Somo la 12: Kushughulika na Walimu wa Uongo

(1 Wakorintho 3, 2 Wakorintho 10-12)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
3
Lesson Number: 
12

Somo la 12: Kushughulika na Walimu wa Uongo

 

(1 Wakorintho 3, 2 Wakorintho 10-12)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Ni nani unayemchukulia kuwa mwalimu wa uongo? Je, ni yule mwenye mafundisho usiyokubaliana nayo? Je, ni yule ambaye mtindo wake wa maisha si ule unaodhani kuwa ni sahihi? Je, ni yule anayetangaza aina ya huduma ya kanisa unayodhani si ya muhimu sana? Nadhani maswali haya ni ya muhimu kwa sababu tafsiri ya Paulo ya mafudisho ya uongo inaonekana kuwa tofauti sana na tafsiri ya mafundisho ya uongo ninayoyasikia leo. Ninasikia walimu wa Biblia wakiitwa “walimu wa uongo” kwa kuwa tu hawakubaliani na mtu anayemuita “mwalimu wa uongo.” Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tutenganishe tofauti kati ya wale tusiokubaliana nao na wale wanaopaswa kuitwa “walimu wa uongo.”

 

  1.    Walimu Wabaya

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 3:10. “Mkuu wa wajenzi mwenye hekima” ni nani? (Paulo anajirejelea.)

 

      1.    Je, Paulo anatarajia kuwa “wajenzi” (walimu) wengine watamfuata katika jaribio la kuwajenga washiriki wa kanisa? (Ndiyo.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 3:11. Kazi ya muhimu sana ya mwalimu anayewajenga Wakristo ni ipi? (Kujenga juu ya Msingi wa Yesu Kristo.)

 

      1.    Unadhani hiyo inamaanisha nin? (Mafundisho yote ya Kikristo lazima yajengwe juu ya Yesu Kristo-kwa jinsi alivyo, kile alichokifanya kwa ajili yetu, na injili yake inayookoa.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 3:12-13. Kuna uzuri gani kujenga kwa dhahabu, fedha, na mawe ya thamani? Kuna ubaya gani kujenga kwa miti, majani, na nyasi? (Moto unakuja, na miti, majani, na nyasi havitastahimili moto.)

 

      1.    Unadhani Paulo anamaanisha nini anaposema “siku ile” italeta moto? (Wanamaoni wengi wanadhani hii inamaanisha ujio wa Yesu Mara ya Pili. Yerusalemu ilikuwa bado haijaangamizwa, hivyo inawezekana hicho ndicho anachokimaanisha Paulo. Inaonekana kwamba tatizo lolote kubwa katika maisha ya Mkristo ni kipimo cha aina ya fundisho ambalo Mkristo amelipokea.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 3:14-15. Nini kinawatokea wale wanaojenga kwa dhahabu, fedha, na mawe ya thamani? Nini kinawatokea wale wanaojenga kwa miti, nyasi, na majani? (Wale wanaojenga kwa kutumia vifaa vizuri wanapata thawabu. Wale wanaojenga kwa kutumia vifaa vibaya “wanapata hasara.”)

 

      1.    Kitu gani kinawatokea wajenzi wabaya? Kitu gani kinawatokea wale waliopokea vifaa dhaifu vya ujenzi? (Mjenzi mbaya “ataokolewa.” Kazi ya wajenzi wabaya haitastahimili moto.)

 

        1.    Unadhani “Kazi ya mtu ikiteketea” inamaanisha nini? Kazi haistahimili, au mwanafunzi haokoki?

 

      1.    Ungewaitaje wale wanaojenga kwa kutumia miti, nyasi, na majani? Je, ungewaita “walimu wa uongo” au ungewaita “walimu wabaya?” (Paulo hawaiti kuwa wa uongo, na ni muhimu kutambua kuwa wanaokolewa. Utakumbuka kwamba wanajenga kwa kutumia vifaa vinavyoteketea kiurahisi juu ya Msingi wa Yesu Kristo.)

 

      1.    Masomo haya yameandikwa kwa ajili ya walimu, lakini nina uhakika wanafunzi wengi wanayasoma. Kuna fundisho gani kwa wanafunzi wanaofundishwa kanuni za Kibiblia? (Ni muhimu sana ukawachagua walimu sahihi.)

 

  1.   Walimu wa Uongo

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 11:2-4. Litafakari hili katika muktadha wa msingi tulioujadili hivi punde. Je, walimu hawa (“yeye ajaye”) wanajenga juu ya msingi wa Yesu Kristo? (Hapana! Wanamtangaza Yesu mwingine, roho tofauti, au injili tofauti.)

 

      1.    Hilo linawezekanaje? Je, kufundisha juu ya Yesu tofauti, Roho tofauti, au injili tofauti itakuwa dhahiri kwa wasikilizaji?

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 11:13-15. Je, udanganyifu uko dhahiri? (Paulo anasema kwamba wanajigeuza kama “watumishi wa haki.” Hii inaashiria kwamba udanganyifu hauko wazi kwa haraka haraka. Hii pia inabainisha kuwa walimu hawa si Wakristo waaminifu ambao wamefikia hitimisho lisilo sahihi kuhusiana na mafundisho ya imani (doctrine).)

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 11:5-6. Ni jambo gani linalowafanya walimu wa uongo waonekane wenye kuvutia au kupendeza kwa nje? (Paulo anaonekana kukiri kwamba walimu hao ni wazungumzaji wazuri katika hadhara kuliko yeye. Hata hivyo, walimu hao hawana maarifa zaidi.)

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 11:7-9. Walimu wa uongo wanafanya jambo gani ambalo Paulo halifanyi? (Wanawalipisha watu kwa kile ambacho Paulo anawapatia bure.)

 

      1.    Je, malipo ya fedha ni kiashiria kikubwa cha mwalimu wa uongo? (Paulo hasemi hivyo. Soma 1 Wakorintho 9:13-14. Anaandika kwamba mwalimu anapaswa kutegemezwa na mwanafunzi na anasema kuwa waumini wa Makedonia “walinipa kadiri ya mahitaji yangu.” Na kwamba “aliwanyang’anya makanisa mengine” ili kuwasaidia wale wa Korintho bure. Kwa uzoefu wangu, ukilipia kitu basi huwa unakithamini. Binti wangu mkubwa alipokuwa akiishi kwangu na nikalipia ankara zote, hakuzima taa zote, hata alipokuwa ameondoka nyumbani. Kwa kuwa sasa anaishi nyumbani kwake, nimegundua uwapo wa giza kila ninapoingia kwake.)

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 10:1-2 na 2 Wakorintho 10:10. Walimu wa uongo wanasema kuwa Paulo amekosea wapi? (Wanakosoa uwapo au mwenendo wake na unenaji wake.)

 

      1.    Je, unagundua tofauti ya muhimu kati ya maoni ya Paulo na yale ya walimu wa uongo? (Walimu wa uongo wanakosoa uwapo wa Paulo na njia anayoitumia. Paulo alikiri kwamba walimu wa uongo walikuwa wahubiri wenye ufasaha na ustadi mkubwa.)

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 10:12. Paulo anaona kasoro gani ya tabia kwa walimu wa uongo? (Wanashindana wao kwa wao.)

 

      1.    Kuna ubaya gani na hilo? Mara zote nimekuwa mshindani. Miongo kadhaa iliyopita, nilikuwa kwenye darasa la kujifunza Biblia lililokuwa na mwalimu mzuri sana. Nilijiuliza ni mambo gani aliyoyafanya ambayo sikuwa nikiyafanya, na yale aliyoyafanya ambayo tayari nilikuwa nikiyafanya. Paulo anasema kuwa washindani “hawana akili.” Ni jambo gani hilo wasilolifahamu?

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 10:15-18. Hili ni jibu la Paulo kwa swali langu la awali. Ni jambo gani hilo ambalo washindani wenye majigambo hawalielewi? (Mungu ndiye anayefanikisha kazi yetu ya utume. Ufundishaji bora bila Roho Mtakatifu kufanyia kazi mioyo hakutimizi chochote.)

 

    1.    Soma Luka 16:8-9. Soma muktadha ikiwa bado hukifahamu kisa hiki. Yesu anasema nini kuhusu wafuasi wake kuwa na “busara” na kutumia “mali isiyo ya haki?” (Mfano huu unanifundisha kwamba ninapaswa kuangalia njia zenye ufanisi mkubwa za kufundisha Biblia. Ikiwa shirika la kilimwengu (secular) linapata wateja wengi, ninapaswa kuangalia linafanya nini ili niweze kuboresha njia ninayoitumia. Ninapomwona mwalimu mzuri mwenye ufanisi, ninapaswa kuona kile ninachoweza kujifunza ili kuwa bora zaidi. Sidhani kama Yesu anatufundisha kuhafifisha injili.)

 

    1.    Kwa kuwa sasa tumetafakari alichokifundisha Paulo kuhusu walimu wabaya na walimu wa uongo, utaelezeaje kwa ufupi tofauti kati ya makundi haya mawili? (Kipimo si, “Je, mtu huyu anakubaliana nami kwa kila jambo?” Bali, ni “Mafundisho ya mtu huyu yanawaelekeza wapi watu kwa kumzingatia Kristo?” Mwalimu wa uongo anabadili mamlaka ya kibinadamu kwa mamlaka ya Kristo, anapotosha injili, na anatumia uongozi wa kiroho kujiendeleza binafsi badala ya kuwaendeleza watu anaotakiwa kuwatumikia.)

 

  1.      Kujivuna

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 11:16-20. Hii ni aina gani ya majivuno? (Huu ni upumbavu wa makusudi na majivuno ya kejeli. Paulo anawakumbusha kuwa wamewavumilia walimu wanaowafanya kuwa watumwa, wanaowararua, wanaonufaika kupitia wao, na hata kuwachapa.)

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 11:21-23. Je, ni sahihi kulinganisha wasifu na walimu wengine? (Paulo anasema kuwa “ananena kama mwendawazimu” anapolinganisha wasifu. Lakini bado anasema hivyo – na nadhani ni muhimu kwake kusema hivyo.)

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 11:24-27. Una maoni gani juu ya kujisifu kwa Paulo? (Paulo anapindua kujivuna kwa walimu wa uongo. Ananukuu mateso yake yote, na si ukuu wake.)

 

      1.    Je, utashawishika kwa njia ya Paulo? (Paulo hajitafutii manufaa binafsi. Hasemi kuwa anavutia. Anasema kuwa Yesu anatosha licha ya udhaifu wake na mateso aliyopitia katika utume.)

 

    1.    Tafakari kidogo kuhusu somo letu la juma lililopita kuhusu uwakili. Juma lililopita tulijifunza kuwa ukarimu wa uaminifu huleta baraka ya Mungu. Hapa Paulo anaonesha kuwa huduma ya utume ya uaminifu inaweza kuhusisha mateso na inaweza isionekane kuwa na mafanikio. Tunapatanishaje kweli hizo? (Baraka ya Mungu si lazima imaanishe faraja ya haraka, usitawi wa haraka, au mafanikio yanayoonekana. Mwalimu mwaminifu anatafuta kutangaza utukufu wa Kristo. Maana halisi ya fundisho la kweli ni kumtangaza Kristo na si mwalimu. Mungu atampa thawabu mwalimu wa kweli, lakini inaweza isiwe sasa hivi.)

 

    1.    Rafiki, je, umejifunza jambo lolote kuhusu walimu wabaya dhidi ya walimu wa uongo? Hebu tuombe ili Roho Mtakatifu atusaidie kuwatathmini walimu kwa usahihi. Na kwamba Roho Mtakatifu alifanye fundisho letu la kweli liwe la uaminifu kwa Kristo na injili yake.)

 

  1.   Juma lijalo: Neema, Upendo, na Ushirika.