wakati wa uandishi wa Zaburi 118:22, je, kungekuwa na mantiki yoyote kulinganisha kuingia kwako kwenye haki langoni na jiwe kuu la pembeni lililokataliwa? (Kwa mara nyingine, hili linaleta mantiki tu kwa kuzingatia habari za Yesu ajaye. Huu ni unabii unaounga mkono hoja yenye mantiki ya kwamba Yesu ni msingi wa wokovu wetu. Yeye ni lango ambalo kupitia kwake tunaingia.)

III.  Mfalme Mshindi

A.  Soma Zaburi 2:1-3. Jibu la swali lililoulizwa kwenye kifungu cha kwanza ni lipi? (Kifungu cha tatu kinatuambia kuwa nia yao ni kuondoa vifungo na kamba.)

1.  Je, uasi ni dhidi ya Bwana pekee? (Hapana. Kifungu cha 2 kinatuambia kuwa pia ni kinyume na “masihi wake.” Uasi pia ni dhidi ya mtu.)

2.  Je, waasi watashinda? (Kifungu cha kwanza kinatuambia kuwa wanafanya ghasia na kupanga “ubatili.”)

3.  Una maoni gani juu ya mtazamo wa uasi kwamba “vifungo” na “kamba” za Mungu vina madhara? (Tumejadili katika masomo yaliyopita ya Zaburi jinsi utii kwa Mungu unavyotupatia amani na ulinzi.)

B.  Soma Zaburi 2:4-6. Kwa nini Mungu anawacheka waasi? (Kwa sababu atamsimika Mfalme wake Yerusalemu.)

C.  Soma Zaburi 2:7-8. Ni Mfalme gani huyu ambaye Mungu atamsimika Yerusalemu? (Mwanaye!)

1.  Hebu subiri kidogo. Je, hii italeta mantiki kwa mtu aliyeishi nyakati za Daudi? Je, hii itaeleweka kuwa ni Mfalme Daudi? Unawezaje kuwa “Mwana” kwa Mungu? (Soma 2 Samweli 7:13-16. Kifungu hiki katika Samweli wa Pili kwa dhahiri kinafungamanisha dhana hii na Mfalme Daudi.)

a.  Utaona kwamba 2 Samweli 7:16 inarejelea kiti cha Daudi “kufanywa imara milele.” Je, hilo bado ni kweli? (Uzao wa Mfalme Daudi hapa duniani uliisha miaka mingi sana iliyopita.)

D.  Angalia tena Zaburi 2:7. Kwa kuwa Yesu ni Mungu, je, anaweza kuwa wa “pekee?” Je, hiyo inathibitisha kuwa kifungu hiki kinamhusu Daudi na si Yesu? (Soma Waebrania 1:5-8. Yesu alipozaliwa na Mariamu, alikuwa wa “pekee.” Waebrania inatuambia kuwa “Mwana” huyu ni “Mungu.”)

E.  Soma Matendo 13:33-34. Vifungu hivi vinawekaje jambo hili pamoja ili kuthibitisha kuwa Zaburi 2 inamrejelea Yesu?

F.  Soma Zaburi 2:9-12. Tunaambiwa “Kumbusu Mwana.” Unalielewaje hilo? (Tuna upendo kwa Yesu. Alikufa ili tuweze kuishi. Yeye ni Mchungaji wetu. Na kifungu cha 9 kinasema Yesu ni mchungaji hatari sana. Kwa sababu hiyo kifungu cha 11 kinasema “tushangilie kwa kutetemeka.”

1.  Unaelezeaje “kushangilia kwa kutetemeka” kwa lugha ya leo? (Tuna bahati kwamba yule Mtu wa Kutisha yuko upande wetu! Yule anayekupenda upeo (unambusu), ndiye anayewafanya maadui wake watetemeke.)

G.  Hebu tubadili uelekeo na tujadili unabii mwingine mkubwa kumhusu Yesu. Soma Zaburi 110:2-6. Kauli hii kuhusu Mfalme ajaye inasema kuwa Yeye pia ni kuhani “kwa mfano wa Melkizedeki.” Je, wafalme wa Israeli pia walikuwa makuhani? (Hapana. Kamwe haikuwahi kutokea)

H.  Soma Waebrania 7:14-17. Je, makuhani wa Israeli walitokana na Yuda? (Kifungu hiki kinasema, “Hapana.” Hilo linaonekana kutomjumuisha Yesu kuwa kuhani.)

1.  Waebrania inapatanishaje tatizo la dhahiri la ukoo wa Yesu na unabii wa kwamba atakuwa Mfalme-Kuhani kwa mfano wa Melkizedeki? (Hii inasema kuwa madai ya Yesu yamejengwa juu ya “nguvu za uzima usio na kikomo,” sio ukoo.)

2.  Soma Waebrania 7:3. Uzao wa Melkizedeki ni upi? (Hana ukoo.)

3.  Kwa nini kitabu cha Mwanzo kinatutambulisha kwa siri Mfalme-Kuhani? (Hili lilimtarajia Yesu kuja kama Mfalme wetu na Kuhani wetu Mkuu. Ni sehemu ya uthibitisho kwamba Yesu ndiye Masihi aliyetabiriwa.)

I.  Rafiki, baada ya uthibitisho huu je, utamkiri Yesu kama Masihi na Mwokozi wako? Je, utamkiri kama Mfalme na Kuhani wako Mkuu? Kwa nini usifanye hivyo sasa hivi?

IV.  Juma lijalo: Mafundisho ya Wakati Uliopita.