Somo la 5: Jinsi ya Kujifunza Biblia

(Zaburi 119, Danieli 2, Mathayo 6)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
2
Lesson Number: 
5

Somo la 5: Jinsi ya Kujifunza Biblia

 

(Zaburi 119, Danieli 2, Mathayo 6)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Mwaka huu ni kumbukizi ya miaka 30 ya kijana wangu kubandika (posting) masomo haya ya kujifunza Biblia mtandaoni. Kuanzia mwaka 1975, nilipokuwa bado mwanafunzi wa sheria, nilikuwa sehemu ya ratiba ya kufundisha mwongozo wa kujifunza Biblia wa Shule ya Sabato kanisani. Kila kanisa jipya nililojiunga nalo lilinikaribisha vizuri kufundisha. Kuandika masomo haya ya Biblia na kuyafundisha darasani kulinilazimisha kujifunza Biblia mara kwa mara. Matokeo yake ni kwamba hii ikawa mojawapo ya baraka kubwa sana maishani mwangu! Nafasi hainiruhusu kufafanua namna nyingi ambavyo kujifunza na kuandika masomo ya Biblia kumenibariki. Kwanza, nadhani imenoa akili yangu. Pili, nina mtazamo chanya kwamba kufundisha Biblia kumenisaidia kuwa mwanasheria mzuri. Tatu, na muhimu zaidi, imenisaidia kumjua Mungu vizuri zaidi. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kama tunaweza kupata uthibitisho kwamba kujifunza Biblia kutayaboresha maisha yako!

 

  1.    Kunoa Uwezo wa Kufikiri

 

    1.    Soma Zaburi 119:98. Mtunga Zaburi anatuambia nini kuhusu jinsi neno la Mungu linavyompa manufaa dhidi ya maadui wake? (Biblia inamfanya kuwa na “hekima.”)

 

      1.    Mtunga Zaburi ana ufahamu wa Biblia kwa kiasi gani? (Anaandika kuwa “ninayo siku zote.” Hii inatuambia kuwa mtunga Zaburi si tu kwamba anaijua, bali pia anaichukulia kama chanzo cha maagizo.)

 

    1.    Soma Zaburi 119:99. Mtunga Zaburi anafurahia manufaa gani mengine kutokana na kujifunza kwake Biblia? (Ana uelewa mkubwa kuliko walimu wake.)

 

      1.    Hii inachukulia (assume) jambo gani kuhusu walimu wake? Je, ni wanafunzi wa Biblia? (Kama ni wanafunzi wa Biblia, hawajatumia muda wa kutosha kwenye Biblia. Lazima watakuwa watu ambao dunia inawachukulia kuwa ni wasomi wazuri.)

 

      1.    Hii inaongezea nini kwenye uelewa wetu wa namna mtunga Zaburi anavyoiendea Biblia? (Anaitafakari.)

 

        1.    Unadhani inamaanisha nini “kuifikiri (kuitafakari)” Biblia? (Nadhani inamaanisha kujifunza Biblia kwa kina na kutafakari kile inachomaanisha.)

 

    1.    Soma Zaburi 119:100. Nani mwingine ana hasara kwa sababu mtunga Zaburi anajifunza Biblia? (“Wazee.”)

 

      1.    Hebu tulijadili hili kidogo. Jambo gani linamfanya mzee kuwa mwerevu? Au kuwa na Hekima? (Kwa muono wangu, vijana wapumbavu wakati mwingine huwa wazee wapumbavu. Jambo ambalo muda unapaswa kutufundisha kila mmoja wetu ni jinsi ya kukabiliana na matatizo. Kwanza kabisa hii itajumuisha kutatua mambo magumu na kuepuka matatizo.)

 

        1.    Ni kwa namna gani kivitendo kujifunza Biblia kunatusaidia katika eneo hilo? (Mtunga Zaburi anatuambia kuwa “anayashika” mafundisho ya Biblia. Biblia ni mwongozo wa kuishi maisha bora. Unaweza kupata mafunzo maishani ama kwa kugongesha uso wako kwenye matatizo, au kujifunza kutokana kwenye Biblia jinsi ya kuepuka matatizo.)

 

    1.    Pitia kwa haraka haraka Zaburi 119:98-100. Ujumbe wa jumla wa mtunga Zaburi ni upi? (Kama wewe ni adui, mwalimu mwenye msaada, au mzee, mtunga Zaburi ana faida kuliko wote hao. Kwa nini? Kwa sababu ya uelewa wake wa Biblia.)

 

    1.    Soma Zaburi 119:101-102. Je, mtunga Zaburi ni mtu anayejua Biblia inachokisema pekee? (Hapana. Anasema kuwa anatii kile ambacho Mungu amekisema kwenye Biblia.)

 

    1.    Soma Zaburi 119:103. Matokeo yake ni yepi kwa mtunga Zaburi? (Maisha ni mazuri. Anapenda kile anachojifunza kutoka kwenye Biblia.)

 

      1.    Watu wangapi wanasema kuwa wanasoma na kujifunza Bibia? (Wengi wanapata ugumu kwa sababu wanakataa kile Biblia inachokisema. Mtunga Zaburi anatuambia kuwa inayafanya maisha yake kuwa mazuri, ndio maana anauona kama uzoefu chanya kabisa.)

 

    1.    Soma Zaburi 119:104-105. Unadhani kwa nini mtunga Zaburi anachukia “kila njia ya uongo?” (Njia yake maishani iko wazi kutokana na kujifunza kwake Biblia. Anaona kwamba kugeuka na kuiacha Biblia hatimaye husababisha huzuni.)

 

    1.    Soma Isaya 55:10-12. Tunapolitii neno la Mungu, tutarajie kuwa na mtazamo wa namna gani? (Tunapitia uzoefu wa furaha, amani, na kusherehekea.)

 

  1.   Siri Zafunuliwa

 

    1.    Soma Mwanzo 1:1 na Waebrania 11:3. Ni muhimu kiasi gani kwako kuelewa jinsi tulivyopata kuwepo katika ulimwengu wetu?

 

    1.    Soma Danieli 2:20-22. Danieli anatuambia nini tunachoweza kujifunza kutokana na kuwa na uhusiano na Mungu? (Mambo ya kina ya ulimwengu yaliyofichwa.)

 

    1.    Soma Danieli 2:16 na Danieli 2:27-28. Ni nini muktadha wa Danieli kusema kuwa Mungu atafunua mambo ya kina yaliyofichwa ya ulimwengu? (Haya ni maelezo ya njozi ya sanamu ya Mfalme Nebukadreza. Alichokifunua Mungu kupitia kwa Danieli na njozi hii ndio historia ya ulimwengu iliyofuatia! Tunasoma habari hii kwenye Biblia na kujifunza kuhusu mustakabali wetu. Hivyo, Biblia inafunua tulipotoka na wapi ulimwengu unakoelekea.)

 

    1.    Hadi kufikia hapa tumeangalia hamasa yetu ya kujifunza Biblia. Hebu tugeukie katika sehemu inayofuata jinsi tunavyopaswa kujifunza Biblia.

 

  1.      Kutenga Muda

 

    1.    Soma Mathayo 6:33. Je, kuna fundisho katika hili kwa ajili ya kujifunza kwetu Biblia? (Tunatakiwa kuipa kipaumbele. Kiuhalisia ninajaribu kuzingatia hili kwa kufanya jukumu langu la kwanza ninapoianza siku liwe kujifunza Biblia ili kwamba niweze kuandika somo hili.)

 

    1.    Soma Matendo 17:10-11. Ni mara ngapi Wayahudi wa Beroya walijifunza Biblia? (Walijifunza kila siku.)

 

      1.    Walikuwa na mtazamo wa namna gani katika kuendea kujifunza kwao? (Walikuwa na hamu ya kuujua ukweli. Walitaka kutenganisha ukweli na uongo.)

 

    1.    Soma Isaya 28:9-10. Biblia inapotuambia kujifunza “amri juu ya amri,” unadhani hiyo inamaanisha nini? (Inamaanisha kwamba tunapaswa kujenga uelewa wetu wa Biblia juu ya fundisho la jumla la Biblia. Uelewa wetu wa ukweli haupaswi kujengwa juu ya kifungu kimoja ambacho kinaweza kisiwe na upatanifu na Maandiko yote ya Biblia yaliyosalia.)

 

    1.    Soma Yoshua 1:8. Unadhani tunaambiwa tusifanye jambo lolote bali kujifunza Biblia? (Sidhani kama ni hivyo. Badala yake, hii inatuambia juu ya kuitafakari Biblia na kile inachotufundisha.)

 

      1.    Una muda kiasi gani wa “kutafakari” maishani mwako? (Watu wengi ninaowafahamu wana jambo la kuwaburudisha linaloendelea muda wote. Wanatazama televisheni, wanaperuzi simu zao, au wanavaa vifaa vya kusikilizia sauti vya masikioni (headphones) vinavyowapitishia muziki au maburudisho mengine. Muda tulivu wa kutafakari unakuwa hadimu.)

 

      1.    Fikiria juu ya nyakati ambazo jambo la kufurahisha au kuhuzunisha lilikuwa linaendelea maishani mwako. Je, ulilitafakari katika nyakati zako za ziada? (Hilo hunitokea. Biblia inatuhamasisha kuwa na uzoefu wa namna hii na Biblia.)

 

      1.    Unadhani Biblia inapendekeza tafakari ya ufahamu (conscious), au tafakari ya bila kujijua (unconscious) inatosha? (Mwanasheria asiye upande wangu anaponitumia jambo kimaandishi, ninajaribu kulisoma mara moja, hata kama nina majuma kadhaa ya kulijibu. Ninafanya hivyo kwa sababu akili yangu itaanza kulifanyia kazi ya kujibu hoja zao bila kufahamu.)

 

        1.    Je, unaweza kufanya hivi na Biblia?

 

  1.   Zana Kutoka Nje

 

    1.    Soma Zaburi 119:18. Mtunga Zaburi anaomba nini? (Hili ni ombi kwamba Mungu amsaidie kuelewa mambo makuu katika Biblia. Hii ni kukiri kwamba tunahitaji msaada wa Mungu ili kuelewa.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 2:11-13. Kwa nini Roho Mtakatifu ni wa muhimu sana katika kuielewa Biblia? (Ni Roho wa Mungu, na hakuna anayemjua Mungu kama anavyojijua.)

 

      1.    Hii inakufundisha nini kuhusu kujifunza Biblia kupitia masomo kama haya? (Ninamwomba Roho Mtakatifu kuniongoza kuandika masomo haya. Lakini hatima ya yote ni kwamba, msomaji anatakiwa kumwomba Roho Mtakatifu ili kuyajua mambo “tuliyokirimiwa na Mungu.”)

 

    1.    Soma Yohana 14:26 na 2 Timotheo 3:16-17. Roho Mtakatifu na Maandiko wanafanyaje kazi pamoja katika usomaji wetu na kuielewa kwetu Biblia? (Roho Mtakatifu anatufundisha na kutufunulia akilini mwetu kweli ambazo tayari tumejifunza. Maandiko hufundisha, huonya, hongoza, na hutuadibisha katika haki ili tuweze kuwa kamili kwa ajili ya kila tendo jema. Utaona kwamba Maandiko “yana pumzi ya Mungu.” Hiyo inaashiria kuwa Roho Mtakatifu ni wakala aliye hai.)

 

    1.    Rafiki, Mungu anaahidi kwamba ikiwa tutajifunza neno lake, na kuufanya mwongozo wake kuwa sehemu ya maisha yetu, hatutafurahia manufaa ya kiakili pekee, bali pia tutakuwa na maisha ya amani na furaha. Je, ungependa kuwa na hayo? Kwa nini usifanye uamuzi sasa hivi kulifanya suala la kujifunza Neno la Mungu kuwa sehemu ya ratiba yako ya kila siku?

 

  1.    Juma lijalo: Mashuja wa Maombi.