Somo la 11: Uwakili na Utume

(2 Wakorintho 8 & 9)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
3
Lesson Number: 
11

Somo la 11: Uwakili na Utume

 

(2 Wakorintho 8 & 9)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Je, kutoa kwa watu wengine ni suala la hesabu rahisi? Ninakupatia dola tano na hivyo ninakuwa maskini kwa dola tano nawe unakuwa tajiri kwa dola tano. Biblia inafundisha kwamba utoaji hutufanya kuwa matajiri, si maskini. Na unausikia ujumbe huo mara zote kutoka kwa watumishi (wa dini) wanaotaka fedha zako. Usichokisikia mara zote ni kwamba kutoa kwa mtu au shirika kunaweza kusiwafanye kuwa matajiri. Je, zawadi inaweza kuwa kitendo cha kupoteza kabisa? Kanuni hiyo ya kupoteza kabisa pia ipo katika Biblia. Hebu kwa mara nyingine tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

  1.    Yesu na Uwakili

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 8:9. Paulo anatoa hesabu rahisi ya sisi kupata karama ya Yesu. Alikuwa maskini na sisi tukawa matajiri. Je, huu ni ufafanuzi ambao haujakamilika wa uwakili wa Yesu?

 

    1.    Soma Wafilipi 2:7-10. Hii inatuambia kuwa ni yepi yaliyokuwa matokeo ya Yesu kujimaliza? (Mungu alimtukuza sana Yesu na akampa “jina lipitalo kila jina.” Kila goti litapigwa mbele yake.)

 

    1.    Soma Ufunuo 5:11-13. Je, ungependa kuwa na uweza (mamlaka) na utajiri? Kifungu hiki kinasema kuwa Yesu alipokea uweza na utajiri kutokana na kafara/sadaka yake.)

 

      1.    Yesu alikuwa Mungu kamili kabla hajajinyenyekeza na kuwa mwanadamu. Mungu anawezaje kupewa kitu ambacho bado hakimiliki? (Ukipitia kitabu cha Mwanzo, kuanzia kwenye anguko la wanadamu hadi kwenye gharika, unaweza kuona kwamba Mungu alikuwa kwenye pambano dhidi ya Shetani. Maisha, kifo na ufufuo wa Yesu vilimpa ushindi na uweza, utajiri na utukufu wa kidunia.)

 

    1.    Soma Malaki 3:10-12. Mungu alitoa ahadi gani kwa Waisraeli? (Kutoa zaka hukupatia baraka zisizo za kawaida (“madirisha ya mbinguni.”) Si tu kwamba hutakuwa na mahitaji tena, bali Mungu ataibariki kazi yako.)

 

    1.    Soma Mithali 21:20 na Mithali 19:19. Kafara ya Yesu ina manufaa gani kwa wale wanaokataa neema yake? (Kwa kuwa tu unampatia mtu fulani fedha haimaanishi fedha hizo zitambariki. Kwa baadhi ya watu ni sawa na wale wasioweza kudhibiti hasira yao. Ukiwaokoa kutoka kwenye matokeo ya tabia yao mbaya, utatakiwa kufanya hivyo tena.)

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 6:1. Inamaanisha nini kupokea neema ya Mungu “bure?” (Baadhi hawataikubali na hivyo karama ilitolewa bila kuwepo na matokeo mazuri.)

 

  1.   Ukarimu Uliofikiriwa kwa Makini

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 9:7. Je, sadaka zetu za hisani zinapaswa kutolewa kwa uangalifu? (Paulo anasema kuwa utoaji ni suala la uamuzi.)

 

      1.    Paulo anapoandika kwamba sadaka haipaswi kuwa ya kusitasita au kulazimishwa, hiyo inakusaidiaje kuelewa kipengele cha uangalifu? (Uamuzi wetu kutoka moyoni haupaswi kutolewa kwa vitisho. Tunapaswa kutaka kutoa. Tunapaswa kutoa kwa moyo wa ukunjufu.)

 

      1.    Hebu tutafakari tena kuhusu utoaji unaowezesha tabia angamizi au unaunga mkono jambo lisilo na ufanisi. Je, utoaji usio na mpango unaendana na maelekezo ya Paulo kwamba utoaji unapaswa kufanyika kwa uangalifu, kwa hiari, na kwa furaha?

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 9:6. Je, hii ni sehemu ya mambo tunayopaswa kuyatafakari pale tunapotoa? (Kuelezea hii kanuni, kama ilivyo kwa kauli iliyopo katika Malaki 3, kunaonesha kwamba kuzitafakari rasilimali zetu kunapaswa kuwa sehemu ya uamuzi wetu wa kutoa. Ukitaka kupata zaidi, unatakiwa kutoa zaidi.)

 

      1.    Mke wangu anatumia muda mwingi zaidi yangu kutafakari jinsi ya kutoa na nani wa kumtolea. Ninakumbuka kipindi fulani cha kufurahisha sana alipoamua kutoa kwa mtu kiwango cha fedha kisichotarajiwa. Muda mfupi baada ya kitendo hicho tulipokea kiasi cha fedha kisichotarajiwa karibia sawa na kiasi tulichotoa. Kisha akatoa zawadi nyingine mpya, na kwa mara nyingine tulipokea kiasi kipya cha fedha kisichotarajiwa. Sikumbuki mambo haya yaliendelea kwa muda gani, lakini yalileta furaha tulipomtazama Mungu akitenda kazi.

 

      1.    Je, baraka ni fedha pekee? Wanafunzi wa Yesu walionekana kuwa maskini katika kipindi cha kazi yao ya utume. (Ingawa Malaki kwa umahsusi anabainisha baraka zinazohusiana na kazi, ninaamini kwamba baraka ni pana zaidi ya fedha. Kwa baadhi ya watu, fedha nyingi si baraka.)

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 9:11. Hadi kufikia hapa, nilichokuwa ninakichukulia ni kwamba tunajadili utoaji wa fedha. Je, hiyo ndio aina pekee ya thawabu iliyojadiliwa na Paulo? (Paulo anarejelea kuhusu “kujazwa kwa kila namna,” na kuwa “wakarimu kwa kila namna.”)

 

      1.    Njia nyingine ni zipi za kutoa thawabu na kuwa wakarimu? (Kutoa muda wako.)

 

      1.    Je, muda ni fedha kwa maana ya kwamba ukiwapa watu muda, utakuwa na muda mwingi? (Tofauti na fedha, sote tuna kipimo sawa cha muda. Lakini nadhani kanuni ya kuongeza bado inatumika. Miaka mingi iliyopita, nilinunua gari lililokwishatumika na nikatamani sana kubadili kilainishi (oil). Siku iliyofuata washiriki wa kanisa walinitaka nitumie ujuzi wangu wa kutengeneza samani (carpentry) kusaidia ujenzi wa kanisa letu jipya asubuhi. Nikaamua kwenda kanisani. Niliporudi nyumbani na kuchungulia chini ya gari, kifaa cha kilainishi kilikuwa na hali ambayo sijawahi kuiona. Nikasimama pale nisijue niende wapi kununua kifaa kwa ajili ya matengenezo. Mara nikajikuta ninaangalia vifaa vyangu vya ufundi vilivyokuwa kwenye mkanda na mshikio wa nyundo ya kung’olea misumari. Nikaona kifaa kinachoendana kikamilifu na kile cha kuhifadhi kilainishi na nikaweza kubadili kilainishi. Kama nisingefanya kazi ya kanisa, nina uhakika ningetumia saa nyingi kuingia duka moja hadi jingine kujaribu kutafuta kifaa sahihi.)

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 9:12-13. Jambo gani jingine chanya linatokea kama matokeo ya ukarimu wako kwa wengine? (Wale unaowasaidia watamtukuza Mungu kwa karama yako.)

 

      1.    Ninapowashauri vijana wadogo kuhusu mustakabali wa kazi zao, huwa ninapendekeza wachague taaluma ambayo watawasaidia watu wengine. Je, huu ni ushauri mzuri, au ungependekeza taaluma ambayo utajiingizia fedha nyingi? (Kuwasaidia wengine kunaweza kutoa mtazamo endelevu wa lengo na furaha. Fedha pekee ni msingi mbaya wa kuchagua kazi ya maisha.)

 

    1.    Tafakari kipengele kingine cha 2 Wakorintho 9:13. Je, tunapaswa kujali kama wale wanaopokea msaada wetu wanamtukuza Mungu? (Mojawapo ya sadaka zangu kuu huwasaidia wengine na vipengele vinavyosaidia katika kazi ya Yesu. Fadhila (sadaka) nyingine, ambayo sijishughulishi, inawasaidia watu wengine lakini haisemi chochote kuhusu kuhamasishwa na dini.)

 

    1.    Soma 1 Timotheo 5:9. Paulo anamaanisha nini anapoandika kuhusu mjane “kuandikwa?” (Vifungu vilivyotangulia vinarejelea kuwasaidia wajane. Hii ni rejea ya kuwa kwenye orodha ya wajane wanaosaidiwa na kanisa.)

 

    1.    Soma 1 Timotheo 5:9-13. Je, mahitaji ndio kigezo pekee cha kuamua wajane wapi wanapokea msaada wa kanisa? (Hapana. Wale wanaotenda mambo mema wanatakiwa kusaidiwa, na wajane wasiofanya hivyo hawatasaidiwa.)

 

      1.    Je, kanuni aliyoitoa Paulo kwa kanisa la awali inapaswa kutumika katika utoaji wako? Je, inapaswa kuwa sehemu ya utoaji wako unaotokana na uamuzi wa moyo wako?

 

    1.    Soma Mambo ya Walawi 19:9-10, Kumbukumbu la Torati 24:19-21 na 2 Wathesalonike 3:10. Hii inatufundisha nini kuhusu kuwasaidia maskini? (Njia ya Biblia inasema kwamba maskini wawe tayari kufanya kazi. Wasipofanya kazi, hawatashiriki mavuno.)

 

      1.    Je, hii inapaswa kuwa sehemu ya uamuzi wetu wa nani wa kumsaidia? (Tunapaswa pia kutafakari kama maskini hana uwezo wa kufanya kazi.)

 

      1.    Je, vifungu hivi vinatufundisha jambo kuhusu kuchukua uamuzi makini wa kuwasaidia wahitaji?

 

      1.    Je, kumpa fedha mhitaji ni uamuzi bora? (Benki ya Dunia inataarifu kuwa kuanzia mwaka 1990-2025 idadi ya watu walio katika umasikini wa kupindukia imepungua kutoka takriban watu bilioni 2.3 hadi watu milioni 831. Maboresho haya hayakutokana na kuhamisha mali kutoka kwa matajiri kwenda kwa maskini, bali uliondolewa kwa ukuaji thabiti wa uchumi uliotokana na kuruhusu sekta binafsi, biashara na ushindani.)

 

    1.    Rafiki, je, utatafakari juu ya msaada wako kwa wahitaji? Kuwa mkarimu hukubariki. Kuwa na busara kuhusu karama/thawabu yako humbariki maskini. Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu aziongoze karama zako?

 

  1.      Juma lijalo: Kushughulika na Walimu wa Uongo.