Somo la 5: Ufunuo na Uvuvio
Somo la 5: Ufunuo na Uvuvio
(Warumi 1, Ufunuo 1, 1 Yohana 1, Hesabu 12)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.
Utangulizi: Fikiria kuhusu kipindi unakua. Familia yako ilikuwa na mtazamo wa jumla wa mambo yaliyokuwa sahihi na mambo ambayo hayakuwa sahihi. Kwa kawaida wazazi wako walifanya mambo kuendana na huu mtazamo wa jumla. Wakati huo huo, wazazi wako walikupatia ushauri mahsusi na maelekezo ya jinsi ya kukabiliana na mazingira tofauti tofauti. Kuyatafakari haya hutupatia mwanga wa jinsi Mungu alivyoyafunua mapenzi yake kwetu. Tuna ufunuo wa jumla wa Mungu kwa kuangalia ulimwengu unaotuzunguka. Lakini Mungu haachi mambo yawe kwa ujumla, alinena kupitia kwa manabii ili kutupatia ushauri katika mazingira mahsusi. Hebu tuzame kwenye Biblia na tujifunze zaidi kuhusu ufunuo wa jumla na ufunuo maalumu!
- Ufunuo wa Jumla
-
- Soma Zaburi 19:1-4. Wanadamu wangapi wanasikia na kuuona utukufu wa Mungu? (Kila mmoja. Mfalme Daudi anayaita “mahubiri” yanayofikisha “maarifa” kuhusu Mungu.)
-
- Soma Warumi 1:18-19. Paulo Mtume anatuambia kuwa kila mtu ambaye si mcha Mungu na asiye na haki hana kisingizio cha kuwa na tabia mbaya. Kwa nini? (Mungu na mpango wake u “dhahiri ndani yao.”)
-
- Soma Warumi 1:20. Ni kwa jinsi gani Mungu na matakwa yake “vi dhahiri ndani yao?” (Katika vitu vilivyoumbwa. Paulo anaandika kwamba uumbaji unatuamnbia angalao kwa kiwango cha chini kuwa tunahitaji kufahamu ili kumpendeza Mungu.)
-
-
- Hilo linawezekanaje? Kwa mfano, ninaamini kuwa kuyadai maisha, kifo, na kafara ya Yesu kwa ajili uetu ndio njia pekee ya wokovu. Uumbaji tunaoweza kuuona unayafunuaje hayo?
-
-
-
- Katika hubiri lake la hivi karibuni kabisa mchungaji wa kanisa langu mahalia alisema, endapo nilimwelewa barabara, kwamba anaamini baadhi ya wasio Wakristo watakuwepo mbinguni. Hili linawezaje kuwa kweli ikiwa Yesu ndiye njia pekee ya kwenda mbinguni?
-
-
- Soma Yohana 14:6 na Matendo 4:12. Vifungu hivi vinaashiria nini kuhusu jinsi mtu anavyookolewa? (Vinaunga mkono mtazamo wangu kwamba Yesu ndiye njia pekee ya kuufikia wokovu.)
-
-
- Kauli hizi mbili za Yesu na Petro ni mifano ya wokovu maalumu. Je, ufunuo wa jumla utarekebisha/utabadilisha (modify) hili?
-
-
-
- Warumi 1:20-21 inatuambia kuwa “asili ya Uungu” wa Mungu i dhahiri tangu uumbaji na hilo linapaswa kuwafanya wanadamu “wamtukuze Yeye kama Mungu.” Una maoni gani juu ya mtu ambaye hajawahi kumsikia Yesu, lakini kwa kuutafakari uumbaji anaamini kwamba Mungu yupo ambaye anapaswa kutukuzwa na kushukuriwa? Je, mtu kama huyo anapata manufaa ya kile ambacho Mungu amekitenda ikiwa Yesu ndiye anayebainisha hicho ndicho haki?
-
-
-
- Hebu tuchukulie kwamba alichokihubiri mchungaji wangu kipo sahihi (angalao kwa uelewa wangu wa kile alichokisema) na kwamba msimamo wangu hauko sahihi. Hiyo inatufundisha nini kuhusu uhusiano kati ya ufunuo wa jumla na ufunuo maalumu? (Ufunuo wa jumla ni muhimu, kwa kadiri ya jinsi ulivyo, lakini ufunuo maalumu unahitajika ili kuwa na uelewa kamili wa mapenzi ya Mungu.)
-
- Njia ya Ufunuo Maalumu
-
- Soma Ufunuo 1:1-2. Ufunuo ulioandikwa na Yohana ulimjiaje? (Mungu Baba alimpatia Yesu, ambaye baadaye alimwambia malaika, ambaye naye alitumwa kwa Yohana ili kumwambia aweze kutuambia.)
-
- Soma 2 Timotheo 3:16-17 na 2 Petro 1:21. Hii inaashiria kwamba waandishi wa Biblia waliamuaje juu ya nini cha kuandika? (Timotheo anasema Mungu “alipulizia” lugha na Petro anasema Roho Mtakatifu “aliwaongoza” wanadamu walioandika. Hii haisemi kuwa Mungu aliwatamkia manabii maneno ya kuandikwa kwenye Biblia neno kwa neno.)
-
-
- Linganisha hilo na jinsi Yohana alivyofafanua namna alivyopokea Kitabu cha Ufunuo. Je, vinaonekana kufanana? (Kwa dhahiri si mara zote vinafanana. Kwanza, Ufunuo 1:2 inarejelea kile ambacho Yohana “alikiona,” na si kile alichokisikia. Pili, malaika si Roho Mtakatifu. Yohana pia alisikia mambo, kwa kuwa Ufunuo 19:9 inaandika kwamba malaika alimpa Yohana maneno mahsusi ya kuandika.)
-
-
- Soma Ufunuo 4:1-2. Hapa Yohana anapewaje ujumbe? (Yupo “katika Roho,” na pia yapo maelekezo mahsusi yaliyonenwa.)
-
-
- Unapata fundisho gani kutoka kwenye vifungu hivi visivyopatana kwenye njia ya uvuvio? (Lazima fundisho ni kwamba ufunuo maalumu unatolewa kwa njia tofauti tofauti – hata kwa nabii huyo huyo. Wakati mwingine maneno kamili yanatolewa, nyakati nyingine njozi inatokea ambayo nabii lazima alifafanue kwa maneno yake. Wakati mwingine Roho Mtakatifu anayaongoza mawazo ya nabii ambaye baadaye anaandika chini mawazo yake.)
-
-
- Soma 1 Yohana 1:1-4. Ni njia gani nyingine ambayo Mungu ameitumia kuwasiliana na wanadamu? (“Lile lililokuwako tangu mwanzo” inamrejelea. Yohana anatuambia kuwa kuchangamana kwake na Yesu alipokuwepo duniani ni ufunuo maalumu ambao Yohana aliuandika ili kukamilisha furaha yetu.)
-
-
- Je, Yesu ni mfano mmoja tu wa ufunuo maalumu? (Hapana. Yeye ni kilele chake. Yohana 14:9 inatuambia kuwa Yesu ni Mungu aliyejidhihirisha mwenyewe: “Aliyeniona mimi amemwona Baba.”)
-
- Mafumbo ya Ufunuo Maalumu
-
- Soma Hesabu 12:5-8. Katika kutetea heshima ya Musa, Mungu anafafanua njia kadhaa ambazo anajifunua kwa wanadamu. Njia za Mungu ni zipi? (Mungu anaposhughulika na manabii wa kawaida, anawasiliana kwa njia ya maono na njozi. Mungu aliposhughulika na Musa, alizungumza naye moja kwa moja.)
-
-
- Utaona kwamba Mungu anasema kuwa hakutumia “mafumnbo” alipozungumza na Musa. Kwa nini Mungu atumie “mafumbo?”
-
-
-
- Je, kitabu cha Ufunuo ni fumbo?
-
-
-
- Je, sanamu katita njozi ya Nebukadneza ilikuwa fumbo? Angalia Danieli 2. (Ufunuo na njozi katika kitabu cha Danieli ni mafumbo.)
-
-
- Soma Mithali 25:2. Hii inaashiria kwamba sababu moja kwa nini Mungu anatumia mafumbo ni ipi? (Mafumbo yanawafanya wafuasi wa Mungu waingie kwa kina kuutafuta uelewa. Mtafutaji anawekeza katika kujifunza ujumbe wa Mungu.)
-
- Soma Mathayo 13:10-13. Wanafunzi wanamuuliza Yesu swali lile lile. Kwa nini asizungumze kwa uwazi? Jibu la Yesu ni lipi? (Mungu anatutaka tumtafute. Anataka tupate thawabu kwa kujifunza zaidi habari zake na mapenzi yake.)
-
- Soma Mathayo 13:13-15. Yesu anatoa sababu gani nyingine ya kutumia mafumbo na mifano? (Inawatenganisha wale wanaojali kuhusu kumwelewa Mungu na wale wasiojali.)
-
- Soma Danieli 12:4. Kitabu cha Danieli kimejaa mafumbo na ishara. Hapa Mungu anatoa sababu gani ya kuifanya mipango yake kuwa ya siri? (Wakati mwingine ni suala la muda. Mungu hataki tujue mambo fulani hadi muda maalumu katika siku zijazo.)
- Chotara?
-
- Tulichojifunza hadi kufikia hapa ni kwamba tukiwa macho ili kuutazama uumbaji tunajifunza mambo ya jumla kuhusu Mungu. Kwa kuongezea, Mungu atatupatia ujumbe mahsusi kuanzia ule unaodhihirishwa bayana hadi ule wa mafumbo. Je, kuna ufunuo chotara, muunganiko wa ufunuo wa jumla na ufunuo maalumu? Je, unaweza kuufikiria muunganiko wowote?
-
- Soma Waebrania 8:3-5. Jiweke kwenye nafasi ya Mwebrania kijana. Ungekuwa na mawazo gani juu ya huduma ya patakatifu? (Ninahisi yangekuwa kama nilivyokuwa kijana nilipokuwa nikienda kanisani. Ni jambo nililolifanya kwa sababu nilikuzwa na kufundishwa kwenda kanisani kila juma.)
-
- Soma Waebrania 8:6. Mwebrania wetu kijana angeweza kuona nini kingine ikiwa kijana huyu angeangalia kwa kina zaidi? (Huduma ya patakatifu ilikuwa unabii wa kile ambacho Yesu atawafanyia wanadamu. Ulikuwa unabii wa jumla kwa maana ya kwamba ulikuwa sehemu ya mazingira yaliyowazunguka, lakini pia ulikuwa unabii maalumu kuhusu mipango ya Mungu kwa ajili ya watu wake.)
-
-
- Aina hii ya ufunuo inakwenda mbali kiasi gani? Waebrania si tu kwamba walikuwa na huduma za patakatifu na Siku ya Upatanisho, bali pia walikuwa na sikukuu nyingine za mwaka. Je, sikukuu hizi ni ufunuo chotara?
-
-
- Soma 1 Wakorintho 5:7. Hii inatuambia nini ambacho Pasaka inakifunua kuhusu siku zijazo?
-
- Soma 1 Wakorintho 15:20-23. Sikukuu ya Malimbuko inatufundisha nini kuhusu mustakabali wa siku zijazo? (Yesu ndiye wa kwanza kufufuliwa, akihakikisha ufufuo wa wale walio wake.)
-
- Je, Sikukuu ya Majuma (Pentekoste) ni ufunuo wa kile anachokifanya Roho Mtakatifu ili kutusaidia kuwavuna waamini? (Jibu ni, “Ndiyo.” Kwa sasa nipo kwenye kikundi cha kujifunza Biblia ambapo tunatafakari kile ambacho sikukuu ambazo hazijatimilizwa zinaweza kutufunulia kuhusu mustakabali wa siku zijazo.)
-
- Rafiki, Mungu ametupatia ufunuo wa jumla na ufunuo maalumu. Asili ya unabii ni kwamba tutaendelea kuwa na ufunuo maalumu, na ikiwa tutakuwa waaminifu, tutaendelea kufumbua mafumbo ambayo Mungu ametupatia kuhusu siku zijazo. Je, utajitoa kuwa msikivu mkubwa kwa yale ambayo Mungu anakuambia?
- Juma lijalo: Maandishi ya Kinabii.
