Somo la 10: Huduma Halisi ya Kikristo
Somo la 10: Huduma Halisi ya Kikristo
(2 Wakorintho 3, 5-7, Yeremia 31)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.
Utangulizi: Juma lililopita nilihudhuria mkutano wa vibanda (maarufu kama makambi)! Nilikuwa nimealikwa kuzungumza kuhusu uhuru wa dini katika mkutano wa uhuru wa dini. Lakini waandaaji waliamua kuongeza siku za mkutano huo na kuwa siku kadhaa za mawasilisho kuhusu uhuru wa dini na injili. Hivyo ukawa “mkutano wa makambi.” Mitazamo ya baadhi ya wazungumzaji ilinirejesha katika ujana wangu nilipokuwa nikihudhuria mikutano ya makambi mara kwa mara iliyolenga utakatifu wa mtu binafsi. Hili lilinifanya nitafakari tena, kwa mara nyingine, mjadala juu ya imani dhidi ya matendo. Ingawa nimekulia katika upande sahihi wa imani, mara zote ni jambo jema kwangu kuwa tayari kukubali uwezekano kwamba mtazamo wangu unahitaji kusahihishwa. Kwa kuwa watu wengi sana husoma masomo haya, ni muhimu kuwa na uwiano sahihi wa jambo hili. Kwa mtazamo huo, nilipata ugumu pale Paulo alipoziita Amri Kumi “huduma ya mauti.” 2 Wakorintho 3:7. Hebu tuzame kwenye mjadala wetu wa barua ya Paulo ili tuone kama tunaweza kuelewa jambo hili kwa usahihi!
- Huduma ya Mauti
-
- Soma 2 Wakorintho 3:2-3. Paulao anamaanisha nini anaposema kuwa barua ya Kristo imeandikwa katika “vibao ambavyo ni mioyo ya nyama?” Na kwa nini analinganisha hilo na “vibao vya mawe?” (Paulo anaandika kwamba waumini ni “barua ya Kristo” kwa wengine. Barua hiyo inaakisiwa mioyoni mwao. Haikuandikwa kwenye mawe.)
-
- Soma 2 Wakorintho 3:5-6. Paulo analinganisha “andiko” na “Roho.” Anamaanisha nini kwa hili? (Andiko linarejelea herufi zinazounda Amri Kumi. Roho inarejelea Roho Mtakatifu.)
-
- Soma 2 Wakorintho 3:7-8. Paulo anaziita Amri Kumi, ambazo zilichorwa katika mawe, “huduma ya mauti.” Nimeambiwa kuwa Amri Kumi ni nakala ya tabia ya Mungu. Je, nilifundishwa vibaya? Unayaelewaje maneno ya Paulo?
-
- Ili kuelewa jambo hili vizuri zaidi, soma Yeremia 31:31-34. Je, Amri Kumi zimekufa? Je, yaliyomo ndani yake hayana umuhimu? (Agano jipya, kwa mujibu wa Yeremia, linaandika sheria ya Mungu mioyoni mwa watu wake.)
-
-
- Paulo anapotofautisha katika 2 Wakorintho 3:7-8 “huduma ya mauti” na “huduma ya Roho,” inaonekana kana kwamba anamuweka Roho Mtakatifu dhidi ya Amri Kumi. Yeremia anatusaidiaje kuelewa kile anachotufundisha Paulo? (Roho Mtakatifu ndiye anayetutia moyo kutenda mambo sahihi. Hivi ndivyo mioyo yetu inavyotuongoza katika njia ya maisha.)
-
-
-
- Kuna tatizo jingine la kimantiki kwenye hii dhana. Kwa nini sheria ile ile, inapoandikwa kwenye mawe iwe sheria ya mauti, lakini inapoandikwa mioyoni mwetu iwe ya utukufu? Je, mahali sheria ilipoandikwa pana umuhimu? (Kwa haraka haraka inaonekana kama ni suala la mahali sheria ilipoandikwa. Nadhani tofauti ni kwamba mioyo yetu (Roho Mtakatifu anenaye ndani yetu) inatupatia mwongozo wa namna ya kuishi. Hii ni tofauti na kujifunza mfululizo wa kanuni ambazo kimsingi zinasem, usifanye hivi, vinginevyo utakufa.)
-
-
- Soma 2 Wakorintho 6:3-7. Je, Paulo anasema kuwa matendo yetu hayana umuhimu? (Kama ujumbe wa injili unatoka mioyoni mwetu, tabia njema ni ya muhimu kwa sababu “inampendekeza” Mungu kwa wengine. Maisha yetu ama yanapendekeza au yanahafifisha huduma yetu ya injili.)
-
-
- Je, umetafakari jinsi mwenendo wako ama unapendekeza au unahafifisha injili? Unapoyatangaza mapenzi ya Mungu, je, unafanya hivyo kwa namna ambayo pia inaakisi neema yake?
-
- Nira
-
- Soma 2 Wakorintho 6:14-17. Inamaanisha nini “kutofungiwa nira na wasioamini?” (Nira ni neno linalotokana na shughuli za kilimo. Angalia Kumbukumbu la Torati 22:10. Kwa kiwango cha chini kabisa, huduma ya Kikristo haipaswi kutuweka kwenye ushirika wa lazima na watu wanaoikataa injili.)
-
-
- Je, jambo hili linahusika kwenye kumwoa au kuolewa na mtu asiyeamini?
-
-
-
- Je, linahusika kuwa na ushirika wa kibiashara na mtu asiyeamini?
-
-
-
- Je, “mtu asiyeamini” ni yeyote yule asiye mshiriki wa madhehebu yako? (Paulo analinganisha neno “asiyeamini” na “Beliari.” Hili si suala la kukubaliana juu ya mambo yote ya injili; ni suala la utii kwa Kristo dhidi ya kutokuamini.)
-
-
- Angalia tena 2 Wakorintho 6:16. Paulo anapoandika kuhusu Wakristo kuwa “hekalu la Mungu aliye hai,” anamaanisha nini? (Paulo anasema kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yetu, na hivyo maisha yetu yanapaswa kuwa tofauti na wale wanaojihusisha na maisha maovu. Paulo anataka tuwaongoe wengine, lakini hadhani kama tunapaswa kuwa na uhusiano wa ndani sana (intimate) na wao.)
-
-
- Kwa kuzingatia mjadala wa Paulo kuhusu “nira” je, matendo yetu yana umuhimu? (Ndiyo. Paulo hatuambii kwamba Amri Kumi zimekufa, na hivyo tunaweza kufanya chochote tutakacho. Matendo yana umuhimu.)
-
- Pazia
-
- Soma 2 Wakorintho 3:11-14. Paulo anasema kuwa agano la kale linaposomwa, “pazia” linasalia mioyoni mwao. Pazia hilo ni lipi? Linawakinga wasione nini? (Pazia linamzuia mtu asione vizuri. Hoja ya Paulo inaonekana kuwa kwamba licha ya kuwa na Kristo walishindwa kuona umuhimu wa kweli na utimilifu wa agano la kale.)
-
-
- 2 Wakorintho 3:14 inatuambia kwamba pazia huondolewa “katika Kristo” pekee. Unadhani Paulo anamaanisha nini kwa kusema hivi? (Bila Kristo, walishindwa kuona agano la kale lilikuwa linajielekeza wapi. Mtu anapomgeukia Bwana, pazia linaondolewa. Yesu alikuwa mtiifu kikamilifu na kubeba adhabu kwa ajili ya dhambi zetu. Kwa hiyo wokovu wetu upo juu yake, na si kwa kutunza kwetu sheria.)
-
-
- Soma 2 Wakorintho 3:15-18. Nini kinatutokea tunapomtazama Yesu kwa ajili ya wokovu wetu? (Tunabadilishwa. Badala yakuiangalia sheria kama njia ya kupata haki, tunamtazama Yesu, aliyekufa kwa ajili yetu. Tunapomtazama, Roho anatubadilisha na kutufanya tufanane naye.)
- Kiumbe Kipya
-
- Soma 2 Wakorintho 5:14-15. Upendo unawezaje kutudhibiti? Nilidhani upendo ni kinyume cha kulazimisha? (Upendo mkubwa sana aliotuonesha Yesu, upendo unaotuokoa kutoka katika mauti, unabadili mioyo yetu na kutufanya tuamue kuishi kwa ajili ya Yesu.)
-
- Soma 2 Wakorintho 5:17. Je, hii inaonekana kana kwamba tunaenenda kama tulivyokuwa tukitenda siku zote kwa kuwa tumeokolewa kwa imani na si kwa matendo yetu? (Kifungu hiki kinasema kuwa sisi ni “kiumbe kipya.”)
-
- Soma 2 Wakorintho 5:18-19. Ni kwa jinsi gani sisi ni “kimbe kipya?” (Hili “linatokana na Mungu.” Paulo anasema kuwa uumbaji huu mpya unatoka kwa Mungu, anayetupatanisha naye kwa njia ya Kristo. Kama tulivyoona katika 2 Wakorintho 3:18, Roho Mtakatifu anatubadilisha.)
-
-
- Tunayo huduma. Inaitwa “upatanisho.” Tunapatanisha nini? (Bila Kristo, dhambi zetu zinatutenganisha na Mungu. Lakini katika Kristo, Mungu ametenda ili kutupatanisha naye kwa kutohesabu makosa yetu dhidi yetu. Huduma yetu ni kushiriki habari hizo njema na kuwasihi watu wengine wapatanishwe na Mungu.)
-
-
- Soma 2 Wakorintho 5:20-21. Yesu amezifanyia nini dhambi zetu? (Ingawa Yesu hakujua dhambi, Mungu alimfanya “kuwa dhambi” kwa ajili yetu. Yesu alibeba dhambi zetu na kufa kwa ajili yetu.)
-
-
- Kifo cha Yesu kwa ajili yetu kina athari gani kwetu? (Sasa sisi tumekuwa “haki ya Mungu.”)
-
-
-
- Paulo anapotuita “mabalozi,” anaashiria kuwa tunapaswa kufanya nini? (Balozi anaiwakilisha nchi. Sasa sisi ni wawakilishi wa kile ambacho Yesu amewatendea wanadamu ili kutuwezesha kuwa na uzima wa milele!)
-
-
- Soma 2 Wakorintho 7:1. Hili linawezaje kuwa kweli? Ikiwa katika Kristo tumekuwa ‘haki ya Mungu,’ kwa nini bado Paulo anatuambia tuutafute utakatifu? (Kusimama kwetu imara katika Kristo hakuondoi ukuaji katika utakatifu. Paulo anawaambia waumini kujitakasa na “kutimiza” utakatifu. Vivyo hivyo, 1 Yohana 3:2-3 inasema kuwa Kristo atakapokuja tutafanana naye, na kwamba kila mtu ambaye ana hili tumaini anajitakasa sasa hivi.)
-
- Rafiki, tunaokolewa kwa neema, na si kwa sheria iletayo mauti. Kile ambacho Yesu ametutendea kinatutia moyo kuendelea katika njia ya utakatifu. Tunatamani kuwa watakatifu kama Yesu. Je, utamwomba Roho Mtakatifu, sasa hivi, akuongoze katika njia ya utakatifu?
- Juma lijalo: Uwakili na Utume.
