Somo la 2: Msingi wa Kitabu cha Mwanzo

Mwanzo 2-4 & 22
Swahili
Year: 
2025
Quarter: 
2
Lesson Number: 
2

Somo la 2: Msingi wa Kitabu cha Mwanzo

(Mwanzo 2-4 & 22)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2025, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kamwe hakuna kilichowahi kufa. Mungu alipowaonya Adamu na Eva katika kitabu cha Mwanzo kwamba watakufa ikiwa watakula kutoka katika mti fulani, je, walikielewa kifo? Wangewezaje kukielewa? Kilichokaribiana kabisa na kukielewa kifo ni uelewa wa jinsi kifo cha kondoo kinavyohusiana na tatizo letu la dhambi. Nadharia iliyopo kwenye mjadala wetu wa Biblia juma hili ni kwamba maana ya kifo na kondoo inakua kadiri tunavyofuata maendeleo yao kwenye Biblia. Si tu kwamba uelewa unakua, bali kamwe hauachi kuhusiana na maana za kale za Kibiblia. Linaonekana kuwa jambo tata kidogo eeh? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kukielewa kuhusu mapenzi ya Mungu!

  1.    Kifo
    1.    Soma Mwanzo 2:8-9. Mungu alitengeneza bustani katika Edeni ambapo alimweka mwanadamu aliyemuumba. Kwa nini Mungu anapanda mti wa kifo mahali hapo – “mti wa ujuzi wa mema na mabaya?” (Hapo awali tulijadiliana kuwa haya yalikuwa ni makubaliano ya pambano kati ya Yesu na Shetani, kama ilivyo kwenye makubaliano ya pambano juu ya Ayubu yanayopatikana katika kitabu cha Ayubu sura ya 1.)
    1.    Soma Mwanzo 2:15-17. Adamu alijua kuwa palikuwepo na Mti wa Uzima na Mti wa Ujuzi wa Mema na Mabaya. Kama angekula kutoka katika mti wa pili, angekufa. Unadhani Adamu alielewaje tofauti iliyopo kati ya kifo na uzima? (Adamu alielewa kwamba alitakiwa kula kutoka katika Mti wa Uzima ili aendelee kuishi. Unadhani alifikiri kuwa endapo angekula kutoka katika Mti wa Mauti angeanza kufa taratibu – kama vile kupatwa na ugonjwa usiotibika? (Neno la Kiebrania (yom) linalomaanisha “siku” utakufa hakika (kifungu cha 17) linaweza kueleweka kama kipindi fulani cha muda. Inawezekana alidhani ni jambo lililo na mwendelezo, kama vile kula kutoka katika Mti wa Uzima.))
    1.    Soma Mwanzo 3:2-7. Je, hii inaimarisha dhana ya kifo cha taratibu? (Ndiyo. Hawakufa mara moja (ghafla).)
    1.    Soma Mwanzo 3:24. Hii inaashiria nini kuhusu kifo cha papo hapo?
    1.    Soma Mwanzo 4:1-5. Kama ungekuwa Kaini, je, ungekasirika? Je, huu ni ubaguzi dhidi ya taaluma ya Kaini? Je, hii haina mantiki? (Isipokuwa kama Kaini alielewa suala kuu lililopo, jambo hili lingeonekana kutokuwa na mantiki.)
    1.    Soma Mwanzo 4:6-8. Elezea kwa nini Kaini alimuua Habili? Kwa nini asijaribu kumshambulia Mungu kwa kanuni yake isiyo na mantiki?
    1.    Hebu turejee nyuma na tusome tena Mwanzo 4:1.  Unadhani Eva alikuwa na matumaini gani kwa Kaini, mzaliwa wake wa kwanza? (Kama alielewa kwa ujumla mpango wa wokovu, angeweza kudhani kuwa alikuwa mwokozi ajaye.)
      1.    Sasa Adamu na Eva wanaelewa nini kuhusu kifo baada ya mauaji ya Habili? (Kwanza, ni jambo la kutisha kabisa. Kinasitisha mipango na njozi. Pili, kinaweza kuwa cha ghafla sana.)
  1.   Wale Wanaokisaidia Kifo
    1.    Soma tena Mwanzo 3:4-5. Wakati walipotenda dhambi, Adamu na Eva walifikiria nini kuhusu Shetani? Alikuwa na wajibu gani katika dunia yao?
    1.    Soma Mwanzo 3:12-13. Je, Adamu na Eva wanawajibika binafsi kwa dhambi yao? Au wanamtuhumu nyoka na Mungu?
    1.    Soma tena Mwanzo 4:8. Unadhani Adamu na Eva wanamlaumu nani kwa kifo cha mzaliwa wao wa kwanza? (Wazazi makini watasema, “Ningefanya nini kwa vizuri zaidi ili kuepuka matokeo haya kwa mwanangu?”)
    1.    Soma Mwanzo 4:10-14. Unadhani Adamu na Eva walikuwa na mwitiko gani kwa jambo hili? (Tunaona kwamba Kaini alifuata nyayo za taaluma ya baba wake. Sasa Kaini amepoteza taaluma yake, na Adamu na Eva wamewapoteza watoto wao wote wawili!)
      1.    Kama ungewauliza Adamu na Eva kuhusu tafsiri yao ya kifo, unadhani wangesema nini? (Kifo si tu upotevu wa uhai. Ni upotevu wa vitu vingi chanya vinavyohusiana na uhai.)
  1.      Mwana-kondoo
    1.    Soma Mwanzo 22:1-2. Utaona kwamba hii inaelezea kuwa Mungu “alimjaribu” Ibrahimu. Kama ungekuwa Ibrahimu, ungelichukulia hili kuwa jaribu la namna gani? (Lingekuwa jaribu la endapo nimezielewa kanuni za Mungu, na mbili kati ya kanuni hizo ni kwamba hukuwaua watoto wako au kuwatoa kama kafara.)
      1.    Soma Mambo ya Walawi 18:21, Mambo ya Walawi 20:3, na Kumbukumbu la Torati 12:31. Je, kuna namna ya kupatanisha vifungu hivi na amri ya Mungu kwa Ibrahimu?
      1.    Soma Mwanzo 21:12. Vipi kuhusu ahadi hii? Inaendanaje na jaribu hili?
    1.    Soma Mwanzo 22:3. Kwa dhahiri, Ibrahimu hakuliangalia jambo hili kama ninavyoliona. Kwa nini Ibrahimu aliondoka “alfajiri” kwenda kutekeleza jambo hili la kutisha? (Ubashiri wangu ni kwamba hakutaka kujadiliana suala hili na mkewe. Inaonesha Ibrahimu alikuwa anatii haraka.)
    1.    Soma Mwanzo 22:4-5. Tunatakiwa kuona kama tunaweza kutatua jambo hili. Sasa tunamwona Ibrahimu kwa dhahiri akiwadanganya vijana wawili kwamba atarudi na Isaka. Siko tayari kukubali kwamba Ibrahimu alikuwa radhi kuua na kudanganya. Jambo gani linaendelea mawazoni mwake? (Jibu lipo kwenye Biblia. Soma Waebrania 11:17-19. Ibrahimu aliamini kuwa kama Mungu alimwamuru atende jambo hili, basi Mungu angemfufua Isaka kutoka katika mauti!)
      1.    Hii inatufundisha nini kuhusu uelewa wa Kibiblia wa kifo?
    1.    Soma Mwanzo 22:7. Kwa nini Isaka hakugundua tatizo hili siku tatu zilizopita? (Hili ni jambo lililoachwa kwa dhahiri ambalo ninadhani Mungu alimfanya asiligundue mapema.)
    1.    Soma Mwanzo 22:8. Hebu subiri kidogo. Je, jibu hili linaendana na kauli iliyopo katika kitabu cha Waebrania kwamba Mungu atamfufua Isaka?
      1.    Soma Yohana 1:29. Je, Ibrahimu analirejelea hili? Kwamba Yesu atatufufua?
    1.    Soma Mwanzo 22:9. Kwa hiyari yake mwenyewe Isaka alilala madhabahuni. Unadhani mazungumzo ya namna gani yaliendelea kati ya Ibrahimu na Isaka?
      1.    Kumbuka kwamba hapo kabla Ibrahimu alimwambia Isaka kuwa Mungu atajipatia mwana-kondoo. Hadi kufikia hapa hilo linaonekana kuwa si kweli.
      1.    Unadhani kuwa Ibrahimu alielezea wazo lake kwa Isaka kwamba Mungu atamfufua?
      1.    Kama ungekuwa Isaka, je, ungekubaliana na jambo hili?
    1.    Awali katika sehemu hii, nilikufanya usome vifungu vya Biblia vilivyoonekana kukinzana moja kwa moja na kile ambacho Mungu alimwelekeza Ibrahimu kukitenda. Umesoma ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu ambayo pia ilikinzana na kile ambacho Ibrahimu aliambiwa kukifanya. Je, suluhisho lililopo katika Waebrania 11:19 linatatua mgongano wote?
    1.    Soma Mwanzo 22:10-12. Kwa nini Mungu alilitenda hili? Je, kweli hili ni jaribu kwa imani ya Ibrahimu? Au ni kielelezo zaidi cha imani tunayopaswa kuwa nayo kwa Mungu? (Kwa dhahiri hili ni jaribu la imani ya Ibrahimu. Fundisho kuu ni kile ambacho Mungu yuko radhi kututendea. Alimtoa Mwanaye kama kafara kwa ajili yetu.)
    1.    Soma Mwanzo 22:13-14. Una maoni gani kuhusiana na jambo hili likithibitisha kile ambacho Ibrahimu alimwambia Isaka katika Mwanzo 22:8 – kwamba Mungu atajipatia? (Matokeo yake ni kwamba jambo hilo lilitokea kuwa la kweli! Ibrahimu hakukiuka amri za Mungu, na alisema ukweli.)
    1.    Kisa hiki ni kigumu kwetu kukitafakari. Inaonekana kwamba Mungu alikiuka amri zake na ahadi yake. Ibrahimu hakudhani kuwa Mungu angejipatia mwana-kondoo, kama Isaka alikuwa mwana-kondoo. Licha ya hayo hatimaye mambo yote yalitatuliwa vizuri! Tunapata mafundisho gani tunayopaswa kujifunza kuhusu kifo na mwana-kondoo? (Kifo ni uhalisia wa kutisha wenye uchungu mkubwa unaoumiza. Suluhisho la kweli, kifo cha Yesu Mwana-kondoo, ni uhalisia wa kutisha kwa Mungu. Habari njema ni kwamba hatimaye Mungu anashughulika na mambo yote hayo!)

 

    1.    Rafiki, je, umetafakari jinsi dhambi zako zilivyomsababisha Mungu kuteseka? Je, ungependa kuwa kwenye nafasi ya Ibrahimu (au Isaka)? Usipuuzie kafara kuu ya Mungu kwa ajili yako. Fanya uamuzi leo, sasa hivi, kwamba utaipokea kafara iliyotolewa kwa ajili yako kwa gharama kubwa kabisa.
  1.   Juma lijalo: Taswira Kutoka Katika Ndoa.