Somo la 1: Muumbaji Anena
Somo la 1: Muumbaji Anena
(Mwanzo 3-4, Waebrania 1, Yoeli 2)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.
Utangulizi: UVIKO uliponilazimisha kufundisha madarasa yangu ya sheria kwa njia ya mtandao, nilipoteza sehemu ya muunganiko wangu na wanafunzi. Kwa kuona vichwa vyao kwenye makasha yaliyopo kwenye kioo ilikuwa kitendo chenye taarifa chache kuliko kuwaona mwili mzima wakiwa wamekaa mbele yangu darasani. Adamu na Eva walipotenda dhambi, mazungumzo yao na Mungu yaliyofuatia, ambayo walijaribu kuyaepuka, yalikuwa ya ana kwa ana. Mtoto wao Kaini alipomwua ndugu yake na kuhukumiwa kuwa “mzururaji,” alikuwa na majuto ya kuvutia sana. Katika Mwanzo 4:13-14 alitangaza kwamba adhabu yake ilikuwa “kubwa, haichukuliki.” Na alifafanua kwamba sehemu ya adhabu yake isiyochukulika ni kwamba “nitasitirika mbali na uso wako [Mungu].” Hebu litafakari hilo! Kaini alijutia kupoteza uhusiano wa ana kwa ana na Mungu. Majuto ya Kaini yanaakisi mazingira yetu. Hatuwezi kuwa na uhusiano wa ana kwa ana na Mungu. Licha ya yote hayo bado Mungu anataka kuwasiliana na sisi. Jinsi anavyofanya hivyo ndio mada ya mfululizo wa masomo haya. Hebu tuzame kwenye swali la jinsi Mungu anavyonena nasi!
- Waliojificha
-
- Soma Mwanzo 3:1-3. Mti uliokatazwa uliwekwa wapi? (“Katikati ya bustani.”)
-
- Soma Mwanzo 2:9. Mti wa Uzima uliwekwa wapi? (“Katikati ya bustani.”)
-
-
- Lilikuwa wazo la nani kuweka mti ambao wanadamu walipaswa kula tunda lake ili waishi (angalia Mwanzo 3:22) karibu na mti ambao ungewaua ikiwa wangekula tunda lake?
-
-
-
- Kwa kuwa Mungu ni mwerevu zaidi kuliko sisi, na hakuna miongoni mwetu ambaye angedhani hili lilikuwa wazo jema, hiyo inakuambia nini kuhusu chanzo cha wazo hili? (Nadhani hili lilikuwa shindano lililoandaliwa kati ya Mungu na Shetani ili kuona kama wanadamu wangekuwa waaminifu kwa Mungu. Shetani hakuruhusiwa kuwajaribu wanadamu wapya mara kwa mara. Hili ni jaribu lililokubalika na pande mbili.)
-
-
- Soma Mwanzo 3:4-6. Katika vifungu vitatu tunaweza kuona jinsi wanadamu walivyotumbukizwa dhambini na kwenye mauti ya milele. Soma Mwanzo 3:7-8. Kwa nini Adamu na Eva walijificha ili Mungu asiwaone? Kaini alipotenda dhambi, alitaka aweze kuuona uso wa Mungu!
-
- Soma Mwanzo 3:9-11. Je, unamwamini Adamu anaposema kuwa sababu yake ya kujificha ili Mungu asimwone ni kwamba alikuwa uchi? (Kimsingi, kifungu cha 7 kinatutaarifu kuwa hakuwa uchi. Nadhani Adamu Aliona haya na kuogopa.)
-
-
- Kwa dhahiri, Mungu alijua mahali Adamu na Eva walipokuwapo na kile walichokifanya. Kwa nini Mungu alikuwa anawaita? (Mungu alitaka kuongea nao.)
-
-
- Hatutapitia adhabu iliyotolewa kwa Adamu na Eva au visingizio vyao vya kipuuzi vya kutenda dhambi. Soma Mwanzo 3:22-24. Kwa nini wanafukuzwa kutoka katika Bustani ya Edeni, nyumbani kwao? (Ili wasiweze kula tunda la Mti wa Uzima na kuishi milele.)
-
- Soma Mwanzo 4:9-10. Katika vifungu hivi tunasoma kwamba Mungu ana mjadala wa ana kwa ana na Kaini. Soma Kutoka 33:11 na Kutoka 33:20-23. Una ufafanuzi gani kwamba Mungu anamwambia Musa atakufa ikiwa atauona uso wa Mungu?
-
-
- Baada ya dhambi ya wazazi wake, na baada ya kumwua ndugu yake, Kaini ana kile kinachosomeka kama mazungumzo ya ana kwa ana na Mungu. Tulijadili katika sehemu ya utangulizi kwamba Kaini hakuweza kuhimili kujificha kutoka kwenye uso wa Mungu. Licha ya hayo Musa anaonekana kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na Mungu pale Mungu anaposema kuwa Musa hawezi kuuona uso wake na akaishi. Jambo gani linaendelea hapa? (Hebu tuongezee Mwanzo 18:1-2 kwenye tatizo hili. Inaonekana kwamba Mungu anaufunika utukufu wake ili wanadamu waweze kuishi, lakini wakati huo huo ana mazungumzo ya ndani (intimate) na wanadamu.)
-
-
-
- Unadhani kwa nini wanadamu watakufa ikiwa watauona uso wa Mungu?
-
-
- Soma 1 Timotheo 6:15-16. Hii inaashiria kuwa sababu ni ipi kwamba hatuwezi kumwona Mungu ana kwa ana? (Anakaa katika “nuru isiyoweza kukaribiwa.” Hiyo ni rejea ya utukufu wa Mungu. Sisi ni wanadamu wadhambi, na yeye ni Mungu asiye na dhambi. Mwanadamu mwenye mwili wa kufa hawezi kustahimili utukufu wa Mungu katika ukamilifu wake. Biblia inaporejelea kile kinachoonekana kuwa mazungumzo ya ana kwa ana na Mungu, ni lazima tufikie hitimisho kwamba Mungu amefanya uwepo Wake upatikane kupitia njia fulani. Amefanya uwepo Wake uweze kustahimiliwa na mwanadamu.)
-
-
- Somo hili halihusu utukufu wa Mungu, linahusu kuwasiliana na Mungu. Vifungu tulivyovisoma hivi punde vinatuambia nini kuhusu hamasa za Mungu na wanadamu kuwasiliana? (Mara nyingi wanadamu wanapokasirikiana au kusikitiana, wanakataa kuzungumza. Mungu alikuwa na sababu ya kukasirika kwamba wanadamu walimgeuka na kutenda dhambi. Licha ya hayo, Mungu alitaka kuzungumza na Adamu na Eva. Kaini alidhihirisha jinsi ilivyokuwa na umuhimu kwake, muuaji wa kwanza, kuzungumza na Mungu. Tunahitaji na tunataka kuwa na uwezo wa kuwasiliana na Mungu.)
-
- Mawakala wa Mungu
-
- Soma Waebrania 1:1-2. Hebu tutumie muda kidogo kwenye hivi vifungu. Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anaposema kuwa Mungu alisema nasi “kwa njia nyingi” kupitia kwa manabii, tunaweza kukumbuka njia zipi? (Njia mojawapo ambayo Mungu alisema na watu ilikuwa kupitia vitabu vya Agano la Kale. Tunakumbuka kwamba wakati mwingine aliwatumia manabii maono, njozi na matendo ya kiishara.)
-
-
- Kabla hatujaingia kwenye mjadala wa wajibu wa Mungu, ngoja nikuulize kwa nini Mungu alisema kupitia kwa manabii? Kwa nini asizungumze na kila mmoja wetu binafsi, kupitia uwepo Wake uliowezeshwa kwa njia ya upatanishi? Kwa nini asizungumze na kila mmoja wetu binafsi kupitia kwa malaika? (Kama umesoma Agano la Kale, utafahamu kwamba Mungu alinena kupitia wale waliokuwa na uhusiano wa pekee na Yeye. Mara idadi ya wanadamu ilipoongezeka kwa uchache, Mungu ananena kupitia kwa watu aliowateua.)
-
-
- Angalia tena Waebrania 1:2. Katika siku za mwisho Mungu alisema nasi kupitia kwa Yesu. Je, hili ndilo jibu kwa swali langu la awali kuhusu kwa nini Mungu hakusema nasi binafsi, hata kupitia uwepo Wake uliowezeshwa? (Kwa dhahiri Yesu ni “uwepo wa Mungu unaowezeshwa kupitia njia ya upatanishi.” Katika kufanyika mwanadamu, Mungu alijidhihirisha kwetu kwa njia ambayo wanadamu waliweza kuona na kusikia. Kusoma masimulizi ya maisha Yake hutupatia ufahamu bora zaidi kuhusu asili na mapenzi ya Mungu.)
-
- Soma Waebrania 1:3. Jambo gani kuhusu Yesu linamfanya kuwa mwasilishaji bora zaidi wa mapenzi ya Mungu kuliko manabii?
-
- Soma Hesabu 12:6-8. Hii inaongezea nini kwenye swali la kwa nini Mungu anawatumia manabii tofauti na kuzungumza na watu wote? (Pendekezo lenye nguvu hapa ni kwamba wengi hawastahili kuwa manabii, na kuongeleshwa na Mungu moja kwa moja ni jambo la nadra sana.)
- Roho Mtakatifu
-
- Soma Yohana 16:7. Tulipoangalia Waebrania sura ya 1 ujumbe ulikuwa ni kwamba Mungu alisema kupitia kwa manabii, kisha akapandisha hadhi namna yake ya kuwasiliana kwa kumtuma Yesu. Kifungu hiki kinaonekana kusema kuwa manufaa mapya katika njia ya Mungu ya kuwasiliana inakuja. Je, hivyo ndivyo unavyokielewa kifungu hiki? Unaelewa kuwa huyu mjumbe anayefuata ni nani? (Yesu anasema kwamba anapoondoka Roho Mtakatifu atakuja – na hilo linatupatia faida.)
-
- Soma Yohana 16:8-13. Roho Mtakatifu ana wajibu gani katika kuwasilisha mapenzi ya Mungu? (Kifungu cha 12 kinatuambia kuwa Roho Mtakatifu atafundisha mambo ambayo Yesu hakuweza kuyafundisha kwa sababu muda wa kufanya hivyo haukuwa sahihi.)
-
- Utabiri wa Yesu wa Roho Mtakatifu kuja kwa uwezo ulitimizwa katika kitabu cha Matendo ya Mitume 2. Je, sasa tumefikia kile kinachoonekana kuwa njia sahihi ya mawasiliano – kwamba Mungu anazungumza na kila mmoja wetu moja kwa moja? (Ni kama vile tumerudi pale tulipoanzia.)
-
-
- Katika aya hizi, tumeona mwelekeo wa jinsi Mungu anavyowasiliana na wanadamu. Kwanza, yalikuwa ni mawasiliano ya ana kwa ana. Kisha yakawa kupitia kwa manabii. Halafu yakawa kupitia kwa Yesu. Sasa yanafanyika kupitia kwa Roho Mtakatifu. Je, ujio wa Roho Mtakatifu umetangua sababu ya Mungu kuwasiliana kupitia kwa manabii? (Jambo moja la kuzingatia hapa ni kwamba Roho Mtakatifu alikuwa akifanya kazi katika Agano la Kale. Matendo 2 ilileta kiwango kipya kabisa cha ushiriki wa Roho Mtakatifu.)
-
-
-
-
- Kama umejibu, “hapana,” kwenye swali la endapo Roho Mtakatifu anatangua mwendelezo wa sababu za manabii, hebu niambie, kwa nini umefikia hitimisho hilo?
-
-
-
- Soma Yoeli 2:28-31. Hii inatufundisha nini kuhusu uhusiano kati ya Roho Mtakatifu na manabii kabla ya mwisho? (Suala la manabii dhidi ya Roho Mtakatifu si suala la ama au. Roho Mtakatifu anawezesha kazi ya manabii.)
-
- Angalia tena Yoeli 2:28-30. Je, hii inaonekana kama Mungu anawatumia wale watu hadimu katika Agano la Kale kuwasiliana na wanadamu? (Mantiki ya hili ni kwamba watu wa namna zote, kutoka katika sekta zote za maisha, wanatabiri. Vijana wadogo wake kwa waume, watumishi wa kiume na wa kike, si kundi la kawaida ambalo kupitia kwao Mungu alizungumza katika Agano la Kale.)
-
-
- Unadhani kwa nini Mungu anafanya mabadiliko haya? (Inaendana zaidi na ukweli kwamba kila mmoja wetu anaweza kumpata Roho Mtakatifu.)
-
-
-
- Tunapaswa kujibuje ujumbe kutoka kwenye kundi hili “la wenye mwili” ambalo sasa linatabiri? Je, tunapaswa kuwajaribu dhidi ya kile Mungu alichowaambia manabii wa Agano la Kale? Je, tunapaswa kuwajaribu dhidi ya kile ambacho Roho Mtakatifu anatuambia? (Soma 1 Yohana 4:1. Kifungu kinasema kuwa tunapaswa kuwajaribu. Biblia inatupatia kiwango cha kipimo.)
-
-
-
- Soma 1 Wathesalonike 5:19-21. Je, tunatakiwa kukataa madai ya kisasa ya unabii kwa kuwa tu ni madai ya unabii? Je, tunatakiwa kuyakubali kwa kuwa tu mtu fulani anasema Roho Mtakatifu ndiye ametoa ujumbe? (“Hapana” kwa yote mawili. Paulo anatuambia tusiutweze unabii, lakini pia anatuambia “tujaribu mambo yote.”)
-
-
- Rafiki, maswali haya ya mwisho yanatuingiza kwenye uchunguzi wa mawasiliano ya Mungu na sisi ambao tunaishi katika siku za mwisho. Mungu ametuonesha nia ya kina ya kuwasiliana na sisi. Je, utaufungua moyo wako kupokea ujumbe wake?
- Juma lijalo: Wito wa Nabii.
