Somo la 8: Katika Zaburi : Sehemu ya 1

Waebrania 9, Yeremia 4, Zaburi 5, 15, 24 & 47
Swahili
Year: 
2025
Quarter: 
2
Lesson Number: 
8

Somo la 8: Katika Zaburi : Sehemu ya 1

(Waebrania 9, Yeremia 4, Zaburi 5, 15, 24 & 47)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2025, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Yerusalemu na hekalu lake la pili vilipoangamizwa na Warumi mwaka 70 B.K., je, huo ulikuwa mwisho wa umuhimu wake? Je, kuibuka upya kwa chuki dhidi ya Wayahudi kunakoendelea sasa kuna umuhimu wowote na siku za mwisho? Mwendelezo wa mashambulizi dhidi ya Wayahudi unaashiria kuwa bado Shetani anaendelea kuamini kuwa Wayahudi bado ni wa muhimu katika pambano lake dhidi ya Mungu. Kitabu cha Zaburi kina rejea nyingi za hekalu na matukio yanayohusiana na unabii wa nyakati za mwisho. Kitabu cha Waebrania kimejikita kwenye umuhimu wa kinabii wa mfumo wa kafara. Hebu tuzame kwenye somo letu la Waebrania na Zaburi na uone jinsi vinavyohusiana na unabii wa nyakati za mwisho!

  1.    Mpango wa Kihistoria
    1.    Soma Waebrania 9:6-7. Je, umetambua kile ambacho mwandishi wa kitabu cha Waebrania anaandika kukihusu? (Huduma za kihistoria za kila siku na kila mwaka katika hekalu la Yerusalemu.)
    1.    Soma Waebrania 9:8-10. Unadhani rejea ya ”ingali ikisimama” inamaanisha nini? (Nadhani hii inarejelea uangamivu wa hekalu. Wakati wa kifo cha Yesu msalabani, Mathayo 27:51 inatuambia kuwa pazia lililotenganisha vyumba viwili vya hekalu “lilipasuka vipande viwili toka juu hata chini.” Tukio hilo lilifungua njia kati ya vyumba hivi viwili. Lakini hili linaonekana kurejelea jambo la kuvutia zaidi, uangamivu halisi wa hekalu. Hilo lilitokea mwaka 70 B.K.)
    1.    Soma Waebrania 9:11-12. “Hema kamilifu zaidi” isiyotoka kwa mwanadamu ni kitu gani? (Lazima hii itakuwa inarejelea hekalu la mbinguni ambapo Yesu alikuja baada ya kusulubiwa kwake.)
      1.    Kuhani mkuu ni nani? (Yesu.)
      1.    Hebu tuchunguze msingi wa hoja uliotolewa na mwandishi wa kitabu cha Waebrania. Kwanza anarejelea mfumo wa kafara wa Agano la Kale. Kisha anarejelea mwisho wake wa kiroho na kiuhalisia kwa kuangamia kwa hekalu. Halafu anatuambia kuwa version mpya na iliyoboreshwa ya mfumo huu ipo mbinguni pamoja na Yesu.)
    1.    Soma Waebrania 9:13-15. Hii inaashiria kuwa Yesu anafanya nini mbinguni? (Kifungu cha 15 kinatuambia kuwa “mauti yamefanyika ili kutukomboa” kutoka katika dhambi zetu. Yesu ni vyote viwili, yaani, kuhani mkuu na dhabihu kwa ajili yetu.)
    1.    Sma Waebrania 9:23-26. Hili linajibuje kwa umadhubuti maswali tuliyoyajadili hivi punde? (Hii inaweka bayana kwamba Yesu yupo mbinguni. Kwamba anatenda kazi kwa ajili yetu ili “azitangue dhambi kwa dhabihu ya nafsi yake.”)
      1.    Utaona kwamba kifungu cha 23 kinarejelea “nakala za mambo yaliyo mbinguni.” Hekalu gani lilikuwepo kwanza, lile la duniani au lile la mbinguni? (Hii inatuambia kuwa ni lile la mbinguni.)
      1.    Hii inakuambia nini kuhusu mpango wa wokovu?
    1.    Soma Waebrania 9:28. Kazi ya Yesu mbinguni inajielekeza kwenye jambo gani? (Kwa Yeye kuja “mara ya pili” duniani ili “kuzichukua dhambi kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.”)
      1.    Je, unaweza kuelezea ni kwa jinsi gani kile tulichokijadili ni unabii? (Mfumo wa kafara unaonesha kile ambacho Yesu atakuwa anakitenda kwa ajili yetu, kile anachotutendea sasa hivi, na jinsi ambavyo hatimaye atakomesha dhambi.)
  1.   Kuingilia Kati Machafuko
    1.    Soma Yeremia 4:22. Watu wa Mungu wana tatizo gani?
    1.    Soma Yeremia 4:23-26. Ni nini matokeo ya watu wa Mungu Kutenda maovu na si mema? (Uangamivu.)
    1.    Soma Yeremia 4:27. Je, kuna habari njema katika hili? (Mungu anasema kuwa “hataikomesha kabisa” nchi. Muktadha wa hili unapatikana katika sura ya 4 ya kitabu cha Yeremia ambapo Mungu anairejelea Yuda na Yerusalemu.)
      1.    Hii inaashiria nini kuhusu mustakabali wa Yerusalemu?
  1.      Mungu Anaokoa
    1.    Soma Zaburi 47:1. Hii inaashiria nini kuhusu asili ya kusifu?
    1.    Soma Ufunuo 14:1-3. Hii inalinganisha sifa mbinguni na kitu gani? (“Sauti” ya maji, “sauti ya radi kuu.”)
      1.   Ni nini mtazamo wa waliookolewa? Je, una mtazamo sawa na huo?
    1.  Soma Zaburi 47:2-4 na Warumi 11:11-12. Kisha soma Warumi 11:17-18. Zaburi 47 inaporejelea “urithi wetu,” je, ni kitu gani hicho? (Inazungumzia juu ya wateule wa asili wa Mungu, Wayahudi.)
    1. Soma Zaburi 47:5-8. Ni nini mustakabali wa watu wote wa Mungu? (Ushindi!)
    1.   Soma Zaburi 47:9. Hii inatuamabia nini kuhusu mwendelezo wa uhusiano wa Mungu na Wayahudi? (Kila mtu anayemchagua Yesu anakuwa “watu wa Mungu wa Ibrahimu.”)
    1.    Soma 1 Wathesalonike 4:13-14. Wafu wanafufuliwaje katika uzima wa milele? (Kwa njia ya Yesu. Kama tulivyoona, mfumo wote wa fakara ulijielekeza kwa Yesu na kwa huduma yake ya sasa mbinguni. Yesu ni ufunguo wa msingi wa uzima wa milele.)
    1.   Soma 1 Wathesalonike 4:15-17. Nani anafufuka kwenda mbinguni Yesu anapokuja mara ya pili? (“Waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.” Hilo litafuatiwa na walio hai Yesu anapokuja mara ya pili.)
    1.   Soma 1 Wathesalonike 4:18. Hizi ni habari za namna gani? (Habari zinazotia moyo!)
  1. Anayeokolewa na Mungu
    1.   Soma Zaburi 15:1. “Hema” la Mungu na “kilima chake kitakatifu” ni vitu gani? (Daudi anaandika kuhusu kuwa mbele ya uwepo wa Mungu.)
    1.   Soma Zaburi 15:2-3. Waliookolewa wanawatendeaje marafiki wao?
    1.   Soma Zaburi 15:4. Mtu aliyeokolewa ana mtazamo gani kwa waovu? (Anawadharau.)
      1. Hebu subiri kidogo! Ninaambiwa (na Yesu) kwamba ninatakiwa “kumpenda” “adui” wangu. Mathayo 5:44. Je, unaweza kupatanisha vifungu hivi viwili? (Katika siku za juma tulijadili Mathayo 5:45 ambapo Yesu anaelezea aina ya upendo anaouonesha Baba. Anachokionesha Mungu kwa waovu ni neema ya kawaida, anawatendea kama anavyomtendea mtu yeyote yule. Hivyo, unawatendea watu waovu/wabaya kwa haki, lakini unapaswa kuwadharau na kuwaheshimu wale “wanaomcha Mungu.”)
      1. “Kuapa kwa hasara yake” inamaanisha nini? (Inamaanisha unayashikilia makubaliano yenu, hata kama mambo hayatakuwa mazuri kwa upande wako.)
    1.   Soma Zaburi 24:3. “Mlima wa Bwana,” na “patakatifu pake” ni kitu gani? (Kwa mara nyingine, kimantiki hii inarejelea uwepo wa Mungu.)
    1.   Soma Zaburi 24:4. Ni nini jibu kwa swali lililoulizwa katika Zaburi 24:3? (Walio na “mikono safi na moyo mweupe.”)
      1. Je, huyo ni wewe?
    1.   Soma Zaburi 5:3-6. Hapa tunaona kauli nyingine kuhusu Mungu kuwachukia watenda maovu. Je, kauli zote hizi (hapa na katika vifungu vilivyotangulia) vinakutia wasiwasi kuhusu wokovu wako? Je, umetimiza vigezo?
    1.   Soma Zaburi 5:7. Angalia tena Zaburi 5:3. Je, rejea za “hekalu takatifu” na “dhabihu” zina umuhimu gani kwenye suala la kukidhi vigezo? (Hii ni haki kwa njia ya imani. Hii inaelekeza usikivu wetu kwenye umuhimu wa mfumo wa kafara wa hekalu katika siku za Yesu za nyuma na kazi yake ya sasa kwa ajili yetu mbinguni.)
      1.   Nini kinahamasisha kile ambacho Yesu ametutendea? (“Upendo wa Yesu usioyumba.”)
    1.   Ruka vifungu kadhaa chini na usome Zaburi 5:11-12. Unakumbushwa jambo gani unaposoma kuwa Mungu anatusambazia ulinzi na kutufunika kama ngao? (Soma Ufunuo 7:9 na Ufunuo 7:13-14. Mavazi yetu meupe ya haki, yaliyofanywa kuwa meupe katika damu ya Mwana-Kondoo, ndio ulinzi wetu na ngao yetu. Katika Yesu tunaingia katika viwanja vya mbinguni!)
    1.   Rafiki, je, ungependa kuwa na kinga na ngao? Je, ungependa kulindwa kwa kile ambacho Yesu amekitenda kwa ajili yako? Ujumbe wa Biblia kuanzia mwanzo hadi mwisho ni kwamba tunaokolewa kwa kafara ya Yesu kwa ajili yetu. Kwa nini usilipokee hilo sasa hivi?
  1. Juma lijalo: Katika Zaburi: Sehemu ya 2.