Somo la 7: Uraia wa Mbinguni

(Wafilipi 3:17-4:23)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
1
Lesson Number: 
7

Somo la 7: Uraia wa Mbinguni

(Wafilipi 3:17-4:23)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2025, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

Utangulizi: Juma hili nimesoma takwimu za kushangaza. Zaidi ya asilimia 50 ya idadi fulani ya watu nchini Marekani wanakiri kuwa na ugonjwa wa afya ya akili. Ukilinganisha na taarifa za awali, idadi hii ya watu inaonekana kuwa ile ile ambayo ushikaji wao wa dini ni wa kiwango cha chini. Mara kwa mara huwa ninasoma kuwa viwango vya wasiwasi viko juu miongoni mwa watu wanaoishi nchini Marekani. Kama suala la kihistoria, hii haileti mantiki. Vizazi vilivyonitangulia vilipigana katika vita viwili vya dunia. Hata hivyo, kamwe Marekani haijawahi kuvamiwa. Inawezekanaje kizazi ambacho hakijakabiliana na wavamizi na hakijapigana vita vyovyote kiwe na wasiwasi au kitaabike na ugonjwa wa afya ya akili? Nadhani jambo la msingi si kile kinachoendelea katika mazingira yanayomzunguka mtu, bali kinachoendelea ndani yake. Katika somo letu la mwisho kwenye kitabu cha Wafilipi Paulo anatukaribisha kwenye maisha kamili ya furaha, maisha yaliyo huru dhidi ya wasiwasi. Hebu tuzame kwenye Biblia na tujifunze zaidi kuhusu aina hiyo ya maisha!

I.    Yaelekeze Macho Yako kwa Joe

A.    Soma Wafilipi 3:17. Kila ninapomsikia mtu akilalamika kuhusu mtazamo wa mshiriki mwingine wa kanisa, wengine wanashauri, “Yaelekeze macho yako kwa Yesu, na wapuuze washiriki wengine wa kanisa.” Je, hicho ndicho anachokishauri Paulo? (Paulo anaandika kuwa tunapaswa kumuiga na wale wanaofuata ushauri wake.)

1.    Unalifafanuaje suala hili? Je, ushauri wa kuyaelekeza macho yetu kwa Yesu si sahihi? Je, badala yake tunapaswa kusema, “Yaelekeze macho yako kwa Paulo?”

2.    Ikiwa tuna mshiriki mzuri wa kanisa, tumpe jina la “Joe,” je, tunapaswa kusema “Yaelekeze macho yako kwa Joe?”

B.    Soma Wafilipi 3:18. Ni nini iliyo hatari ya kuyaelekeza macho yetu kwa washiriki wenzetu wa kanisa? (Paulo anatuambia kuwa “wengi” huenenda kama “adui wa msalaba wa Kristo.”)

1.    Mara ngapi umemwona kiongozi wa kanisa akienenda kama mfuasi wa Yesu, lakini baadaye anaanguka majaribuni? Ni kwa jinsi gani ushauri wa Paulo wa kuyaelekeza macho yetu kwenye mifano mizuri unatumika hapa? Ni lini kiongozi huyo alibadilika kutoka kuwa mwema hadi mbaya?

2.    Suluhisho mojawapo ni kuepuka kumng’ang’ania kama mfano mshiriki yeyote wa sasa wa kanisa. Kuna ubaya gani na ushauri huo?

C.    Soma 1 Wakorintho 11:1 na Waefeso 5:1. Je, Paulo anajichanganya? Au, tumeshindwa tu kuangalia kwa kina ushauri wa Paulo?

D.    Litafakari hili: Kwa namna kadhaa Yesu ni mfano mgumu wa kuigwa. Kamwe hakuoa. Kamwe hakuwa na watoto. Kama mtu mzima kamwe hakuajiriwa na mtu yeyote. Alikuwa Mungu kamili na mwanadamu kamili. Alikufa akiwa kijana mdogo. Alikuwa mlengwa wa Shetani mara kwa mara, licha ya hayo hakuwa na dhambi. Ni kwa jinsi gani Yesu ni mfano bora wa kuufuata?

E.    Kwa upande mwingine, soma Waebrania 4:15. Hii inatuambia kuwa Yesu “alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote.” Unadhani hii inamaanisha nini? (Ingawa inajidhihirisha wazi Yesu hakujaribiwa kwa matatizo ya ndoa au malezi ya mtoto, majaribu mengi yanaangukia kwenye matabaka makubwa mbalimbali. Lazima hii inamaanisha kuwa Yesu alikabiliana na masuala ya asili ya majaribu yote. Kutokana na hili tunaiga mtazamo wa Yesu. Tunafuata mafundisho yake. Nadhani Paulo anatuambia kuwa tunapaswa kuwa na mtu ambaye ni mfano wa kuigwa wa kisasa kwa sababu yumkini mtu huyo anakabiliana na matatizo hayo hayo kama tunayokabiliana nayo.)

1.    Nilipopendekeza kuwa majaribu mengi yanaangukia kwenye matabaka ya aina mbalimbali, je, unakubaliana na kauli hii? Je, unaweza kupendekeza jaribu la msingi linalofanana? (Chukulia kiburi na ubinafsi kama msingi mkuu wa majaribu mengi.)

F.    Soma Wafilipi 3:19. Hatimaye Paulo anawaelezea wale tusiopaswa kuwafuata. Anasema “mungu wao ni tumbo.” Je, tunapaswa kupuuza mifano ya watu wanene au wale wanaobandika (post) picha za vyakula vyao kwenye kurasa za Facebook? (Anachokimaanisha Paulo hapa kina mjadala mkubwa. Soma Mathayo 15:10-11. Yesu anazungumzia kundi la watu linalojikita kwenye kanuni za kidini za ulaji. Anasema kuwa zingatio halisi linapaswa kuwa kwenye kile tunachokisema.)

1.    “Utukufu wao u katika fedheha yao.” Hii inamaanisha nini? (Tafakari nyuma kwenye mjadala wetu wa Wafilipi 3:8-9. Paulo anaziita juhudi zake za kujiokoa kuwa ni “mavi.” Hilo linaendana vizuri na dhana ya kwamba sheria za kidini za ulaji hazituokoi.)

2.    “Waniao mambo ya duniani.” Unadhani hii inamaanisha nini? (Tukisalia kwenye fikra hii, itamaanisha wale ambao usikivu wao umejikita kwenye uzingativu wa mambo halisi yanayoonekana. Lakini hatupaswi kupuuza tatizo la wale wanaopenda mambo ya duniani.)

G.    Soma Wafilipi 3:20-21. Tukiziangalia kauli za Paulo katika vifungu vya 19-21 kwamba vinatoa maana ya jumla, je, hiyo inabadili majibu yako ya awali kwa kile kilichomaanishwa katika Wafilipi 3:19? (Haitabadili majibu yangu niliyoyapendekeza. Tofauti inayotolewa ni kati ya wale wanaomwangalia Yesu kwa ajili ya uzima wao wa milele, na wale wanaojiangalia wenyewe.)

II.    Furaha

A.    Soma Wafilipi 4:1-3. Tatizo gani linazungumziwa na Paulo? (Wanawake wawili kanisani ambao wote wawili wanafanya kazi ya kutangaza injili wanashindana.)

B.    Soma Wafilipi 4:4. Ni nini muktadha wa Paulo kutuambia “kufurahi?” Kuwa na furaha? (Ni kutokubaliana kulikobainishwa katika vifungu vya 1-3. Ni vigumu kufurahi tunapokuwa katika kutokubaliana.)

C.    Soma Wafilipi 4:5. Tunashughulikiaje mijadala kanisani? (Paulo anatuhimiza tuwe na busara.)

1.    Je, huo ni wito wa kufikia maafikiano (compromise)? (Ni wito wa kubainisha kipi ni cha muhimu na kipi si cha muhimu. Kama ilivyo kwa utambuzi kwamba kile unachokisema ni cha muhimu zaidi kuliko jinsi au kile unachokula. Ninaweza kulisema hili bila upendeleo kwa sababu nimekuwa mla mbogamboga (vegetarian) kwa muda wa miaka 62! Ninaonekana kama mtu ambaye amejikita kwenye tumbo lake – ambalo hata hivyo ni kubwa kwa mla mbogamboga.)

D.    Soma Wafilipi 4:6-7. Ni nini msingi wa kuachana na wasiwasi na kuingia kwenye amani na furaha? (Kumgeukia Mungu kwa ajili ya msaada kwa kila kitu. Mshukuru Mungu. Mungu “atawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Atawapeni amani.)

1.    Kuna sehemu ya jamii ya Kimarekani inayoonekana kuwa na hasira kupitiliza. Sehemu ya kundi hilo iliingia kwenye Kanisa la Kibaptisti la Kusini (Southern Baptist Church) ili kupinga suala la kisiasa. Kwa nini walilenge kanisa? (Hawamheshimu Mungu. Hasira inaakisi ongezeko la idadi kubwa ya watu wasiomwamini Mungu.)

2.    Tafakari hili kidogo. Kama ulijisikia kwamba jamii ilikuwa inakugeuka, kwamba serikali ilikuwa inatenda jambo lisilo sahihi, ungekuwa na mwitiko (reaction) gani? (Kama unaiamini Wafilipi 4:6 ungemgeukia Mungu. Kama humwamini Mungu yumkini ungekuwa na hasira zaidi na zaidi na usiyetumia akili (irrational).)

E.    Soma Ufunuo 21:8. Unaelezeaje tabia ya kwanza iliyoorodheshwa kwa waliopotea kwamba ni kuwa “mwoga?” (Hii inaendana kikamilifu na kauli za Paulo. Kama tunaye Mungu wa kumgeukia tunaweza kuwa na amani na furaha tukimtumaini yeye. Kama hatuna Mungu, basi tuko peke yetu, tukiendelea kukata tamaa, kuwa na hasira, na kuchanganyikiwa.)

III.    Mtazamo wa Mawazo

A.    Soma Wafilipi 4:8-9. Unadhani Intaneti imesaidia kusababisha waoga na watu wenye uwazimu? (Habari njema kuhusu Intaneti ni kwamba inafanya maarifa yapatikane kwa urahisi na inatoa mwanya kwa wachapishaji wakubwa wanaotamani kusukuma mtazamo fulani. Jambo baya kuhusu Mtandao kimsingi ni lile lile. Unaweza kufahamu mambo mabaya yakitokea katika ulimwengu ambayo usingeyafahamu kama ungekuwa na uhaba wa taarifa. Ikiwa una mtazamo finyu wa mawazo unaotafuta migogoro, unaweza kuupata kwa urahisi.)

1.    Paulo anashauri nini juu ya kile tunachopaswa kukiweka akilini mwetu? (Mambo ya kusifu. Mambo yanayokubalika. Mambo masafi yanayopendeza.)

a.    Je, hili linaweza kutendeka katika zama za Intaneti? (Ndiyo. Wewe ndiye chujio.)

b.    Ni nini matokeo ya kujikita kuweka mambo sahihi akilini mwako? (“Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.”)

B.    Soma Wafilipi 4:10-13. Kihistoria, masuala ya kifedha yako juu kwenye orodha ya vitu vinavyosababisha wasiwasi. Ni nini jibu la Paulo kwenye mashaka kuhusu fedha? (Mungu anaweza kutufanya turidhike.)

1.    Kuna tafiti zinazoonesha kuwa ni vigumu kuwa masikini baada ya kuwa tajiri, kuliko kuendelea tu kuwa masikini. Je, Paulo alikuwa tajiri? (Ndiyo, anasema kuwa amepitia uzoefu wa “kushiba” na “kuwa na vingi.”)

C.    Soma Wafilipi 4:19. Vipi ukihisi uhitaji? Vipi kama unapungua? (Tunayapokea kupitia kwa Yesu. Nadhani mtazamo wa kutumaini na amani umefungashwa kwenye ahadi ya uzima wa milele.)

D.    Soma Wafilipi 4:14-18. Hebu tuangalie nyuma ya kile anachokisema Paulo kwa Wafilipi na kuuliza “Ungejisikiaje kama ungekuwa Paulo?” Ungejisikiaje endapo kanisa moja pekee ndilo lingekusaidia? (Hii ni mojawapo ya changamoto alizokabiliana nazo Paulo. Alielewa ilimaanisha nini kumtegemea Mungu.)

E.    Rafiki, je, ungependa kuwa na furaha na amani zaidi maishani mwako? Furaha na amani ni vitu vigumu zaidi kupatikana katika ulimwengu unaoongezeka hasira kwa kasi. Kwa nini usimgeukie Mungu kwa ajili ya jibu kwa kila tatizo?

IV.    Juma lijalo: Ukuu wa Kristo Katika Yote.