Somo la 13: Kusimama Katika Mapenzi Yote ya Mungu

(Wakolosai 4:7-18)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
1
Lesson Number: 
13

Somo la 13: Kusimama Katika Mapenzi Yote ya Mungu

 

(Wakolosai 4:7-18)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Tumefika kwenye somo letu la mwisho katika mfululizo wa masomo haya. Hii ni hotuba ya Paulo ya kuwaaga washiriki wa kanisa lililopo Kolosai. Namna Paulo anavyowaelezea watenda kazi wenzake ni fundisho kwetu sote. Mnapomjadili mtu mnayemfahamu, je, pia mnabainisha mambo mabaya kumhusu? Au unayaweka katika hali chanya? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

  1.    Tikiko

 

    1.    Soma Wakolosai 4:7-8. Unadhani washiriki wa kanisa la Kolosai walimjua Tikiko? (Haionekani kama wanamfahamu.)

 

    1.    Soma Waefeso 6:21-22. Je, kutoa habari za Paulo na kuwahamasisha washiriki ndio wajibu wa msingi wa Tikiko?

 

      1.    Unafikia hitimisho gani unapoona kwamba kimsingi Paulo aliandika kitu kile kile kumhusu Tikiko kwa makanisa mawili?

 

  1.   Onesimo

 

    1.    Soma Wakolosai 4:9. Paulo anamwelezeaje Onesimo?

 

      1.    Je, inaonekana kama Wakolosai wanamfahamu Onesimo? (Ndiyo. Paulo anasema kuwa Onesimo ni “aliye mtu wa kwenu.” Ikimaanisha miongoni mwa watu kutoka Kolosai.)

 

    1.    Soma Filemoni 1:10-12 na Filemoni 1:15-18. Paulo anatuambia nini kumhusu Onesimo? (Kwamba ni mtumwa aliyekimbia. Paulo anamrudisha kwa bwana wake. Lakini Paulo anaandika kwamba Onesimo ni “moyo” wa Paulo. Paulo anampenda Onesimo na anamwangalia kana kwamba ni mtoto wa Paulo.)

 

    1.    Angalia tena Wakolosai 4:9. Je, ungeandika utangulizi kwa namna iyo hiyo?

 

      1.    Au ungebainisha kuwa Onesimo ni mtumwa aliyekimbia?

 

      1.    Unadhani Paulo anamaanisha nini anapomwelezea Onesimo kama “aliye mtu wa kwenu?” (Paulo anaweza tu kuwa anasema kwamba Onesimo anatoka mji huo huo. Lakini inawezekana zaidi anasema kuwa Onesimo ni Mkristo mwenzao, na si mtumwa.)

 

  1.      Aristarko

 

    1.    Soma Wakolosai 4:10. Kuna uhusiano gani kati ya Paulo na Aristarko? (Wote wawili ni wafungwa.)

 

    1.    Soma Matendo 19:29-31. Jambo gani limemtokea Aristarko, na Paulo anataka kufanya nini kuhusiana na jambo hilo? (Muktadha ni kwamba Paulo amekuwa akihubiri kuhusu Yesu pale Efeso, ghasia zikaanza ili kumlinda Artemis, mungu mke wa eneo lile, na Aristarko anakamatwa na kuburuzwa na wafanya fujo. Paulo anataka kuingia kwa haraka na kumwokoa Aristarko, lakini watendakazi wenzake wanadhani kuwa hili si wazo zuri.)

 

    1.    Soma Matendo 27:1-2. Aristarko ana uhusiano gani wa karibu na Paulo? (Yupo gerezani na Paulo zaidi ya mara moja. Alipata mateso mikononi mwa wafanya fujo ambao uwezekano mkubwa ni kwamba walikuwa wanamtafuta Paulo. Unaweza kusema kwamba mara zote yupo katika eneo hatarishi pale mambo mabaya yanapomtokea Paulo.)

 

  1.   Marko na Barnaba

 

    1.    Soma tena Wakolosai 4:10. Ni nani ambaye Wakolosai walimfahamu? Marko au Barnaba? (Ukweli kwamba Paulo anamuita Marko binamu [mjomba] wa Barnaba, inatuambia kuwa walimfahamu (au angalau walifahamu habari za) Barnaba.)

 

      1.    Kwa nini Paulo asiwe na uhakika kama Marko atakuja?

 

      1.    Unadhani Paulo alituma maelekezo gani kuhusiana na Marko?

 

    1.    Soma Matendo 15:36-40. Historia ya Yohana Marko ikoje linapokuja suala la kujitoa kwa ajili ya kazi ya injili? (Hapo awali aligeuka na kuachana na injili. Paulo na Barnaba hawakukubaliana kuhusu kumpatia nafasi nyingine.)

 

    1.    Wakolosai 4:10 inatufunulia nini kuhusu hamasa ya Barnaba katika mgogoro huu? (Yohana Marko ni familia. Ninahisi ukweli huu ulimhamasisha Barnaba, na huenda pia uliathiri mtazamo wa Paulo juu ya mgogoro.)

 

      1.    Unadhani hii ndio sababu Paulo hana uhakika kuhusu kama Marko atajitokeza ili kufanya kazi na Wakolosai? (Soma 2 Timotheo 4:11. Hii inatuonesha kuwa Yohana Marko sasa amekuwa msaidizi wa kuaminika.)

 

      1.    Je, unakuwa na kinyongo dhidi ya watu ambao wamewahi kukuangusha? (Jambo la msingi hapa ni kwamba Marko amejithibitisha kuwa mtu wa “kufaa sana.” Kama mshiriki wa kanisa mara kwa mara ananiangusha kwa kushindwa kufanya kile alichoahidi kukifanya, ninaacha kumwomba msaada mshiriki huyo. Huku si kuwa na kinyongo, ni kutenda kilicho bora kwa ajili ya kanisa.)

 

  1.    Yusto na Wayahudishaji

 

    1.    Soma Wakolosai 4:11. Paulo anamaanisha nini kwa maneno, “watu wa tohara?” (Anamaanisha kwamba wao ni Wayahudi, kama Paulo alivyo Myahudi.)

 

      1.    Paulo anarejelea nini? (Watoa maoni hawakubaliani, lakini Adam Clarke anaandika kuwa Paulo anawarejelea Aristarko, Yohana Marko, na Yusto.)

 

      1.    Kwa nini maoni haya ni ya kufaa? Hapo awali Paulo aliandika katika Wakolosai 3:11 kwamba tofauti za aina hii kanisani hazifai? (Paulo anamaanisha jambo tofauti. Palikuwepo na uhasama wa jumla kuhusu kuwaongoa Mataifa, na mgogoro juu ya namna gani waongofu wa Mataifa walitakiwa kuwa wa “Kiyahudi.” Paulo anatuambia kwamba wanaume hawa wenye asili ya Kiyahudi walimuunga mkono.)

 

    1.    Angalia tena Wakolosai 4:11. Unahitimisha nini Paulo anapoeleza kuwa hawa “ni watu watakatifu” wenye asili ya Kiyahudi wanaomuunga mkono? (Paulo anaonekana kukata tamaa kwa ukweli huu.)

 

  1.   Epafra

 

    1.    Soma Wakolosai 4:12-13 na Wakolosai 4:16. Epafra ni mtumishi wa namna gani anayefanya bidii pale anapoomba? (Kwa mujibu wa maoni ya the Popular New Testament, mada anayoitumia Paulo kwa Epafra, “mtumwa wa Yesu Kristo,” ni ya kipekee. Paulo anaitumia tu kujielezea, na mara moja kumwelezea Timotheo.)

 

      1.    Je, kujitahidi sana kwenye maombi ni jambo jema? (Ndiyo! Aina hii ya maombi itawasaidia Wakolosai “kusimama wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu.” Usiache kuwaombea wengine kwa udharura.)

 

        1.    Unadhani inamaanisha nini kusimama wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu? (Roho Mtakatifu amekuongoza kuwa na ujasiri katika uelewa wako wa mapenzi ya Mungu.)

 

    1.    Katika vifungu vya 13 na 16 Paulo analirejelea kanisa la Laodikia. Soma Ufunuo 3:14-17. Je, kanisa lililoko Laodikia lina aina zile zile za matatizo kama kanisa lililoko Kolosai? (Hapana. Laodikia imeridhika mno na i kipofu kiroho. Wakolosai wana kanisa ambalo kimsingi li na afya lakini linapigana dhidi ya fundisho la uongo.)

 

      1.    Kwa nini basi Paulo anawaambia Wakolosai wawape Walaodikia barua yao? (Ilikuwa miji inayokaribiana (miji jirani) katika bonde la Lycus.)

 

      1.    Hebu subiri kidogo! Kwa nini jiografia iwe jibu bora, au hata jibu zuri? (Jiografia yenyewe haiwezi kuwa jibu pekee. Si kila mtu katika kanisa moja ana mapambano ya kiroho yanayofanana. Wakati ridhaa (kuridhika) inaweza isiwe tabia inayowaelezea Wakolosai, inawezekana kwamba baadhi ya washiriki walikuwa na tatizo hili.)

 

  1.      Luka na Arkipo

 

    1.    Soma Wakolosai 4:14. Kwa nini Paulo ahitaji tabibu wakati miujiza ilijaa tele katika kanisa la awali? (Matabibu wanafahamu kwamba wajibu wao ni kuusaidia mwili katika kujiponya wenyewe. Bila kujali kama muujiza unatokea pole pole au haraka, Mungu ndiye mwanzilishi wa uponyaji.

 

    1.    Soma Wakolosai 4:17. Arkipo ni nani? (Soma Filemoni 1:1-2. Ni kama vile hatufahamu chochote kumhusu Arkipo, isipokuwa tu kwamba ni mtenda kazi mwenza wa Paulo.)

 

    1.    Soma Wakolosai 4:18. Tafakari juu ya namna Paulo anavyohitimisha barua yake kwa Wakolosai. Ni nini umuhimu wa sehemu hii ya barua yake kuandikwa kwa mkono wake mwenyewe? (Unaithibitisha na kuihalalisha barua.

 

      1.    Kwa nini Paulo anaandika kuhusu minyororo yake? (Huenda mnyororo ulifungwa kwenye mkono wake wa kulia, hivyo kufanya uandikaji wake kuwa mgumu zaidi.)

 

      1.    Kwa nini maneno ya mwisho ya Paulo yanahusu neema? (Ni ujumbe wa muhimu sana wa barua yake kwa Wakolosai. Tunaokolewa kwa neema pekee.)

 

    1.    Rafiki, kwa sehemu fulani Paulo aliandika barua hii kutokana na wasiwasi wake kwamba washiriki wa kanisa lililopo Kolosai walitishiwa na wale waliojenga hoja kuwa matendo yaliwastahilisha kuokolewa. Paulo aliwaandikia (Wakolosai 1:22) kwamba Yesu anatuweka kama “watakatifu, wasio na mawaa wala lawama” mbele ya Mungu. Je, utaipokea na kuikubali neema ya Mungu sasa hivi?

 

  1.     Juma lijalo: Tunaanza mfululizo mpya wa masomo juu ya “Kukua Katika Uhusiano na Mungu.”