Somo la 11: Vikwazo
Somo la 11: Vikwazo
(Marko 4 & 5)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.
Utangulizi: Je, umewahi kupitia jambo lililokatisha matumaini na ndoto zako kuhusu maisha ya baadaye? Tangu ujana wangu nilidhani Mungu alinitaka niwe mwanasheria na kulifanyia kazi kanisa. Nilisoma kwa bidii, nikapata alama nzuri masomoni, na nikaendelea kimasomo hadi mahala nilipohitaji kufanya mtihani wa Law School Admission Test (LSAT). Hii leo, wanafunzi wanajiandikisha mara kwa mara kwenye kozi kwa ajili ya kujiandaa na LSAT. Hakuna aliyenipendekezea hilo. Nilifanya mtihani huku nikiwa sijui chochote kuhusiana na LSAT. Matokeo ya mtihani yalinivunja moyo. Je, sasa sitakuwa mwanasheria? Kikwazo kikubwa namna gani hiki! Kwa kuwa sikumaliza mtihani kwa muda uliotengwa, baba wangu alinipendekezea nifanye kozi ya kujifunza kusoma haraka na kufanya tena mtihani. Nilizingatia ushauri wake na alama zangu ziliongezeka kwa takriban 20%. Mojawapo ya shule za juu kabisa za sheria katika zama za leo ilinikubali kujiunga nayo kama mwanafunzi. Biblia inatufundisha nini kuhusu vikwazo? Hebu tuzame kwenye Biblia na kujifunza zaidi!
- Vikwazo Vinavyofuatana
-
- Soma Marko 5:21-23. Je, Yairo na mkewe wameteseka kwa kikwazo? (Ndiyo. Binti wao “yu katika kufa.”)
-
-
- Yairo alikuwa na hamu kubwa ya uponyaji kiasi gani? (Alianguka miguuni pa Yesu na “akamsihi” amsaidie.)
-
-
- Soma Marko 5:24. Je, Yesu amekubali kumwokoa binti wa Yairo? (Inaonekana hivyo kwa sababu Yesu anaelekea nyumbani kwake.)
-
- Soma Marko 5:25-26. Ni kwa kiwango gani mwanamke huyu alikuwa amekata tamaa? (Alikuwa anaumwa na hali yake ilizidi kuwa mbaya. Alikuwa amekwishatumia vyote alivyokuwa navyo ili kutibiwa na matabibu.)
-
-
- Uzoefu wake na matabibu ulikuwaje? (Si tu kwamba hali yake ilikuwa ilizidi kuwa mbaya, bali pia “aliteswa mengi” chini ya utabibu wao.)
-
-
-
- Je, utasema kuwa alipitia vikwazo vingi? Je, matumaini yake kwa mustakabali wake yalikuwa yamefifia?
-
-
-
- Tafakari aina ya ugonjwa wake. Je, hii ilikuwa aina ya ugonjwa ambayo ingeongeza matatizo ya ziada?
-
-
- Soma Mambo ya Walawi 15:25-27. Je, angeweza kuwa na uhusiano wa kawaida na watu wengine? (Hapana. Alikuwa najisi. Kila aliyevigusa vitu vyake atakuwa najisi.)
-
- Soma Marko 5:27-29. Kama ungeombwa utoe ushauri kuhusu mpango wa mwanamke huyu, je, ungependekeza kitu gani? (Anaweza kumfanya Yesu kuwa najisi. Yesu anaweza asipende kitendo hicho.)
-
-
- Matokeo ya mpango wake ni yepi? (Anaponywa.)
-
-
- Soma Marko 5:30-33. Hali ya kimawazo ya mwanamke huyu ikoje? (Ana hofu kubwa kiasi kwamba anatetemeka. Alidhani alikuwa kwenye matatizo kwa kumgusa Yesu.)
-
-
- Nani mwingine aliye matatizoni? (Yairo! Binti wake anakaribia kufa na Yesu anacheleweshwa na mwanamke ambaye, kama ilivyo kwa wengine wengi, aligusa vazi la Yesu.)
-
-
- Soma Marko 5:34. Yesu anatangaza uponyaji na anamwambia mwanamke huyu aende kwa amani. Hajamkasirikia. Nani anapaswa kukasirika? (Kama Yairo anaelewa mazingira ya mwanamke huyu kikamilifu, anapaswa kukasirika. Ucheleweshaji huu unaweza kusababisha ampoteze binti wake. Kuchelewesha uponyaji wa mwanamke huyu kwa hakika hakutasababisha tatizo lolote. Alikuwa hivyo kwa muda wa miaka kumi na miwili. Kuchelewesha uponyaji wake kwa muda wa saa kumbi na mbili za ziada hakutakuwa na athari yoyote.)
-
- Soma Marko 5:35. Je, jambo baya kabisa limetokea? Je, Yairo na mkewe wameteseka kikwazo kisicho na mantiki kabisa? (Hivyo ndivyo ambavyo ningeliangalia jambo hili. Tutaona kwamba binti wa Yairo ana umri wa miaka kumi na miwili tu.)
-
-
- Wale waliotoka nyumbani mwa Yairo wana fikra gani juu ya hali ile? (Jaribio la wokozi limeshindwa. Msimsumbue tena Yesu.)
-
- Kuvishinda Vikwazo.
-
- Mwanamke mwenye kutokwa damu alikishindaje kikwazo chake? (Aliendelea kumtafuta Yesu bila kukata tamaa – hata pale ambapo inawezekana watu “wenye busara” walimuonya kuwa hili halikuwa wazo zuri.)
-
- Soma Marko 5:36. Utaona katika Marko 5:33 kwamba mwanamke huyu alikuwa na hofu. Yesu anatuambia kuwa Yairo alikuwa amejawa hofu. Unadhani hiyo inamaanisha nini? (Walikuwa na wasiwasi juu ya mustakabali wao.)
-
- Soma Marko 5:37. Ukisoma kwa makini, je, unaweza kuniambia Yairo alikuwa na mwitiko gani? (Alikuwa akimwongoza Yesu kuelekea nyumbani kwake. Lazima itakuwa aliendelea kumwongoza Yesu. Hii inafunua kwamba amepokea wito wa Yesu katika Marko 5:36 wa “kuamini” tu.)
-
- Soma Marko 5:38-40. Marafiki wa Yairo na wanafamilia wanakuwa na mwitiko gani kwa Yesu? (Wanadhihaki kwa kicheko kile ambacho Yairo alikuwa ameweka tumaini lake.)
-
- Soma Marko 5:41-42. Yairo amekuwa na mwitiko gani kwenye kikwazo cha kutisha? (Nimekwambia kuwa ningekuwa na hasira juu ya suala hili. Lakini hakuna ushahidi katika Biblia kwamba Yairo alikuwa amekasirika. Anaendelea kufanya kazi na Yesu hata baada ya binti wake kufariki.)
-
-
- Ni jambo gani ambalo lingekukasirisha (nadhani hata wewe ungekasirika)? (Kwa mtazamo wa kibinadamu, Yesu hana vipaumbele. Hakuweza kutofautisha suala la dharura na ugonjwa sugu.)
-
-
-
-
- Hebu tuliangalie suala hili kimantiki. Yairo alikuwa na madai gani kwenye muda wa Yesu? Je, Yesu alikuwa na wajibu wowote kwake? (Yairo alikuwa anamsihi Yesu aende. Pendekezo langu la hasira limejengwa juu ya kukubali kwa Yesu kwenda na kisha kuchelewa kusiko kwa lazima kabisa kulikosababisha kifo cha binti wake.)
-
-
-
-
-
- Hatimaye, je, ucheleweshaji ulikuwa na maana yoyote? (Hapana.)
-
-
-
-
- Tunapata fundisho gani kutokana na ukweli kwamba hatimaye kuchelewa hakukuwa na tofauti yoyote? (Tunatakiwa kumtumaini Yesu. Hatupaswi kudogosha uwezo wake.)
-
-
-
- Hebu tuliweke hili kivitendo maishani mwako. Je, umewahi kuwa na kikwazo kinachohusisha kifo cha mwanafamilia wako? Je, ulikasirika kwamba Mungu hakumwokoa mwanafamilia huyo?
-
-
-
-
- Je, unaamini kuwa Yesu atamfufua mwanafamilia wako katika uzima wa milele?
-
-
-
-
-
- Kwa kuzingatia umilele, je, ucheleweshaji huo utaleta tofauti yoyote?
-
-
-
- Kisa cha kifo cha Lazaro kinapatikana katika sura ya 11 ya kitabu cha Yohana. Hebu tutafakari maeneo yanayopatana na kisa cha Yairo. Yesu ana uhusiano gani na Lazaro na dada wake wawili? (Soma Yohana 11:5. Yesu aliwapenda.)
-
- Soma Yohana 11:14 na Yohana 11:20-21. Je, Martha anamtuhumu Yesu?
-
-
- Je, Mariamu amefadhaika sana kiasi kwamba hata haendi kumlaki wala kumsalimu Yesu?
-
-
- Soma Yohana 11:32. Ni jambo gani la kwanza analolisema Mariamu kwa Yesu? (Dada wote wawili hawaelewi kwa nini Yesu hakumwokoa kaka yao.)
-
-
- Hili linatufundisha nini? (Ni mwitiko wa kawaida kabisa kuuliza kwa nini Yesu hakuondoa kikwazo maishani mwako.)
-
-
- Soma Yohana 11:43-44. Hii inatuonesha nini? (Yesu ana mamlaka juu ya kifo. Tunatakiwa kumtumaini.)
- Chombo (Mashua/Mtumbwi)
-
- Soma Marko 4:35-36. Lilikuwa wazo la nani kuvuka Bahari ya Galilaya? (Yesu ndiye aliyependekeza.)
-
- Soma Marko 4:37-38. Je, wanafunzi wamepitia kikwazo? (Ndiyo.)
-
-
- Kikwazo hiki ni kikubwa kiasi gani? (Wanadhani watakufa.)
-
-
-
- Hoja yao ni ipi kwa Yesu kuingilia kati na kuokoa maisha yao? (Kwamba anajali. “Si kitu kwako kuwa tunaangamia?”)
-
-
- Angalia tena Marko 4:38. Una maoni gani juu ya Yesu kulala wakati wa dhoruba kuu ya upepo? (Linaonekana kuwa jambo lisolowezekana.)
-
-
- Hebu tukiweke kisa hiki kwenye vikwazo vilivyopo maishani mwetu. Je, ilionekana kwamba Yesu alikuwa amelala na hakuja kukuokoa?
-
-
-
- Je, ulijenga hoja kwamba anapaswa kukujali?
-
-
- Soma Marko 4:39 na Marko 4:41. Je, hii inafanana na kisa cha Yairo – watu wanadogosha uwezo wa Yesu?
-
-
- Je, dada wawili wa Lazaro walidogosha uwezo wa Yesu?
-
-
- Soma Marko 4:40. Yesu anawakemea nini wanafunzi? Walipungukiwa nini? (Yesu anasema hawana imani.)
-
-
- Hilo linawezaje kuwa kweli? Walimgeukia Yesu kwa ajili ya msaada kwenye dhoruba! (Kutokuwa kwao na imani na kutokuwa kwao na amani kulitokana na kudogosha uwezo wa Yesu.)
-
-
- Rafiki, kikwazo kinapokujia maishani mwako, je, utaamini kuwa Yesu ana mamlaka kamili mbinguni na duniani? Hakuna kitu chochote kinachokomesha uwezo wake wa kutatua vikwazo vyako. Hata hivyo, suluhisho na muda wa utatuzi wa suluhisho hilo vinaweza visiendane na mipango yako. Je, utakubali, sasa hivi, kumtumaini Mungu kikamilifu?
- Juma lijalo: Shiriki Habari Zake.
