Somo la 12: Kuishi Pamoja Sisi kwa Sisi

(Wakolosai 3:18-4:6)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
1
Lesson Number: 
12

Somo la 12: Kuishi Pamoja Sisi kwa Sisi

 

(Wakolosai 3:18-4:6)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Baadhi ya Wakristo wanaona kwamba kuishi na watu wengine ni vigumu. Uhusiano wao wa ndoa unahitaji kufanyiwa kazi mara kwa mara. Hawajui jinsi ya kuhusiana na watoto wao. Uhusiano wa kikazi kwa ujumla si wa kufurahisha. Je, huu ni mkosi tu? Au, ikiwa mara kwa mara una uhusiano usio mzuri na watu wa aina mbalimbali, je, hii inahusiana na jinsi ulivyo? Au huyu ni Shetani tu anayeanzisha matatizo maishani mwako kwa sababu wewe ni mwaminifu kwa Mungu? Huenda hii inahusiana na jinsi ulivyo. Shetani hana haja ya kusababisha matatizo kwako kwa sababu tayari unajisababishia matatizo ya kutosha. Somo letu juma hili linahusiana na ushauri wa Paulo wa kuishi na watu wengine. Hebu tuzame kwenye somo letu na tuone kile tunachoweza kujifunza ili kuboresha uhusiano wetu na wale wanaotuzunguka!

 

  1.    Familia

 

    1.    Soma Wakolosai 3:18-19. Ushauri kwa wake “kuwatii” waume wao una mwisho wa kufurahisha. Unaishia kwa kusema “kama ipendezavyo katika Bwana.” Unadhani hiyo inamaanisha nini?

 

      1.    Je, ni kauli tu ya kwamba kumtii mume ndicho ambacho Mungu anadhani ni sahihi kwa wake?

 

      1.    Au ni ukomo wa kumtii mume? (Tukiviangalia vifungu vyote viwili, tunaweza kuona kwamba mke na mume wanatakiwa kuzitii sheria za Mungu. Chochote alichokimaanisha Paulo kwa kusema “kama ipendezavyo katika Bwana,” vifungu hivi viwili vikichukuliwa pamoja vinaonesha kwamba kumtii mume kunategemeana na wanandoa kumtii Mungu.)

 

    1.    Angalia tena Wakolosai 3:18. Unadhani “kutii” inamaanisha nini? (Soma Waefeso 5:22-23 ambao Paulo anatupatia ufafanuzi kamili. Paulo anasema kuwa kumtii mume ni sawa na Kanisa kumtii Yesu.)

 

    1.    Soma Mwanzo 3:16 ambapo Mungu anatoa adhabu kwa Eva na Adamu kwa kutenda dhambi. Je, hivi ndivyo wanawake walivyoishia kuwa na maelekezo ya kuwatii waume wao?

 

      1.    Ikiwa ndivyo, je, hii ni adhabu tu ya moja kwa moja, au kuna kipengele chanya katika hilo?

 

      1.    Je, inaendana na adhabu iliyotolewa katika Mwanzo 3:17 kwa Adamu kwamba kilimo kitakuwa kigumu?

 

    1.    Hebu tuangalie tena Wakolosai 3:19. Kisha soma Waefeso 5:25 ili kupata taswira kamili. Inamaanisha nini kumpenda mke wako kama Yesu “alivyolipenda kanisa, akajitoa kwa ajili yake?”

 

      1.    Je, itakuwa vigumu kumtii mume mwenye mtazamo kama huu?

 

      1.    Kama mume atashindwa kutimiza wajibu wake wa Waefeso 5:25, je, mke anakuwa huru dhidi ya wajibu wa kutii? Au wajibu huu wa mwanamke na mwanaume unajitegemea kila mmoja?

 

    1.    Soma Wakolosai 3:20-21. Watoto wanapoambiwa kuwatii wazazi wao, je, huu ni wajibu maishani mwao mwote? (Neno la Kiyunani la watoto ni “tekna” ambalo kwa mujibu wa maoni ya IVP New Testament, hapa linawarejelea “watoto wadogo wanaoishi nyumbani.”)

 

      1.    Utaona kuwa utii unahitajika katika “kila jambo.” Hakuna ukomo wa “kama ipendezavyo katika Bwana.” Unadhani ni kwa nini iko hivi? (Wazazi wana uzoefu mkubwa ikilinganishwa na watoto.)

 

    1.    Katika Wakolosai 3:21 “akina baba” wanaambiwa “wasiwachokoze” watoto wao. Je, huu ni udhaifu kwenye matakwa ya watoto kutii?

 

      1.    Kwa nini hili linakomea kwa akina baba tu?  Watoto wanaambiwa wawatii wazazi wote wawili. (Akina baba ni viongozi wa familia, hivyo wao ndio wana uwezekano mkubwa wa kuchokoza.)

 

      1.    Jambo gani hasa linazuiwa kwenye kanuni ya “msiwachokoze?” Kwani kwa ujumla watoto hawaenendi kana kwamba wamechokozwa unapowaambia wasifanye jambo fulani? (Soma kitabu changu pendwa cha siku nyingi, Kumbukumbu la Torati 4:2. Akina baba (na walimu wa dini) wanapotunga sheria wanazodhani kuwa ni nzuri, na kuzihusianisha na Mungu, wanakuwa kwenye hatari ya kuwafanya watoto wawe na chuki, wakasirike au wachukie. Kwa ujumla nia ya mwenye mamlaka ni nzuri, lakini matokeo yake yanaweza kuwa ni kujitenga maishani mwao mwote na kukata tamaa.)

 

  1.   Mahala pa Kazi

 

    1.    Soma Wakolosai 3:22. Yumkini hakuna anayesoma hapa ni mtumwa halisi, ikimaanisha kuwa chini ya mamlaka kamili ya mtu. Je, unadhani ushauri huu pia unatumika kwa waajiriwa? (Kama uliingia kwa hiari yako kwenye makubaliano mahala pa kazi, ushauri wa Paulo unaonekana kuwa wa kuvutia sana. Kuwa mwajiriwa mwaminifu.)

 

      1.    Kwa nini Paulo anamchomeka Mungu kwenye ushauri wake? Kwa nini aandike, “mkimcha Bwana?”

 

    1.    Soma Wakolosai 3:23-24. Sasa Paulo anatoa uhusiano na Mungu wenye mantiki. Unaweza kufafanua uhusiano huo? (Paulo anasema kuwa Mungu ndiye anayetoa thawabu kwa kazi iliyotendeka kwa uaminifu. Hivyo, unapaswa kujichukulia kama unamfanyia Mungu kazi.)

 

      1.    Ukifanya kazi kwa bidii, na kwa ubora, je, maisha yako ya kazi yatakuwa mazuri? (Yatakuwa mazuri kwa sababu Mungu ndiye mwajiri wako wa mwisho. Anatoa thawabu kwa bidii ya kazi.)

 

      1.    Je, unadhani kuwa waajiriwa wanaofanya kazi kwa bidii, wanaofanya kazi kwa ubora, wanapadishwa cheo? (Hicho ndicho ninachokiona. Kwa ujumla kupandishwa cheo kunamaanisha kazi nzuri – ambayo kwa yenyewe ni thawabu.)

 

    1.    Soma Wakolosai 3:25. Kwa nini Paulo anahitimisha onyo hili kwa maneno, “hakuna upendeleo?” (Waajiriwa wavivu, wasio waaminifu wanapenda kumlaumu mtu mwingine kwa matatizo yao eneo la kazi. Paulo anawaambia kwamba matatizo yao katika eneo la kazi ni kasoro zao wenyewe; si kwamba kuna mtu anafanya upendeleo dhidi yao isivyo mantiki.)

 

    1.    Soma Wakolosai 4:1. Vifungu vichache vilivyotangulia ninawafundisha wanafunzi wangu kama sehemu ya kutawala hisia (emotional intelligence) kulikojengwa juu ya Biblia. Ili kuepuka mwonekano wa kwamba ninachukua upande wa mwajiri, pia ninawafundisha kifungu hiki. Paulo anatoa onyo gani kwa waajiri na wasimamizi wa kazi? (Hawatakiwi kuwaonea waajiriwa kwa sababu mwajiriwa na mwajiri wana bwana mmoja – ambaye ni Mungu.)

 

  1.      Kuzungumza na Watu Wengine

 

    1.    Soma Wakolosai 4:2-3. Kama ungekuwa Paulo, ombi lako la msingi kwa Mungu lingekuwa lipi? (Kutoka gerezani!)

 

      1.    Ombi la msingi la Paulo ni lipi? (Amsaidie kupata fursa bora zaidi za kupeleka injili. Hii inaendana na Wakolosai 3:2 ambapo Paulo anatuelekeza kuyaweka mawazo yetu kwenye “mambo yaliyo juu,” badala ya mambo ya duniani.)

 

    1.    Soma Wakolosai 4:4. Angalia nyuma katika Wakolosai 4:3. Paulo anamwomba Mungu aongee kwa wazi kuhusu jambo gani? (Kuhusu “siri ya Kristo.”)

 

      1.    Je, hili ni jambo tunalopaswa kumwomba Mungu? Ambalo tunaweza kulisema kwa uwazi? (Hili ni tatizo zaidi kwenye masuala ya kitaaluma, kwamba watu wanaandika na kuzungumza ili kukuonesha jinsi walivyo na akili tofauti na mawasiliano ya dhahiri. Wahariri wa magazeti wanahakikisha kuwa makala zao zinaandikwa ili kwamba wale wenye uwezo wa wastani wa kusoma wanaweza kuelewa. Hilo ndilo linalopaswa kuwa lengo letu tunapopeleka injili.)

 

    1.    Soma Wakolosai 4:5. Unaweza kufafanua Paulo anamaanisha nini anaposema “mkiukomboa wakati?” (Kama unatumia Facebook, unapaswa kutafakari ushauri wa mke wangu: “Kubishana na mtu kwenye Facebook kamwe hakumshawishi mtu yeyote.” Baadhi ya hoja ni upotevu wa muda tu.)

 

    1.    Soma Wakolosai 4:6. Paulo anapotuambia ushauri huu ni kutoa majibu sahihi, hii inachukulia (assume) jambo gani? (Kwamba tunapewa changamoto, au angalao kuulizwa maswali.)

 

      1.    Je, mara zote maelezo yak oni ya neema? Hususan pale unapoulizwa maswali?

 

      1.    Unadhani Paulo anamaanisha nini anaposema “yakikolea munyu?” (Chumvi inawezesha ladha. Hii inamaanisha kuwa hakikisha jibu lako linavutia kadiri inavyowezekana.)

 

    1.    Soma Matendo 13:10; Tito 1:10-13; Wagalatia 5:12; na Wafilipi 3:2. Je, Paulo ana tafsiri tofauti ya “ya neema” kuliko tafsiri tuliyo nayo leo? Au kuna jambo jingine linaloendelea hapa? (Kuamini kwamba Paulo aliufuata ushauri wake mwenyewe, lazima tuhitimishe kwamba hotuba ya neema haimaanishi kutoongea kwa ukali. Badala yake, lazima imaanishe kuongozwa kwa mafundisho ya Biblia na kilicho bora kwa manufaa ya msikilizaji.)

 

      1.    Je, umemsikiliza mtu anayejenga hoja ambaye, huku akiongea kwa utulivu na uwazi mkubwa, kwa dhahiri anazivunjavunja hoja za mpinzani wake? (Nadhani hiki ndicho anachokimaanisha Paulo anaposema hotuba “ya neema,” “iliyokolea munyu.”)

 

      1.    Paulo anaporejelea kujua “jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu,” je, anaashiria kwamba unapaswa kuwajibu watu tofauti tofauti kwa namna tofauti? (Kuijua hadhira yetu na kuandaa majibu yetu kwa maarifa hayo ni muhimu.)

 

    1.    Rafiki, ukiona kwamba unapata shida kuendana na watu wengine, je, somo hili la ushauri wa Paulo limekusaidia? Kwa nini pia usimwombe Roho Mtakatifu aongoze mwingiliano wako na watu wengine, kwa kuongezea kuufuata ushauri wa Paulo?

 

  1.   Juma lijalo: Kusimama Katika Mapenzi Yote ya Mungu.