Somo la 2: Wito wa Nabii

(Mwanzo 12, 1 Wafalme 18, Isaya 6, Danieli 2, Marko 1)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
4
Lesson Number: 
2

Somo la 2: Wito wa Nabii

 

(Mwanzo 12, 1 Wafalme 18, Isaya 6, Danieli 2, Marko 1)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Kama ningekuomba unipe majina ya baadhi ya manabii muhimu, ungewakumbuka manabii gani? Danieli angekuwa wa kwanza kunijia akilini. Nani mwingine? Je, unamkumbuka nabii yeyote kutoka katika Agano Jipya? Juma hili tutawaangalia kwa haraka haraka manabii watano mashuhuri: Ibrahimu, Eliya, Isaya, Danieli, na Yohana Mbatizaji. Je, inaonekana kuwa jambo la ajabu kwako kuwaita Ibrahimu na Yohana manabii? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

  1.    Ibrahimu

 

    1.    Soma Mwanzo 12:1. Fikiria kwamba Mungu anakuja kwako na amri hii. Kwa haraka haraka ungefikiria nini? Je, ungetii bila kuuliza swali? (Abramu anaambiwa kuondoka na kuacha kila kitu anachokijua – nchi yake, marafiki wake, na familia. Na haambiwi anakokwenda.)

 

    1.    Soma Mwanzo 12:2-3. Mbali na Mungu kumwomba Abramu aondoke, Mungu anampa hamasa gani? (Kwamba atamfanya kuwa maarufu. Atakuwa “taifa kubwa” na atabarikiwa. Mungu pia anasema jambo linaloonekana kuwa na utata: “na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”)

 

    1.    Soma Mwanzo 12:4-5. Utaona kwamba Abramu ana umri wa miaka 75 anapoambiwa kuondoka. Je, kimsingi Abramu anaondoka na kuwaacha watu wote? (Hapana. Anaondoka na mkewe pamoja na mpwa wake.)

 

      1.    Tunasoma kwamba Abramu pia aliwachukua “watu waliowapata huko Harani.” Je, hawa ni watumwa? Je, walikuwa waongofu? Je, ni watumishi wanaolipwa? (Kifungu hakituambii ikiwa waliingia katika utumishi wake kwa hiari, kwa njia ya deni, kwa kuzaliwa, kwa kununuliwa, au kwa mchanganyiko wa njia hizo.)

 

    1.    Soma Mwanzo 17:4-7. Sasa ahadi ya Mungu inapanuka kutoka kwa Ibrahimu kuwa baba wa taifa kubwa, na kuwa baba wa “mataifa.” Mungu anachukua hatua gani kuelekea kwa Ibrahimu kuwa na uzao wote huu – hata kama kwa sasa ana umri wa miaka 99 na hana mtoto kupitia Sara? (Mungu anabadili jina lake kutoka Abramu kuwa Ibrahimu.)

 

      1.    Kama ungekuwa Abramu, ungejisikiaje kuhusu mabadiliko haya ya jina?

 

    1.    Soma Mwanzo 22:1-2. Mungu anamuita Isaka “mwana wa pekee” wa Ibrahimu. Lakini je, Ibrahimu hakuwa pia na mwana mwingine aitwaye Ishmaeli? Kwa nini kumuita Isaka mwanaye wa pekee? (Isaka ni mwana wa pekee wa Ibrahimu aliyeahidiwa, mwana ambaye kupitia kwake Mungu alisema agano lingeendelea.)

 

      1.    Mungu anamwambia Ibrahimu afanye nini na mwanawe wa pekee, mwana ambaye atamfanya Ibrahimu kuwa baba wa mataifa? (Kumtolea “sadaka ya kuteketeza.”)

 

        1.    Ungeitikiaje amri hii?

 

    1.    Soma Mwanzo 22:10-13. Je, Ibrahimu anatii? Je, Mungu alimwepusha kumpoteza mwanawe? (Ibrahimu anatii. Lakini Mungu anamwepusha dhidi ya kumpoteza mwanawe.)

 

    1.    Soma Mwanzo 20:7. Je, kimsingi Biblia inamuita Ibrahimu nabii? (Ndiyo.)

 

      1.    Ni kwa jinsi gani kafara ya Isaka pia inafanya uzoefu wa Ibrahimu kuwa wa kinabii? (Inaonesha mapema, karne nyingi kabla, utayari wa Baba kumtoa Mwanawe.)

 

      1.    Unaichukuliaje kafara ya Mungu Baba na Mwanawe kwa ajili yako? Je, unaweza kutilia shaka upendo wa Mungu kwako? (Maelezo haya yanafanya ukubwa wa zawadi ya Mungu kuwa jambo la kibinafsi sana kwa kila mzazi. Huu ni unabii ulioonyeshwa kivitendo.)

 

  1.   Eliya

 

    1.    Soma 1 Wafalme 18:17. Kwa nini Mfalme Ahabu anamuita Eliya mtaabishaji? (Soma 1 Wafalme 17:1. Eliya alimwambia Mfalme Ahabu kuwa patakuwepo na ukame hadi Mungu atakaposema vinginevyo. Ukame huu ndio taabu ambayo Mfalme Ahabu alikuwa anaurejelea.)

 

    1.    Soma 1 Wafalme 18:18. Sababu ya ukame ni ipi? (Watu wa Mungu hawamtii Yeye, badala yake wanamfuata Baali.)

 

    1.    Soma 1 Wafalme 18:19. Eliya anamwamrisha Mfalme Ahabu? (Hii inaonesha mfalme alikuwa amefikia hali ya kukata tamaa (desperate).)

 

    1.    Soma 1 Wafalme 18:21 na 1 Wafalme 18:23-24. Eliya anapendekeza jambo gani? (Onesho kati ya uwezo wa Baali na uwezo wa Mungu. Anataka watu waone nani ni Mungu wa kweli na kisha wamchague Mungu.)

 

    1.    Soma 1 Wafalme 18:25-28. Mambo yanaiendeaje timu ya Baali?

 

    1.    Soma 1 Wafalme 18:30 na 1 Wafalme 18:37-39. Mambo yanamwendeaje Eliya na Mungu?

 

    1.    Soma Malaki 4:5-6. Unauelewaje unabii huu? (Soma Luka 1:17. Huu unamwelekea Yohana Mbatizaji akitimiza unabii huu.)

 

      1.    Ninasumbuliwa na maneno “siku ile iliyo kuu na kuogofya.” Hii inaonekana kama ujio wa Yesu Mara ya Pili. Je, unabii huu utakuwa na matumizi ya aina mbili?

 

  1.      Isaya

 

    1.    Soma Isaya 6:1-3. Isaya anaandika kile alichokiona. Kama ungemwona Mfalme yule yule, ungekuwa na mwitiko gani? Ungekuwa na mawazo gani?

 

    1.    Soma Isaya 6:5. Je, ungesema kuwa “umepotea,” au ungedai kuwa wewe ni wa pekee sana kiasi cha kuwa na maono haya ya Mungu?

 

      1.    Mwitiko wa Isaya unatuambia nini kumhusu? (Ni aina ya mtu mnyenyekevu ambaye Mungu anaweza kumtumia.)

 

    1.    Soma Isaya 6:6-7. Hii ni teolojia sumbufu. Ikiwa upatanisho wa dhambi unahitaji tu kaa la moto na malaika, Yesu angejiokolea muda na kujiepusha na matatizo. Unalielewaje hili?

 

      1.    Kaa hili la moto lilitoka wapi? (Kutoka madhabahuni. Malaika hasemi ni madhabahu ipi, lakini chanzo kimojawapo kinaweza kuwa madhabahu iwakayo moto daima katika ua wa makuhani. Angalia Mambo ya Walawi 6:12-13. Huenda pia ulitoka katika madhabahu ya mbinguni.)

 

    1.    Soma Warumi 3:23-26. Dhambi zilishughulikiwaje kabla Yesu hajafa msalabani? (Kafara ya Yesu haifanyi kazi kwa wakati ujao tu, bali pia kwa kurudi nyuma. Hii inaonesha kuwa upatanisho wa Isaya haukutoka kwa kaa la moto na malaika, bali kutoka kwa kile atakachokifanya Yesu katika siku zijazo.)

 

      1.    Je, hii inafanana na Ibrahimu, kwamba mazungumzo yake na Mungu yanatupatia mtazamo wa wakati ujao?

 

    1.    Soma Isaya 53:3-5. Je, Isaya alikuwa zaidi ya mtu ambaye hali ya maisha yake ilitabiri mambo yajayo? (Naam, hakika. Kifungu hiki ni utabiri sahihi wa kile ambacho Yesu atamtendea Isaya na mwanadamu mwingine yeyote yule anayeipokea kafara ya Yesu.)

 

  1.   Danieli

 

    1.    Soma Danieli 2:3-5. Je, hii ni ratiba ya siku ya kawaida kazini kwa Wakaldayo? (Natumai hapana. Vinginevyo hakuna ambaye angekaa kwa muda mrefu kwenye hiyo nafasi.)

 

    1.    Soma Danieli 2:29-30. Nani anawaokoa Wakaldayo na Danieli? (Mungu. “Yeye afunuaye siri” alimpa mfalme ndoto na alimpa Danieli tafsiri ya ndoto.)

 

    1.    Soma Danieli 2:31-35. Kama ungeota hii ndoto, ungebashiri kuwa inamaanisha kitu gani?

 

    1.    Soma Danieli 2:36-38. Kama ungekuwa Danieli, je, ungefurahia kutoa tafsiri hii kwa mfalme? (Hadi kufikia hapa hizi ni habari njema kwa mfalme. Mfalme ndiye kichwa cha dhahabu anayetawala juu ya wote.)

 

    1.    Soma Danieli 2:39-40. Unadhani mfalme atakuwa na mwitiko gani kwenye sehemu hii ya ndoto yake? (Uzuri wa habari unaendelea kupungua. Babeli haitasalia milele.)

 

    1.    Soma Danieli 2:41-43. Kuna jambo gani la muhimu katika unabii huu? (Mambo kadhaa. Kwanza, Danieli anatumiwa na Mungu kufunua mustakabali wa falme za dunia. Pili, hii inatuthibitishia kuwa Mungu anajua mambo yajayo kwa sababu tunaishi katika kipindi cha “kidole” cha historia. Tatu, tunajifunza kwamba hakuna taifa moja litakaloitawala dunia katika kipindi chetu.)

 

    1.    Soma Danieli 2:44-45. Mustakabali ni upi? (Falme zote za dunia zitaangamizwa na Mungu ataweka ufalme “utakaosimama milele.”)

 

      1.    Je, huu ni unabii wa muhimu sana wa Biblia?

 

  1.    Yohana Mbatizaji

 

    1.    Soma Marko 1:2-4. Nani aliyetabiri ujio wa Yohana Mbatizaji? (Isaya.)

 

    1.    Soma Yohana 1:28-30. Yohana anatoa madai gani makubwa mno kumhusu Yesu? (Yesu ni Mwana-kondoo wa Mungu ambaye atazichukua dhambi za ulimwengu.)

 

      1.    Hiyo inatuambia nini kuhusu uelewa wa Yohana juu ya utume wa Yesu? (Yohana anaelewa kuwa Yesu amekuja kushughulika na dhambi ya wanadamu.)

 

    1.    Soma Mathayo 11:7-9. Nani anayemuita Yohana nabii?

 

  1.   Jambo la Pamoja/Linalofanana

 

    1.    Unapowatafakari hawa manabii watano, jambo gani la pamoja linawaunganisha wote? (Wote kwa njia tofauti tofauti wanatuambia kuhusu ujio wa Yesu. Yesu atafanya jambo lisilofikirika kwa kujitoa mwenyewe kwenye mateso na kifo, atatuokoa kutoka katika dhambi zetu, na atatawala kwa ushindi milele!)

 

    1.    Rafiki, ikiwa huamini kwamba Biblia ni ya kuaminika, unawezaje kuwaelezea manabii hawa, kutoka katika nyakati tofauti, wakitabiri kuja kwa Yesu? Kwa nini usifanye uamuzi, sasa hivi, kuwa mwamini wa Biblia na mfuasi wa Yesu?

 

  1.      Juma lijalo: Manabii wa Agano la Kale.