Somo la 8: Kuwa na Imani

(Mathayo 11, Waebrania 11, Mathayo 15, Waefeso 2)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
2
Lesson Number: 
8

Somo la 8: Kuwa na Imani

 

(Mathayo 11, Waebrania 11, Mathayo 15, Waefeso 2)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Rafiki wangu wa karibu niliyefanya naye kazi kwenye kesi nyingi mara kwa mara alikuwa akitumia muda wake wa chakula cha mchana kutembea na kuzungumza nami kuhusiana na Biblia. Alikuwa Mkatoliki ambaye, kama alivyoongea kwa mzaha, “alisoma Biblia yake.” Baadaye maishani, alipitia majanga kadhaa. Mke wake alikataa kuambatana naye kwenye kazi yake mpya na muhimu ya kisheria. Muda mfupi baadaye, alipoteza kazi yake mpya. Kisha akaambiwa kuwa alikuwa na ugonjwa wa saratani. Nilimtembelea muda mfupi kabla hajafariki. Aliniambia kuwa alifahamu kwamba ningependa kuzungumza naye kuhusu imani yake, lakini hilo halikuwa jambo ambalo angetaka kulijadili. Kisha akafariki. Hakuwa mtu wa kwanza niliyemfahamu aliyekuwa na imani kubwa, lakini akaonekana kuikatia tamaa alipokabiliana na dhiki/taabu na kifo. Kuishika imani yetu ni jambo la muhimu sana. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusiana na kuishika imani!

 

  1.    Imani Katikati ya Taabu na Kifo

 

    1.    Soma Marko 8:11-12 na Mathayo 11:2-3. Katika matukio haya mawili tunaona Mafarisayo na Yohana Mbatizaji wanamuuliza Yesu kuhusu ishara kama yeye ndiye Masihi. Kuna tofauti gani kwenye hayo maombi mawili? (Mafarisayo wanahojiana na Yesu na kujaribu kumjaribu Yesu. Yohana Mbatizaji hakuwa adui wa Yesu.)

 

      1.    Unadhani kwa nini Yesu alikataa kuwapatia Mafarisayo ishara?

 

        1.    Je, hili lilikuwa suala la kuhamasisha imani?

 

    1.    Soma Mathayo 11:4-6. Je, Yesu anawapa ishara wanafunzi wa Yesu?

 

    1.    Soma Yohana 1:32-34. Je, hapo awali Yohana Mbatizaji alielezea imani yake kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu? (Ndiyo. Alikuwa na ushahidi wa dhahiri kabisa kwamba Yesu alikuwa Masihi.)

 

      1.    Unadhani kwa nini imani ya Yohana ilisitasita? Kwa nini sasa hana uhakika? (Nadhani Yohana amekata tamaa kwamba Yesu hajafanya lolote kumfanya aachiwe kutoka gerezani.)

 

      1.    Angalia tena ishara katika Mathayo 11:5. Je, hizi ni Ishara zinazomnufaisha Yohana?

 

      1.    Unadhani Yesu anamwambia nini Yohana katika Mathayo 11:6? Ni kwa namna gani Yohana Mbatizaji anaweza “kukosewa (offended)” na Yesu? (Inaleta mantiki kuamini kwamba Yohana Mbatizaji alikuwa kama wanafunzi wa Yesu. Walitarajia kwamba Yesu angesimika ufalme wake duniani. Ni kwa jinsi gani basi Yohana, ambaye alimtambulisha Yesu kwa ulimwengu, aachwe kuozea gerezani?

 

    1.    Soma Mathayo 11:11-12. Ni kwa jinsi gani Yohana ni vyote viwili, yaani, mkuu na mdogo? Kwa nini Yesu anamzungumzia Yohana na nguvu/vurugu? (Yohana si “mdogo” kwa tabia au uaminifu. Bali, hata mtu mdogo anayeishi kwa kuzingatia maisha, kifo, na ufalme wa Yesu ana faida ambayo Yohana hakuishi kuishuhudia. Rejea ya nguvu/vurugu inaweza kujumuisha upinzani mkali ambao tayari umemweka Yohana gerezani na muda mfupi tu ujao utamuingiza kwenye kifo. Kwa upana zaidi, Yesu anaonekana kusema kuwa ufalme wa mbinguni unatangazwa mbele ya upinzani mkali.)

 

      1.    Mazungumzo haya na wanafunzi wa Yohana yanawafundisha nini wale, kama ilivyokuwa kwa rafiki wangu, ambao imani yao inatetereka kutokana na taabu? (Tunatakiwa kushikilia imani yetu, tukiamini kuwa Yesu amechukua hatua kwa ajili ya wokovu wetu na hatimaye atafanya mambo yote kuwa sawa. Tunaweza tusielewe kinachoendelea, lakini tunatakiwa kumwamini Yesu.)

 

  1.   Imani na Matokeo Yasiyo Sawa

 

    1.    Soma Waebrania 11:1-2. Je, tafsiri hii ya imani inaonekana kuwa sahihi kwako? (Imani ni kuamini katika mambo ambayo bado hayajatokea. Hii ndiyo hali aliyokuwa nayo Yohana Mbatizaji.)

 

    1.    Soma Waebrania 11:32-34. Ni lini watu hawa waliona imani yao ikitimizwa? (Wakati bado wakingali hai.)

 

    1.    Soma Waebrania 11:35-38. Fikiria kwamba vifungu hivi vinayaelezea maisha yako na ulikuwa na marafiki wa Kikristo ambao maisha yao yalifafanuliwa na vifungu vya 32-34. Ungejisikiaje? Wivu? Hasira? Je, ungeamini kuwa maisha hayatendi haki? Mungu hatendi haki?

 

    1.    Ninamkumbuka rafiki wangu mwema aliyekuwa mshiriki wa kanisa langu. Alikuwa mwerevu, mzuri, aliyeelimika, na alikuwa na kazi nzuri. Aliniambia kwa siri kwamba inaonekana kuwa watu wengine walikuwa na hali bora kuliko yeye. Alionekana kudhani kwamba haikuwa haki kwamba hakuwa na “mafanikio.” Kisha akafariki katika umri wa miaka 50. Tuseme nini kuhusu maisha yake? (Soma Waebrania 11:39-40. Waebrania inatuambia kuwa hata wale waliopokea ushindi mkuu katika haya maisha hawakupokea ahadi ya mwisho hapa duniani. Mungu ametoa jambo bora zaidi: ufufuo, ufalme, na maisha yaliyokamilishwa tutakayoyaishi pamoja.)

 

      1.    Je, kuitazamia ahadi ya Yesu ndio tafsiri ya imani?

 

  1.      Imani na Dhamira

 

    1.    Soma Mathayo 15:22. Mkananayo huyu anasema nini kumhusu Yesu? (Anaonesha kuwa anaamini Yesu ni Masihi.)

 

    1.    Soma Mathayo 15:23. Unakuwa na mwitiko gani pale mtu anapokupuuzia? Hususani pale unapodhani inaweza kutokana na wao kuwa na hadhi ya juu sana kuzungumza na wewe?

 

    1.    Soma Mathayo 15:24-26. Unakuwa na mwitiko gani mtu anapokuita “mbwa?” Anapomaanisha kuwa watoto wako ni “mbwa?”

 

    1.    Soma Mathayo 15:27-28. Kuna fundisho gani juu ya imani tunalopaswa kujifunza hapa? (Tunatakiwa kushikilia imani yetu kwa nguvu hata pale mazingira yanapofedhehesha.)

 

      1.    Kwa nini Yesu alimfanya mwanamke huyu apitie udhalilishaji? (Yesu hayuko kwenye biashara ya kutudhalilisha. Anatupenda. Yesu anaileta imani ya mwanamke huyu hadharani, si kwa lengo la kumdhalilisha, bali kusifia imani yake na kuwafundisha wanafunzi wake kwamba imani ya kudumu inaweza kupatikana hata miongoni mwa wale ambao walikuwa na mwelekeo wa kuwadharau au kuwapuuza. Kisa hiki kinatupatia fundisho sote tangu kizazi hata kizazi kuishikilia imani hata katika mazingira ya udhalilishaji.)

 

      1.    Mfikirie rafiki niliyembainisha katika sehemu ya utangulizi. Je, ilikuwa ni udhalilishaji kwa mkewe kumwacha? Je, ilikuwa ni udhalilishaji kupoteza kazi yake ya hali ya juu? Ongezea hili katika hilo kwamba mimi, mwanasheria wake mdogo kwa miaka mingi, nilimtafutia kazi yake iliyofuatia. Alikuwa rafiki mwenye afya nzuri sana. Je, ni udhalilishaji kwa mtu mwenye afya nzuri kufa mapema kwa saratani?

 

  1.   Imani Katika Uwanja Sawia

 

    1.    Soma Waefeso 2:1-3. Hivi punde tu tumejadili kuwa tunaweza kuona kuwa watu wengine wanaonekana kuishi maisha bora kuliko sisi. Hii inatuambia nini kuhusu nafasi yetu kwa wengine? (Sote tuna hitaji kubwa sana la msaada.)

 

    1.    Soma Waefeso 2:4-6. Tumaini letu pekee la wokovu na kupandishwa hadhi ni lipi? (Yesu atatuinua na kutuketisha mahali pa mbinguni tukiwa pamoja naye.)

 

    1.    Soma Waefeso 2:7-9. Yesu atatupatia aina gani za “wingi wa neema upitao kiasi?” (Neema yake ni zawadi. Wema wake ni zawadi. Kingine kitakachoambatana nacho mbinguni, ni “wingi” na “upitao kiasi.”)

 

      1.    Nini kinachotakiwa kwetu? (Imani.)

 

      1.    Hatutakiwi kufanya nini ili kupokea hii zawadi? (Matendo hayatufaidishi zawadi. Wokovu unapatikana kwa neema kwa njia ya imani, na kazi yote ya wokovu ni zawadi ya Mungu, “wala si kwa matendo.”)

 

      1.    Ujumbe wa jumla kwetu ni upi? (Tushikilie! Tusiiache imani yetu.)

 

    1.    Soma Waefeso 2:10. Hii inatuambia nini kuhusu matendo yetu? (Hayatuokoi, lakini tuliumbwa ili kutenda matendo mema. Tunapaswa “kuenenda” katika matendo mema.)

 

  1.    Imani na Ustahamilivu

 

    1.    Soma Ufunuo 14:12. Tunaambiwa tufanye nini? (Kuvumilia. Kuendelea kuishika imani hata kama inaweza kuwa vigumu.)

 

    1.    Soma Ufunuo 14:9-11. Watu wengine wanaendeleaje? Wale wanaokata tamaa na kujisalimisha? (Hatima ya wale wanaomkataa Mungu inatisha sana kiasi kwamba wito wa kuvumilia ndio njia rahisi. Haijalishi uaminifu unaweza kuonekana kuwa mgumu kiasi gani sasa, ni bora sana kuliko kumwasi Mungu.)

 

    1.    Angalia tena Ufunuo 14:12. Maisha ya mtakatifu yanaonekanaje? (Imani na utii.)

 

    1.    Rafiki, kuwa imara! Usigeuke na kuacha kumwamini Mungu hata kama maisha yanakuwa magumu. Yesu hataki uteseke, na anaahidi kwamba ukimshikilia utaishi milele katika furaha.

 

  1.   Juma lijalo: Dhambi, Injili, na Sheria.