Somo la 9: Upatanisho na Tumaini

(Wakolosai 1:20-29)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
1
Lesson Number: 
9

Somo la 9: Upatanisho na Tumaini

 

(Wakolosai 1:20-29)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Mojawapo ya mambo yasiyofurahisha katika kazi yangu ya uanasheria ni kwamba pande zote mbili hazipendani. Chama cha wafanyakazi hakikumpenda mteja wangu kwa sababu mteja wangu hakutaka chochote kinachohusiana na chama cha wafanyakazi na akanitaka nimsaidie. Mteja wangu hakukipenda chama cha wafanyakazi kwa sababu kilikuwa kinajaribu kumfukuza kazi. Kwa nini? Kwa sababu ama mteja wangu alikuwa anasimamia imani zake za kidini au anasimamia haki zake za uhuru wa maoni. Kuna nyakati chama cha wafanyakazi kiliamua kutumia vurugu. Je, unafahamu kuwa Mungu “anawachukia wote watendao ubatili?” Zaburi 5:5. Yohana 15:18 inatuambia kuwa ulimwengu “unamchukia” Yesu. Nasi tutarajie ulimwengu utuchukie pia. Hiyo inaonekana kama mambo mengi yasiyopendeza! Somo letu juma hii linahusu jinsi Yesu alivyobadilisha chuki hii. Hebu tuzame kwenye somo letu na tuone kile alichotutendea Yesu ili kuleta upatanisho na tumaini maishani mwetu!

 

  1.    Waliopatanishwa

 

    1.    Soma Wakolosai 1:20. Yesu alivipatanisha “na nafsi yake” vitu vyote mbinguni na duniani. Je, unadhani kuwa mbingu ilikuwa na mgogoro na Yesu?

 

      1.    Je, wanadamu walikuwa na mgogoro na mbingu?

 

    1.    Soma Wagalatia 3:10 na Wagalatia 3:13. Yesu ametutendea nini? (Yesu alipozichukua dhambi zetu msalabani, alichukua laana ya kutokutii kwetu. Kwa muda huo Yesu alikuwa na mgogoro na mbingu. Sisi wadhambi, kabla Yesu hajatufia dhambi zetu, tulikuwa na mgogoro na mbingu.)

 

    1.    Soma Wakolosai 1:21-22. Vifungu hivi vinatuambia kuwa matendo yetu maovu yalisababisha mfarakano na uhasama. Je, hilo sasa limekwisha? (Ndiyo. Kupitia kifo cha Yesu, anaweza kutuwakilisha kama watakatifu, wasio na lawama, na wasioweza kushutumiwa.)

 

      1.    Hebu subiri kidogo. Je, Yesu anafanana na muuza magari yaliyotumika asiye mwaminifu anayeonesha kuwa gari halina tatizo wakati kimsingi lina ubovu?

 

      1.    Au, tumeacha kutenda matendo maovu?

 

      1.    Au, kuna jambo jingine limetokea? (Kura yangu inaangukia kwenye jambo jingine lililotokea, na tena lisilo na kifani. Bado Wakristo wanatenda maovu. Wale waliompokea Yesu bado wanaokolewa licha ya hayo matendo maovu. Hili linawezekana kwa sababu kifo cha Yesu kwa ajili yetu kilifunika dhambi zetu zote.)

 

  1.   Jambo la Pekee (Lisilofuata Kawaida) – (The Exception)

 

    1.    Soma Wakolosai 1:23. Je, kuna jambo lisilofuata kawaida kwenye kanuni hii? Je, kuna “jambo lililofichika?” (Ndiyo. Kuongolewa kwa damu ya Yesu, kuokolewa kwa kafara yake, lazima “tudumu katika ile imani.”)

 

      1.    Inamaanisha nini “kudumu katika ile imani?” (Paulo anasema kuwa lazima tuendelee “kutumaini” katika injili. Lazima tuendelee kuamini kuwa Yesu ametuokoa.)

 

      1.    Hili linaonekana jambo rahisi sana. Kwa nini mtu ageuke na kuliacha tumaini alilo nalo ndani ya Yesu? Ninaami, kwa kuwa nimepitia uzoefu wa jaribu hili, kwamba nyakati nyingine kishawishi cha dhambi kina nguvu kubwa mno. Mtu anayemjua na kumpenda Yesu anatambua kuwa kuigeukia dhambi hiyo si uchepukaji wa muda mfupi kwenye uhusiano. Bali ni “kuhama,” badiliko linalolikimbia tumaini katika Yesu. Hauko tena “imara na thabiti.”)

 

    1.    Angalia tena Wakolosai 1:23. Paulo anaeleza kuwa injili hii “ilihubiriwa katika viumbe vyote vilivyo chini ya mbingu.” Nina maswali mawili:

 

      1.    Mbingu zinaitafakarije? Je, wale waliomsababishia Yesu mateso makubwa sana wanatakiwa kulipa adhabu? Je, wenye chuki wanaondoka bila adhabu?

 

      1.    Inaonekana Shetani na malaika wake walioanguka hawapewi fursa hii ya kugeuka. Kwa nini? (Nadhani walipewa fursa ya kugeuka. Tatizo ni kwamba “wamehama” kiasi kwamba si tu kwamba wanalikataa tumaini, bali pia wapo kwenye vita inayoendelea dhidi yake?

 

  1.      Paulo Anayeteseka

 

    1.    Soma Wakolosai 1:24. Unaelewaje Paulo anaposema “nayatimiliza yale yaliyopungua” kwenye mateso ya Kristo? Je, anasema kuwa anateseka zaidi ya Yesu?

 

      1.    Nani au kitu gani kinaamua “yale yaliyopungua” katika mateso ya Yesu? (Huu ndio msingi wa uelewa. Maadui wa Mungu ndio wanaoamua kitu gani kinapungua kwa maana ya kwamba wangependa kumwadhibu Yesu zaidi. Kwa kuwa Yesu amerejea mbinguni, Paulo anasema kuwa sasa yeye ndiye mlengwa wa wale wanaomchukia Yesu.)

 

    1.    Soma Wakolosai 1:25, lakini endelea kuwazia kifungu cha 24 akilini mwako. Je, kuna lengo katika mateso ya Paulo? (Haya si mazingira ambayo wenye chuki wanatafuta walengwa na wakamchagua tu Paulo. Badala yake, Paulo analengwa kwa sababu ya kazi yake kwa ajili ya Wakristo wenzake.)

 

  1.   Siri Iliyofichwa

 

    1.    Soma Wakolosai 1:26-27. Ninakufanya usome vifungu vifupi, lakini sitaki ukose msingi wa kauli ya Paulo unaopatikana katika vifungu vya 24-27. Ni siri gani ambayo Paulo anaifanya ijulikane kwa watakatifu?

 

      1.    Je, ni kwamba injili sasa inapaswa kwenda kwa Mataifa? Sasa wanajumuishwa kwa watu wa Mungu?

 

      1.    Je, ni kwamba Yesu anakaa ndani ya wafuasi wake?

 

      1.    Je, ni kwamba kwa sababu ya Yesu sote tuna tumaini la mbinguni? (Siri ni mambo yote haya matatu.)

 

      1.    Je, unaona sehemu moja ya siri kama muhimu zaidi kuliko siri nyingine? (Soma Warumi 8:11. Dhana ya kwamba sasa Mungu atakaa ndani ya wafuasi wake, ikiwemo Mataifa, ni mapinduzi katika uelewa wa mwanadamu wa Mungu.)

 

    1.    Soma Wakolosai 1:28. Paulo anasema “ambaye sisi tunamhubiri,” huyu “sisi” ni nani? (Paulo na Wakristo wenzake.)

 

      1.    Ujumbe wa Paulo ni onyo na tangazo. Unaonya dhidi ya nini? (Neno la Kiyunani halimaanishi “onyo dhidi ya hatari.” Bali, neno la kawaida kabisa ninaloliona ni “asa.” Ikimaanisha kusahihisha mtafaruku.)

 

    1.    Sehemu ya mwisho ya Wakolosai 1:28 ni muhimu. Somo letu la juma lililopita na la juma hili yanapigilia msumari dhana ya kuhesabiwa haki kwa imani pekee. Kuhama pekee kutoka kwenye tumaini letu kwa Yesu kunaweza kutufanya tupoteze wokovu wetu. Katika muktadha huo, Paulo anatuambia kuwa sehemu ya lengo lake katika kufundisha ni “kumlea kila mtu mtimilifu katika Kristo.” Inamaanisha nini kuwa “mtimilifu katika Kristo?”

 

      1.    Na utaufundishaje huo utimilifu?

 

    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 4:2 na Kumbukumbu la Torati 12:32. Pia soma Mithali 30:6 na Ufunuo 22:18-19. Maonyo haya yanahusikaje na utimilifu (ukomavu) wa Kikristo? (Watu wasio wakomavu, watu wanaoamini kuwa mawazo yao yanaweza kuirekebisha Biblia, ndio wale wanaoongeza au kupunguza maneno kutoka kwenye neno la Mungu.)

 

      1.    Hii inatusaidiaje kuelewa kuhesabiwa haki kwa imani pekee? (Ukimtumaini Yesu kwa ajili ya wokovu wako, basi utalitumaini neno lake. Ukilitumaini neno lake, basi unatambua kuwa linawakilisha njia kamilifu kwa ajili ya maisha ya mdhambi. Wakristo watimilifu (wakomavu) ni Wakristo watiifu. Kwa “utiifu,” ninamaanisha wanatii mafundisho ya Biblia.)

 

    1.    Soma Wakolosai 1:29. Je, kuna nyakati unajisikia kuwa na “nguvu kidogo?”

 

      1.    Kama umejibu, “ndiyo,” Paulo anafundisha kuwa suluhisho lake ni lipi? (Yesu si tu kwamba anatupatia wokovu wetu, bali pia atatusambazia nguvu yetu.)

 

    1.    Rafiki, wokovu wako unapatikana bure. Huwezi kuufanyia kazi ili kuupata. Anachokitaka Mungu kutoka kwako ni kuendelea katika imani yako katika kile ambacho Yesu amekutendea. Mtazamo huu wa utegemezi, wa tumaini na imani, unamaanisha kuwa huongezei wala kupunguza kile ambacho Mungu ametupatia. Badala yake imani iliyokomaa na thabiti huwafanya wafuasi wa Yesu kuishi maisha yanayoendana na mapenzi yake. Je, utafanya uamuzi, sasa hivi, kuiweka imani yako katika kile ambacho Yesu amekutendea?

 

  1.    Juma lijalo: Kutimilika Katika Kristo.