Uzinzi wa Kiroho (Hosea)

(Hosea 1-3 & 6)
Swahili
Year: 
2013
Quarter: 
2
Lesson Number: 
1

Utangulizi: “Kubeza” sio neno la kawaida sana siku hizi. Lakini sote tunafahamu jinsi kubeza kunavyoumiza. Tunahisi kubezwa pale tunapokataliwa na mtu mwingine kuchaguliwa kuchukua nafasi yako. Wengine wanapata uzoefu huu kutoka kwa wazazi wao, wengine kutoka kwa watoto wao, wengine kwenye mahusiano katika uchumba, wengine kwenye ndoa, na wengine kazini mwao. Huenda nawe umeshawahi kupitia uzoefu huu katika miktadha yote hiyo. Kubezwa (kudharauliwa) kunauma sana. Somo letu juma hili linahusu sisi kumbeza/kumdharau Mungu. Inaonekana kutokuwa na mantiki kabisa, lakini tunafanya hivyo kila wakati. Hebu tuzame kwenye mfululizo wetu mpya wa masomo ili tujifunze zaidi kuhusu “uzinzi wa kiroho!”

  1. Gomeri
    1. Soma Hosea 1:1. Je, Hosea ni nani na ni mtu wa namna gani? (Yeye ni nabii. Kupitia kwa Hosea Mungu anazungumza ili kufikisha ujumbe wake kwa watu.)
    2. Soma Hosea 1:2. Unawezaje kumwoa mke mzinzi? Bado hujaoa, kwa hiyo haiwezekani kufanya uzinzi kwenye ndoa yako, sawa? (Sote tunawafahamu wanaume na wanawake ambao hawajaoa na kuolewa wakijihusisha na vitendo vya ngono kabla ya ndoa. Mtu akiwa anafanya kitendo hiki mara kwa mara, ni vigumu sana kuacha tabia hii mara baada ya yeye kuwa kwenye ndoa. Ninakisia Mungu anamwambia, “Oa mwanamke mjanja/mdanganyifu.”)
      1. Je, jambo hili litaonekanaje pale ambapo wewe ni nabii?
      2. Je, litachukuliwaje na waumini wenzako utakapowaambia kuwa, “Mungu ameniambia nimwoe mwanamke mdanganyifu?”
        1. Ndio kwanza tu Hosea alikuwa anaanza kazi yake kama nabii, je, jambo hilo linajihusishaje na kufuata amri ya Mungu?
      3. Je, Hosea atakuwa na watoto wa namna gani? (Watoto waliozaliwa na mwanaume mwingine.)
        1. Fikiria magumu yaliyopo katika jambo hili. Je, ni kitu gani kinachofanya jambo hili kuwa gumu? (Sio tu kwamba mkeo amemchagua mtu mwingine dhidi yako, lakini pia unakuwa unakumbushwa jambo hili kila siku kila unapomwona mtoto.)
      4. Kwa nini Mungu alimwambia Hosea kufanya hivyo? (Mungu anasema ni kwa sababu jambo hili linaelezea wanadamu kutokuwa na uaminifu naye.)
      5. Kama ningekuwa Hosea ningesema, “Vipi kuhusu njia nyingine? Niambie tu Mungu, nami nitaelewa.” Kwa nini jibu hilo sio zuri sana (yaani halitoshelezi)?
      6. Je, umewahi kumsikiliza kiongozi wa kidini au mzungumzaji ambaye ulidhani kuwa hakuwa mwaminifu/mnafiki?
        1. Kama Hosea angeambiwa maumivu anayoyapata Mungu kwa sababu watu wake hawakuwa waaminifu, je, Hosea angeonekana kutokuwa mwaminifu? (Watu waliodhauriwa/waliobezwa wanaelewa asili ya hisia za Mungu kuhusu sisi kutokuwa waaminifu kwake.)
  2. Wototo
    1. Soma Hosea 1:3-5. Tumejadili kwamba mtoto aliyezaliwa na mwanaume mwingine ni mwendelezo wa ukumbusho wa mara kwa mara wa mkeo kutokuwa mwaminifu. Je, ni ukumbusho gani tunaouona hapa? (Kinyume chake. Mtoto anapewa jina liwe ukumbusho wa watu wasio waaminifu kuhusu kutokuwa kwao waaminifu.)
      1. Je, ni nani mahsusi anayetajwa kutokuwa mwaminifu? (Mfalme Yehu.)
    2. Soma 2 Wafalme 10:28-31. Ni kwa namna gani Yehu sio mwaminifu? (Anafanya mambo mkanganyiko. Anamwangamiza Mfalme Ahabu aliye mwovu pamoja na ibada ya Baali, lakini anaendelea kuabudu ndama wa dhahabu. Rejea katika Hosea 1:4 inayorejea “mauaji katika Yezreeli” ni ya mashaka (haiaminiki), kwa kuwa baadhi ya mauaji yaliyotekelezwa pale Yezreeli yalikuwa ni maelekezo ya Mungu. 2 Wafalme 10:30.)
      1. Je, kutokuwa na uamninifu kwa Yehu kunatufundisha nini? (Tunaweza kufanya mambo makuu kwa Mungu, lakini bado tusiwe waaminifu kama tusipompa Mungu moyo wetu wote.)
    3. Soma Hosea 1:6-7. Mungu anawezaje kusema kuwa hatawapenda tena au kuisamehe Israeli, lakini atairehemu nyumba ya Yuda? Nilidhani kuwa Mungu anasamehe mara zote!
      1. Soma Mathayo 12:31-32. Kwa nini dhambi nyingine zinasamehewa na dhambi nyingine hazisamehewi?
        1. Kama unaamini katika Utatu Mtakatifu, maneno ya Yesu ni magumu zaidi kuyaelewa! (Maonyo ya Yesu yanajihusisha na mtazamo wetu dhidi ya Roho Mtakatifu na asili ya kazi ya Roho.)
      2. Soma Wagalatia 5:16-18. Kwa nini jukumu la Roho Mtakatifu ni muhimu sana maishani mwetu? (Tukielewa jukumu la Roho Mtakatifu maishani mwetu, tutaelewa kwamba Yesu hawi dikteta anapozungumzia dhambi isiyosamehewa. Mungu anaendelea kuwa tayari kutusamehe, lakini tunapomkataa Roho Mtakatifu, tunafunga mlango wa wokovu. Tunapoukimbia uwezo utakaotuongoza kwenye toba na maisha tunayoishi kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu, sio tu kwamba tumemkataa Mungu, tunakuwa tumekataa pia njia zake za wokovu. Mungu hawi dikteta, tunakuwa tumemkataa.
    4. Angalia tena Hosea 1:7. Je, Mungu anaiokoaje nyumba ya Yuda? Je, ni kwa matendo yake yenyewe? (Hapana. Mungu anasema kuwa wokovu hautakuja kwa uwezo wa mwanadamu, bali Mungu ataingilia kati.)
    5. Soma Hosea 1:8-11 na Warumi 9:25-26. Je, ni jambo gani linalotabiriwa kupitia kuzaliwa kwa huyu mwana? (Soma Warumi 9:22-24 na 1 Petro 2:10. Hosea anakitazamia kipindi ambacho watu wa Mataifa pamoja na Wayahudi watamrudia Mungu. Kipindi ambacho watamrudia Yesu.)
    6. Unadhani ni kwa nini Mungu aliruhusu Hosea ateseke kupitia kwa mwanamke asiye mwaminifu na watoto haramu ili kufikisha ujumbe wa Mungu? Kwa nini asitoe unabii tu? (Hii ni taswira nyingine ya mjadala wetu wa awali. Kama unaweza kujifunza kutoka kwa watu wengine, hilo ni jambo zuri. Lakini, ukijifunza jambo kutokana na uzoefu wako mwenyewe, tendo hilo linapeleka ujumbe nyumbani.)
  3. . Hukumu
    1. Soma Hosea 2:9-13. Tusipomtii Mungu, je, ni jambo gani tunaloweza kulitegemea? (Hukumu.)
    2. Angalia tena Hosea 2:11. Kwa nini Mungu akomeshe nyakati ambazo watu wanamgeukia? (Angalia tena Hosea 2:13. Sherehe hizi hazina maana pale ambapo hisia zetu za dhati zinajielekeza kwa miungu ya uongo na tunamsahau Mungu wa kweli.)
  4. Wokovu
    1. Soma Hosea 3:1. Hebu subiri kidogo. Rejea nyuma kidogo na upitie tena Hosea 1:6-7. Mungu anawezaje kusema kuwa anawapenda wana wa Israeli wakati ambapo hapo kabla alisema, “Sitairehemu tena nyumba ya Isaraeli, ili kwamba niwasamehe tena?”
      1. Je, Mungu anajichanganya yeye mwenyewe? Au, je, hii ni kauli ya “kijanja” ambayo kiuhalisia inamaanisha kuwa Hosea hana haja ya kumpenda Gomeri?
      2. Jiweke kwenye nafasi ya Gomeri. Je, ungependa kuonyeshaje upendo kwa mwenzi ambaye bado anajihusisha na mahusiano ya kizinzi?
      3. Je, hili linatufundisha nini kuhusu asili ya upendo wa Mungu kwetu? (Upendo wa Mungu uko pale pale hata pale tunapomkataa. Tatizo kwetu sisi, kama tulivyojadiliana hapo awali, ni kwamba sisi ndio wasimamizi wa wokovu wetu. Ingawaje Mungu anatupenda, tunaweza kumkataa Roho Mtakatifu, na hivyo kuziba njia ya toba.)
    2. Soma Hosea 6:1. Je, ni haki kusema kwamba Mungu aliwararua vipandevipande, na kwamba Mungu aliwajeruhi? (Walimkataa Mungu. Mungu akaweka hukumu. Lakini, haionekani kuwa haki kumlaumu Mungu katika jambo hilo.)
    3. Soma Hosea 6:2. Je, hili linaleta jambo gani akilini? (Soma 1 Wakorintho 15:3-4. Huu ni ujumbe wa Pasaka! Huu ni ujumbe wa wokovu! Huu ni unabii wa Bwana mfufuka!)
      1. Tafakari jambo hili: katikati ya kisa kichungu cha uzinzi, Mungu anatukumbusha juu ya uamuzi wake wa kufa kifo kichungu kwa niaba (ajili) ya watu wazinzi. Upendo wa ajabu namna gani! Neema ya ajabu namna gani!)
    4. Soma Hosea 6:6. Je, lengo la Mungu kwa ajili ya maisha yetu ni lipi? (Mungu anahitaji upendo wetu. Anatutaka tuwaonyeshe watu wengine rehema. Ameweka mfumo wa msamaha wa dhambi, lakini kile anachokitaka sana ni uaminifu wetu!)
    5. Rafiki, Mungu anaonyesha upendo usio na mantiki tena usiozuilika/usiodhibitika dhidi yako! Je, utamwomba Roho wa Mungu aishi ndani yako? Je, utadhamiria kuishi maisha yanayojielekeza kwenye utakatifu na rehema? Kwa nini usijiwekee dhamira hiyo hivi leo?
  5. Juma lijalo: Upendo na Hukumu: Mungu Katika Njiapanda (Hosea)