Somo la 7: Taswira ya Upendo

(1 Wakorintho 13)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
3
Lesson Number: 
7

Somo la 7: Taswira ya Upendo

 

(1 Wakorintho 13)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Upendo una maana gani? Siku hizi, upendo una maana nyingi sana kiasi kwamba karibu umepoteza maana yake halisi. Chukulia, kwa mfano, neno “upendo mkali.” Je, hiyo haionekani kama kauli inayojikinzanisha? Unawezaje kuwa mkali kwa mtu unayempenda? Licha ya hayo. Watu wengi wakomavu wanaelewa kwamba wakati mwingine kuwa mkali ni sehemu ya upendo. Chukulia, kwa mfano, Mungu alipowatoa Adamu na Hawa katika Bustani ya Edeni. Mungu aliendelea kuwapenda sana kiasi cha kuwa tayari kujitoa Mwenyewe kwa ajili yao. Lakini kwa mtazamo wa haraka haraka, kuwafukuza kutoka Edeni hakukuonekana kuwa tendo la upendo. Kichwa cha somo letu ni “Taswira ya Upendo.” Kama huna uhakika sura ya kitu unachotaka kukichora ikoje, utaanzaje kukichora? Hilo ndilo jukumu lililo mbele yetu. Somo letu juma hili linahusu ufafanuzi wa Paulo kuhusu upendo. Hebu tuzame kwenye somo letu ili tuelewe vizuri zaidi maana ya upendo!

 

  1.    Umuhimu wa Upendo

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 13:1-3. Upendo ni wa muhimu kiasi gani? (Unaonekana kuwa na umuhimu wa kipekee sana.)

 

      1.    Hebu tujikite kwenye 1 Wakorintho 13:2. Fikiria kwamba unaelewa “siri zote na maarifa yote.” Kwa kuongezea, fikiria kwamba imani yako ni kubwa mno kiasi cha kuweza kuhamisha milima. Kama ningekupa uchaguzi kati ya hayo yote au upendo, ungechagua nini? (Kwa kuwa sina uhakika upendo unamaanisha nini hasa, ningechagua maarifa na nguvu.)

 

        1.    Paulo anasema kwamba kama ungefanya uchaguzi wangu, wewe “si kitu.” Anachokitetea Paulo si kweli kiuhalisia. Kama mtu angekuwa na maarifa yote na kuelewa siri zote, huyo angekuwa mwanadamu mwenye maarifa kuliko wote duniani. Mfikirie Mfalme Sulemani. Hilo bila shaka ni jambo kubwa sana. Kwa kuwa ninaamini Biblia ni ya kweli, tunahitaji kuchunguza Paulo anamaanisha nini. Unadhani anamaanisha nini?

 

      1.    Hebu tujikite kwenye 1 Wakorintho 13:3. Kama mtu angegawa mali zake zote na hata kukubali kufa, bila shaka ingekuwa kweli kwamba mtu huyo “hakupata faida yoyote” ikiwa hana upendo. Kwa namna fulani, sidhani kama hicho ndicho anachokimaanisha Paulo. Je, Paulo anasema kuwa kujitoa mhanga kwa kiwango cha juu kabisa ni jambo baya au jema? (Anaonekana kusema kuwa ni jambo jema.)

 

        1.    Biblia yote inafundisha nini kuhusu kujitoa mhanga? (Kujitoa mwenyewe hata kufikia kuyatoa maisha yako ndicho hasa alichotufanyia Yesu.)

 

        1.    Inawezekanaje jambo hilo lisifae chochote?

 

    1.    Hebu tuangalie kauli za Paulo kwa namna nyingine. Kama ungetakiwa kumwelezea Mkristo mkamilifu, ungefanyaje? (Anachokielezea Paulo katika 1 Wakorintho 13:2-3 ni taswira ya Mkristo mkamilifu, isipokuwa tu sehemu ya upendo. Paulo hakosoi karama za Mkristo mkamilifu.))

 

    1.    Hebu pia tuzingatie muktadha. 1 akorintho 12 inazungumzia karama za roho. 1 Wakorintho 14 inarudi tena kuzungumzia karama za roho. Kwa nini Paulo anaingiza sura inayohusu upendo katikati ya mjadala wa karama? (Hii inaunga mkono zaidi hitimisho kwamba Paulo hasemi kuwa karama na vipawa vya roho si kitu, bali kwamba nguvu ya kiroho isiyoambatana na tabia ya upendo haina maana yoyote kiroho.)

 

      1.    Kwa hiyo Paulo anatufundisha nini kuhusu upendo? (Anatuambia kwamba kuwa na upendo ni sifa ya muhimu kwa Mkristo. Haitoshi kuwa mkamilifu katika mambo mengine yote. Paulo anapoandika kwamba karama kubwa “haina maana yoyote,” anasema kwamba karama peke yake hazitoshi.)

 

    1.    Kama umekuwa mshiriki wa kanisa kwa muda mrefu, bila shaka utakuwa umewaona watumishi wenye karama za hali ya juu wanaofanya uzinzi. Hilo linatokeaje? (Sababu mojawapo ni kwamba mtumishi mwenye karama anajipenda kuliko anavyompenda mkewe, familia yake, au waumini wake. Kwa yeye kutokuwa na upendo kunaangamiza ndoa yake na huduma yake. Karama zake “hazina maana.”)

 

  1.   Kuufafanua Upendo

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 13:4-7. Fikiria mtu wa karibu maishani mwako anakuuliza, “Ninawezaje kujua kwamba unanipenda?” Utajibuje swali hilo?

 

      1.    Paulo ana njia ya pekee ya kuchora taswira ya upendo. Anasema kuwa mitazamo saba inafafanua upendo, na mitazamo minane inafafanua kutokuwepo kwa upendo. Hebu tuipitie.

 

        1.    Mitazamo gani inaendana na upendo? (Uvumilivu. Fadhili. Kufurahia kweli. Kuvumilia yote. Kuamini yote. Kutumaini yote. Kustahimili yote.)

 

          1.   Je, mitazamo hii ndio namna ambayo ungedhihirisha kwamba unampenda mtu?

 

        1.    Mitazamo ipi haiendani na upendo? (Wivu. Majivuno. Kiburi. Ufidhuli. Kung’ang’ana kupata unachokitaka. Maudhi. Chuki. Kufurahia udhalimu.)

 

          1.   Kama mtu angedai kwamba humpendi, je, mifano hii ingekushawishi kwamba kweli huna upendo?

 

      1.    Ninapoangalia mitazamo mizuri na mibaya, hitimisho langu ni kwamba inafafanua ama watu wema au wabaya. Lakini sidhani kama moja kwa moja inafafanua upendo au kutokuwepo kwa upendo. Nimekosea kwa kiasi gani?

 

    1.    Tumekuwa tukiitazama 1 Wakorintho 13:4-7 kama ufafanuzi wa upendo. Je, ingekuwa sahihi zaidi kusema kwamba Paulo anatupatia kipimo cha kutambua upendo? Kwamba kama upendo ukiingia chumbani, hivi ndivyo utakavyojidhihirisha kitabia?

 

      1.    Kama hiki ni kipimo cha kutambua upendo, wewe ungepimwa na kupata matokeo gani?

 

      1.    Unaonesha mitazamo mingapi mizuri na mibaya maishani mwako?

 

      1.    Njia moja ya kujipima kuhusiana na sifa hizi ni kubadilishana jina lako na “upendo.” Kwa mfano, “Bruce ni mvumilivu.” “Bruce hana wivu.”

 

    1.    Angalia tena 1 Wakorintho 13:6. Inamaanisha nini “kufurahia kweli” badala ya “kufurahia uovu?” (Hii inaunga mkono dhana ya upendo mkali (tough love). Upendo hauhitaji kukubaliana, kuidhinisha, au kuepuka migogoro pale ambapo kuna uovu. Wakati mwingine upendo husahihisha, hurekebisha nidhamu, huonya, au hupinga uovu. Utakumbuka kwamba Paulo anasisitiza kuwa Wakorintho wanakabiliana na dhambi kubwa iliyokuwako kanisani. Kwa hiyo uvumilivu na fadhili havihitaji kujifanya/kujidanganya kwamba uovu ni mzuri.

 

      1.    Vipi kuhusu 1 Wakorintho 13:7 inayosema watu wenye upendo “huvumilia yote,” au “hustahimili yote?” (Maoni ya mchambuzi wa Biblia J. Vernon McGee yanasema kuwa “kuvumilia” hujumuisha “fikra ya ulinzi.” Upendo huweka mwavuli kwa watu wengine. Kuhusu “kustahimili,” anasema kuwa “upendo hubaki imara wakati wa majaribu.” Hiyo ni tofauti na kuvumilia uovu.)

 

      1.    Paulo anamaanisha nini anaposema kuwa upendo “huamini yote?” Mtoto wako anapodanganya kuhusu kosa alilofanya, je, lazima uamini uongo wake? (Kwa mara nyingine, McGee anapendekeza kwamba Paulo anamaanisha kuwa hatupaswi kuwashuku watu. Haimaanishi kuwa tunapaswa “kuamini kila jambo bila kutumia hekima.”)

 

    1.    Je, unaweza kuelezea kwa ufupi 1 Wakorintho 13:4-7 kwa sentesi moja au mbili? (Upendo ni kuondoa nafsi yako kutoka katika kiini cha maisha yako. Ni kujitoa kwa dhati kutafuta mema ya wengine ambako huakisiwa katika mwenendo wako.)

 

  1. Mustakabali wa Upendo

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 13:8-10. Mustakabali wa upendo ni upi? (Utadumu kuliko karama zako za roho!)

 

      1.    Ukamilifu utakuja lini? (Hii inarejelea kuja kwa Yesu Mara ya Pili. Tutabadilishwa, na karama zetu za roho ambazo hazijakamilika zitakamilishwa kikamilifu.)

 

      1.    Karama gani mahsusi zinasemwa kuwa zina mwisho wake? (Kunena kwa lugha, unabii, na maarifa.)

 

        1.    Je, kuna sababu maalumu kwa nini kunena kwa lugha na unabii vitakoma? (Unabii utatimia. Mbinguni tutakuwa na lugha moja.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 13:11-12. Kwa nini Paulo anaandika kuhusu watoto na watu wazima? (Anachomaanisha ni kwamba mitazamo yetu isiyo mikamilifu itafikia ukamilifu mbinguni.)

 

      1.    Paulo anazungumzia nini anaposema tutaonana “uso kwa uso?” (Tutamwona Yesu uso kwa uso. Tutamwona Yeye ambaye ni upendo mkamilifu.)

 

      1.    Paulo anatuambia nini anapoandika, “kama mimi nami ninavyojuliwa sana?” (Tayari Mungu anatujua kikamilifu. Tutakapomwona uso kwa uso, kumjua kwetu hakutakuwa tena kwa sehemu au kwa namna isiyo wazi, bali kutakuwa kamili.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 13:13. Paulo anapoandika kuwa “katika hayo lililo kuu ni upendo,” je, analinganisha upendo na imani na tumaini tu? (Analinganisha moja kwa moja upendo na imani na tumaini. Kwa muktadha mpana zaidi, mambo yote matatu ni makubwa kuliko karama za roho zinazovutia, lakini upendo ni mkuu kwa sababu kamwe hauishi na kwa sababu huzipa karama thamani zake halisi za roho. Ndio maana Paulo anaendelea kutuhimiza “kuutafuta na kuufuatilia upendo.”)

 

    1.    Rafiki, ulipojipima kwa kutumia kipimo cha Paulo cha upendo, ulipata alama ngapi? Ikiwa wewe, kama ilivyo kwangu, unahitaji maboresho, kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu, sasa hivi, akubadilishe na kukufanya uwe mtu mwenye upendo zaidi?

 

  1.   Juma lijalo: Nguvu ya Ufufuo wa Kristo.