Somo la 6: Maandishi ya Kinabii
Somo la 6: Maandishi ya Kinabii
(Yeremia 36, Luka 1)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.
Utangulizi: Katika mfululizo wa masomo yetu hadi kufikia hapa, tunaona kwamba Mungu anapeleka ujumbe kwa manabii wake ambao nao wanaufikisha kwa watu kwa njia mbalimbali. Njia mojawapo ni kwamba manabii wanauandika ujumbe huo. Je, umetafakari ni baraka ya namna gani kuweza kuandika mambo? Nilipoanza kufundisha darasa la kujifunza Biblia, ujifunzaji wangu wote uliishia kwa mimi kuuliza maswali yaliyosalia tu akilini mwa wanafunzi. Hilo likanifanya nitafakari kuwa ikiwa nitaandika maswali hayo kwa ajili ya watu wengine kuyasoma, muda ambao niliutumia kujifunza Biblia ungetumika kwa ufanisi zaidi. Mara baada ya Intaneti kufanya suala la uchapishaji kuwa na gharama ndogo, maswali yangu yaliwafikia makumi kwa maelfu ya wanafunzi wa Biblia. Kuwa na Biblia iliyoandikwa ni msingi wa kufikisha ufunuo maalumu wa Mungu. Hebu tuchimbue neno lililoandikwa kwa kina zaidi!
I. Gombo la Yeremia
A. Soma Yeremia 36:1-2. Mungu amempa Yeremia kazi gani? (Kuandika yale ambayo Mungu amemwambia.)
1. Maelekezo haya yanajumuisha kipindi gani? (Mungu anamwambia Yeremia aandike kila neno alilomwambia ambalo lilikuwa kinyume na Israeli na Yuda (na mataifa mengine). Haya yalikuwa maneno ya maonyo.)
B. Soma Yeremia 36:3. Lengo la Mungu ni lipi katika maandishi haya? (Anataka watu wake wageuke kutoka kwenye njia zao ovu ili aweze kuwasamehe.)
C. Soma Yeremia 36:4. Hiki ni nini? Mungu alimwambia Yeremia aandike maneno. Kwa nini tunamwona Baruku akiandika haya maneno? (Nimeangalia maoni kadhaa na yanaashiria kuwa Baruku alikuwa mwandishi. Huyu ni mtu aliyeelimika na mwenye ujuzi wa kusoma na kuandika.)
1. Kwa nini Yeremia ahitaji mwandishi stadi ikiwa anachokifanya Baruku (kifungu cha 4) ni kuandika kile alichokisema Yeremia? (Nilipoanza kazi yangu ya sheria, bosi wangu aliniambia kuwa niwe na mazoea ya kutoa imla (dictate) ili barua zangu ziandikwe. Nilitoa imla barua kwenye zangu na hata nyaraka zangu za kisheria. Hii ilinifundisha kuwa imla ni ujuzi na watu hawaongei kwa namna ile ile wanayoandika. Hiyo inanifanya nitafakari kuwa kilichoishia kuandikwa kwenye gombo kilikuwa juhudi za pamoja kati ya Yeremia na Baruku.)
D. Soma Yeremia 36:5-6. Sasa tumefahamu kuwa sababu ya maneno ya Yeremia kuandikwa ni ipi? (Yeremia alizuiwa kuingia katika nyumba ya Bwana (hekaluni.))
1. Tunajifunza nini kuhusu faida za kuandika? (Maandishi yanakwenda mahali ambapo mnenaji hawezi kufika. Hii ni faida moja kubwa ya kuandika.)
2. Unaweza kufikiria faida gani nyingine za kuandika? (Maandishi yanahifadhi kumbukumbu ya Yeremia juu ya kile alichokisema Mungu na kwa kiasi kikubwa yanapunguza hatari ya ujumbe kukengeushwa kwa kuwa unawasilishwa kwa watu wengine mara kwa mara.)
E. Hebu turukie mbele na tusome jinsi Baruku alivyoelewa wajibu wake. Soma Yeremia 36:17-18. Baruku anauelewaje wajibu wake? (Anathibitisha kwamba aliandike kile Yeremia alichokitamka. Anasema kuwa aliandika “maneno” jambo linaloashiria wajibu mdogo kwa Baruku kuliko uzoefu wangu wa kutoa imla nilioupendekeza.)
F. Kwa ufupi Yeremia 36:8-20 inabainisha kuwa Baruku anafanya kile ambacho Yeremia anakisema. Maneno yanawafanya maafisa wa mfalme kuogopa. Hivyo wanaamua kumwambia mfalme. Soma Yeremia 36:21-23. Mfalme anayafanyia nini maneno ya kwenye gombo? (Anayachoma moto.)
G. Soma Yeremia 36:27-28. Hii inatufundisha nini kuhusu maandishi yetu yanayotangaza uelewa na maarifa ya kumjua Mungu? (Tunatakiwa kutoa nakala. Kuangamiza nakala ya neno la Mungu hakuangamizi neno la Mungu.)
H. Soma Yeremia 36:29-31. Nini kitamtokea Mfalme Yehoyakimu aliyechoma gombo la chuo? (Atakufa. Wanawe hawatarithi kiti chake. Majanga na maafa yatakuja.)
I. Soma Yeremia 36:32. Ni nini mustakabali wa gombo la Yeremia? (Anaongezea kauli za wakati ujao kutoka kwa Mungu. Anaandika maneno ya Mungu katika sehemu moja.)
J. Soma Yeremia 37:1. Sasa mfalme ni nani? (Babeli imechukua udhibiti, Konia mwana wa Yehoyakimu si mfalme. Yehoyakimu amefariki. Mfalme mpya anachaguliwa na Babeli. Maafa aliyoyatabiri Mungu yamekuja.)
II. Wasaidizi
A. Tumeona kwamba Yeremia alimtaka mwandishi Baruku kuandika maneno kutoka kwa Mungu. Hilo linaibua swali kuhusu kama uzoefu wa Baruku ni wa kipekee? Soma Warumi 16:22. Je, Tertio aliandika kitabu cha Warumi? (Soma Warumi 1:1 na Warumi 1:7. Paulo anasema kuwa yeye ndiye mwandishi wa barua kwa Warumi.)
1. Unayaelezeaje madai ya Tertio? Kwa nini madai hayo yapo kwenye barua ya Paulo? (Jibu la asili ni kwamba Tertio anafanana na Baruku.)
B. Soma 1 Wakorintho 16:21, Wakolosai 4:18, na kisha 2 Wathesalonike 3:17. Hii inatuambia nini? (Paulo hakuandika barua hizi kwa mkono wake. Lakini “alizisaini.” Paulo anasema kwamba huu ni utamaduni wake wa kuandika na kuthibitisha barua zake. Kwa mara nyingine, tunaona kwamba mwandishi aliandika barua ambayo sasa ipo kwenye Biblia.)
C. Soma 1 Petro 5:12. Silwano ni nani? (Petro anapoandika kwamba “kwa mkono” wa Silwano “amewaandikia kwa maneno machache” wale walioorodheshwa katika 1 Petro 1:1, tunaona kwamba Silwano alitimiza wajibu kama alivyotimiza Baruku na Tertio.)
D. Soma 1 Wathesalonike 1:1. Je, hii ni barua kutoka kwa wote watatu? (Hiki ndicho inachokisema.)
1. Utaona kwamba mmojawapo kati ya hao watatu ni Silwano. Je, huyu ni mwandishi ambaye sasa amepandishwa cheo kuwa na hadhi ya mwandishi wa barua?
E. Soma 1 Wathesalonike 1:2-5. Huyu “sisi” na “wetu” ni nani? (Lazima hii inamjumuisha Silwano. Barua hii ni mradi wa pamoja. Wakati Paulo ndiye mtu wa msingi, hii inatuambia kuwa msaidizi anaweza kushiriki na wengine yeye binafsi maneno kutoka kwa Mungu.)
F. Soma Matendo 17:14-15. Nani anayefanya kazi na Paulo? (Sila na Timotheo.)
G. Soma tena 1 Wathesalonike 1:1. Je, inawezekana kwamba Sila pia anaitwa Silwano? (Inawezekana kwamba Silwano ni jina rasmi kwa Kilatini na Sila ni ufupisho unaofahamika na wengi.)
1. Hii inatufundisha nini? (Kwamba msaidizi mwandishi kimsingi anaweza kuwa mjumbe wa Mungu wa kujitegemea.)
III. Wasimamizi wa Mungu (God’s Organizers)
A. Soma Luka 1:1-3. Luka anasema kuwa aliandikaje kitabu hiki? (Luka anaandika kwamba yeye ni msimamizi. “Aliandika kwa utaratibu.”)
1. Ni kitu gani hasa anachokisimamia Luka? Mawazo yake? Kumbukumbu yake? (Luka anatuambia kuwa “mashahidi wenye kuyaona” na watumishi wametoa maelezo yanayomhusu Yesu. Ninaelewa hili kumaanisha kwamba Luka anajumuisha kwa namna ya usimamizi maelezo ya watu wengine yaliyoandikwa na yaliyosimuliwa. Maoni ya John MacArthur yanataarifu kuwa takribani asilimia sitini ya maandishi yaliyomo katika kitabu cha Marko yanarudiwa katika kitabu cha Luka.)
B. Soma Luka 1:4. Kwa nini Luka anasimamia na kuandika yale ambayo wengine wameyashuhudia? (Anasema kuwa hilo litatupatia “uhakika” juu ya injili.)
1. Je, hilo litakufanya uwe na uhakika zaidi au uwe na mashaka? Luka hasemi kwamba Roho Mtakatifu alimwambia afanye hivyo. Anasema tu kwamba “nimeona vyema mimi nami” (kifungu cha 3) kufanya hivi. (Katika chumba cha mahakama mashahidi kadhaa wanaokubaliana na kile kilichotokea wanafanya ubainishaji wa ukweli uwe wa uhakika zaidi kuhusiana na jambo linalohusika.)
C. Fikiria juu ya kile anachokisema Luka katika Luka 1:1-4. Kwa nini anaandika hilo katika sehemu ya utangulizi? (Anataka tujue jinsi alivyounganisha barua yake.)
1. Ungesemaje kama kamwe Luka asingebainisha kuwa barua yake ilitegemea maandishi na maneno ya watu wengine?
a. Je, ungelichukulia hilo kama kufeli (hutakuwa na uhakika sana katika kile alichokiandika), au utalichukulia hilo kama kufeli kimaadili (kuficha utegemezi wake kwa watu wengine)?
D. Soma 1 Mambo ya Nyakati 29:29-30. Nathani na Gadi hawana kitabu katika Agano la Kale. Je, mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati anatuambia kuwa alitumia maandishi ya manabii wengine?
E. Soma 2 Mambo ya Nyakati 9:29. Kwa mara nyingine tunaona rejea ya historia nyingine za Sulemani zilizoandikwa. Je, mwandishi wa Kumbukumbu la Torati inazitegemea rejea hizo? (Anaonekana kuzirejelea kama nyaraka za ziada zinazoweza kusomwa au ambazo zingeunga mkono maandishi yake.)
1. Tunapaswa kuelewaje matumizi ya vyanzo vya nje? Je, itakuwa sahihi kuhitimisha kuwa mfano wa kuvutia (inspiration) hujifungamanisha na matumizi ya mwisho ya nyaraka kwa mwandishi wa Biblia, na si lazima kwenye chanzo halisi ambako kilipatikana?
F. Soma 2 Wakorintho 4:5-7. Je, mazingatio yetu yanapaswa kujikita kwa mjumbe au kwa Mungu? (Manabii ni vyombo vya kidunia. Mungu ndiye kitovu (focus) chetu sahihi.)
G. Rafiki, habari njema ni kwamba ujumbe wa Mungu umeandikwa ili tuweze kuusoma na kuufuata. Habari mbaya ni kwamba kuyakataa mapenzi ya Mungu yaliyofunuliwa mara zote kuna athari. Kwa nini usidhamirie, sasa hivi, kusoma na kufuata maandiko ya manabii yaliyovuviwa?
IV. Juma lijalo: Sasa Sikia Hili!
