Somo la 9: Huduma Inayosukumwa na Upendo
Somo la 9: Huduma Inayosukumwa na Upendo
(2 Wakorintho 1)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.
Utangulizi: Je, umewahi kupitia nyakati ambazo matatizo yako yalionekana kuwa makubwa kupita kiasi? Vipi ikiwa matatizo hayo hayakuwa kosa lako? Vipi ikiwa matatizo hayo yalitokea kwa sababu ulikuwa unajaribu kufanya mapenzi ya Mungu? Ikiwa matatizo hayo hayakuhusiana na uamuzi wako mbaya, huenda ulijiuliza, “Mungu yuko wapi katika jambo hili? Kwa nini anaruhusu haya yatokee?” Mbali na changamoto zako binafsi, je, paliwahi kuwepo nyakati ambazo marafiki wako wa kanisani walikabiliana na magumu, nawe hukujua useme nini ili kuwafariji? Juma hili Paulo anaeleza matatizo aliyokabiliana nayo pamoja na waumini wa Korintho. Mjadala wake utatusaidia kuelewa kwa kina jinsi ya kukabiliana na matatizo. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!
- Jambo Jema Kuhusu Matatizo
-
- Soma 2 Wakorintho 1:3-4. Jambo jema kuhusu mateso ni lipi? (Ikiwa tumepitia mateso na Mungu ametufariji, tumejifunza jambo fulani kuhusu jinsi ya kuwafariji wengine.)
-
-
- Ni sifa zipi mbili za Mungu zinaweza kutusaidia tunapokabiliana na matatizo? (Yeye ni Baba wa “rehema.” Yeye ni “Mungu wa faraja yote.”)
-
-
- Angalia tena 2 Wakorintho 1:4. Je, umewahi kumwona mtu akijaribu kukufariji lakini akifanya hivyo kwa njia isiyofaa? (Ikiwa ndivyo, hilo lilikufundisha kuwa si kila jitihada za kukufariji zinafanikiwa.)
-
-
- Ninakumbuka kwenye msiba fulani mtu mmoja alijaribu kutoa faraja kwa kusema, “Usiwe na wasiwasi; hii ni sehemu ya mpango wa Mungu.” Una maoni gani juu ya jaribio hilo la kuleta faraja? (Inaweza kufanya ionekane kana kwamba Mungu ndiye aliyesababisha kifo cha mtu huyo moja kwa moja. Na inaweza kufanya ionekane kana kwamba Mungu alikuwa na mambo ya muhimu zaidi kuyatekeleza kuliko kumwacha mpendwa wako aendelee kuishi.)
-
-
-
- Jaribio lenye utata la kutoa faraja linalohusiana na hilo lililobainishwa hivi punde ni kueleza kile unachokiona kama sababu ya Mungu kuruhusu kifo hicho. “Mungu alitaka kumtumia mpendwa wako kuwafundisha wengine wasivute sigara.” Je, hilo linafariji?
-
-
-
-
- Utaona kwamba kichwa cha somo hili ni “Huduma Inayosukumwa na Upendo.” Ni muhimu kiasi gani kuzingatia ikiwa faraja unayotoa ni jaribio la kuonyesha upendo?
-
-
-
- Soma 2 Wakorintho 1:5-7. Paulo anarudia dhana ya kwamba kupitia uzoefu wa mateso na faraja hutusaidia kuwabariki wale ambao pia wanapitia mateso. Unadhani kwa nini analirudia somo hili? (Kwa sababu mateso yetu na faraja ya Mungu si tu uzoefu binafsi; Mungu anaweza kuvitumia kutuwezesha kuwasaidia wengine.)
-
- Kadiri watu wanavyoishi muda mrefu zaidi, ndivyo wengi wetu tunavyokabiliana na ugonjwa wa kusahau (dementia), ama kwetu binafsi au kwa watu tunaowapenda. Hebu tuchunguze mafunzo halisi niliyojifunza kutokana na mateso ambayo mimi na mama wangu tuliyapitia katika ugonjwa wake wa mwisho.
-
-
- Mama yangu alifariki kwa ugonjwa wa Alzheimer, ambao ni aina fulani ya ugonjwa wa akili. Jambo moja nililoligundua ni kwamba ugonjwa wa Alzheimer unaweza kuathiri vichujio ambavyo hapo awali mtu alivitumia kuishi vizuri na watu wengine. Kwa mfano, mama wangu, ambaye kamwe hakuonekana kukasirika, alianza kuwa na hasira za mara kwa mara. Mfano mwingine, kamwe sikuwahi kumsikia mama yangu akiapa. Lakini sasa alianza kuapa mara kwa mara. Maarifa hayo yanawezaje kuwa faraja kwa wengine? (Yanaweza kuwasaidia wanafamilia kuelewa kwamba tabia inayoumiza inaweza kusababishwa na ugonjwa huo na si lazima ichukuliwe kibinafsi.)
-
-
-
- Matokeo mengine ya ugonjwa wa Alzheimer ni kwamba unasahau mahali unapoweka vitu. Wakati mwingine unaviweka sehemu za ajabu kabisa [zisizo za kawaida]. Mama wangu alidhani kwamba kuna mtu alikuwa anavunja nyumba na kuingia nyumbani kwake na kuiba vitu alivyokuwa ameviweka mahali aliposahau. Maarifa hayo yanawezaje kuwa ya faraja? (Yanatusaidia kuelewa kwamba tuhuma za wizi zinaweza kutokana na kupotea kwa kumbukumbu na kuchanganyikiwa badala ya kutowaamini wengine kwa dhati.)
-
-
-
- Hatimaye, jambo lililonisumbua sana ni kwamba ndugu wa mbali walisisitiza kuwa nimpeleke mama wangu katika kituo cha malezi ambako angepata uangalizi wa karibu. Mama wangu alinisihi nisimwondoe nyumbani kwake. Maisha ya mama wangu yalikuwa katika hatari kubwa zaidi alipobaki nyumbani kwake. Kama umewahi kumwona rafiki au ndugu akifariki kutokana na ugonjwa wa Alzheimer, ungenishauri nifanye nini? Ungetoa ushauri gani wa faraja na wenye kuonesha upendo? (Kama kwa wakati huo ningejua kile ninachokijua sasa hivi, ningemwacha mama yangu nyumbani kwake hadi pale ambapo angeshindwa kujihudumia. Uhuru wake ulikuwa wa thamani kubwa zaidi kuliko kuongeza kwa kiasi kidogo maisha yake magumu yaliyokuwa mbele yake.)
-
- Faida ya Paulo Katika Kuwafariji Wengine
-
- Soma 2 Wakorintho 1:8-10. Ni sifa zipi alizokuwa nazo Paulo zilizomwezesha kuwafariji watu wa Korintho? (Mateso yake yalikuwa makali sana kiasi kwamba alidhani kuwa angekufa.)
-
-
- Mateso haya ya kutisha yalimfundisha nini Paulo? (Kumtegemea Mungu kikamilifu. Kama Mungu atawafufua wafu, basi anaweza kuwaokoa wale wanaohofia kwamba wanakufa.)
-
-
- Soma 2 Wakorintho 1:11. Nilisikiliza wasilisho kuhusu tafiti zinazochunguza manufaa ya maombi kwa wagonjwa. Utafiti mmoja wa hivi karibuni umebaini kwamba maombi ya kumwombea mtu ana kwa ana yalipunguza maumivu na wasiwasi, wakati utafiti mkubwa wa maombi ya kumwombea mgonjwa kwa mbali haukuonesha nafuu kwenye matatizo yaliyotokana na upasuaji wa moyo. Paulo anasema nini kuhusu maombi ya kuwaombea wengine? (Anasema kuwa, “maombi ya wengi” yalichangia katika baraka waliyopokea. Tafiti za kisayansi zinaweza kuwa na ugumu wa kupima kazi ya Mungu, lakini Paulo aliamini wazi kwamba maombi ya wengine yalikuwa na umuhimu.)
- Paulo Ajitetea
-
- Soma 2 Wakorintho 1:12-14. Paulo anaposema kuwa Wakorintho “wanatuelewa kwa sehemu tu,” hilo linaashiria kwamba tatizo ni lipi? (Kutoaminiana kumeibuka kutokana na kushindwa kwa Wakorintho kuelewa kikamilifu barua ya Paulo.)
-
-
- Hilo linapaswa kutufundisha nini pale tunapokuwa hatumfurahii mtu fulani? (Tunapaswa kuhakikisha kuwa tunachukua hatua tukiwa na taarifa kamili. Hatupaswi kudhania mambo mabaya zaidi.)
-
-
- Soma 2 Wakorintho 2:17. Ukweli kwamba Paulo analazimika kujitetea unaashiria nini kuhusu mashtaka yaliyoletwa dhidi yake? (Mashtaka ni kwamba Paulo si mkweli. Yupo kwenye huduma kwa ajili ya kujipatia fedha.)
-
- Angalia tena 2 Wakorintho 1:12-13. Paulo anajenga hoja gani inayoonesha kwamba yeye ni mkweli, na si “mchuuzi” wa neno la Mungu? (Tabia yake ilikuwa rahisi – hakujihusisha kwenye mpango mgumu ambao watu wangeweza kushindwa kuuelewa.)
-
-
- Hebu tusimame kidogo na kutafakari yote tuliyoyasoma. Unadhani kwa nini Paulo alijadili mateso yake kabla hajaingia kwenye utetezi wa matendo yake? (Mateso ya Paulo yanaweka msingi wa hoja kwamba yeye ni mkweli katika uhusiano wake na Wakorintho.)
-
-
- Soma 1 Wakorintho 4:19 na 1 Wakorintho 16:5-7 ili kugundua shambulio jingine dhidi ya Paulo. Je, Paulo alikuwa na mipango thabiti ya safari? (Paulo alipanga kwenda Korintho na alikuwa na rasimu ya ratiba. Lakini, safari yake ilitegemea mapenzi ya Mungu.)
-
- Soma 2 Wakorintho 1:15-17. Hii inaashiria nini kuhusu kile wanachokisema Wakorintho kuhusu mipango ya safari ya Paulo ya kuwaona? (Inaonekana ni kama vile wanamkosoa. Wanaonekana kusema alikuwa “akibadilisha-badilisha mawazo.”)
-
-
- Je, umewahi kupitia uzoefu wa jambo hili linapokuja suala la familia kukutembelea au wewe kuitembelea? (Wazazi wangu walikuwa na wivu kuhusu sisi kutumia nao muda wa kutosha.)
-
-
-
- Je, umewahi kupitia uzoefu wa jambo hili katika muktadha tofauti, ambapo mtu anakuambia kuwa anapanga kukusaidia lakini hafanyi hivyo?
-
-
- Soma 2 Wakorintho 1:18-20. Paulo anajibuje pendekezo la kwamba mipango yake iliyobadilika inaonesha kuwa yeye si mtu wa kuaminika? (Anajielekeza kwenye kuaminika kwa ujumbe aliohubiri. Yesu Kristo hakuwa “Ndiyo na Siyo.” Ahadi zote za Mungu zinapata “Ndiyo” zao katika Kristo. Mipango ya safari ya Paulo iliyobadilika haimaanishi kwamba ama injili yake au sifa yake haiaminiki.)
-
- Soma 2 Wakorintho 1:21-24 na 2 Wakorintho 2:1. Kwa nini Paulo hakwenda Korintho kama washiriki wa kanisa walivyotarajia? (Paulo anasema kuwa hakwenda kwa sababu alitaka kuwaepusha na maumivu mengine.)
- Barua ya Uchungu
-
- Soma 2 Wakorintho 2:4 na 2 Wakorintho 7:8. Paulo alifanya nini kama mbadala wa kwenda kuwatembelea? (Aliwatumia barua Wakorintho iliyowafanya “wahuzunike.”)
-
-
- Unadhani kwa nini alituma barua badala ya kwenda yeye mwenyewe? Je, barua ilikuwa na msongo mdogo? (Barua inamfanya mpokeaji atafakari ujumbe wote kwa utulivu zaidi.)
-
-
- Soma 2 Wakorintho 7:9-11. Je, barua ilisaidia? (Ndiyo. Ilizaa toba. Hii inaonesha mafanikio ya mkakati wa Paulo wa kuandika badala ya kuwatembelea.)
-
-
- Zingatia kifungu cha 10. Tukitubu tabia yetu mbaya, matokeo ni yepi? (Wokovu bila majuto.)
-
-
-
- Je, kuna jambo katika maisha yako ya zamani bado linakuletea majuto? Je, huzuni ya kimungu dhidi ya mambo yetu ya zamani inapaswa kuzaa nini? (Toba inayojielekeza kwenye wokovu. Tofauti na huzuni ya kidunia, huzuni ya kimungu inatusogeza kwa Mungu badala ya kutupeleka kwenye kukata tamaa.)
-
-
- Rafiki, je, umeona upande mzuri wa mateso? Je, umeona jinsi marekebisho yanayotolewa kwa upendo yanavyoweza kusababisha huzuni ya muda lakini hatimaye yakazaa jambo jema? Mawazo haya yote mawili yanaweza kuonekana kuwa na mashaka mwanzoni, lakini Biblia inatuonesha jinsi Mungu anavyoweza kubadili mateso yetu kuwa baraka kwa wengine, na jinsi karipio la kimungu linavyoweza kutuongoza kwenye toba na wokovu bila kujutia. Mwombe Roho Mtakatifu akuongoze katika njia ya upendo unapokabiliana na changamoto hizi.
- Juma lijalo: Huduma Halisi ya Kikristo.
