Somo la 8: Nguvu ya Ufufuo wa Kristo

(1 Wakorintho 15)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
3
Lesson Number: 
8

Somo la 8: Nguvu ya Ufufuo wa Kristo

 

(1 Wakorintho 15)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Hoja zenye mantiki huwa na muundo fulani. Muundo huo unahitaji angalao kigezo mantiki (msingi wa hoja) kimoja, na mara nyingi vigezo mantiki viwili, kabla ya kufikia hitimisho. Mfano huu hapa. Murray ni panzi. Panzi wote ni wadudu. Kwa hiyo, Murray ni mdudu. Hitimisho ni kwamba Murray ni mdudu, na misingi muhimu ya hoja ni kwamba Murray ni panzi, na panzi wote ni wadudu. Katika somo letu juma hili, Paulo anajenga hoja inayohitimisha kwamba kuna ufufuo wa wafu. Ukweli muhimu wa hitimisho hilo ni kwamba Yesu alifufuka kutoka katika wafu. Kisha Paulo anajenga hoja kwamba ufufuo wa Yesu, kama “malimbuko” ya wale waliofariki, unatoa hakikisho la ufufuo wa baadaye wa wale walio wake. Hebu tuchimbue hoja ya Paulo kuhusu ufufuo!

 

  1.    Hoja Kuhusu Ufufuo wa Wafu

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:13. Paulo anatupatia msingi gani wa hoja kuhusu ufufuo wa wafu? (Ikiwa hakuna ufufuo wa wafu, basi Kristo hakufufuka.)

 

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:20. Paulo anaweka wazi ukweli gani unaohusiana na msingi huu wa hoja? (Kristo amefufuka katika wafu.)

 

      1.    Ikiwa Kristo amefufuka, hiyo inatuambia nini kuhusu madai kwamba hakuna ufufuo wa wafu? (Lazima madai hayo yatakuwa ya uongo. Kwa hiyo, kuna ufufuo wa wafu.)

 

  1.   Athari/Matokeo Ikiwa Yesu Hakufufuliwa

 

    1.    Ukweli muhimu-kwamba Yesu amefufuka katika wafu-ni pendekezo gumu sana kulithibitisha kwa watu wasiojua chochote kuhusu Ukristo. Lilikuwa gumu kiasi cha kutosha kujenga hoja kwamba Mungu angeweza kusulubiwa. Lakini hoja ya ziada kwamba Mungu aliyesulubiwa alifufuka na kuurudia uzima ilikuwa changamoto kubwa zaidi. Utajengaje hoja kwamba Yesu alifufuka katika wafu?

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:14. Athari ya kwanza ni ipi ikiwa Yesu hakufufuka katika wafu? (Ikiwa si kweli, imani za kidini za Wakorintho ni za uongo na hazina maana.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:17. Hebu turudi nyuma na tuchunguze hoja za Paulo zinazounga mkono ukweli wa imani za kidini za Wakorintho. Soma 1 Wakorintho 15:1-2. Kwa nini Wakristo wa Korintho wanapaswa kuamini kuwa imani zao za kidini ni za kweli? (Paulo anawakumbusha kwamba tayari waliikubali injili kuwa ya kweli, na ukweli huu unawaokoa.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:15. Hoja ya pili ya Paulo inayounga mkono ukweli kwamba Yesu amefufuka katika wafu ni ipi? (Ikiwa ukweli huo ni wa uongo, si tu kwamba Wakorintho wanawadanganya wengine, bali wanamwakilisha Mungu kwa uongo.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:16-17. Athari gani zaidi zinafuata ikiwa Yesu hakufufuka? (Ikiwa ufufuo si wa kweli, si tu kwamba Wakorintho hawajapokea imani “isiyo na maana” bali jambo baya zaidi ni kwamba bado wako katika dhambi zao. Hawana tumaini la siku zijazo.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:18. Paulo anajenga hoja gani ya nne yenye mantiki kuhusu ufufuo wa Yesu katika wafu? (Ikiwa si wa kweli, basi marafiki wote na wanafamilia wa Wakorintho waliofariki wametoweka. Wamepotea na hawataonekana wala kusikika tena.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:19. Paulo anajenga hoja gani ya tano yenye mantiki kuhusu ufufuo wa Yesu katika wafu? (Ikiwa si wa kweli, Wakristo ni kundi la wapumbavu linalopaswa kuhurumiwa na wale wanaouelewa ukweli.)

 

      1.    Kauli ya Paulo inaweza kueleweka vibaya kiurahisi. Kama pasingekuwepo na tumaini la maisha ya baadaye, je, Ukristo bado ungefundisha njia nzuri ya kuishi? (Ninaamini kwamba hilo ni kweli. Maisha ya Kikristo ni maisha yaliyoishi vizuri.)

 

  1.      Ushahidi wa Ufufuo wa Yesu

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:3-4. Ushahidi gani upo kuhusu ufufuo wa Yesu? (Paulo anasema kuwa “Maandiko,” ikimaanisha Agano la Kale, yana utabiri wa kina kuhusu kifo na ufufuo wa Yesu.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:5. Ushahidi gani mwingine upo kuhusu ufufuo wa Yesu? (Petro (Kefa) na wanafunzi wengine waliosalia walimwona Yesu akiwa hai baada ya kuwa ameuawa.)

 

      1.    Kwa kuwa wanafunzi walikufa kwa kushiriki imani hii, walikuwa na nia gani ya kusema uongo kuhusu ufufuo?

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:6. Huu ni ushahidi wa namna gani? (Paulo anaandika kwamba zaidi ya wafuasi 500 wa Yesu walimwona akiwa hai baada ya kusulubiwa kwake, na wengi wao wanaweza kuulizwa kuhusu kile walichokiona.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:7-8. Jambo gani ni la pekee kuhusu ushuhuda huu wa kuona kwa macho? (Hawa ni viongozi wa kanisa. Je, ungekuwa kiongozi wa kanisa kwa msingi wa kile ulichojua kuwa ni uongo?)

 

      1.    Jibu la wazi kwa swali lililotangulia ni, “Hapana” – isipokuwa kama kulikuwa na malipo ya fedha. Je, kulikuwa na faida kuwa kiongozi katika kanisa la awali? (Hapana. Mateso ndilo jambo lililokuwa na uwezekano mkubwa kutokea. Na hili ni kweli hasa kwa Paulo ambaye anataarifu kuwa yeye pia ni shuhuda aliyeona kwa macho.)

 

  1.   Teolojia Inayounga Mkono Ufufuo wa Yesu

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:20-22. Uelewa wetu ni kwamba Adamu ndiye aliyetuingiza kwenye mauti ya milele. Unadhani kwa nini dhana hiyo ya kiteolojia ni ya kweli? (Kwa sababu Adamu na Hawa walichagua kutokumtii Mungu, dhambi iliingia katika ulimwengu wetu.)

 

      1.    Je, hiyo ni haki? (Mara kwa mara tunarithi athari-nzuri na mbaya-kutokana na uamuzi ambao sisi wenyewe hatukuufanya. Tunazaliwa katika ulimwengu ambao umeathiriwa kwa kiwango kikubwa na wale waliotutangulia.)

 

      1.    Yesu amegeuzaje kosa la Adamu? (Adamu alituletea kifo, Yesu anatuletea uzima. Yesu ni “malimbuko” kwa wale wanaofufuliwa.)

 

        1.    Angalia kwa kina dhana hii. Tulifanya matendo gani ili kurithi adhabu ya kifo ya Adamu? (Hakuna tulichofanya. Hatukufanya chochote ili kuzaliwa katika ulimwengu ulioanguka, ingawa baadaye tunatenda dhambi zetu wenyewe.)

 

        1.    Ikiwa hatukupata urithi wa Adamu kwa matendo yetu wenyewe, je, inaleta mantiki kwamba tunaweza kupokea karama ya Kristo ya uzima bila kuipata kwa matendo yetu? (Ndiyo. Uzima wa milele ni karama ya Mungu kwa wale walio wa Kristo.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:23-24. Kristo alifufuka siku tatu baada ya kifo chake. Ufufuo wetu kutoka katika wafu utatokea lini? (Wakati wa kuja kwa Yesu Mara ya Pili atakapokuwa ameshinda kila utawala na mamlaka kinzani.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:25-26. Inamaanisha nini kwa kifo kuangamizwa? (Kifo hakitakuwepo tena kwa wale waliookolewa.)

 

  1.    Majibu kwa Maswali

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:29. Paulo amekuwa akijenga hoja kuhusu ufufuo wa wafu. Hapa anataarifu kuwa watu wengine wanasema kwamba mtu anaweza kubatizwa kwa niaba ya mtu aliyefariki. Ikiwa mtu asiyeamini amefariki, je, unaweza kumpa uzima wa milele kwa ubatizo wakilishi? (Kama mtu amefariki, mtu huyo amevuka kipimo cha kumkiri na kumpokea Yesu.)

 

      1.    Je, Paulo anaidhinisha dhana ya ubatizo kwa wafu? (Sidhani. Paulo anataarifu kile ambacho watu wengine wanakisema. Anachokimaanisha Paulo ni kwamba madai haya hayana mantiki isipokuwa kama wafu watafufuliwa ili kuishi tena.)

 

      1.    Tuchukulie kwamba Paulo anaidhinisha, na si tu kutaarifu mitazamo ya watu wengine. Tunapaswa kulielewaje hili? (Njia ya msingi ya kulielewa hili ni kwamba ubatizo wetu ni ukubali wa maisha, kifo, na ufufuo wa Yesu. Ubatizo wetu unakiri na kupokea kifo chake na ufufuo wake unafanya ufufuo wetu uwezekane. Hii inaleta mantiki kamilifu katika muktadha wa hoja ya Paulo.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:35. Je, Paulo anachukulia kwamba wafu waliofufuliwa watakuwa na miili badala ya kuwepo kama roho zisizo na miili? (Ndiyo. Swali lenyewe linauliza aina gani ya “mwili” watakao kuwa nao.)

 

      1.    Soma 1 Wakorintho 15:42–44. Tutakuwa na mwili wa namna gani? (Mwili usioharinbika, wenye utukufu, na nguvu, yaani, “mwili wa kiroho.” Mwili wa kiroho bado ni mwili; Paulo haelezei roho isiyo na mwili.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:36-39. “Chembe [punji] tupu” ya mwili wako ni kitu gani? (Ninaamini ni alama ya siri (code) inayokutambuisha.)

 

      1.    Unapaswa kutarajia nini kuhusu mwili wako mpya? (Mungu anatupatia mwili mpya, na Paulo anaufananisha na “nyama.” Hitimisho lenye mantiki ni kwamba huu ni mwili halisi kwa sababu vinginevyo rejea ya nyama za wanyama haina mantiki yoyote.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:51-55. Ufufuo ambao tutapokea miili yetu mipya utatokea lini? (Wakati wa “parapanda ya mwisho.” Yesu anapokuja tena anawafufua wafu na kuwabadili katika miili yao mipya.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 15:57. Tunapaswa kumshukuru nani kwa ushindi huu dhidi ya kifo?

 

    1.    Rafiki, je, umeshawishika kwamba Yesu alifufuka kutoka katika wafu? Ikiwa ndivyo, ufufuo wake unamaanisha kwamba wewe-na kila aliye wake-anaweza kuwa na tumaini la uhakika wa ufufuo na uzima wa milele. Je, utashiriki tumaini hilo na wale ambao bado hawaamini? Kwa nini usidhamirie kufanya uamuzi huo sasa hivi?

 

  1.   Juma lijalo: Huduma Inayosukumwa na Upendo.