Somo la 3: Manabii wa Agano la Kale
Somo la 3: Manabii wa Agano la Kale
(Yakobo 5, 1 Wafalme 22, 2 Wafalme 22, Yeremia 14)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.
Utangulizi: Je, manabii wa Agano la Kale wanatofautiana na manabii wa Agano Jipya, au tofauti na manabii walioishi baada ya Biblia kukamilika? Mantiki inaashiria kuwa wanatofautiana. Wakati chanzo pekee cha taarifa kutoka kwa Mungu kwenye mada kilikuwa ni nabii (kama ilivyo kwa sehemu ya Agano la Kale), ilikuwa muhimu kwa nabii kuleta ujumbe wa kweli. Lakini Biblia ilivyokamilika, wafuasi wa Mungu walikuwa na msingi wa kuaminika wa kupima kama mtu anayedai kuwa nabii alikuwa ananena kuendana na namna Mungu alienenda katika siku za nyuma. Hili si tu jambo la kutumia mantiki. Yoeli 2 inaonekana kuwaelezea manabii wengi wa siku za mwisho, jambo linaloashiria kwamba manabii wachache wa Agano Jipya walikuwa na wajibu mkubwa wa kuelezea kwa usahihi mapenzi ya Mungu. Hebu turukie kwenye somo letu la manabii wa Agano la Kale!
I. Manabii wa Agano la Kale Kama Sisi?
A. Soma Yakobo 5:15-16. Je, unapaswa kutubu dhambi zako kwa kuhani ili usamehewe? Vipi kuhusu kuungama kwa mtu mwingine ambaye unamwamini? (Kifungu cha 16 kinazungumzia kuungama dhambi kwa mtu mwingine.)
B. Soma Zaburi 51:1-4. Daudi anasema kuwa tunatenda dhambi dhidi ya nani? (Dhambi zetu zi kinyume na Mungu “peke yake.” Mungu ndiye anayesamehe dhambi. Hiyo inamaanisha kwamba kuungama dhambi kwa mtu mwingine hakuna matokeo ya msamaha.)
1. Je, hilo linaonekana kuwa jambo sahihi kwako? Daudi amezini na Bathsheba na akafanya mpango wa mumewe, Uria, auawe kwenye mapambano. Wengine wanaweza kusema kwa usahihi kuwa Daudi amewatenda dhambi? (Panaweza kuwapo waathirika wa dhambi zetu, lakini dhambi yenyewe ni dhidi ya Mungu. Mungu pekee ndiye anayeweza kutusamehe.)
a. Soma Hesabu 5:6-7. Panapokuwepo waathirika wa dhambi yetu, tunatakiwa kufanya nini? (Tunatakiwa kutoa fidia. Kwa Daudi hapakuwepo na fidia halisi tofauti na kumtunza Bathsheba.)
b. Hivyo hapa Yakobo anazungumzia nini anapoandika kwamba tunapaswa kutubu dhambi zetu kwa wanadamu wenzetu? (Kuna uwezekano Yakobo anatuambia kwamba tukiwaambia watu wengine changamoto zetu, wanaweza kutuombea.)
C. Soma Yakobo 5:17-18. Eliya anahusikaje na mjadala wa Yakobo kuhusu kushirikishana changamoto zetu na Wakristo wenzetu? (Rejea ya ghafla ya Yakobo kwa Eliya inaonekana kuwa ya kushtukiza hadi unapotambua kwamba Yakobo anazungumzia kuhusu uwezo wa Mkristo mwingine kukuombea. Uzoefu wa Eliya wa maombi unaonesha uwezo kamili wa maombi. Moto ulishuka kutoka mbinguni Eliya alipoomba. Aliomba na mvua haikunyesha kwa muda wa miaka mitatu. Aliomba tena na mvua ikanyesha!)
D. Angalia tena Yakobo 5:17. Anaandika kuwa Eliya alikuwa “mwanadamu mwenye tabia moja na sisi.” Yakobo anasema nini kuhusu maombi yetu? (Yakobo anasema kwamba sisi tunafanana na Eliya. Sisi pia tunaweza kupata majibu makubwa kwa maombi yetu.)
E. Soma Yakobo 5:19-20. Yakobo anaashiria kwamba moja ya shabaha ya maombi yako inapaswa kuwa ipi? (Kuwalenga wale walioiacha imani.)
F. Soma 1 Wafalme 19:2-4. Baada ya Eliya kuwashinda manabii 450 wa Baali, na kuita moto kutoka mbinguni ili kuthibitisha Mungu ndiye alikuwa Mungu pekee, sasa Eliya anaogopa, anakimbia, na anatamani kufa. Unadhani kwa nini hali hiyo imeandikwa kwenye Biblia? (Hiki ndicho anachokimaanisha Yakobo. Kwa namna nyingi Eliya alikuwa mtu wa kawaida aliyekuwa anatenda mambo makubwa kupita kiasi kwa Mungu kwa njia ya maombi. Unaweza kutenda mambo makuu kwa ajili ya Mungu kama ilivyokuwa kwa nabii Eliya wa Agano la Kale.)
II. Mikaya Nabii wa Kweli
A. Soma 1 Wafalme 22:2-5. Uhusiano kati ya manabii wa Yuda na Israeli ukoje katika kipindi hiki? (Ni marafiki. Ni washirika.)
1. Nani anayeonekana kuwa wa kiroho zaidi? (Yehoshafati. Anataka maelekezo ya Mungu kwa ajili ya mpango wowote wa kivita.)
B. Soma 1 Wafalme 22:6-7. Yehoshafati anataka nini cha ziada? Ana sauti 400 za kinabii zikisema kwamba Mungu atawapa ushindi. (Kwa dhahiri Yehoshafati ana mashaka. Ukweli wa Mungu si jambo la idadi. Hivi karibuni, nimekuwa nikiwasikia wanenaji wakisema kuwa wananena kwa “sauti ya kinabii,” na nina uhakika hawaneni kwa ajili ya Mungu.)
C. Soma 1 Wafalme 22:8-9. Ahabu ndiye Mfalme wa Israeli. Kwa nini Ahabu hamtaji Mikaya kwa Yehoshafati? (Anamchukia kwa sababu kamwe Mikaya hasemi chochote kizuri kumhusu Ahabu.)
D. Ahabu anamtuma mtu akamlete Mikaya. Soma 1 Wafalme 22:13-14. Vifungu hivi vinasema nini kuhusu tabia ya Mikaya?
E. Soma 1 Wafalme 22:15. Je, tumejifunza kwamba Mikaya hakuwa na tabia njema kiasi hicho? Je, amebadili mawazo kuhusu kuendelea kuwa mtu pekee anayepinga maoni ya wengine?
F. Soma 1 Wafalme 22:16-18. Utalielezeaje jambo hili? Ahabu hataki kumsikiliza Mikaya kwa sababu mara zote anasema mambo ambayo Ahabu hataki kuyasikia. Lakini sasa ahabu anamsihi Mikaya “aseme ukweli?” (Mikaya hayachukulii mambo kwa uzito. Sidhani kama Mikaya aliamua kuacha kushikilia kanuni zake. Ahabu pia hachukulii kwa uzito anaposema kuwa amekuwa akimwambia Mikaya aseme ukweli. Ahabu hakutaka kusikia kutoka kwa Mikaya.)
G. Soma 1 Wafalme 22:19-22. Mikaya anakanushaje kauli ya Mfalme kwamba mara zote anasema mambo mabaya kumhusu Mfalme? (Mikaya anasema ushauri wake utamwokoa Ahabu.)
1. Kama Mungu anataka Ahabu afe, kwa nini Mikaya anamuonya? (Huenda hii inatuonesha kuwa unabii unaohusiana na hukumu pia unaweza kuwa onyo. Sasa Ahabu anajua kwa uhakika nini kitatokea ikiwa ataendelea. Kifo chake hakisababishwi na kutoyajua mapenzi ya Mungu, bali kwa uamuzi wake wa kuyapuuzia.)
H. Soma 1 Wafalme 22:26-28. Ikiwa Mikaya anasema ukweli kuhusu mapenzi ya Mungu, basi atapata mateso gerezani kwa mustakabali unaoonekana! Kwa nini Ahabu anaamrisha hivyo? (Ama anakaidi au anadhani kuwa Mikaya ana uwezo wa kubadili mustakabali wa Ahabu.)
I. Soma 1 Wafalme 22:34-35. Ahabu anafariki, kama ambavyo Mikaya alitabiri. Hii inatupa mafunzo gani kuhusu manabii wa kweli wa Agano la Kale? (Wanaweza wasiwe maarufu. Wanaweza kupata mateso kutokana na unabii wao wa kweli. Hata hivyo, wananena kwa ajili ya Mungu!)
III. Hulda Nabii Mke
A. Soma 2 Wafalme 22:3-5. Yosia anawazia mradi gani akilini mwake? (Anafanya uamuzi, angali akiwa kijana, kukarabati hekalu la Mungu Yerusalemu.)
B. Soma 2 Wafalme 22:8-10. Wakati akikarabati hekalu, kitu gani kimeonekana? (“Kitabu cha Torati.” Kuna mabishano juu ya kile kilichoonekana, lakini inaweza kuwa Vitabu vyote Vitano vya Musa, yaani, vitabu vitano vya kwanza vya Agano la Kale.)
C. Soma 2 Wafalme 22:11-13. Ni jambo gani jema kwamba walikipata Kitabu cha Torati? (Mfalme Yosia aligundua kwamba walikuwa wanakiuka mapenzi ya Mungu na kwamba Kitabu cha Torati kinatabiri mambo mabaya kwa wale ambao hawakuwa watiifu.)
D. Soma 2 Wafalme 22:14. Hulda ni nabii mwanamke. Hii inaibua suala la nabii kuwa chanzo pekee cha taarifa kutoka kwa Mungu wakati hakuna vifungu vilivyoandikwa. Kwa nini watu wamemwacha kabisa Mungu – kwa kuwa Kitabu cha Torati kimepotea – na nabii mke hajasema chochote? Kwa hakika ukweli unamshangaza Mfalme Yosia. The Bible Knowledge Commentary inasema kuwa manabii maarufu akina Yeremia, Sefania, na huenda Nahumu pia waliishi katika kipindi hiki.)
E. Soma 2 Wafalme 22:15-17. Je, watu walihitaji Kitabu cha Torati au nabii ili kufahamu kuwa hawapaswi kutoa kafara kwa miungu mingine? (Ukweli kwamba Kitabu cha Torati kimepotea ni kutokana na uzembe wa watu wa Mungu. Kukosa kwao heshima kwa Kitabu cha Torati yumkini kunaakisi kukosa kwao heshima kwa manabii wa Mungu.)
F. Soma 2 Wafalme 22:18-20. Mfalme Yosia atatendewaje kwa sababu ana hamu sana ya kumtii Mungu? (Hatapitia uzoefu wa uangamivu unaokuja.)
IV. Yeremia na Manabii wa Uongo
A. Soma Yeremia 14:13-14. Yeremia anamwambia Mungu kuhusu manabii wa uongo. Mungu anawaelezeaje manabii wa uongo? (Anasema kuwa wanasema uongo.)
B. Angalia tena kifungu cha 14. Unadhani “unabii wa maono ya uongo” inamaanisha nini? (Manabii wa uongo wanasema uongo, lakini wanaweza kuwa wamejidanganya wenyewe pia.)
C. Rafiki, haikuwa rahisi kuwa nabii wa Agano la Kale. Walikuwa na udhaifu kama sisi, lakini kwa uwezo wa Mungu waliweza kufanya mambo makubwa. Je, utaomba kwamba Mungu akuruhusu kutenda mambo makubwa kwa uwezo wake?
V. Juma lijalo: Manabii wa Agano Jipya.
