Ufalme wa Kristo na Sheria

(1 Wakorintho 15, Ufunuo 21 7 22)
Swahili
Year: 
2014
Quarter: 
2
Lesson Number: 
13

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, wewe u sehemu ya Ufalme wa Mungu? Ikiwa unasoma masomo haya, pengine jibu ni, “Ndiyo.” Ninapoona mambo hayaendi vizuri hapa duniani, au ninaposikitishwa na siasa za nchi, kwanza ninapaswa kukumbuka kwamba mimi ni raia katika Ufalme wa Mungu. Tunawezaje kufahamu kwamba Ufalme wa Mungu ni jambo halisi? Je, mafunzo yetu kuhusu sheria yanaendanaje na imani yetu juu ya Ufalme wa Mungu? Tunapomalizia mfululizo wetu wa masomo juu ya sheria, hebu tuzame kwenye Biblia zetu ili tujifunze kinachomaanishwa kuwa raia katika Ufalme wa Mungu!

  1. Ufalme wa Mungu – Je, ni wa Kweli?
    1. Soma 1 Wakorintho 15:1-2. Je, chaguzi gani mbili tulizonazo juu ya injili? (Kwa upande mmoja, tunaweza kuiamini na kuisimamia. Kwa upande mwingine, tunaweza kuichukulia kwa urahisi na inakuwa ni ya kazi bure.)
    2. Soma 1 Wakorintho 15:3-7. Je, ukweli wa msingi kabisa wa injili ni upi? Je, “cha kwanza kabisa kwa umuhimu” ni kipi? (Jambo hilo ni kwamba Yesu alizifia dhambi zetu, kama ilivyotabiriwa na Biblia, alizikwa na kufufuka kutoka mautini. Tukio hili lilishuhudiwa na watu wengi.)
    3. Soma 1 Wakorintho 15:12-13. Baadhi ya watu hawaamini kuwa kuna ufufuo wa wafu. Je, mantiki ya matokeo ya mtazamo huo ni ipi? (Mtazamo huo unakanusha “ukweli wa msingi kabisa” ya kwamba Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu na kufufuka kutoka katika mauti.)
    4. Soma 1 Wakorintho 15:14. Kuna mambo mengi sana mazuri yanayohusu injili. Kwa nini imani na kuihubiri injili “ni bure” pasipo ufufuo?
      1. Mfululizo wetu wote wa masomo ya robo hii ulikuwa unahusu sheria. Nimekuwa nikisema kwa kurudia rudia kwamba tulipewa sheria na Mungu ili tusigonge vichwa vyetu kwenye sheria ya asili. Ni kwa jinsi gani jambo hilo linaweza lisiwe na maana? (Ikiwa Yesu alikufa moja kwa moja, basi sheria ilimuua. Ikiwa sheria ilimuua Yesu, basi itamuua kila mmoja wetu. Kwa hivyo, hata dhana inayosema kwamba sheria inatusaidia hatimaye isingekuwa sahihi kwa sababu sheria ingetuua.)
    5. Soma 1 Wakorintho 15:15-16. Tatizo gani jingine lililopo kwenye ujumbe wetu ikiwa Yesu hakufufuliwa kutoka katika wafu? (Sisi ni waongo!)
    6. Soma 1 Wakorintho 15:17-19. Kila ninapojaribiwa kuyaacha mapenzi ya Mungu na kujiingiza kwenye maisha ya dhambi, fikra yangu ya kwanza huwa ni “Ninawezaje kuishi bila uwepo wa Mungu?” Katika mapambano ya maisha, katika changamoto za maisha, kuwa na Mungu maishani mwangu limekuwa jambo la msingi. Paulo anawezaje kusema kuwa “kumtumaini Kristo” katika maisha haya pekee ni jambo la kusikitisha? (Nadhani anachomaanisha ni kwamba itakuwa ni sawa na mimi kulitumaini jino katika kipindi cha miaka yote hii. Jambo hili linaweza kuonekana kuwa la msaada, lakini ni jambo la kusikitisha sana kwa sababu nina tumaini la uongo.)
    7. Soma Mathayo 4:8-10. Je, hapa jaribu ni lipi?
      1. Je, jambo hili linatufundisha nini kuhusu imani ya Yesu katika Ufalme wa Mungu? (Kama Yesu angeshindwa, basi angepoteza kila kitu. Yesu alikuwa na uhakika kwamba atashinda. Hakuwa na hitaji la Shetani kumpatia falme za hapa duniani, kwa kuwa ataukomboa ulimwengu kwa ajili ya Ufalme wa Mungu.)
  2. Ufalme wa Mungu - Ukweli
    1. Soma 1 Wakorintho 15:20-22. Je, ukweli ni upi kuhusu ufufuo wa Yesu? (Kwamba alifufuka, na kwa hiyo tuna uhakika wa ufufuo wetu.)
    2. Soma 1 Wakorintho 15:6-8. Fikiria kidogo kauli za Paulo kuhusu injili kutokuwa na manufaa ikiwa Yesu hakufufuka kutoka katika wafu. Paulo anasema kwamba Yesu mfufuka alimtokea. Je, kauli za Paulo zinaaminika kwa kiwango gani? (Hii inaonesha kuwa Paulo hana nia ya kusema uongo kuhusu Yesu mfufuka. Anasema kuwa alimwona Yesu. Hana mashaka juu ya kile alichokiona. Kusema uongo juu ya jambo hilo kungeonesha kwamba alikuwa na maisha ya kusikitisha. Nani anapenda kuwa na maisha ya kusikitisha?
    3. Soma 1 Wakorintho 15:23-25. Je, ni kipindi gani tunachokiona kuhusu ufufuo wetu? (Yesu alifufuka kwanza. Wanaofuatia ni wale wanaoitwa “matunda ya kwanza” na kisha tunafufuliwa kabla ya kipindi cha “mwisho.”)
      1. Je, tunayo faida gani sisi kama raia katika Ufalme wa Mungu? (Ufalme wetu upo mikononi mwa Mungu. Falme za duniani zinaangamizwa.)
    4. Soma 1 Wakorintho 15:26. Jambo gani jingine litakaloangamizwa mwishoni? (Mauti! “Adui yetu wa mwisho” ataangamizwa.)
      1. Kwa nini hilo ni muhimu tunapoifikiria sheria? (Warumi 7:10-11 inatuambia kuwa Amri Kumi hutuletea mauti. Ikiwa kifo kinaangamizwa, hii inamaanisha kwamba pambano la mwisho dhidi ya dhambi limekwisha. Mungu ametupatia uzima wa milele!)
  3. Ufalme wa Mungu – Mustakabali
    1. Soma Ufunuo 21:1-3. Je, mustakabali wa Ufalme wa Mungu ni upi? (Utawekwa katika dunia itakayofanywa upya.)
      1. Kwa kuwa huu ni “Ufalme wa Mungu,” je, Mungu atakuwa wapi? (Atakaa pamoja nasi duniani!)
    2. Soma Ufunuo 21:4. Tofauti gani ya msingi itakuwepo katika huu Ufalme? (Hakuna machozi, mauti, maombolezo, wala maumivu.)
      1. Hilo linatufundisha nini kuhusu mtazamo wa Mungu dhidi ya mambo haya pale yanapotokea maishani mwetu sasa hivi? (Mungu anapingana nayo. Mungu atayaangamiza.)
    3. Soma Ufunuo 21:5. Je, ahadi ya Mungu inaaminika? (Mungu anamwambia Yohana kwamba hataki Yohana akosee jambo hili. Anasema, “Andika” kwa sababu ninataka watu wawe na uhakika kwamba wanaweza kuwa na uhakika kwamba hiki ndicho nilichokisema.)
    4. Soma Ufunuo 21:6-7. Mojawapo wa uchunguzi wa kale ni kwa ajili ya chemchemi ya ujana. Yesu anatuambia kuwa atatunywesha “chemchemi ya maji ya uzima.” Je, Mungu anaweka ahadi gani nyingine ya kupendeza? (Tutakuwa watoto wake. Atakuwa Baba wetu.)
    5. Soma Ufunuo 21:8. Hii ni orodha ya kufurahisha sana. Tunaweza kutikisa vichwa vyetu kuashiria kukubaliana kuwaacha wachukizao, wauaji, na waongo katika Ufalme wa Mungu kwa sababu tunahitaji mahali pa kuaminika pa kuishi milele. Lakini, jambo hili linaendanaje na dhana ya neema?
      1. Je, wauaji, waongo, na wachukizao hawawezi kuyategemea maisha makamilifu na kifo cha Yesu? Hivi punde tu tumejifunza hii ilikuwa kanuni ya msingi sana ya Ufalme wa Mungu!
      2. Wadhambi wengine, wazinzi, wachawi, na waabuduo sanamu wanaonekana kutokuwa tishio kubwa. Je, unaelezeaje suala hili? (Angalia jinsi orodha hii inavyoanza: “waoga, wasioamini.” Fungu la kwanza tulilojifunza lilikuwa ni 1 Wakorintho 15:1 lililowataja wale walioipokea injili na kuisimamia. Kumwamini Mungu, kumtumaini, ni jambo la msingi sana. Ikiwa huamini wala kutumaini, basi maisha yako yanajielekeza katika kuwatumaini watu wengine (wachawi, waabuduo sanamu), na kujipatia kipaumbele (waongo, wazinzi, wachukizao, na wauaji). Maisha yetu yanaakisi ikiwa kama tunaamini na kuchukua msimamo kuwa upande wa Mungu.)
    6. Soma Ufunuo 21:15-16. Yerusalemu Mpya ina umbo la mraba lenye urefu wa maili 1,400 katika upande mmoja. Umbali huu ni sawa na umbali uliopo kati ya mji wa Washington, D.C. na Denver, Colorado. Ni maili 1,659 kutoka Yerusalemu hadi Moscow. Hebu fikiria eneo la Yerusalemu Mpya, ambapo kila ukuta una urefu wa maili 1,400! Fikiria mji wenye urefu wa maili 1,400! Unadhani kutakuwa na mamlaka/utawala wa aina gani katika huo mji?
    7. Soma Ufunuo 22:1-3. Je, njia kuu ya Yerusalemu Mpya inaonekanaje? (Ina mto unaopita katikati yake. Mti wenye mashina pande zote mbili za mto unaambaa ambaa sanjari na kuta za mto.)
      1. Je, lengo la mto na matunda ya mto ni lipi? (Kutupatia uzima na kutufanya kuwa wenye afya.)
      2. Unaweza kufikiria ni aina gani za maduka na migahawa iliyopo bembezoni mwa njia kuu? Je, unaweza kufikiria kula chakula kwenye mgahawa karibu na sehemu ya kutembelea? Hakuna haja ya kuwa na wasiwasi juu ya kalori/chakula!
    8. Soma Ufunuo 22:6-7. Rafiki, je, unaamini? Je, unataka kuwepo mahali pale? Kiini cha injili ni kuamini kwamba Yesu anafanya uzima wa milele uwezekane kwetu. Kiini cha injili ni kumtumaini Mungu. Hiyo inamaanisha kwamba tunaamini katika neema yake ya pekee, na tuna tumaini kwamba sheria yake ni mwongozo wake wa upendo maishani mwetu. Je, utaiweka, sasa hivi, imani na tumaini lako kwa Yesu na kuungana na Ufalme wa Mungu?
  4. Juma lijalo: Tutaanza mfululizo mpya uitwao Mafundisho ya Yesu.