Somo la 4: Nafasi ya Biblia

(Zaburi 19, Mithali 30, Mathayo 7)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
2
Lesson Number: 
4

Somo la 4: Nafasi ya Biblia

 

(Zaburi 19, Mithali 30, Mathayo 7)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Nilipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Andrews, nilikuwa kwenye Baraza la Wanafunzi. Nilikuwa na rafiki katika Baraza ambaye mawazo yake yalifanana na yangu. Sote tulijiita “waasi.” Rafiki huyu aliishia kuwa na kazi nzuri katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani na mara zote nimefanya kazi na Wakristo na wahafidhina. Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje wana sifa ya kuwa na msimamo wa kiliberali kisiasa. Siku hizi mtazamo wa rafiki wangu kisiasa unatofautiana kabisa na wangu. Hilo limetokeaje kwa wavulana wawili walioanza na mitazamo inayofanana? Ufafanuzi wa dhahiri ni kwamba baada ya muda fulani kupita tulishawishiwa na watu wanaotuzunguka. Huu ni mmojawapo wa kweli muhimu za maisha: tunabadilishwa kwa mambo tunayoyang’ang’ania na kuyashikilia. Angalia 2 Wakorintho 3:18. Unatumia kiasi gani cha muda kuangalia televisheni (runinga) ukilinganisha na kusoma Biblia? Je, unahitaji kubadilishwa? Hebu tuzame kwenye somo letu la nafasi ya Biblia katika kuyabadilisha maisha yetu!

 

  1.    Taa

 

    1.    Soma Zaburi 119:104-105. Kwa dhahiri hili ni jambo la kiishara. Unadhani inamaanisha nini?

 

      1.    Hebu tuanze na “njia yangu.” Ni nini hicho? (Njia yetu ni mwelekeo wa maisha yetu.)

 

      1.    Nini kinamaanishwa tunaposema “miguu yangu?” (Taswira hii ya picha inakuonesha ukijongea katika njia ya maisha.)

 

      1.    Biblia ina nafasi gani katika kuyafungua maisha yako? (Biblia inakupatia uelewa wa nini cha kufanya maishani.)

 

    1.    Soma Zaburi 19:7-9. Unaweza kuzipata wapi sheria ya Mungu, ushuhuda wake, amri zake, na maagizo yake? (Hii inaielezea Biblia.)

 

      1.    Biblia inaweza kukufanyia nini kwenye uwezo wako wa akili? (Inafanya mambo marahisi yawe ya busara.)

 

      1.    Biblia inaweza kufanya nini kwa ajili ya uelewa wako? (Huyatia macho yako “nuru,” ikimaanisha mtazamo wako kwa ulimwengu.)

 

    1.    Soma Zaburi 19:10. Ni nini thamani ya maboresho haya kwenye fikra na uelewa wako? (Yana thamani ya juu sana. Ni kiwango cha dhahabu.)

 

      1.    Kwa nini inasemwa kwamba Biblia ni tamu kama asali? (Haya si maelekezo ya mapishi, bali kauli ya kwamba maisha yako yatakuwa “matamu,” yatafurahisha.)

 

    1.    Soma Zaburi 19:11-12. Baadhi ya Wakristo wanadai kwamba kwa kuwa wao ni waaminifu, wanashambuliwa mara kwa mara na pepo wachafu. Vifungu hivi vinasema jambo gani linalounga mkono dhana ya kwamba maisha yaliyoishiwa kwa kuzingatia Biblia ni “matamu?” (Kujifunza Biblia hutuonya juu ya matatizo. Tunaweza kuzitambua kasoro na makosa yetu na kuyasahihisha. Hitimisho lenye mantiki ni kwamba matatizo mengi yanaibuka maishani kutokana na uamuzi wetu mbaya, kuliko kutokana na mashambulizi ya pepo wachafu.)

 

      1.    Ni vigumu kiasi gani kuona makosa na kasoro zetu? (Kifungu hiki kinaashiria kuwa ni vigumu kuona makosa yetu wenyewe. “Yamefichwa” kwetu.)

 

        1.    Kwa nini kujifunza Biblia ni suluhisho la matatizo haya yaliyofichika? (Kwa uzoefu wangu, tunaposoma Biblia Roho Mtakatifu anatutahadharisha kwenye mgogoro kati ya kile tunachojifunza na mtindo wetu wa maisha.)

 

  1.   Kuipokea Nuru

 

    1.    Soma 2 Timotheo 3:16-17. Biblia ina mamlaka kiasi gani? (Ina “pumzi ya Mungu.”)

 

      1.    Hiyo inamaanisha nini? Watu wanaponipa maelekezo, ninapendelea maelekezo hayo yaandikwe au yasemwe, na si ya “pumzi.” (Maneno haya “kupuliziwa pumzi,” yanatukumbusha kazi ya Roho Mtakatifu. Pia yanatuambia kuwa Mungu hakutoa nakala iliyoandikwa wa kile ambacho mwandishi wa Biblia anapaswa kukiandika.)

 

      1.    Ni nini matokeo ya mwisho pale Mkristo anapojifunza Biblia? (Ukamilifu. Kukamilishwa kwa ajili ya kila tendo jema.)

 

      1.    Hivi karibuni tulijifunza kwamba dhambi ilianza duniani kwa sababu Eva hakumwamini Mungu. Unawafahamu watu wangapi wanaoyategemea mawazo yao, badala ya mafundisho ya Biblia?

 

        1.    Je, hilo linakuelezea? (Vifungu hivi vinaashiria kuwa hatutakuwa “kamili” au “kukamilishwa” vizuri kama hatutamwamini Mungu kwa kutegemea mantiki yetu ya mambo.)

 

    1.    Soma 1 Wathesalonike 2:13. Jambo gani linaweza kuelezea utayari wa baadhi ya watu kubadilisha (substitute) maoni yao na mafundisho ya Biblia? (Kutoguswa kwamba haya ni maneno ya Mungu.)

 

    1.    Soma Waebrania 4:12-13. Je, unataka “kukatwakatwa?” (Hakuna anayetaka kuchomwa kisu.)

 

      1.    Biblia inafafanua nini hapa? Je, ni kizuri au kibaya? (Sababu mojawapo ya uzuri wa mantiki, na kudharauliwa sana na watenda maovu, ni kwamba inajielekeza kwenye ukweli. Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anatueleza kwamba tunapoelewa ukweli wa Biblia, huondoa udanganyifu binafsi (kujidanganya).)

 

        1.    Je, umewahi kupitia uzoefu huo? Maneno ya Biblia, yaliyojawa Roho Moatakifu, kupenya moyoni mwako na ukasalimu amri kwenye ukweli?

 

    1.    Soma Mithali 30:2-3. Maneno haya yaliandikwa na Aguri. Unadhani Aguri anafikiri kuwa kuna kasoro gani maishani mwake? (Anajiona mpumbavu. Kwa dhahiri, maisha hayamwendei vizuri.)

 

      1.    Aguri anakosa nini? (Hekima na maarifa ya Mungu.)

 

    1.    Soma Mithali 30:4. Kwa nini Aguri anadhani maarifa ya Mungu ni ya muhimu sana? (Anauangalia uumbaji na kusema Mungu ana jambo la kumfundisha.)

 

    1.    Soma Mithali 30:5. Ukisoma, kuelewa, na kutii kilichomo ndani ya Biblia, matokeo yake ni nini? (Unakingwa dhidi ya mambo mabaya maishani.)

 

    1.    Soma Mithali 30:6. Kwa ujumla huwa ninanukuu Kumbukumbu la Torati 4:2 kwa ajili ya kanuni hii, lakini inapatikana sehemu kadhaa katika Biblia. Unaposikia fundisho la Biblia, ni mara ngapi unaonywa dhidi ya kuongeza neno kwenye kile Biblia inachokisema tofauti na kuonywa dhidi ya kutokutii?

 

      1.    Ninakumbuka siku moja nikiwa kwenye kambi la kanisa nikila na mwinjilisti maarufu. Mshiriki wa kanisa akaja kulalamika kuwa mojawapo ya viungo kilikuwa na kitu alichodhani kuwa hatupaswi kukila. Baada ya kuondoka, mwinjilisti akaniambia kwa siri, “Tuna watu wengi wenye mitazamo ya ajabu kanisani kwetu.” Biblia inaonya kwamba ni nini hatari ya kuongezea neno kwenye Biblia? (Tutaonekana kama waongo. Mungu anaweza kutukaripia. Kwa hakika hatutakuwa na aina ya ushuhuda unaoufanya ulimwengu ufikiri, “Ninataka hilo.”)

 

  1.      Mwamba

 

    1.    Soma Mathayo 7:24-25. Je, Yesu anazungumzia juu ya ujenzi wa nyumba? Ikiwa sivyo, “nyumba” yetu ni ipi? (Yesu anazungumzia maisha yetu.)

 

      1.    Nyumba yako ikoje? Je, maisha yanakuendea vizuri?

 

    1.    Angalia tena Mathayo 7:25. Je, inaonekana kuwa mambo yanaenda vizuri kwenye nyumba anayoielezea Yesu? (Ni kinyume chake tu. Inashambuliwa na upepo, mvua, na mafuriko.)

 

    1.    Soma Mathayo 7:26-27. Yesu anamaanisha nini? (Kwamba ukiyajenga maisha yako kwenye mafundisho ya Yesu, utasalia imara utakaposhambuliwa. Lakini ukishindwa kuyajenga maisha yako kwenye mafundisho ya Yesu, maisha yako yataporomoka.)

 

      1.    Kifugu cha 27 kinapotuambia kuwa “anguko lake lilikuwa kubwa,” unaelewa nini kuhusiana na hilo? (Maisha ya mtu huyu yaliishia kwenye maafa makubwa.)

 

    1.    Soma Yoshua 1:7-8. Aina gani ya muda tunapaswa kuutumia kwenye Biblia ili “upate kufanikiwa sana kila uendako?” (Kutafakari “mchana na usiku” ndio jukumu lenyewe.)

 

      1.    Utangulizi wa somo hili unatupatia mfano wa jinsi tunavyoshawishiwa na kubadilishwa na ushirikiano wetu wa namna mbalimbali. Unatumia kiasi gani cha muda “kutafakari” mambo yanayokinzana na Biblia? (Tukitumia muda mwingi kwenye mambo yanayokinzana na Biblia kuliko muda tunaoutumia kwenye Biblia, matokeo yanatabirika.)

 

      1.    Je, kuna mambo mengine ya kuzingatiwa hapa? Je, kuna vigezo vingine tunavyotakiwa kuvizingatia kuhusiana na mambo yanayotushawishi? (Roho Mtakatifu ni kigezo cha muhimu. Shetani hapatikani kila mahala (not omnipresent). Televisheni haipatikani kila mahala. Roho Mtakatifu anapatikana kila mahala ikiwa tutamwomba aingie maishani mwetu.)

 

    1.    Rafiki, Biblia ndio mwongozo wa kuishi maisha mazuri. Ni mwongozo wa maisha yajayo. Kwa nini usijichimbie kwenye mwongozo wa Mungu kwa ajili ya maisha yako? Kwa nini usijitoe kufanya hivyo sasa hivi?

 

 

  1.   Juma lijalo: Jinsi ya Kujifunza Biblia.