Uanafunzi na Maombi

(Mathayo 6)
Swahili
Year: 
2014
Quarter: 
1
Lesson Number: 
3

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, maisha yako kimaombi yakoje? Kama maisha yako yapo kama yangu, basi jibu lako litakuwa ni, “hayatoshelezi na yanahitaji kuboreshwa.” Ninapokuwa nikitembea wakati wa asubuhi, huwa ninajaribu kuomba na kuutafuta uongozi wa Mungu kwa ajili ya uandishi wa hili somo. Hata hivyo, mawazo yangu huwa yanafanana na mnyama mdogo ajulikanaye kwa jina la kuchakuro (squirrel) ambaye mara kwa mara huwa anajaribu kujitumbukiza kwenye mambo mengine mengi. Endapo unadhani kwamba maisha yako kimaombi yanahitaji kuboreshwa, basi hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone jinsi tunavyoweza kuboresha mazungumzo yetu na Mungu!

  1. Maandalizi ya Maombi
    1. Soma Mathayo 6:5 na Mathayo 6:1. Nani anayezungumza hapa? (Yesu.)
      1. Je, ni kanuni gani ya maisha anayotuambia? (Mungu hatoi thawabu kwa utendaji kazi unaolenga kujitukuza.)
      2. Je, ni thawabu ya aina gani inazungumziwa hapa? (Thawabu hii haiwezi kuwa ni ya wokovu, kwani ingekuwa hivyo basi matendo yetu yangetupatia wokovu. Lazima itakuwa ni thawabu binafsi inayotolewa na Mungu hapa duniani au mbinguni.)
      3. Katika miaka ya hivi karibuni nilifanya na kuwa na urafiki na mwanateolojia mkubwa ambaye ni mnyenyekevu sana. Huwa ninakuwa na nia mchanganyiko mara zote ninapokuwa nikihubiri na kufundisha. Mojawapo ya sehemu ya nia hizo ni kwamba huwa ninajitahidi kufanya vizuri ni kuwafanya watu wanichukulie kwamba mimi ni mahiri sana, na nia nyingine ni kuwasaidia watu waielewe Biblia vizuri zaidi. Nilimuuliza huyu mtakatifu mnyenyekevu kuhusu suala hili na akaniambia kuwa yeye pia huwa ana nia mchanganyiko. Kama jambo hili ni kweli kwako pia, je, fungu hili linamaanisha nini? (Ama unajaribu kujipatia thawabu au unapewa thawabu na Mungu. Je, utapendelea thawabu ipi?)
      4. Je, ni kanuni gani ya maombi tunayojifunza hapa? (Maombi hayapaswi kuwa na lengo la kujitukuza. Hayapaswi kulenga “kujivuna.”)
    2. Soma Mathayo 6:6. Kwa nini maombi ya sirini ni bora zaidi? (Yanaepusha tatizo la kuomba ili kusikiwa na watu – na Mungu anatupatia thawabu.)
      1. Je, tatizo hili linaenea hadi kwa watu wengine katika maeneo mengine ya huduma za kanisa – yaani watu wanajihusisha na huduma za kikanisa ili waonekane? (Nimegundua kwamba watu wanaotoa maombi ya kuombewa kanisani, wanataka kuhubiri. Watu walio na wimbo maalum, wanataka kuhubiri. Bila kujali sehemu mahsusi ya huduma ya kanisa, watu wengine huwa wanataka kuibadili huduma hiyo na kuwa hubiri dogo. Kwa nini jambo hili linatokea? Nahisi linahusiana na kujitukuza nafsi.)
    3. Soma Mathayo 6:7-8 na 1 Wathesalonike 5:16-18. Kwa upande mmoja tunaambiwa tusibwabwaje, na kwa upande mwingine tunaambiwa “tuombe bila kukoma.” Je, unayalinganishaje haya mawazo mawili? (Hivi sasa nina kipaumbele kikuu cha kumwombea ndugu wangu wa karibu sana. Ni vigumu sana kwangu kuepuka “kubwabwaja” (kurudiarudia ombi langu tu). Jambo moja nililojifunza kwa miaka mingi ni mtazamo wa maombi. Kuifanya sehemu moja ya akili yako iwasiliane na Mungu kwa ajili kuomba ulinzi wake usiokoma.)
      1. Je, umewahi kufikiria juu ya maombi kufananishwa na mtu anayezungumza nawe? Je, unafurahia mtu mwingine kurudia jambo moja mara zote kama ilivyokuwa kwa “Alzheimer?” (Hapana! Nina uhakika Mungu pia hapendelei jambo hilo.)
      2. Kama kurudiarudia jambo kunaachwa, je, tunamfanyaje Mungu atambue kwamba jambo fulani ni la msingi sana kwetu? (Tunaweza tu kulisema jambo hilo. Wakati huo huo, nadhani Mungu anaelewa pale tunapotaka kuzungumzia jambo fulani lililo la muhimu sana kwetu kwa kurudiarudia. Hata hivyo, hatupaswi kurudiarudia maneno yale yale bila kuyatafakari akilini.)
    4. Hebu tuangalie tena Mathayo 6:8. Ikiwa tayari Mungu anayafahamu mahitaji yangu (na ninaamini jambo hili kwa uhakika kabisa), ni kwa nini basi ninahitajika kuomba? (Hii inasaidia kutafuta suluhu ya matatizo yaliyobainishwa kwenye mjadala wetu wa awali. Kama maombi hayalengi kumfunulia Mungu mambo ambayo tayari anayafahamu, basi kwa kiwango kikubwa kabisa lazima maombi yatakuwa ni kwa faida yetu wenyewe. Kubwabwaja hakutatutia moyo, bali kumshirikisha Mungu mambo yetu ya ndani kabisa kutatutia moyo.)
  2. Maombi ya Mfano
    1. Soma Mathayo 6:9. Unadhani ni kitu gani hasa anachokimaanisha Yesu anaposema “basi ninyi salini hivi?” Je, tunapaswa kurudia hili ombi maalum?
      1. Endapo tumekariri na kunukuu hili ombi, je, tutakuwa tunabwabwaja bila kutafakari?
      2. Endapo ungekuwa unawafundisha watu kuomba, je, ungewafundishaje? (Tunatoa mifano ya vitu ili kuwasaidia kujifunza. Katika uzoefu wangu wa maombi maishani, huwa ninachukulia kila sehemu ya Sala ya Bwana kuwa mfano wa kutufundisha juu ya mpangilio na mada ya maombi yetu. Hebu tuchimbue jambo hili kwa kina zaidi katika sehemu inayofuata.)
    2. Soma tena Mathayo 6:9. Je, maombi yetu yanapaswa kuanzaje? (Jambo la kwanza ni kutoa sifa. Nadhani kila ombi linapaswa kuanza kwa kumsifu Mungu.)
      1. Kwa nini? Je, Mungu anahitaji kusifiwa ili aweze kujibu maombi yetu? (Inabadili mawazo yetu yaelekee kwenye ukweli kwamba kipaumbele chetu cha kwanza maishani ni kumpa Mungu utukufu. Inatukumbusha juu ya ukuu wa Mungu – ambaye pia ni Baba wetu! Wazo zuri ajabu!)
    3. Soma Mathayo 6:10. Je, mada gani inafuatia katika maombi yetu? (Yesu atakapokuja tena, lengo la Mungu litafikiwa na dhambi, kifo na ugonjwa vitakoma. Tunataka mapenzi ya Mungu yatimizwe maishani mwetu na katika dunia sasa hivi. Hapa ndipo tunapoweza kuzungumza na Mungu juu ya malengo yetu na matatizo yetu maishani.)
    4. Soma Mathayo 6:11. Je, hapa Mungu anatutia moyo tuombe juu ya nini? (Mahitaji yetu! Bwana, tupatie kile tunachokihitaji. Ni jambo jema kuwaombea watu wengine, lakini Mungu pia anatuhamasisha tujiombee sisi wenyewe.)
    5.  
    6. Soma Mathayo 6:12. Katika ombi lako halisi, je, huwa unajadili mada gani kwanza? (Silika yangu ya kawaida huwa ni kuomba kwa ajili ya msamaha wa dhambi zangu. Kwa namna fulani hivi nadhani huo ndio unaopaswa kuwa mpangilio wa mambo kabla sijaingia kwenye jambo jingine lolote lile.)
      1. Unadhani kwa nini msamaha wa dhambi unapaswa kufuata baada ya kusifu, matatizo na mahitaji? (Kuomba msamaha hakuakisi kipaumbele cha kwanza cha Mungu kwa ajili ya maombi maishani mwetu.)
      2. Angalia mstahilishaji wa msamaha. Je, msamaha wa dhambi zetu umejengwa juu ya nini? (Soma Mathayo 6:14-15: kuwasamehe watu wengine.)
        1. Je, kuna mtu ambaye bado hujamsamehe? Kama hivyo ndivyo, je, maneno ya Yesu yanaashiria nini? (Kwamba Mungu hatasamehe dhambi zako. Hili ni jambo zito sana.)
        2. Je, kwa ujumla una mtazamo wa kusamehe dhidi ya wale wanaoshindwa kufikia viwango vyako?
    7. Soma Mathayo 6:13 na Yakobo 1:13-15. Yesu anamwambia Mungu asitutie majaribuni, bali Yakobo anasema kuwa jambo hilo haliwezekani. Je, tunapaswa tu kuachana na hii sehemui ya hili ombi kwa sababu hatuna haja ya kuwa na wasiwasi juu ya Mungu kututia majaribuni?
      1. Soma Mathayo 4:1. Hapa, Yesu anaongozwa na Roho Mtakatifu majaribuni. Je, Yakobo amechanganyikiwa tu?
    8. Hebu tusome baadhi ya mafungu mengine ambayo yanaweza kutusaidia. Kwanza, soma Mathayo 26:38-39. Je, hapa Yesu anaomba jambo gani? (Yesu anaingia katika kipindi cha jaribu la kutisha. Katika hali ya kawaida (hali ya asili) anataka aepuke jambo hili. Anaomba kwamba Mungu aondoe jaribu.)
    9. Pili, soma Ayubu 1:9-12. Je, wajibu wa Mungu ni upi katika majaribu yaliyofuatia maishani mwa Ayubu? (Mungu aliyaruhusu.)
  3. Je, unaweza kuona jambo lenye kufanana baina ya Yakobo 1:13 na haya mafungu mengine, hususan Mathayo 4:1? (Hakuna hata fungu moja kati ya haya tunapoona Mungu akimjaribu mtu yeyote. Mara zote Shetani ndiye anayetoa majaribu. Muda mrefu nimekuwa nikidhani kwamba katika Mathayo 4:1 Roho Mtakatifu alimwongoza Yesu kwa Shetani kabla Shetani hajajiandaa kikamilifu. Jaribu la kwanza halionekani kuwa ni matokeo ya aina ya maandalizi tuliyoyaona katika Bustani ya Edeni. Kwa hiyo, majaribu yatatujia sisi sote, na ninadhani Yesu anaomba kwamba majaribu yasiruhusiwe kutujia pale ambapo tuna uwezo mdogo wa kukabiliana nayo. Kimsingi, anachokisema Yakobo juu ya majaribu na mchakato wetu wa fikra unapaswa kuashiria ukweli kwetu sisi sote.)
    1. Hebu tuangalie sehemu ya mwisho ya Mathayo 6:13. Je, hili linaendanaje na mjadala tuliokuwa nao hivi punde juu ya udhibiti wa Mungu pale tunapojaribiwa? (Yesu anaomba kwa ajili ya ushindi dhidi ya dhambi na dhidi ya Shetani.)
      1. Je, hii inaashiria mada gani kwenye maombi yetu? (Tunapaswa kuomba kwa ajili ya tatizo letu la dhambi. Tunapaswa kuomba msaada wa Mungu ili tuweze kuishi maisha matakatifu.)
      2. Je, ni kwa njia gani nyingine tunaweza kuokolewa kutoka kwa Shetani? (Hapa ndipo ambapo huwa ninaomba kwa ajili ya familia yangu, kwa ajili yangu na mahitaji ya watu wengine ili waweze kuokolewa kutoka kwa Shetani.)
    2. Tafsiri ya Biblia ya “New International Version” (ambayo mafungu ya Biblia yananukuliwa katika somo hili kwa lugha ya Kiingereza) haina maneno “kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.” Hiyo ni kwa sababu hakuna miswada ya kale hata mmoja iliyo na hii lugha. Inaonekana mtu aliyekuwa akinakili Biblia alipitiwa na kuyaongezea maneno hayo. Hata hivyo, ninayapenda maneno hayo kwa hiyo huwa ninamalizia maombi yangu kwa jinsi ile ile nilivyoyaanza – kwa kumsifu Mungu.
    3. Rafiki, je, utatenga muda wa pekee na wenye utulivu kwa ajili ya Sala ya Bwana (ombi lililopo katika Mathayo 6) na kuitumia kama mfano kwa ajili ya maombi yako kwa Mungu?
  4. Juma lijalo: Kuwafanya Watoto Kuwa Wanafunzi