Somo la 3: Umoja Katika Kristo

(1 Wakorintho 1 & 3, Wafilipi 2)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
3
Lesson Number: 
3

Somo la 3: Umoja Katika Kristo

 

(1 Wakorintho 1 & 3, Wafilipi 2)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Je, umewahi kuliona kanisa lililo na mgawanyiko? Je, umewahi kuingia kwenye kanisa ambapo unaweza kuona mgawanyiko kwa kuangalia tu mahali watu walipokaa? Ninakumbuka nilipokuwa kijana mdogo wakati nikienda kanisani kwa bibi yangu katika mji wa Ironwood, Michigan. Ilionekana kwamba watu wa kitaaluma (professionals) wote walikaa upande wa kushoto na wale ambao kazi zao hazikuwahitaji kuwa na elimu ya shahada ya kwanza walikaa upande wa kulia. Nilipokuwa katika shule ya sheria, niligundua katika mgahawa kwamba wanafunzi wote weusi walikaa katika meza moja. Nikadhani kuwa hilo ni jambo la kusikitisha, hivyo nikakaa kwenye meza yao. Waliokuwa kwenye meza hiyo walininyanyasa. Sikuondoka, lakini sikurudia tena kukaa kwenye meza hiyo! Kama mwanasheria mchanga, mimi na mke wangu tulihudhuria kwenye kanisa ambalo washiriki weusi wanakaa upande mmoja na washiriki wazungu wanakaa upande mwingine. Baada ya kuhamia kanisa jingine, nilirudi katika kanisa lile na kutoa hubiri juu ya maridhiano kati ya makundi ya rangi tofauti (racial reconciliation). Baada ya hubiri langu, baadhi ya marafiki wangu weusi wakaniambia, “Natumai walikuwa wanasikiliza,” na marafiki wangu wazungu wakaniambia kwa siri, “Natumai walikuwa wanasikiliza.” Je, kuna suluhisho lolote kwa migawanyiko kanisani? Au hiyo ni kawaida tu ya jinsi mambo yalivyo? Hebu tuzame kwenye somo letu na tusome ushauri wa Paulo kuhusiana na mada hiyo!

 

  1.    Majibu kwa Migawanyiko

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 1:10. Hatua ya kwanza ya Paulo kuondoa mgawanyiko kanisani ni ipi? (Kila mmoja anatakiwa kukubaliana kwamba hakutakiwi kuwapo kwa mgawanyiko wowote. Tunatakiwa kuungana “katika nia moja na shauri moja.”

 

      1.    Tafakari lengo la Paulo la kuwa “katika nia moja.” Je, hilo linawezekana?

 

      1.    Je, kuwa “katika nia moja” kunahitaji maoni yanayofanana kabisa kuhusu kila jambo, au Paulo anasisitiza hasa uaminifu wa pamoja kwa Kristo unaokataa makundi yanayogawanyika?

 

      1.    Fikiria mojawapo ya mabishano yenye utata mkubwa katika makanisa ya Kiprotestanti nchini Marekani leo. Baadhi ya makanisa yanaidhinisha vitendo vya ushoga kiasi kwamba mashoga wanaweza kuhudumu kama viongozi wa kiroho (makasisi au wachungaji). Je, tunapaswa kuwa “na nia moja” katika suala hilo?

 

      1.    Hivi karibuni kanisa la United Methodist liliamua kuachana na sehemu ya jina lake “united” na kugawanyika kutokana na suala la viongozi wa kiroho mashoga na ndoa za watu wa jinsia moja. Makanisa mengi yalijiondoa kwenye madhehebu hayo, na Kanisa la Global Methodist likaanzishwa mwaka 2022. Mwaka 2024, Kanisa la United Methodist liliondoa zuio lake dhidi ya viongozi wa kiroho mashoga pamoja na adhabu zinazohusiana na ndoa za watu wa jinsia moja. Je, hali hii inaendana na ushauri wa Paulo wa kuwa na “nia moja?” ikiwa unadhani kanisa linakumbatia dhambi za dhahiri, je, unaanzisha kanisa jipya lenye washiriki wenye mtazamo unaofanana?

 

      1.    Paulo pia anatuambia kuungana katika “shauri moja.” Unadhani hiyo inamaanisha nini? (Tuchukulie kwamba unakubaliana nami kuwa vitendo vya ushoga haviendani na mafundisho ya Biblia. Hapo tuna nia moja. Swali linalofuata ni: “Tunawatendeaje mashoga katika kanisa letu?” Uamuzi unatofautiana katika jambo hilo.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 1:11-12. Misingi ya migawanyiko niliyoiibua hadi sasa ni elimu, mbari (rangi), na kutokubaliana juu ya vitendo vya ngono. Msingi wa mgawanyiko ambao Paulo anauzungumzia ni upi? (Makundi madogo ndani ya kanisa yaliyojengwa juu ya uongozi. Kila kundi lina kiongozi wanayempenda.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 1:13-17. Unaelezeaje njia aliyoitumia Paulo kwenye mgawanyiko huu miongoni mwa washiriki wa kansia? (Anatoa hoja ya kimantiki dhidi ya mgawanyiko. Anabainisha kuwa Yesu hakugawanyika.)

 

      1.    Je, hoja za kimantiki na wito wa kuwa na umoja katika Yesu, vitasaidia kuondoa mgawanyiko unaotokana na elimu, mbari, na jinsia?

 

        1.    Je, unaona maeneo yote matatu ya mgawanyiko yakihusisha tatizo lile lile la msingi?

 

        1.    Katika kujibu swali lililotangulia, je, majivuno ndio tatizo la kawaida?

 

  1.   Kiini cha Mgawanyiko

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 3:1-3. Paulo anabainisha jambo gani la kwanza kama kiini cha mgawanyiko? (Ni wachanga kiroho-bado wakienenda kama watu wa mwilini-na hawako tayari kwa “chakula kigumu.”)

 

      1.    Je, hicho ndicho kiini cha tatizo kinachosababisha mgawanyiko kanisani leo? (Jibu langu ni, “ndiyo,” kwa sababu katika baadhi ya masuala baadhi ya washiriki hukataa kukubali mafundisho ya wazi ya Biblia.)

 

      1.    Jibu la Paulo katika suala hili ni lipi? Anasema kuwa aliwalisha “maziwa,” na aliwaita kama “watu wa mwilini” na si “watu wa kiroho.”

 

        1.    Tutautumiaje ushauri wa Paulo leo? (Tunapaswa kuelewa kuwa wanaosababisha migawanyiko ni wachanga kiroho. Tunapaswa kuelewa kwamba hawamsikilizi Roho Mtakatifu.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 3:4-7. Paulo anapoandika kwamba watu wanaosababisha migawanyiko ni “wanadamu tu,” je, anahalalisha mwenendo wao? (“Kuhalalisha” huenda likawa neno kubwa kupita kiasi. Paulo anaonyesha kuelewa matendo yao. Huu ndio utambuzi wake wa tatizo.)

 

      1.    Unaweza kuliwekaje jibu la Paulo? (Anajenga hoja ya kimantiki inayohusiana na ukuaji wa mimea.)

 

    1.    Soma Wafilipi 2:5-8. Nani anayepaswa kuwa mfano kwa wote wenye mwelekeo wa kuleta mgawanyiko? (Yesu. Paulo anawaambia waamini kuwa wanaweza kuwa na nia ya Yesu ikiwa wanataka.)

 

    1.    Soma Wafilipi 2:6-9. Sifa gani ya Yesu ni tiba ya mgawanyiko? (Unyenyekevu.)

 

      1.    Hebu tuone kama tunaweza kutumia suluhisho hili kwenye migawanyiko niliyoibainisha katika sehemu ya utangulizi. Watu wa kitaaluma (professionals) wanapoketi upande mmoja na wale wasio na shahada ya kwanza wanapoketi upande mwingine wa kanisa, je, kiburi ndio tatizo? (Ndiyo. Nilikuwa kwenye sherehe ya kanisa na mke wa daktari akatuambia tuliokuwa tumekaa pamoja, “Ni vizuri kwa sisi wanataaluma kuwa pamoja.” Nilipokea kauli hiyo kwa hisia hasi kabisa. Lakini jambo hili lina pande zote mbili. Katika kanisa la Ironwood, wafanyakazi wa kawaida (vibarua) waliwachukia watu wa kitaaluma kwa sababu walikuwa wageni na walikuwa wakichukua nafasi za uongozi.)

 

      1.    Je, kiburi ndicho kipo nyuma ya mgawanyiko wa kimbari (rangi) kanisani? (Kwa mara nyingine jibu langu ni, “Ndiyo.” Baada ya hubiri langu kuhusu upatanisho wa kimbari kila upande wa mgawanyiko wa kimbari ulikuwa na matumaini kwamba upande mwingine ulijifunza jambo-kwa dhahiri bila kuwa na unyenyekevu wa kutosha kudhani kwamba wanaweza kujifunza jambo fulani.)

 

      1.    Vipi kuhusu nilipokaa kwenye meza ya wanafunzi weusi nilipokuwa katika shule ya sheria? (Huenda ilikuwa ni majivuno ya maoni yangu yaliyonifanya nidhani kwamba kwa kukaa pamoja nao, kwa kuwa nilikuwa mzungu, kungesaidia kutatua kile nilichokiona kuwa ni tatizo. Nadhani majivuno yalikuwa nyuma ya mwitikio wa wanafunzi weusi kwa sababu walitaka kunidhalilisha kwa msingi wa rangi.)

 

      1.    Vipi kuhusu mabishano yanayohusu vingozi wa kiroho mashoga na ndoa za watu wa jinsia moja? (Kimsingi, “majivuno” ndio mada kuu ya harakati za ushoga. Lakini sote tunapambana na dhambi. Watu wa jinsia tofauti hawawezi kujivunia kwamba vitendo vya ushoga si dhambi yao mahsusi. Lazima dhambi zote zishughulikiwe na kukataliwa. Tatizo gumu zaidi hutokea pale watu wasipotaka kubadili mwenendo wao na badala yake wanataka kanisa libadili fundisho lake. Hili ni jambo jipya katika uzoefu wangu.)

 

  1.      Suluhisho?

 

    1.    Angalia tena 1 Wakorintho 3:1-2 na usome Wafilipi 2:8-11. Je, kuelewa njia hii kutoka unyenyekevu hadi kutukuzwa kunahitaji ukomavu wa Kikristo? (Hivi ndivyo ninavyomwelewa Paulo. Wakristo wakomavu wanaelewa kwamba njia ya Yesu kupitia udhalilishaji ndiko kulikomfikisha kwenye utukufu. Hilo linasaidia kufafanua kwa nini baadhi ya watu kanisani kamwe hawaachani na migawanyiko. Tunaweza kuiacha tunapozidi kukomaa katika injili ya Yesu. Yesu, ingawa alikuwa sawa na Mungu, alichagua njia ya unyenyekevu wa hali ya juu kabisa na hivyo akatukuzwa sana.)

 

      1.    Paulo alijaribu kuwashawishi washiriki wachanga kiroho kwa kutumia hoja za mantiki. Je, hiyo ndio njia pekee ya kuwasaidia washiriki ambao hawajakomaa kiroho?

 

      1.    Roho Mtakatifu ana nafasi gani katika kutatua tatizo la uchanga kiroho na majivuno?

 

    1.    Rafiki, je, utauangalia mgawanyiko kwa mtazamo mpya? Je, utauelewa kuwa unaakisi kiburi/majivuno na uchanga, na kumwomba Roho Mtakatifu akugawie unyenyekevu halisi wa Kikristo? Kwa nini usiliombe hilo saa hivi?

 

  1.   Juma lijalo: Dhambi Katika Kanisa.