Somo la 6: Karama za Roho

(1 Wakorintho 12-14)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
3
Lesson Number: 
6

Somo la 6: Karama za Roho

 

(1 Wakorintho 12-14)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Hivi karibuni, mshiriki wa kanisa langu aliniuliza, “Ni nani aliyekuchagua kufundisha darasa la Shule ya Sabato?” Lilikuwa swali zuri. Nilitafakari nyuma nilipokuwa katika shule ya sheria na kanisa langu mahalia liliponiomba nifundishe darasa. Katika kila kanisa nililokwenda baada ya hapo, kiongozi fulani aliniomba nifundishe. Wakati huo huo, hakuna aliyewahi kuniomba niimbe. Ni kinyume chake tu. Mwalimu wa taaluma aliyenialika kujiunga na kwaya alibadili uamuzi wake muda mfupi baadaye na kuniondoa kwenye kwaya. Je, unawafahamu washiriki wa kanisa wanaosisitiza kuwa na jukumu fulani kanisani? Paulo anatuambia katika 1 Wakorintho 12:31 “kuzitaka sana karama zilizo juu.” Viongozi na watenda kazi kanisani wanapaswa kuchaguliwaje? Je, uchaguzi huo unategemea uelewa wetu kuhusu karama za roho? Je, unategemea malengo yetu? Hebu kwa mara nyingine tuzigeukie Biblia zetu na tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

  1.    Hotuba ya Roho Mtakatifu

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 12:1. Lengo la Paulo ni lipi katika sehemu hii ya barua yake kwa Wakorintho? (Anataka kuwafundisha kuhusu karama za roho.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 12:2. Je, sanamu zinazungumza? (Paulo anaziita “bubu.” Hazisemi chochote.)

 

      1.    Paulo analeta tofauti gani kati ya ibada yao ya zamani na kazi ya Roho Mtakatifu? (Sanamu zao za zamani zilikuwa bubu, lakini Mungu aliye hai huzungumza na kufunua kweli kupitia Roho wake.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 12:3. Je, Roho Mtakatifu anazungumza? (Ndiyo, kupitia kwa washiriki.)

 

      1.    Inaonekana jambo la ajabu kwamba wakati pekee mtu anapoweza kusema “Yesu ni Bwana” ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Je, unadhani hicho ndicho anachokisema Paulo? (Sidhani kama Paulo anawaza tu kuhusu maneno hayo; bali, anaandika kuhusu kunena kwa mguso. Ni uwezo wa ushawishi wa Roho Mtakatifu unaomwezesha mtu kukiri kwa dhati kwamba Yesu ni Bwana.)

 

      1.    Paulo anaandika kuhusu wale wanaosema “Yesu amelaaniwa.” Nani anayeweza kudhani kwamba Roho Mtakatifu angehamasisha kauli kama hiyo? Jibu dhahiri ni “Hakuna hata mtu mmoja.” Ikiwa Paulo hasemi jambo lililo wazi, hapa anatufundisha nini? (Anaonya kuhusu wale wanaodai kuzungumza kwa niaba ya Mungu, lakini ambao ujumbe wao unamshambulia Yesu.)

 

      1.    Utafikia hitimisho gani la jumla kutokana na kifungu cha tatu? (Una vidokezo kama Roho Mtakatifu ndiye anayevuvia maneno ya Mkristo kwa kuzingatia yale anayoyasema Mkristo huyo.)

 

  1.   Karama za Roho Mtakatifu

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 12:4-7. Ni kwa namna gani nyingine Roho Mtakatifu anajidhihirisha kupitia kwa Wakristo? (Kwa njia ya karama, huduma, na kazi mbalimbali.)

 

      1.    Je, kila mtu anatarajiwa kuwa na karama ile ile, kujishirikisha kwenye huduma ile ile, au kufanya kazi ile ile? (Hapana.)

 

        1.    Unadhani kwa nini Paulo anasisitiza jambo hili kuhusu tofauti zilizopo katika kile Wakristo wanachokisema au kukitenda kanisani?

 

    1.    Angalia tena 1 Wakorintho 12:4–7. Udhihirisho wote huu tofauti una jambo gani la kufanana? (Unatoka kwa Mungu yule yule na unatolewa kwa manufaa ya wote.)

 

      1.    Je, fundisho la 1 Wakorintho 12:3 linatumika hapa? (Ikiwa kile kinachosemwa au kutendwa kinakuza “manufaa ya wote,” basi huenda kinaongozwa na Roho Mtakatifu.)

 

    1.    Soma Mathayo 6:1 na Mathayo 6:5. Je, umewahi kuwaona washiriki wa kanisa wakijihusisha kwenye tabia ya namna hii?

 

      1.    Kauli ya Paulo kuhusu “manufaa ya wote” inaendanaje hapa? (Ikiwa karama, huduma, au kazi fulani kanisani inaonekana kumtukuza anayeifanya, basi hiyo si huduma ya “manufaa ya wote” iliyovuviwa na Roho Mtakatifu.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 12:8-10. Nimehesabu na kuona Paulo akibainisha karama tisa tofauti. Wewe umehesabu ngapi? Karama ngapi kati ya hizo zinaonekana katika kanisa lako mahalia? Je, ni chini ya asilimia 50?

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 12:11. Nani anayechagua karama ipi, huduma gani, au kazi gani ambayo mshiriki ataitenda kwa kanisa kwa manufaa ya wote? (Roho Mtakatifu.)

 

      1.    Paulo anaandika kuhusu karama nyingi, lakini Roho mmoja. Hiyo inatufundisha nini kuhusu mgawanyo kanisani?

 

  1.      Mwili wa Kristo

                            

    1.    Soma 1 Wakorintho 12:12-13. Paulo anashughulikiaje suala la uanuwai wa watu? (Anasema kuwa wale wenye asili tofauti kabisa wanatakiwa kuenenda kama “mwili mmoja.”)

 

      1.    Je, lengo ni uanuwai wa watu? Au lengo ni mwili mmoja? (Uanuwai wa watu ni hali ya ubinadamu; si lengo.)

 

    1.    Miongo kadhaa iliyopita, nilianza kuona katika nyezo za elimu ya kidunia msisitizo mkubwa kwa ajili ya uanuwai wa watu. Lengo lilikuwa kuonyesha tofauti zilizopo miongoni mwa watu. Lengo halikuwa kuzingatia umoja. Je, unaweza kufikiria kisa cha Biblia kinachoonyesha tofauti zilizopo kati ya watu?

 

    1.    Soma Mwanzo 11:5-8. Biblia inatufundisha nini kuhusu kufanya uanuwai kuwa lengo? (Watu wanapokuwa wamoja, ikiwa ni pamoja na kuwa na lugha moja, hakuna lisilowezekana kwao kwa mujibu wa Mungu. Katika kisa hiki, Mungu alianzisha utofauti wa lugha na mahali ili kufanya maendeleo yao kuwa magumu zaidi.)

 

      1.    Fundisho kwa kanisa letu leo ni lipi? (Lazima lengo ni umoja na si uanuwai katika mwili wa Kristo. Roho mmoja ndilo lengo.)

 

  1.   Kutamani Katika Mwili wa Kristo

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 12:14-18. Je, umewahi kukutana na washiriki wa kanisa kama hawa? Wanasema kuwa isipokuwa kama watakuwa na nafasi fulani kanisani, wataliacha kanisa.

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 12:19-21. Paulo anaelezea tatizo halisi la mtazamo wa kudai ofisi fulani. Je, pia kuna tatizo la dhambi katika mtazamo huo? Vipi kuhusu kutamani?

 

      1.    Nani ambaye hatimaye anaamua nafasi na kazi ya kila mshiriki katika mwili wa Kristo? (Mungu.)

 

      1.    Ikiwa unashikilia nafasi ya uongozi kanisani, uliipataje nafasi hiyo?

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 12:22-24. Paulo anawajibuje wale wanaotamani “nafasi” za juu? (Kanisa linapaswa kutatua suala hili kwa kuwapa heshima ya pekee wale wanaoshikilia nafasi za chini.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 12:27-31. Paulo anapangilia karama za roho kwa kuzingatia viwango, jambo linaloweza kuonekana kuongeza tatizo katika karama iliyo kuu. Paulo anasema nini kuhusu kutaka karama kuu? (Anasema tunapaswa “kutaka sana karama zilizo kuu.”)

 

      1.    Je, hiyo inamaanisha kuwa pendekezo lolote kuhusu tamaa si sahihi? (Hapana. Paulo anapongeza shauku ya kutaka karama zinazolijenga kanisa; hapendekezi wivu wa kudai ofisi, cheo, au hadhi kwa ajili yako mwenyewe.)

 

  1.    Lugha

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 13:1. Sura hii inahusu upendo, lakini tutaahirisha mjadala huo hadi juma lijalo. Paulo anasema nini kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuhusu karama ya lugha? (Anaiita “kelele.”)

 

      1.    Paulo anaandika juu ya “lugha za wanadamu na za malaika.” Lugha za malaika ni zipi?

 

    1.    Angalia tena 1 Wakorintho 12:10 na rejea ya karama ya lugha. Je, hii inaonekana kuwa kama Matendo 2 ambapo lugha za kigeni zilihusishwa?

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 14:27-28. Je, hii inaonekana kama Paulo anaandika kuhusu lugha za kigeni?

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 14:2. Je, hii inaonekana kama Paulo anaandika kuhusu lugha ya kigeni?

 

      1.    Nimeuliza maswali haya kuhusu lugha kwa sababu ninadhani kuna uwezekano mdogo sana yanahusisha tu kuzungumza lugha za kigeni. Katika mkutano mmoja mkubwa, mhubiri na wasaidizi wake walijitolea “kumwekea mikono” mtu yeyote ambaye angejitokeza mbele ili kuwapa nguvu za Roho Mtakatifu. Walichokimaanisha hasa ni kuwapa karama ya lugha. Binafsi ninatafuta karama zote za Roho Mtakatifu zinazopatikana, hivyo nilikwenda mbele na mmoja wa wasaidizi akaweka mikono juu yangu. Lakini hakuna kilichotokea. Kwa nini? (Roho Mtakatifu alichagua kutonipa karama hiyo. Hilo linaweza kuwa jambo jema kwa kuwa mimi si mshiriki wa kanisa la kikarismatiki (la kipentekoste).)

 

    1.    Soma tena 1 Wakorintho 14:2. Ingawa sikupewa karama ya lugha, bado nina wasiwasi kuhusu kukosa kitu cha muhimu. Ni lugha gani hiyo “isiyosema na watu, bali husema na Mungu?” Lugha za malaika ni zipi (1 Wakorintho 13:1)? (Ninaamini lugha inayozungumza na Mungu, yaani lugha ya malaika, ni lugha inayotumika katika maombi ya faragha.)

 

      1.    Una maoni gani? Je, umewahi kupitia uzoefu kama huu?

 

    1.    Rafiki, kila mtu anapenda karama. Kwa nini usidhamirie, sasa hivi, kumwomba Mungu akujulishe ni karama gani au zipi za roho alizokupatia? Changamoto yangu kwako ni kutumia karama zako kuendeleza manufaa ya wote badala ya maslahi yako binafsi.

                                     

  1.   Juma lijalo: Taswira ya Upendo.