Upatanisho: Sadaka ya Utakaso

(Mwanzo 4, 2 Samweli 14, Mambo ya Walawi 16)
Swahili
Year: 
2013
Quarter: 
4
Lesson Number: 
5
 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kwa miaka mingi nimekuwa nikisumbuliwa na mantiki inayohusu upatanisho. Kwa nini basi dhambi zetu zinahitaji kifo cha Yesu? Kwa upande mwingine, kwa nini kifo cha Yesu kinatosha kuondoa dhambi zetu? Upatanisho haukuwa kama swali la hisabati, lililo na njia ya ukokotoaji ulio dhahiri. Suala hili lilihusisha mambo ambayo sikuyaelewa. Somo la thamani kabisa kutoka katika somo letu la mahali patakatifu ni jibu kwa swali la kwa niniYesu alipaswa kufa. Kwa nini upataniso unaleta mantiki. Hebu tuingie kwenye somo letu la Biblia la juma hili ili tuweze kujifunza zaidi!

  1.  Kukiuka Utawala wa Sheria
    
    1. Soma Mwanzo 9:5-6 na Hesabu 35:30. Je, adhabu ya mauaji ni ipi? Je, utawala wa sheria wa Mungu ukoje? (Kifo.)
    2. Soma Mwanzo 4:8-10. Kitu gani kilipaswa kumtokea Kaini? (Alipaswa kuuawa.)
    3. Soma Mwanzo 4:11-15. Unadhani kwa nini Mungu si tu kwamba alishindwa kumwua Kaini, bali pia alimlinda kwa umadhubuti dhidi ya haki iliyostahili – inayotokana na utawala wa sheria wa Mungu?
    4. Soma 2 Samweli 14:4-6. Je, umewahi kukisikia kisa hiki hapo kabla? (Kinafanana kidogo na kisa cha Kaini ha Habili.)
    5. Soma 2 Samweli 14:7. Familia inataka haki, lakini mama haitaki hiyo haki. Kwa nini? (Atawakosa wana. Mumewe amefariki, na sasa wanaye wote wawili watakufa endapo haki itatendeka. Kuna hii kauli ya “urithi” inayoweza kukufanya uhisi kuwa wanandugu walikuwa na kitu zaidi ya haki mawazoni mwao.)
      1. Je, unadhani kauli ya mama inaelezea hukumu isiyo ya kawaida aliyopewa Kaini? Hata hivyo, kumbuka kuwa Adamu bado yu hai. (Nadhani hii inadokeza sababu ya hukumu ya Kaini. Lingekuwa janga la kutisha kwa Hawa kuchukulia kwamba dhambi yake imesababisha kifo cha wanaye wote wawili.)
    6. Soma 2 Samweli 14:8-9. Hii ni kauli isiyo ya kawaida. Kwa nini hatia iwe juu ya mfalme au ihamishiwe kwa mama? Si yeyote kati yao aliyetenda hilo kosa la jinai. Wote walionesha upendo na huruma. (Maoni ya Jamieson, Fausset na Brown kuhusu hili fungu yanaeleza kwamba kukiuka utawala wa sheria kulizidi “haki ya pekee ya kifalme.” Uwajibikaji wa kosa ulipaswa kwenda mahali fulani. Kwa kuwa mfalme, kutokana na ombi la mama, alikiuka utawala wa sheria, mfalme ndiye anayepaswa kuwajibika. Kwa kuwa mama alimwomba mfalme akiuke utawala wa sheria, badala yake mama anasema, “mimi ndiye nitakayewajibika.”)
    7. Katika kitabu cha Mathayo 27 tunasoma kisa cha kushtakiwa kwa Yesu. Soma Mathayo 27: 15-18. Kwa nini Pilato anafikiria juu ya uamuzi anaopaswa kuutangaza juu ya Yesu? (Anadhani kuwa Yesu hana hatia!)
    8. Soma Mathayo 27:20-23. Je, Pilato anapaswa kumwachia Yesu huru? (Ndiyo, kwa hakika. Umati hautoi sababu za kutosha za Yesu kuuawa. Unajaribu kumshurutisha Pilato. Mbaya zaidi, katika Mathayo 27:19 mke wa Pilato anamwambia kuwa Mungu amemtumia ujumbe kwamba asimdhuru Yesu.)
    9. Soma Hesabu 35:31 na Warumi 6:23. Kitabu cha Warumi hakisemi kuwa sisi ni wauaji, bali kinasema kuwa mshahara wa dhambi ni mauti. Je, Mungu anakiuka utawala wa sheria kwa mara ya pili? Tumejadili ukiukaji uliohusisha kutomuua Kaini (pamoja na sisi). Sasa tunaona kuwa fidia ya wauaji pia inazuiliwa!
      1. Je, tunaweza kuelezea jambo hili kwa kusema kuwa sote tunakufa kwa sababu ya kuingia kwa dhambi ulimwenguni? Kama hilo linaonekana kuwa jibu jepesi, je, tunawaelezeaje Eliya (2 Wafalme 2) na Henoko (Waebrania 11:5) waliochukuliwa mbinguni bila kuonja mauti?
  2. Uwajibikaji Kutokana na Ukiukwaji wa Utawala wa Sheria
    1. Tumeona kuwa mfalme alipokiuka utawala wa sheria, alikubali kuwajibika kutokana na ukiukwaji huo. Tunapokiuka sheria ya nchi, au sheria ya Mungu, je, mwathirika ni nani?
      1. Soma Zaburi 51:3-4. Mfalme Daudi anazungumza, na anazungumzia kitendo chake cha uzinzi na mauaji. Anawezaje kusema kwamba ametenda dhambi dhidi ya Mungu “peke yake?” (Nchini Marekani, malalamiko ya mhalifu yatawasema “Watu” dhidi ya mtu anayetuhumiwa; na si mwathirika mahsusi wa kosa dhidi ya mtu anayelalamikiwa. Dhana ni kwamba unapotenda kosa, unakiuka haki za umma. Hii inaakisi wazo kwamba dhambi zi kinyume na Mungu, anayeutawala ulimwengu.)
    2. Kama Mungu ndiye mwathirika wa kweli (na mwathirika pekee) wa dhambi zetu, kwa nini asiseme, “Ninasamehe,” na kusahau juu ya hili suala la Mungu kulipa adhabu ya ukiukaji wa utawala wa sheria?
    3. Soma Mika 7:18. Je, Mungu anafanya nini kuhusiana na dhambi yetu? (Anatusamehe. Hii inaonesha kuwa Mungu anaweza kusema, “Ninasamehe!” Nchini Marekani, Rais (au Gavana wa Jimbo) anaweza kuwasamehe wakosaji.)
      1. Kwa hiyo ninauliza tena, kwa nini mtu yeyote anapaswa kufa kama Mungu ana uwezo wa kusamehe? (Bado ni upotovu wa utawala wa sheria. Mtu anayepotosha utawala wa sheria lazima awajibike kwa upotovu huo. Hata hivyo, mwathirika wa kosa lililotendeka anayo madai mazuri juu ya kubadili utawala wa sheria.)
  3. . Utatuzi
    1. Soma Mambo ya Walawi 1:3-5 na Yohana 1:29. Unadhani kwa nini Mungu alitoa haya maelekezo ya kafara ya wanyama katika Agano la Kale?
      1. Je, yanafananaje na Yesu? (Hapa ndipo mantiki ya upatanisho inapooana. Mungu alikiuka utawala wa sheria kwa kutokutuua kwa ajili ya dhambi zetu. Huku akiwa Mtoa maamuzi, Mungu aliwajibika dhidi ya uamuzi huo kwa kukubali kufa badala yetu. Hata hivyo, alitutaka tuelewe uhusiano kati ya dhambi na mauti, na kwa hiyo Mungu alianzisha mfumo wa utoaji kafara wa mahali patakatifu ambao ulitukumbusha juu ya uhusiano kati ya dhambi na mauti na kuashiria suluhisho la tatizo la dhambi.)
    2. Hebu tutafakari dhana iliyo kwenye hitimisho kwamba Yesu anawajibika na tatizo. Je, dhana hizo ni zipi? (Kwanza, dhana kwamba Yesu anapaswa kuchukua adhabu kutokana na dhambi zetu inaonesha kuwa Yeye ni Mungu. Kama ilivyo kwa Mfalme, anayo mamlaka juu ya tatizo. Shetani anakubali kuwa Yesu ni Mungu. Pili, hii inaonesha umuhimu wa pekee wa sheria ya Mungu na dhamira yake kwamba utawala wa sheria unapaswa kuheshimiwa. Mwisho, ni uthibitisho wa maelezo ya uumbaji juu ya anguko la wanadamu.)
    3. Soma Yeremia 17:1. Hili limeandikwa wapi? (Limechorwa ndani ya mioyo yetu na katika madhabahu. Rejea hii ya dhambi na madhabahu katika mahali patakatifu inaashiria umuhimu wa mfumo wa mahali patakatifu.)
  4. Utakaso
    1. Soma Mambo ya Walawi 16:15-19. Tulipojifunza kuwa mfalme aliyekiuka utawala wa sheria aliwajibika kwa kosa lililotendeka, tuliona nini? (Dhambi ilihama kutoka kwa mtu mwenye hatia kwenda kwa mfalme.)
      1. Katika mfumo wa mahali patakatifu, dhambi za mtu zilihama kwenda kwa mnyama aliyetolewa kafara. Je, uhamisho gani mwingine tunaouona kwenye haya mafungu? (Unyunyizwaji wa damu ya mnyama aliyetolewa kafara unaonekana kuhamisha dhambi kwenda mahali patakatifu pamoja na kwenye samani zake.)
    2. Soma Mambo ya Walawi 16:7-10 na Mambo ya Walawi 16:20-22. Je, kitu gani sasa kimetokea kwenye dhambi zilizohamishiwa mahali patakatifu? (Zinahamishiwa tena kwa mbuzi aliye hai. Mbuzi hafi, anapelekwa jangwani.)
    3. Tukirejea kwenye wazo kwamba mtu anayekiuka utawala wa sheria anapaswa kuwajibika, na mfumo wa kafara wa mahali patakatifu unamwashiria Yesu akiwajibika juu ya dhambi zetu kwa sababu hakutuua, je, unaelezeaje hamisho la dhambi? Kwa nini mfumo wa mahali patakatifu pia una somo linalohusu hamisho la dhambi? (Mungu hataki tusalie dhambini. Hatimaye, si mdhambi wala mwanakondoo alibeba dhambi. Dhambi ilihamishiwa mahali patakatifu na hatimaye ilihamishiwa kwa mbuzi.)
      1. Je, kuna somo gani la kiroho tunalojifunza katika hili jambo? (Kiuhalisia dhambi zetu zinaondolewa. Yesu halipii tu adhabu badala yetu, bali pia dhambi zetu zinaondolewa.)
      2. Kama mnyama aliyetolewa kafara alimwashiria Yesu, je, mbuzi anamwashiria nani? (Kuachiliwa kwa dhambi zetu. Yesu alikubali adhabu kwa ajili ya dhambi zetu, lakini pia aliandaa mustakabali wa ondoleo la dhambi zetu.)
    4. Rafiki, fikiria kile Yesu alichokutendea. Alikupa uzima kwa kukiuka utawala wa sheria. Aliichukua hatia yako. Yesu alikufa badala yako (kwa ajili yako). Je, unapaswa kuitikiaje jambo hili? Kwa nini leo usikubali kafara yake kwa ajili yako, ufurahie uondoaji wake wa dhambi zako, na udhamirie kuishi kama mtu anayetaka dhambi isiwemo maishani mwake?
  5. Juma lijalo: Siku ya Upatanisho.