Somo la 5: Yote kwa Utukufu wa Mungu

(1 Wakorintho 8 & 10, Warumi 14)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
3
Lesson Number: 
5

Somo la 5: Yote kwa Utukufu wa Mungu

 

(1 Wakorintho 8 & 10, Warumi 14)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Je, umewahi kujikuta katika hali ambayo ulikuwa sahihi kabisa, lakini mwishowe ukaishia kushindwa? Katika sheria za Marekani, jambo hili halipaswi kutokea. Unapokuwa na ushahidi mkononi, unajenga hoja kuhusu matumizi (tafsiri) sahihi ya sheria, na ikiwa una umahiri mkubwa na unatumia mantiki basi unashinda, sivyo? Kwa uzoefu wangu, jibu ni, “Si mara zote.” Hoja za Kibiblia zinaweza hata kutokuwa na uhakika zaidi. Kwanza, si kila mtu anakubaliana na kile kinachosemwa na kifungu cha Biblia. Ikiwa hakuna makubaliano kuhusiana na sheria, ambacho ndio kipimo cha hukumu, unawezaje kuwa na mjadala wenye mantiki? Pili, kuwa sahihi juu ya kile ambacho Biblia inakisema si mara zote inakuelekeza kufikia kwenye hitimisho sahihi. Hilo linawezekanaje? Tunahitaji kumuuliza Paulo! Somo letu juma hili linaanza kwa kuwa sahihi juu ya Biblia, lakini kukosea katika hitimisho letu. Hebu tuzame katika dhana hii inayotia wasiwasi ili tuelewe vizuri zaidi kile ambacho Paulo anatufundisha!

 

  1.    Sanaa ya Kuwa Sahihi na Kukosea kwa Wakati Mmoja

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 8:1-3. Paulo anaandika kuwa ujuzi “huleta majivuno” wakati upendo “hujenga.” Je, hilo linaonekana kama kichocheo cha maafa? Kwamba maarifa ni mabaya, hisia ni nzuri? Au, je, kuuita upendo kuwa ni jambo la hisia tu si kitendo cha haki?

 

      1.    Sababu kuu inayoifanya Marekani ifanikiwe ni kwamba imejengwa juu ya “Utawala wa Sheria.”  Hiyo inamaanisha kuwa hatupaswi kufanya uamuzi wa kimahakama kiholela (yaani, bila utaratibu wowote) kwa kutegemea hisia au mihemko ya wakati huo. Tunaamua kilicho sahihi kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa. Jambo gani linaweza lisiwe sahihi katika hilo?

 

      1.    Utaona kwamba Paulo anasema kuwa “ujuzi” “huleta majivuno.” Je, anamaanisha kuwa kuuelewa ukweli kunakufanya uwe na kiburi?

 

      1.    Paulo pia anaandika kwamba upendo “hujenga.” Je, kuwa mwenye upendo ni bora kuliko kuwa sahihi?

 

    1.    Hebu subiri kidogo! Angalia tena 1 Wakorintho 8.1. Je, dhana ya “upendo kuutawala ujuzi” ina mipaka katika eneo moja dogo la mjadala? (Ndiyo! Paulo anaweka mipaka ya mjadala kwenye “chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu.”)

 

      1.    Je, jambo hili linakufanya ujisikie nafuu au vibaya zaidi?

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 8:4-6. Je, mtu mwenye maarifa makubwa ana mtazamo gani juu ya sanamu? (Sanamu si lolote wala chochote (si kitu.) Kuna Mungu mmoja tu wa kweli.)

 

      1.    Kama una maarifa haya ya msingi, je, “unajivuna,” au wewe ni mtu mwenye elimu nzuri kuhusu Biblia?

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 8:7. Una maoni gani juu ya watu wasioelewa kweli zote? (Ningewaita “watu wenye taarifa chache.”)

 

      1.    Je, Paulo anatuambia kuwa watu wenye taarifa chache wapo? (Ndiyo. Anasema, “si wote walio na maarifa haya.”)

 

      1.    Paulo anawaitaje wale wasio na uelewa thabiti kuhusu asili ya Mungu? (Anawaita, “dhaifu.”)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 8:8. Kwenye suala la kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu, je, kula chakula hicho kunaathiri uhusiano wetu na Mungu? (Paulo anasema, “Hapana.” Wakristo wenye maarifa makubwa wanajua kwamba sanamu si kitu.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 8:9-11. Je, maarifa yetu ya hali ya juu kwamba sanamu si kitu ndio mwisho wa mjadala? (Hapana. Kula chakula kilichotolewa sanamu kutamdhuru Mkristo dhaifu kwa sababu bado hajaishinda imani yake ya zamani, ama kwa hakika, kwamba sanamu ni kitu fulani.)

 

      1.    Je, watu wenye taarifa chache wanapaswa kudhibiti matendo ya watu wenye taarifa nyingi?

 

      1.    Fikiria tena kuhusu kauli ya Paulo kwamba maarifa “hujivuna” lakini upendo “hujenga.” (Hii inafafanua tatizo. Ingawa mtu anayesema “sanamu si kitu” yuko sahihi kabisa, kutumia maarifa hayo bila kujali muumini anayehangaika hakuonyeshi upendo.)

 

      1.    Kwa nini walio dhaifu wawatawale “wenye nguvu” katika maarifa yao kumhusu Mungu? Na, ikiwa chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu hakumaanishi chochote, kuna ubaya gani kwa mtu dhaifu kutiwa moyo kula chakula hicho? (Si tendo la upendo kumtia moyo mtu mwingine kukiuka dhamiri yake.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 8:12-13. Je, ni dhambi kuenenda kwa namna inayoendana na maarifa yako ya hali ya juu? (Paulo anasema, “Ndiyo.”)

 

      1.    Je, mwitikio wako ungekuwa kumwambia Mkristo mwenye taarifa chache, “Njoo hapa nikufundishe jambo fulani?” Au “Achana na mawazo yako yasiyo na mwelekeo?”

 

    1.    Hebu turudi nyuma na tuchunguze tena 1 Wakorintho 8:7. Je, tatizo ni ukosefu tu wa taarifa au akili? (Hapana. Paulo anatutambulisha kwenye dhana ya dhamiri dhaifu-dhamiri iliyoundwa kutokana na ushirika wa zamani wa mtu na ibada ya uabudu sanamu.)

 

      1.    Je, umewahi kufikiria kwamba dhamiri yako inaweza kukosea? (Hii inafanya suala hili kuwa gumu zaidi. Mjadala si kati ya watu wenye maarifa na wasio na taarifa tu. Ni kati ya wenye maarifa na wale ambao uzoefu wao wa zamani umeunda dhamiri zao.)

 

  1.   Je, Hii ni Kanuni Yenye Mipaka Dhidi ya Fadhila ya Maarifa?

 

    1.    Habari njema ni kwamba anaweka ukomo wa fundisho lake kwenye chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu. Ingekuwa vigumu kiasi gani kuepuka kula katika hekalu la sanamu?

 

      1.    Tafakari kwa makini kuhusu suala hili.  Je, fundisho la Paulo lina ukomo kwenye chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu tu? Katika mazingira yangu, ukomo wa fundisho hilo hauna athari yoyote katika maisha yangu ya kila siku kwa sababu hakuna ambacho ningefikiria kukila kimehusishwa na sanamu.

 

    1.    Soma Warumi 14:1-2 na Warumi 14:5-6. Je, Paulo amepanua wigo wa “upendo juu ya maarifa” hadi kufikia kula nyama na kuadhimisha siku maalumu?

 

    1.    Soma Warumi 14:21. Je, Paulo amechora upya duara na kuwa kubwa zaidi kwa kujumuisha kunywa divai na “lolote linalomsababisha ndugu yako kukwazwa?”

 

    1.    Soma Warumi 14:19. Sura za mwanzo za 1 Wakorintho zinajumuisha kauli thabiti dhidi ya zinaa. Je, tunapaswa “kuitupa Biblia” na kufuata chochote kinacholeta amani na kujengana?

 

    1.    Soma Warumi 14:1. Katika masuala gani tunapaswa kuwastahi “walio dhaifu katika imani?” (Paulo anaweka ukomo wa mjadala huu kwenye “maoni” – mambo ambayo Wakristo waaminifu wanaweza kutofautiana kwa dhamiri safi. Ukomo wa Waarumi 14 ni mabishano kuhusiana na maoni. Tafsiri ya Biblia ya KJV inayaita “mabishano yenye mashaka” na tafsiri ya Biblia ya NIV inayaita “masuala yanayoweza kubishaniwa.”)

 

      1.    Je, kuitunza Sabato ni “jambo linaloweza kubishaniwa,” au “ugomvi juu ya maoni?” (Kuitunza Sabato kulianzishwa wakati wa Uumbaji, kukathibitishwa tena katika utolewaji wa Amri Kumi, na kukaadhimishwa katika wikiendi ya Pasaka Yesu alipopumzika kaburini siku ya Sabato ili kusherehekea ushindi wake juu ya dhambi. Yesu na wanafunzi wake waliitunza Sabato. Ama kwa hakika, katika Marko 2:28 Yesu alitangaza kuwa “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato pia.” Hakuna, yaani hakuna kabisa, amri katika Biblia zinazotuagiza kuitakatifuza siku ya kwanza ya juma. Suala si jambo linaloweza kubishaniwa lililojengwa juu ya kifungu cha Biblia.)

 

        1.    Kwa hiyo Paulo anazungumzia nini pale anapoandika katika Warumi 14:6 kuhusu kuadhimisha siku? (Baadhi ya maoni ya kale yanaandika kuwa Paulo anarejelea sikukuu za Kiyahudi. Inaonekana kwamba walitaka watu waende kanisani siku ya Jumapili badala ya kuamini kwamba siku zote ni sawa. Angalia Warumi 14:5.)

 

    1.    Soma Warumi 14:22. Je, huu ni wito wa unafiki uliotakaswa? (Paulo hawaambii walioelimika kulegeza masharti (compromise) kwenye imani yao katika mambo yanayoweza kubishaniwa. Anawaambia tu wayafanye kuwa siri kwa ndugu walio dhaifu.)

 

  1.      Hakuna Kulegeza Masharti (No Compromise)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 10:5-11. Nini kiliwatokea wale walioabudu sanamu na uasherati, wakamjaribu Kristo, na kunung’unika? Hii inatupa onyo gani? (Uasi wao ulileta hukumu ya Mungu, na wengi walikufa.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 10:18-21. Je, inaonekana kana kwamba mtu tofauti ndiye aliyeandika 1 Wakorintho 8?

 

      1.    Ungetatuaje jambo hili? (Tunaanza na msingi wa kwamba sanamu si kitu. Kwa hiyo, chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu si jambo la kuhangaikia. Wakati huo huo, pepo ni kitu. (Wote ni malaika walioanguka.) Ikiwa unakuza mambo ya kishetani, basi wewe si sehemu ya ushirika wa Mungu.)

 

      1.    Dhana ya “masuala yanayoweza kubishaniwa” inaendanaje na uelewa wetu wa suala hili (Kukuza mambo ya kishetani si suala linaloweza kubishaniwa. Huu ndio msingi wa uelewa. Paulo hataki tupoteze muda kwa kutofautiana kimawazo kwenye masuala yanayoweza kubishaniwa. Hata hivyo, pale suala linapokuwa ni kama tunamtumikia Mungu au kuonesha utii na uaminifu kwa mashetani, basi kinachotarajiwa ni utiifu. Mbadala wake ni kifo.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 10:31. Kanuni gani ya jumla inatawala uhuru wetu wa Kikristo na pia kujali kwetu wengine?

 

    1.    Rafiki, kwa umri wangu nimejifunza kuwa si lazima nirekebishe kila jambo lisilo sahihi ninalolisikia. Biblia inaeleza jambo hili kwa usahihi zaidi. Ikiwa jambo linaweza kubishaniwa, onyesha upendo na usiwavunje moyo wasio na ufahamu au wale walio na dhamiri dhaifu. Ikiwa Biblia inaonyesha wazi kwamba suala linahusisha kuchagua kati ya uaminifu kwa Mungu na uaminifu kwa Shetani, basi hakuna kulegeza masharti kunakoruhusiwa. Je, utajifunza Biblia na kumsikiliza Roho Mtakatifu ili uweze kutofautisha kati ya mambo ya kubishaniwa na masuala ya msingi?

 

  1.   Juma lijalo: Karama za Rohoni.