Somo la 5: Mataifa: Sehemu ya 2
Somo la 5: Mataifa: Sehemu ya 2
(Mwanzo 2-3, Danieli 2 & 7)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2025, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Ukiulizwa, “Una uthibitisho gani kwamba Mungu yupo,” utajibu nini? Jambo moja ambalo ungeweza kulibainisha ni kwamba unabii wa kale umetimia. Jambo gani litahitajika kwa hilo kutokea? Utamhitaji si tu Mungu (Supreme Being), bali Yule anaoufahamu mustakabali unaokuja. Je, hiyo inamaanisha kuwa Mungu pia anaudhibiti mustakabali (future)? Ikiwa Mungu anawadhibiti wafalme na falme, hiyo itajumuisha uthibitisho zaidi wa uwepo wa Mungu na uwezo wake. Hiyo inaibua swali jingine, “Ikiwa Mungu anawadhibiti wafalme na falme, kwa nini tunao wafalme waovu na falme ovu?” Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!
- Sehemu Ovu ya Maarifa
-
- Soma Mwanzo 2:15-17. Kama ungelikuwa Adamu, ungelielewaje onyo hili? Je, ungedhani kuwa tunda la mti huo lilikuwa na sumu? Au ungedhani kuwa maarifa yalikuwa ya hatari? Au ungedhani kuwa chanzo kingine cha kifo kilikuwa kimebebwa ndani ya amri hiyo?
-
- Soma Mwanzo 3:3-6. Hawa alionekana kudhani kuwa kuligusa tu tunda kungesababisha kifo. Nyoka alielezeaje maarifa ya uovu? (Kuujua uovu ilikuwa jambo zuri. Ni jambo ambalo miungu ingeujua.)
-
-
- Ukisoma sura yote ya Mwanzo 3 utaona kwamba maisha yanabadilika haraka na si kwa uzuri kwa Adamu na Hawa kwa sababu walikula tunda la mti uliokatazwa. Hivi karibuni tulijifunza kuwa mambo yalikuwa mabaya zaidi pale kifungua mimba wao alipomuua kijana wao wa pili. Je, ni jambo zuri kuujua uovu?
-
-
-
- Kwenye utangulizi niliuliza kwa nini, ikiwa Mungu ndiye aliyeshikilia usukani, tunao wafalme waovu na falme ovu? Sasa mjadala wetu unaashiria kuwa jibu ni lipi? (Wanadamu wanayachagua mazingira yanayowazunguka kwa sehemu kubwa. Sisi ndio tuliowaweka madarakani wafalme waovu na falme ovu.)
-
-
-
- Je, tunapaswa kuepuka kujifunza kuhusu uovu? (“Ndiyo,” ndilo litakalokuwa jibu sahihi kutokana na kosa la Hawa.)
-
-
- Angalia tena Mwanzo 3:6 ambapo Hawa anatafakari kuwa kuujua uovu ni sawa na kuwa “mwerevu.” Je, kuna ukweli wowote katika hilo? Je, mara kwa mara unakuwa makini na uovu unapoingia katika mazingira yenye uwezekano mkubwa wa kuwa hatarishi? (Nilikuwa na tabia ya kukaa mgahawani mahali ambapo ninaweza kuuona mlango. Kukaa hotelini katika sakafu za ghorofa ambazo zinafikika kwa urahisi na ngazi za kutokea moto unapoibuka. Kuwatupia jicho madereva hatarishi ninapokuwa ninaendesha gari.)
-
-
- Je, unaona tatizo lolote kwenye majibu yangu? (Inaonekana ninajitumainia mwenyewe badala ya kumtumaini Mungu. Sehemu mbaya kuliko zote katika jambo hili ni kudhani kuwa watu wengine wanapanga uovu juu yangu.)
-
- Kuzifagilia Mbali Falme
-
- Soma Danieli 2:1-4. Mfalme anasema kuwa “roho yake ilifadhaika” kuhusiana na ndoto. Unadhani nani alifadhaisha “roho yake?” (Angalia Warumi 8:16: Roho Mtakatifu.)
-
- Soma Danieli 2:5-6. Je, mfalme ni meneja mbaya? Kwa nini awaambie washauri wake kuwa atawakata “vipande vipande” kama wasingeielezea ndoto kwanza na pili, kuitafsiri? (Soma Danieli 2:9. Mfalme Nebukadreza aliamini kuwa ndoto yake ilikuwa ya muhimu, na hakuwaamini washauri wake. Alidhani kuwa kama wangeweza kuielezea upya ndoto yake angeweza kulitegemea jibu lao kwa kile inachomaanisha.)
-
- Soma Danieli 2:17-19. Nani anayejua jibu la ndoto ya mfalme? (Mungu.)
-
- Soma Danieli 2:26-30. Kimsingi, Mungu yu nyuma ya ndoto na tafsiri ya Danieli ya ndoto hiyo. Kwa nini Mungu alimpa ndoto Mfalme Nebukadreza? Je, hii ni kukuza taaluma ya Danieli tu? Au kipimo cha imani yake?
-
-
- Kwa nini Mungu amwamini mfalme mwovu kwa kumpa ndoto hii? Mtu ambaye anawatishia waajiriwa wake kwamba atawatesa badala ya kupoteza kazi zao tu?
-
-
- Soma Danieli 2:31-36. Kama unafahamu lolote kuhusu unabii huu, je kuna falme zozote zinazoifanya sanamu hii kubwa kuwa falme za kimungu? (Hazipo. Uelewa wa jumla wa wanafunzi wa Biblia ni kwamba falme hizo ni Babeli, Uajemi (Medo-Persia), Uyunani, na Rumi.)
-
-
- Je, unadhani kwamba Mungu aliwachagua wafalme hao na falme hizo?
-
-
-
- Angalia Danieli 2:44. Kifungu hiki kinasema kuwa Mungu “aliusimamisha” ufalme huu. Je, hiyo inamaanisha kuwa hakuzisimamisha falme zilizotangulia?
-
-
-
- Falme zote zinazowatawala watu wa Mungu zimeshindwa na Babeli (ikimaanisha kushindwa kulikosababisha Danieli apelekwe Babeli), pia zina uwezo juu ya Israeli. Tunapaswa kuhitimisha nini kutokana na hilo? (Hii inarejea nyuma zaidi hadi kwenye 1 Samweli 8 ambapo watu wanataka kutawaliwa na Mfalme. Ingawa baadhi ya wafalme wa Israeli na Yuda walifanya kazi na Mungu katika kutawala, serikali kamili ya kikasisi haitaibuka hadi Danieli 2:44.)
-
- Mwisho wa Falme
-
- Soma Danieli 7:1-3. Hii ni ndoto au maono ya nani? (Hii ni ndoto ya Danieli. Hatafsiri ndoto ya mtu mwingine.)
-
-
- Unadhani “pepo za mbinguni” zinawakilisha nini? (Soma Ufunuo 7:1. Hii inarejelea “pepo za nchi” na malaika wakiwazuia. Hiyo inanifanya nitafakari kuwa “pepo za mbinguni” ni nguvu kutoka mbinguni.)
-
-
-
- Unadhani “bahari” inawakilisha nini? (Soma Danieli 7:15-17. Baadaye Danieli aliambiwa kuwa hawa ni wafalme ambao “watatokea duniani.”)
-
-
-
-
- Unaelezeaje kwamba wanyama hawa wanaweza kutokea katika maeneo yote mawili, yaani, baharini na duniani? (Baadhi ya maoni yanaiangalia “bahari” ikirejelea mataifa ya kipagani. Kinachomaanishwa ni kwamba falme nne zinaibuka duniani ambazo hazimtii Mungu.)
-
-
-
- Soma Danieli 7:4-6. Unadhani wanyama hawa watatu wanawakilisha nini? (Maoni mengi niliyoyapitia yanadhani kuwa hii inaendana na Danieli 2. Kwa hiyo, wanyama hao ni Babeli, Uajemi, na Uyunani.)
-
-
- Kwa nini Mungu anarudia unabii ule ule? (Kwa nini unarudia rudia mambo? Ili msikilizaji aelewe kwamba ni jambo la muhimu.)
-
-
-
- Ni kitu gani hasa unachokiona ambacho ni muhimu kwa unabii huu? (Tafakari kwamba watu wa Mungu walikuwa mateka. Hilo lingeweza kuwafanya kuhitimisha kuwa Mungu wao hakuwa na uwezo. Hakuwa msimamizi. Kimsingi, Mungu wao alibainisha falme zijazo kwa maelfu ya miaka. Na alibainisha tabia ya falme hizo.)
-
- Ufalme wa Milele
-
- Katika Danieli 7:19 Danieli anamtazama mnyama wa nne kwa upekee, mnyama anayewafuatia wanyama watatu ambao tumewajadili hivi punde. Tofauti na ilivyokuwa kwa Danieli, hatutamwangalia kwa kina mnyama wa nne sasa hivi, badala yake tutasonga mbele na kusoma Danieli 7:21-22, na kisha tutasoma Danieli 7:26-27. Kisha vilinganishe na Danieli 2:44-45. Hitimisho la kawaida la ndoto ya Nebukadreza na ndoto ya Danieli ni ipi? (Mungu anashinda!)
-
- Hebu tuangalie taarifa za kina zaidi. Soma Danieli 7:9-12. Jambo gani la pekee ambalo ufalme wa mwisho na wa milele unalitenda kwa falme zilizotangulia? (Unazihukumu.)
-
-
- Angalia rejea zote za moto kwa kuzihusianisha na Mungu. Kwa nini pawepo na moto wote huu mbinguni? (Kumbuka wakati hili lilipokuwa linaandikwa. Moto ni nguvu. Ni nishati.)
-
-
-
- Je, unaona mwelekeo kwenye unabii huu? (Samweli alikuwa mwamuzi akifanya kazi kwa niaba ya Mungu. Nafasi yake ilichukuliwa na wafalme. Lakini hatimaye wafalme wanahukumiwa na Mungu.)
-
-
- Soma Danieli 2:43-45. Jiwe ambalo halikuchongwa kwa mkono wa mwanadamu linaangamiza falme zote zilizotangulia. Hii inamaanisha nini kwako? (Uwezo wa Mungu unazishinda falme zote zilizotangulia ambazo ziliwazuia watu wa Mungu.)
-
- Soma Isaya 2:1-3 na uilinganishe na Danieli 2:45. Zingatia rejea ya “mlima” katika vifungu vyote viwili. Unadhani hiyo inamaanisha nini? (Isaya anauita “mlima wa nyumba ya Bwana.” Mungu yuko juu na anatukuzwa. Jiwe moja tu lililochongwa kutoka kwenye mlima ule linaangamiza falme zote za kibinadamu.)
-
- Rafiki, je, unataka kuwa sehemu ya Ufalme wa Mungu? Mungu anayetabiri historia ya dunia, na kisha anatuambia kuwa Yeye na wale wanaomfuata wanashinda. Kwa nini usichague upande wa ushindi sasa hivi?
- Juma lijalo: Kuielewa Kafara.