Somo la 9: Dhambi, Injili, na Sheria

(Waamuzi 14 & 16, Warumi 3, Mathayo 5-7)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
2
Lesson Number: 
9

Somo la 9: Dhambi, Injili, na Sheria

 

(Waamuzi 14 & 16, Warumi 3, Mathayo 5-7)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Je, unapenda kujadili dhambi? Vipi kuhusu dhambi zako? Watu wengi ninaowafahamu hawapendi kutembelewa na mwakilishi wa kanisa ili kujadili dhambi zao. Unapojadili dhambi na Wakristo wengine, je, unajikita kwenye hasara binafsi zinazotokana na kutenda dhambi – ikiwemo kupoteza uzima wa milele? Kujifunza kwangu Sala ya Bwana kunanielekeza kudhani kuwa Yesu anatupatia njia tofauti. Mathayo 6:9-10 inaelezea malengo mawili. Kwanza, kumtukuza Mungu. Pili, kuyafanya mapenzi ya Mungu yatimie duniani kama yanavyotimia mbinguni. Mungu alitupatia Amri zake Kumi ili kutuongoza katika kuishi maisha mazuri. Maisha yanayoepuka matatizo makubwa. Wakati ambapo Mungu wetu mwenye upendo anajali kuishi kwetu vizuri, manufaa makuu yanayotokana na maisha mazuri ni utukufu yanayompa Mungu. Hebu tuichimbue sheria, dhambi, na kile ambacho tayari Mungu amekitenda kuhusiana navyo!

 

  1.    Samsoni

 

    1.    Soma Waamuzi 14:1-3. Wazazi wa Samsoni wanapowarejelea Wafilisti kama “wasiotahiriwa,” walikuwa na wasiwasi gani? (Wazazi walipinga Wafilisti kutoshiriki agano la imani la Israeli. Mungu alikataza waziwazi kuoana na Wakanaani. Angalia Kumbukumbu la Torati 7:3-4. Wafilisti hawakuwa Wakanaani, lakini sababu ya Mungu ya zuio kimantiki ilihusika kwa Wafilisti.)

 

      1.    Je, Samsoni alikuwa mtiifu kwa wazazi wake? Je, alikuwa anatafuta ushauri kutoka kwa wazazi wake? (Hapana. Alisema uamuzi wake binafsi ulikuwa mzuri kiasi cha kutosha.)

 

    1.    Soma Waamuzi 14:8-9. Kwa nini Samsoni hakuwaambia wazazi wake alikoipata asali? (Tukio hili lisilo la kawaida lilikiuka, angalau, sheria inayohusu kugusa mzoga wa mnyama najisi. Mambo ya Walawi 11:27 inamjumuisha mnyama kama vile simba na kusema kuwa kuugusa mzoga wake humfanya mtu kuwa najisi. Kwa kuongezea, wito wa Unaziri wa Samsoni ulihitaji kutijenga kipekee kwa Mungu, na Hesabu 6:6-7 inaonesha kuwa kugusana na kifo (maiti) hakukuendana na wito huo.)

 

      1.    Je, hapa Samsoni anatenda dhambi? (Kura yangu ni, “ndiyo.”)

 

    1.    Soma Waamuzi 14:4. Je, tumejifunza kwamba wazazi hawakuwa sahihi kwenye ushauri wao uliojengwa juu ya Biblia kutomuoa mwanamke wa Kifilisti? Au, hapa Samsoni ametenda dhambi? (Hii haimaanishi wazazi wa Samsoni walikuwa na makosa. Bali, kimamlaka Mungu alikuwa anatumia uchaguzi mbaya wa Samsoni kama fursa dhidi ya Wafilisti.)

 

    1.    Soma Waamuzi 14:15. Je, ndoa ya Samsoni ni mpango mzuri kwa ajili ya mkewe mpya na familia yake?

 

    1.    Soma Waamuzi 16:20-21. Tumeruka sehemu kubwa ya maisha ya Samsoni yenye utata. Kukiuka sheria za Mungu kumemfanyia nini Samsoni?

 

    1.    Soma Waamuzi 16:27-30. Una maoni gani juu ya hatima ya Samsoni?

 

      1.    Ingeweza kuwa na tofauti gani endapo angemtii Mungu tangu ujanani mwake?

 

    1.    Soma Waebrania 11:32-34. Hii inaitwa “Sura ya Imani,” na Samsoni ni mmojawapo wa mashujaa waliohusishwa. Una mwitiko gani juu ya hili?

 

    1.    Soma Waebrania 11:1-2. Samsoni ni miongoni mwa wale waliosifiwa na Mungu! Je, ameokolewa? (Sifikirii kama hakuokolewa.)

 

      1.    Unalifafanuaje hili? (Injili ni kwamba wokovu huja kwa imani, si matendo. Tutaijadili injili katika sehemu inayofuata.)

 

  1.   Injili

 

    1.    Soma Mathayo 5:17-20. Yesu anamaanisha nini anaposema kuwa alikuja “kutimiliza” torati?

 

      1.    Nani, ambaye katika kipindi cha maisha ya Yesu duniani, alikuwa mwangalifu zaidi juu ya kuishika sheria kuliko waandishi na Mafarisayo?

 

    1.    Soma Warumi 3:21-23 na Warumi 3:28. Je, hii ni njia tofauti ya kuifikia haki? (Ndiyo, ni “haki ya Mungu” inayopatikana “pasipo sheria.” Ni njia ya kweli.)

 

    1.    Soma Warumi 3:24-26. Je, hii inafafanua jinsi Yesu alivyoweza kusema kuwa alikuja “kutimiliza” torati? (Yesu aliitimiliza torati kwa kuishika kwa ukamilifu, kwa kudhihirisha maana yake halisi, na kwa kutimiliza mfumo wa kafara kwa njia ya kifo chake. Hakuifuta sheria; alionesha maana yake kamili na kutimiza adhabu yake kwa ajili yetu.)

 

    1.    Soma Mwanzo 15:6 na Warumi 4:5-7. Haki yetu inawezaje “kuzidi” ile ya waandishi na Mafarisayo? (Sasa tunaona kuwa haki ya Yesu, pale tunapoipokea, hutoa haki ambayo inaizidi haki ya waandishi na Mafarisayo kwa mbali sana.)

 

      1.    Je, haki ya Samsoni ilizidi ile ya waandishi na Mafarisayo?

 

  1.      Sheria

 

    1.    Soma Warumi 3:31. Kama tuna njia tofauti na ya kweli kuufikia wokovu, na tunayo, hilo linawezaje “kuithibitisha” sheria?

 

    1.    Kwa muda usiopungua miaka kumi kuna barabara niliyokuwa nikipita kwa gari langu kutoka ofisini kwenda uwanja wa ndege. Nilipokuwa nikielekea uwanja wa ndege moja kwa moja (automatically) nilikuwa nikitumia barabara hii. Siku moja niligundua kwamba nikiendesha gari hadi kuvuka uwanja wa ndege, ningeweza kutoka barabara kuu na kuingia kwenye barabara ndogo ambayo (cha kushangaza) ilikuwa ya moja kwa moja na kutumia muda mfupi. Unadhani niliirudia tena barabara yangu ya zamani? Kama haki kwa imani ni njia sahihi ya kuifikia haki, kwa nini nirejee kwenye njia ya waandishi na Mafarisayo? (Njia ya imani si tu “sahihi,” bali ndio njia pekee inayowezekana.)

 

      1.    Ikiwa jibu kwa swali la awali ni kwamba kamwe hatutarudi nyuma, basi tunapaswa kuelewaje kwamba lazima “tuithibitishe” sheria? (Ikiwa kitabu cha Warumi hakizungumzii kurudi nyuma kwenye njia ya kufanya kazi kwa ajili ya wokovu wetu, lazima iithibitishe sheria kwa sababu nyingine. Inaweza kuwa sababu gani hiyo?)

 

    1.    Soma Warumi 6:1-2. Hii inatuambia nini kuhusu faida za matendo? (Sheria inatuambia namna ya kuishi. Hatutaki kuishi dhambini. Alichotutendea Yesu kinaonesha umuhimu wa kushindwa kwa dhambi.)

 

    1.    Soma Warumi 6:6. Hii inatupatia taswira gani ya dhambi? (Inasema kuwa dhambi “inatutumikisha.” Je, unataka kuwa mtumwa? Sheria ya Mungu inatuongoza kwenye maisha bora – maisha ambayo hatutumikishwi.)

 

    1.    Soma Mathayo 7:21. Je, Yesu anatuambia kuwa tulichojifunza hivi punde katika kitabu cha Warumi si sahihi? Je, njia ya waandishi na Mafarisayo ambao waliamini walikuwa wakiyatenda mapenzi ya Baba wao, kimsingi ndio njia bora?

 

      1.    Je, tuna ukinzani kati ya mafundisho ya Yesu na Paulo (katika kitabu cha Warumi)?

 

    1.    Hebu tuendelee. Soma Mathayo 7:22-23. Utetezi wa waliopotea ni upi? (Wanaonekana kudai njia ya waandishi na Mafarisayo kwa sababu wanaorodhesha matendo yao mema.)

 

      1.    Je, kweli haya ni matendo yao mema? Kinahitajika kitu gani kufanya unabii kwa jina la Yesu, kutoa pepo kwa jina lake, na kutenda mambo makuu kwa jina lake? (Ikiwa madai haya ni ya kweli, na hilo ni swali kubwa, matendo haya yalitendwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.)

 

      1.    Ikiwa Roho Mtakatifu, ambaye ni Mungu, alishirikiana nao kutenda mambo haya, Mungu anawezaje kusema, “Sikuwajua ninyi kamwe?” Wangeweza kujibu, “tukumbuke, sisi ni washirika wako wa zamani.” Unalifafanuaje hili?

 

    1.    Hebu tupitie tena Mathayo 7:21. Ikiwa watu hawa waliopotea wanasema ukweli (suala ambalo nina mashaka nalo, kwa kuwa wapotofu wanaweza kusema uongo), unadhani Yesu anamaanisha nini kwa kauli “afanyaye mapenzi ya Baba yangu?” (Nadhani tatizo kuu ni kwamba watu hawa wanayategemea matendo yao (matendo makuu) kama sababu ya kuingia katika ufalme wa mbingu.)

 

    1.    Hebu tupitie Sala ya Bwana kwa mara nyingine. Soma Mathayo 6:9-10. Sababu gani imetolewa hapa ya utii wa sheria? (Tunampa Mungu utukufu (jina lako litukuzwe) kwa mapenzi ya Mungu kutimizwa “hapa duniani kama huko mbinguni.”)

 

      1.    Angalia tena Mathayo 6:5. Je, hii inakukumbusha wale wanaodai matendo makuu kama ufunguo wao wa kuingia mbinguni? (Inaakisi hatari ile ile ya kiroho. Matendo yalifanyika kwa ajili ya kushangiliwa hadharani, kama jinsi maombi yalivyofanyika ili kuwafurahisha watu wengine.)

 

    1.    Soma Mwanzo 12:1-3 na Mwanzo 18:19. Unadhani kwa nini Mungu alimchagua Abramu kwa ajili ya utume huu? (Mungu alitaka kushirikiana na mtu ambaye angeutangaza ufalme wa Mungu hapa duniani.)

 

      1.    Mungu alitakiwa kuchagua kutoka kwa watu wangapi kwa ajili ya utume huu? (Mungu alimchagua Abramu kutoka katika dunia yote.)

 

      1.    Ni nini yangekuwa matokeo ya Abramu kumtii Mungu? (Atabarikiwa. Na atakuwa baraka kwa ulimwengu.)

 

    1.    Rafiki, utume aliopewa Abramu ndio sasa utume waliopewa wale wote wanaomfuata Mungu. Mungu hakutupatia amzi zake ili kutupatia mzigo au kutuangamiza. Alizitoa ili kutubariki, ili kutuweka huru kutoka kwenye utumwa wa dhambi, na kuleta utukufu kwa jina lake. Kama ilivyokuwa kwa ahadi ya Mungu kwa Abramu. Kuishi maisha ya uaminifu humtukuza Mungu. Je, utadhamiria, sasa hivi, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kuyafanya maisha yako yawe bora huku ukimtukuza Mungu?

 

  1.   Juma lijalo: Toba na Msamaha.