Somo la 4: Dhambi Kanisani

(1 Wakorintho 5 & 6)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
3
Lesson Number: 
4

Somo la 4: Dhambi Kanisani

(1 Wakorintho 5 & 6)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

Utangulizi: Kabla tu ya kuandika utangulizi huu, nilikuwa na mazungumzo mazuri sana na mjukuu wangu wa kike. Yuko karibu kuingia katika umri wa ujana (rika balehe), na tulizungumza kuhusu umuhimu wa kuchagua marafiki wake wa karibu kwa uangalifu. Kila mtu anayesoma haya amewahi kuathiriwa na marafiki. Wengine, kutokana na ushawishi mbaya walioupata wakati wa ujana wao, maisha yao yalibadilika kabisa. Namkumbuka mama mmoja alinipigia simu kuhusu mwanawe. Alikuwa ndani ya gari wakati marafiki zake walipoamua kumfanyia ukatili kijana mwingine. Mambo yaliharibika na mwathirika akafariki. Katika mazingira kama haya, marafiki wanaweza kukufanya upatikane na hatia ya mauaji. Chaguzi zinazobadilisha maisha mara nyingi hufanywa mtu akiwa bado mdogo. Ushawishi wa marafiki zetu huendelea katika maisha yetu yote. Somo letu juma hili linahusu ushawishi ambao dhambi inayovumiliwa inaweza kuwa nao ndani ya kanisa na jinsi Wakristo wanavyopaswa kutatua migogoro baina yao. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone ni mafundisho gani tunaweza kujifunza leo!

I.    Uasherati

A.    Soma 1 Wakorintho 5:1-2. Juma lililopita tulijadili jinsi dhambi ya zinaa inavyosababisha mgawanyiko kanisani. Hapa Paulo anaibua tatizo gani linalohusiana na hilo? (Paulo anaandika juu ya kanisa ambalo si tu kwamba linavumilia dhambi ya zinaa, bali pia linajivunia (kwa kiburi) uvumilivu huo.)

1.    Je, hilo ni tatizo hata leo? (Ndiyo, baadhi ya makanisa yanajivunia kuvumilia mambo ambayo Biblia inayaita dhambi.)

2.    Je, mtazamo sahihi wa dhambi isiyotubiwa kanisani ni upi? (Mtu anayejitambulisha kuwa mshiriki wa kanisa ambaye anaendelea waziwazi bila kutubu dhambi nzito anapaswa kuondolewa katika ushirika wa kanisa.)

3.    Hebu tujadili hili. Hoja ya leo ni kwamba ni afadhali kuwaacha kanisani washiriki wanaoendelea waziwazi katika dhambi bila kutubu kwa sababu kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kushawishika kutambua dhambi yao na kurejeswa. Una maoni gani juu ya hoja hiyo?

B.    Soma 1 Wakorintho 5:5. Hili linajibuje swali kuhusu kumwacha mdhambi wa wazi kanisani ili kuongeza nafasi yake ya kuongoka? (Paulo anasema kinyume chake kabisa. Kumkabidhi mtu huyo kwa Shetani kunaweza kumwokoa.)

1.    Unadhani kumkabidhi kwa Shetani kunafanyaje kazi? (Kuondoshwa kanisani, tofauti na kuendelea kuungwa mkono na kanisa, humfanya mtu atambue uzito wa dhambi yake. Hilo linaweza kumfanya atubu.)

II.    Kanisa na Dhambi

A.    Soma 1 Wakorintho 5:6-7. Hili linaashiria kuwa tatizo la kuvumilia dhambi ya waziwazi ni lipi? (Dhambi, kama ilivyo chachu, itawashawishi wengine kanisani.)

B.    Angalia tena 1 Wakorintho 5:1 ambapo Paulo anasema kuwa dhambi hii “haipo hata katika Mataifa.” Hii inaibua tatizo gani kwa kuwaacha kanisani watenda dhambi wa waziwazi? (Paulo hajali tu juu ya ushawishi wake kwa washiriki wengine wa kanisa; bali pia anajali sifa ya kanisa.)

1.    Tuchukulie kwamba utamaduni unaolizunguka eneo hili ulikubali mwenendo wa namna hii. Je, kukubalika kwake kiutamaduni kungefanya iwe sahihi kwa kanisa kumwacha mtu huyu aendelee kuwa mshiriki? (Hapana. Kiwango cha kanisa kinatokana na Neno la Mungu, na si utamaduni unaolizunguka. Kutokubali kwa Mataifa kulifanya uvumilivu wa Wakorintho kuwa wa kudhuru zaidi kwenye ushuhuda wa kanisa.)

C.    Soma 1 Wakorintho 5:9-11. Je, ushauri wa Paulo unatumika zaidi ya kwenye dhambi ya zinaa pekee?

D.    Soma 1 Wakorintho 5:12-13. Mara ngapi umeambiwa kwamba kuhusiana na dhambi ndani ya kanisa hatupaswi “kuhukumu?” Paulo anasema nini kuhusu kufaa kwetu kuwahukumu washiriki wenzetu? (Paulo anasema kwamba kanisa linapaswa kutoa hukumu ya maadili kwa wale walio ndani ya kanisa, huku hukumu ya walio nje ikiachwa kwa Mungu.)

1.    Paulo anamwita mtu tunayepaswa kumhukumu kuwa “mtu mwovu.” Je, hili ni muhimu? (Nadhani ni muhimu. Hatupaswi kuwafukuza wadhambi wanaojitahidi kupambana na udhaifu wao kutoka kanisani. Mkazo uko kwa mwamini/muumini anayedumu waziwazi na bila kutubu katika uovu mkubwa.)

III.      Kuchunguza kwa Kina Asili ya Uasherati

A.    Hebu turukie mbele na tusome 1 Wakorintho 6:12-14. Kwa nini Paulo anatuambia kuwa chakula na matumbo vitaangamizwa?

1.    Paulo anatoa hoja gani dhidi ya uasherati ambayo haitoi kuhusu chakula? (Paulo anatuambia kuwa baadhi ya uamuzi ni muhimu zaidi kuliko uamuzi mwingine.)

B.    Hebu tusome tena 1 Wakorintho 6:12. Je, hii inakukumbusha Kumbukumbu la Torati 4:2? (Kumbukumbu la Totari inatuambia kuepuka kuita mambo kuwa dhambi wakati si dhambi. Paulo anaeleza kuwa baadhi ya mambo, ingawa si dhambi, hayana manufaa.)

1.    Je, mjadala huu una uhusiano wowote na mjadala wa Paulo kuhusu tumbo? (Nadhani Paulo anasema kwamba linapokuja suala la ulaji tuna chaguzi nyingi, baadhi ya changuzi zikiwa bora kuliko nyingine. Lakini linapokuja suala la uasherati, chaguzi mbaya zina matokeo mabaya sana.)

2.    Maoni ya John MacArthur yanasema kuwa Mungu anasamehe dhambi zote, na yananukuu Waefeso 1:7. Kuna mtu aliwahi kuniambia jambo hili katika muktadha wa dhambi ya zinaa, na mwitikio wangu ulikuwa kwamba baadhi ya dhambi ni nzito zaidi kuliko dhambi nyingine. Je, unakubaliana kwamba baadhi ya dhambi ni nzito zaidi kuliko nyingine?

C.    Soma 1 Wakorintho 6:15-18. Biblia inajibuje swali kuhusu baadhi ya dhambi kuwa nzito zaidi kuliko nyingine? (Vifungu hivi zinaeleza kuwa dhambi ya zinaa ni nzito zaidi. Dhambi ya zinaa ni “dhidi” ya miili yetu wenyewe, ilhali dhambi nyingine zote ziko “nje ya mwili.”)

1.    Unadhani hiyo inamaanisha nini?

2.    Paulo anaielezeaje? (Mtu anayeunganishwa na Bwana anakuwa roho moja pamoja naye. Kwa kuwa mwili wa muumini/mwamini ni mali ya Kristo, mwamini hawezi kwa haki kuunganisha mwili huo na kahaba. Ngono huunda muunganiko wa ‘mwili mmoja’ hata pale umoja huo unapokiuka mpango wa Mungu wa ndoa.)

D.    Soma 1 Wakorintho 6:19-20. Wangapi kati yenu mmewahi kumsikia mtu fulani akinukuu maneno “mwili wetu ni hekalu la Mungu” kama hoja kuhusu lishe? Je, hiyo ni sahihi? (Hii ni kinyume na kile anachokiandika Paulo. Anasema kuwa chakula na tumbo si vya muhimu ikilinganishwa na chaguzi za ngono.)

1.    Ninakumbuka tukio moja la kusikitisha ambapo kanisa liliniomba nikutane na mshiriki mmoja wa kanisa mashuhuri aliyejihusisha kwenye uzinzi. Mshiriki huyo wa kike aliniambia, “Jambo hili halikuhusu.” Je, hilo ni kweli? (Kwa yeye kuwa mshiriki wa kanisa kuliyafanya matendo yake kuwa “mambo” ya kanisa. Lakini jambo la muhimu zaidi ni kwamba, jambo hili linadhuru utukufu wa Mungu kinyume na 1 Wakorintho 6:20. Kanisa linapaswa kushughulikia jambo kama hilo kwa usiri, kwa unyenyekevu, na lengo lake likiwa ni kumrejesha mhusika.)

E.    Baadhi ya wasomaji wanaweza kuuliza kwa nini uasherati ni wa pekee kwa kuwa ni dhambi dhidi ya mwili? Ukizingatia kwamba, miili yetu ya sasa ni miili inayokufa na tutapewa miili mipya. Na ni kwa jinsi gani ngono inaviunganisha “viungo vya Kristo na kuvifanya kuwa viungo vya kahaba?” Je, haya ndio maswali yako? (Nadhani tunatakiwa kurudi nyuma kidogo na kuangalia picha kubwa zaidi ili kuelewa jambo hili.)

F.    Soma Mithali 5:15-18. Biblia inalinganisha tendo la ndoa na kushiriki maji. Je, unaweza kulinganisha hili kwenye mjadala wetu hadi sasa, au hili halina mantiki kwako? (Maji yanawakilisha uzima. Paulo anapozungumzia kuhusu sisi kuwa “wamoja” kwa njia ya tendo la ndoa, anarejelea kauli ya Mwanzo 2:24 ya “mwili mmoja” na kauli ya Mwanzo 1:26-28 kuhusu Adamu na Eva kuwa kama waanzilishi wa uhai. Sababu inayofanya ngono nje ya ndoa kuwa kundi la pekee la dhambi ni kwamba Mungu alitupatia uzima. Aliwapa wanadamu uwezo wa kuumba uhai. Unapounganisha uwezo huo wa kutoa uhai na mtu ambaye si mwenzi wako, unakuwa umetenda dhambi dhidi ya mwili wako mwenyewe na dhidi ya uhusiano wako wa pekee na Mungu na mwenzi wako.)

IV.    Kutatua Migogoro

A.    Soma 1 Wakorintho 6:1-3. Paulo anazungumzia tatizo gani? (Washiriki wa kanisa wanaoshtakiana katika mahakama za kiraia.)

B.    Soma 1 Wakorintho 6:4-6. Kwa nini ni tatizo kuwashtaki washiriki wenzako wa kanisa? (Kunaliaibisha kanisa. Inaashiria kuwa kanisa halina mtu mwenye hekima kutatua migogoro.)

C.    Soma 1 Wakorintho 6:7-8. Je, uko tayari kudhulumiwa ili kulinda sifa ya Mungu? (Mke wangu alikuwa na madai dhidi ya kanisa letu ambayo, kama yangeshtakiwa mahakamani, yasingeweza kudhibitiwa nasi na yangeweza kuligharimu kanisa mamilioni ya dola. Tuliyashughulikia ndani ya kanisa, na jibu tulilopewa ni kwamba kurekebisha mambo kungegharimu fedha nyingi sana. Tuliamua “kukubali kudhulumiwa” badala ya kulidhuru kanisa.)

D.    Rafiki, linapokuja suala la ngono nje ya ndoa, linapokuja suala la kushughulika na washiriki wenzako wa kanisa, je, utajitoa kufuata njia inayoleta utukufu kwa Mungu? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu akuwezeshe kutenda yale yanayomtukuza Mungu?

V.    Juma lijalo: Yote kwa Utukufu wa Mungu.