Somo la 11: Ruthu na Esta

Ruthu 1-4, Esta 3-9
Swahili
Year: 
2025
Quarter: 
2
Lesson Number: 
11

Somo la 11: Ruthu na Esta

(Ruthu 1-4, Esta 3-9)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2025, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Vitabu vingapi vya Biblia vina majina ya wanawake? Kwa Waprotestanti, jibu ni “viwili, Ruthu na Esta.” Tunavyo vitabu hivi kwa ajili ya somo letu juma hili. Kwa nini mfululizo wa masomo ya unabii ujumuishe vitabu hivi viwili? Wanawake ni ishara yenye nguvu ya unabii wa kidini. Wanawake ni wawakilishi wa vyote viwili, yaani, kanisa la kweli na mamlaka ya kidini yaliyo ya kiovu. Ni kwa jinsi gani Ruthu na Esta kwa ujumla wanaendana na ishara hizo? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

I.     Naomi and Ruthu

A.     Soma Ruthu 1:1-2. Hii familia ndogo kutoka Bethlehemu inalazimika kuondoka na kuacha nyumba yao kwa sababu ya njaa. Bethlehemu inamaanisha “Nyumba ya Chakula,” kwa mujibu wa commentary ya David Guzik. Lilikuwa eneo lenye utajiri wa kilimo. Je, hii ni nuksi tu? (Soma Kumbukumbu la Torati 11:13-17. Hii sio nuksi, huku ni kutokutii kwa taifa. Maoni ya Kale ya Kikristo (The Ancient Christian Commentary) yanaenda mbali zaidi na kutuambia kuwa utamaduni wa Kiebrania ni kwamba mume, kwa sababu alikuwa kidedea katika kutokutii kwa kabila la Yuda, alifukuzwa kutoka katika nchi.)

B.     Soma Ruthu 1:3. Je, ulikuwa uamuzi mzuri kuamua kwenda katika nchi ya Moabu? (Hapana. Walihamia Moabui ili kuepuka kufa, licha ya hayo Elimeleki anafariki na kumwacha mkewe na wanawe wawili.)

C.     Soma Ruthu 1:4. Je, ni uamuzi wa busara kuwaoa wake wa Kimoabi? (Si kwa ujumla wake. Kuoana na Mmoabi hakukuzuiliwa, lakini Kumbukumbu la Torati 23:3-6 iliwazuia Wamoabi wasiabudu pamoja na watu wa Mungu.)

1.     Kwa nini uoane na mtu ambaye asingeweza kuabudu pamoja nawe? (Safari ya muda mfupi sasa imekuwa ya miaka kumi na inawezekana wana waliamua kwamba kamwe wasingerudi kwao. Kama baba wao alifukuzwa, hilo linaweza kuonekana kama kizuizi zaidi cha kutorejea.)

D.     Soma Ruthu 1:5. Sasa wana wawili wanafariki. Je, hii ni kwa sababu waliwaoa Wamoabi? Kwa sababu walishindwa kurudi Yuda? (Biblia haisemi chochote, imekaa kimya. Lakini Mungu hawabariki kwa sababu hakuna mwana hata mmoja kati yao wawili aliyezaa mtoto.)

E.     Ruka vifungu kadhaa na usome Ruthu 1:13 na Ruthu 1:20-21. Naomi anayachukuliaje maafa yaliyotokea maishani mwake? (Anasema kuwa mkono wa Munguu uko kinyume naye. Hata anadhani kuwa jina lake linapaswa kubadilishwa ili kuakisi kutopendelewa huko.)

F.     Soma Ruthu 1:6-9. Naomi anawachukuliaje wakamwana wake? (Anasema kuwa walikuwa wema kwake.)

1.     Je, Naomi anakuwa mwema kwao? (Ndiyo, wangeweza kumsaidia Naomi, lakini badala yake anapendekeza kuwa watakuwa na maisha mazuri zaidi katika nchi ya Moabu.)

G.     Soma Ruthu 1:14-16. Je, Ruthu anajitolea nafsi yake? Je, anadhamiria kumfuata Mungu wa Yuda?

1.     Angalia maoni ambapo Naomi anapendekeza kuwa kuigeukia miungu ya kipagani ni uchaguzi wenye mantiki. Hiyo itaathirije fikra ya Ruthu?

H.     Soma Ruthu 1:17-18. Hebu niambie: unadhani ni kwa jinsi gani Ruthu alikuwa imara sana kumfuata Mungu wa kweli katikati ya maafa yote haya?

II.     Boazi na Ruthu

A.     Soma Ruthu 1:22 na Ruthu 2:1-2. Hatutaingia kwa kina kwenye sheria za masazo ya mavuno. Tambua tu kwamba wajane walikuwa na haki ya kukusanya kilichodondoshwa na wafanyakazi wa mkulima au walichoshindwa kuokota. Ni kitu gani kilicho muhimu kumhusu Boazi? (Yeye ni ndugu.)

B.     Soma Ruthu 2:20-23 ili kuona taarifa ya Ruthu kuhusu kazi za siku. Je, Boazi amemwona Ruthu?

C.     Soma Ruthu 3:2-5. Naomi anampendekezea nini Ruthu?

D.     Soma Ruthu 3:7-10. Boazi amelewa kidogo lakini anashtuka kutoka usingizini na kumkuta mwanamke miguuni pake. Anakuwa na mwitiko gani?

1.     Utayatafsirije maneno ya Ruthu katika kifungu cha 9? (Anaomba/anasihi kwa Sheria ya Kilawi. Angalia Kumbukumbu la Torati 25:5-6.)

2.     Boazi anayaelewaje maneno ya Ruthu? (Anatambua kwamba anamfukuzia/anamtongoza.)

E.     Soma Ruthu 3:11-13. Je, hii ni posa ya arusi isiyo ya uhakika?

1.     Je, Mungu anambariki Ruthu?

F.     Soma Ruthu 4:1-4. Ndugu wa karibu anakubali kwamba atanunua ardhi iliyomilikiwa na Elimeleki, marehemu mume wa Naomi. Sasa mipanhgo ya Boazi na Ruthu inakwendaje?

G.     Soma Ruthu 4:5-6. Je, huu ni mkakati wa majadiliano wa Boazi? “Jambo la ziada kidogo, unaponunua ardhi unamnunua Ruthu pia, huyu Mmoabi.” (Nadhani hiki ndicho alichokipanga Boazi.)

1.     Je, kupangilia mambo mapema ni jambo jema? Au Boazi anaingilia tu mpango wa Mungu?

H.     Soma Ruthu 4:13-17. Maisha ya Naomi yamebadilikaje? Maisha ya Ruthu yamebadilikaje?

1.     Sababu ya mabadiliko ni ipi? (Ninasema kuwa ni uaminifu wa Ruthu kwa Mungu wa kweli. Sasa Naomi ana mjukuu wa kiume!)

2.     Je, huyu ni mjukuu wa kiume kama mjukuu yeyote yule? (Hapana! Mjukuu huyu ni babu wa Mfalme Daudi!)

3.     Tafakari kisa hiki katika muktadha wa suala hili kuwa uzao wa Kimasihi. Je, baadhi ya uamuzi unakuwa na umuhimu mkubwa?

4.     Rafiki, kuwa mwaminifu kwa Mungu ni jambo la muhimu kiasi gani?

III.     Esta

A.     Soma Esta 3:1-2. Kwa nini Mordekai hakuinama wala kumsujudia Hamani? Ilikuwa amri ya mfalme! (Soma Esta 3:3-4. Ni kwa sababu Mordekai ni Myahudi. Hili ni suala la uhuru wa dini.)

B.     Soma Esta 3:5-6. Hamani anakuwa na mwitiko gani? Je, ni mwitiko wenye mantiki? (Hapana. Sio tu kwamba anataka kumwua Mordekai, bali pia anataka kuwaua Wayahudi wote katika ufalme wote!)

1.     Hamani ni mtu wa namna gani?

C.     Soma Esta 3:8-11. Kwa nini Hamani anawasilisha jambo hili kama suala la kifedha?

D.     Soma Esta 3:13. Nini yangekuwa matokeo ya kuwaua Wayahudi wote katika sehemu zote za ufalme? (Hiyo ingewajumuisha Wayahudi ambao walirejea kulijenga upya hekalu katika Yerusalemu. Ingekuwa tishio kwa uzao wa Kimasihi.)

E.     Soma Esta 4:1. Je, Mordekai anadhani kuwa mambo yote haya yanatokana na kosa lake?

F.     Soma Esta 4:13-14. Mordekai anataka Esta aingilie kati kwa ajili yao kwa mfalme. Lakini hilo linayahatarisha maisha yake. Angalia Esta 4:11. Mordekai anajenga hoja gani kwa Esta? (Anasema kuwa maisha yake (Esta) yako hatarini bila kujali atakachokifanya. Anaashiria kuwa Mungu amemweka katika nafasi hii.)

1.     Je, nafasi ya Esta ni uteuzi wa Mungu?

G.     Soma Esta 4:16. Esta anaomba nini? (Maombi!)

H.     Soma Esta 5:1-4. Kama huu ni uteuzi wa Mungu, je, kweli maisha ya Esta yako hatarini?

I.     Karamu maalumu kwa ajili ya mfalme, Malkia Esta na Hamani inafanyika. Hebu tuyaangalie mazungumzo. Soma Esta 7:3-6. Unadhani Hamani alijua mazungumzo haya yalikuwa na mwelekeo gani? Je, alifahamu kuwa Esta alikuwa Myahudi?

J.     Soma Esta 7:7-10. Je, Esta alipaswa kujaribu kuingilia kati ili kuokoa uhai wa Hamani?

K.     Soma Esta 9:1-2 na Esta 9:4-5. Pia soma Esta 9:13-14. Je, hii ni haki?

1.     Hebu tuliangalie hili kwa kuzingatia pambano kati ya wema na uovu. Ni nini lililokuwa lengo la Shetani kuwaangamiza Wayahudi? (Anawachukia watu wa Mungu. Alitaka kumzuia Masihi anayekuja.)

2.     Badala yake ni jambo gani linatokea? (Watu wa Mungu wanainuliwa, watu wa Shetani wanaangamizwa.)

L.     Soma Esta 4:14. Ujasiri wa Esta ni wa muhimu kiasi gani katika kisa hiki? 

1.     Je, Mordekai yuko sahihi anaposema kuwa kama Esta atashindwa basi Mungu atatafuta njia nyingine ya kuwaokoa watu wake?

M.     Rafiki, wanawake hawa wawili walibadili mwelekeo wa historia. Au sivyo? Mungu anawatafuta mashujaa. Anawatafuta watu wa kubadili mwelekeo wa historia. Je, mtu huyo atakuwa wewe? Je, utasimama kwa ajili ya Mungu hata kama mazingira yanaweza yasiwe ya kustarehesha? Hata kama mambo hayo yanaweza kuyaweka maisha yako katika hatari kubwa? Kwa nini usidhamirie leo kusimama imara kwa ajili ya Mungu? Usimfanye Mungu amtafute mtu mwingine.

IV.     Juma lijalo: Watangulizi.